Sekta ya Mawasiliano inakua kwa kasi na kutoa mchango mkubwa katika
ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Idadi ya watumiaji wa huduma za
mawasiliano ya simu nchini imeongezeka kutoka laini za simu za
kiganjani milioni 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32 mwezi
Desemba, 2014. Gharama za kupiga simu zimepungua katika kipindi hicho
kutoka Shilingi 112 hadi Shilingi 34.9 kwa dakika.
Kupungua kwa gharama hizo kumetokana na Sera na mazingira mazuri ya
uwekezaji yaliyowezesha kuongezeka kwa watoa huduma na hivyo kuongeza
ushindani wa kibiashara. Pamoja na mazingira hayo mazuri, uamuzi wa
Serikali kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umewezesha watoa
huduma kutumia huduma za mkongo huo badala ya kila mmoja kujenga
miundombinu yake.
Aidha, kumekuwa na ongezeko la huduma nyingine kupitia mawasiliano ya
simu za mkononi kama vile, miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na
bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki. Inakadiriwa kuwa watumiaji
wapatao milioni 12.3 wanatumia huduma za miamala ya kibenki kwa
kutumia simu za kiganjani. Vilevile, watumiaji wa huduma za intaneti
wameongezeka kutoka milioni 3.6 mwaka 2008 hadi watumiaji milioni 11.3
mwaka 2014.
Serikali ya awamu ya nne ya Dr. Jakaya Kikwete ,imekamilisha Awamu
ya Kwanza na ya Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye
urefu wa kilomita 7,560 ambao uliunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote
Tanzania, baadhi ya Makao Makuu ya Wilaya na pia kuunganisha na nchi
jirani. Awamu ya Tatu ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa utaziunganisha
Wilaya zote nchini na kukamilisha uunganishaji wa maeneo ya Unguja na
Pemba.
Awamu hiyo itahusisha pia ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia
Kumbukumbu katika Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma. Katika
Awamu ya Nne, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano
ambao ni Airtel, Tigo, Vodacom na Zantel, inajenga Mikongo ya Mijini
(Metro Fibre Ring Networks), ambapo hadi mwezi Machi 2015, jumla
kilomita 91 zilikuwa zimekamilika katika Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, ujenzi wa Mikongo unaendelea katika Miji ya Arusha na Mwanza
ambapo jumla ya kilomita 94 zimejengwa. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
utakapokamilika, utawezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa
haraka zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Vilevile, utaboresha
mawasiliano baina ya Tanzania na nchi jirani pamoja na nchi nyingine
duniani baada ya kuunganishwa na Mikongo ya Kimataifa ya SEACOM, EASSy
na SEAS ambayo tayari imefika hapa nchini.
Serikali ya awamu ya nne imeingia Makubaliano ya Ushirikiano na
Kampuni ya VIETTEL (Viettel Joint Stock Company – VIETTEL) ya Vietnam
kuwekeza katika maeneo yasiyokuwa na mawasiliano vijijini. Kampuni
hiyo itajenga kwa awamu miundombinu ya Mkongo wenye urefu wa kilometa
13,000 kwa kutumia teknolojia rahisi katika Wilaya zote nchini pamoja
na kujenga miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa
na mawasiliano. Vilevile, Kampuni hiyo itaziunganisha Ofisi za Wakuu
wa Wilaya, Hospitali za Wilaya, Ofisi za Polisi za Wilaya na Ofisi 65
za Posta katika mkongo pamoja na kupeleka na kutoa huduma za
intaneti bila malipo katika shule tatu za Serikali katika kila
Wilaya kwa kipindi cha miaka mitatu. Uwekezaji huo
utakapokamilika utaleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano katika maeneo
ya vijijini, jambo ambalo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.
katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mikongo ya
Mijini katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma kwa
kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano nchini. Aidha, itaanza
Awamu ya Tano ya ujenzi wa Mkongo ambao utahusu kupeleka huduma kwa
watumiaji wa mwisho (last mile connectivity) ambao ni pamoja na watu
binafsi, Shule za Msingi, Sekondari na Vituo vya Afya ili kuwawezesha
kutumia fursa za TEHAMA katika elimu mtandao, maktaba mtandao na afya
mtandao.
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment