Wednesday, 7 September 2016

[wanabidii] Kumbe Mbowe msaliti wa nguvu ya umma?

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limefanya uamuzi mgumu dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe. Uamuzi wa kumshinikiza alipe malimbikizo ya deni lake la kodi kwa shirika hilo la taifa, deni la zaidi ya shilingi bilioni moja. 

Mbele ya NHC, Mbowe kupitia kampuni yake ya Mbowe Hotels Ltd ni mdaiwa sugu na hili limethibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Agosti 24, mwaka huu.
Pengine si tu mbele ya NHC bali hata mbele ya Watanzania wengi, Mbowe ni mdaiwa sugu kwa kurejea takwimu hizo rasmi za NHC, ambalo ni shirika mali ya wananchi linalojiendesha kibiashara ili hatimaye kutoa gawiwo kwa serikali kuu na kuboresha hali za makazi ya wananchi nchini.

Kwa hiyo na kwa vyovyote vile, hujuma yoyote dhidi ya shirika la umma ikiwamo hii ya kutolipa kodi ni sawa na hujuma dhidi ya umma ambao chama anachokiongoza Mbowe kimekuwa kikijinadi kupitia salamu yake ya "nguvu ya umma."
Tayari Mbowe amekwishafanya utetezi dhidi ya tuhuma hizi za kuitwa mdaiwa sugu wa NHC. Kwa bahati mbaya, utetezi wake umebeba siasa, pengine kwa sababu tu ya kutafuta kichaka na kuficha aibu ya kihistoria ya kuwa miongoni mwa wadaiwa vinara na sugu wa NHC.

Katika utetezi wake wa Agosti 24, mwaka huu, baada ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC kutangaza kuwa mwanasiasa huyo ni mdaiwa sugu, Mbowe alitoa taarifa kwa umma akijitetea kwa kupiga porojo za kisiasa, kwanza akikiri kuwapo deni ama mgogoro wa kibiashara wa miaka mingi baina ya kampuni yake na NHC.

"Kumekuwepo na ukakasi wa muda mrefu kuhusiana na mkataba wetu wa umiliki, uendelezaji na uendeshaji wa jengo hili unaochagizwa na msimamo wangu wa kisiasa," anasema Mbowe na kuendelea; "Haki na Uhuru wetu wa kufanya biashara kama raia wengine umekuwa ukiingiliwa mara kwa mara katika mazingira yanayoambatana na vitisho kiasi ambacho maamuzi kadhaa hayafanyiki kwa hofu ya kisiasa kwamba itakuwa kumwongezea nguvu mpinzani."

Anasisitiza akitaka Watanzania waelewe kuwa hadaiwi. Bado anapiga siasa akisema; "Sitafungwa fikra, sitafungwa mdomo na sitaacha kuutetea ukweli, haki na demokrasia katika nchi hii kwa misingi ya kulinda kinachodhaniwa ni maslahi yangu ya kibiashara." Anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifungwa fikra na midomo ndani ya nchi hii kwa kuogopa hila na ghiliba za watawala.

Anasema; "Ni heri kufa masikini nikiwa nimesimamia ukweli, kuliko kuishi tajiri niliyetawaliwa na ubinafsi, woga, hofu na ubatili."
Lakini pamoja na kauli hiyo ya kukanusha kudaiwa katikati ya hoja za kisiasa, NHC kwa niaba ya Watanzania, uongozi wake umesimama imara kudai haki ya umma. Unaweza kujiuliza Mbowe ni mtu wa namna gani pale maslahi yake yanapokinzana na umma? Je, yuko tayari kwa kiasi gani kulinda maslahi yake bila kujali athari kwa umma? Mbowe anapaswa kufahamu haya.

NHC kudai wadaiwa si siasa
Pengine historia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imemkalia kando Mbowe huyu wa Chadema. Nitamkumbusha jambo ili afute hoja zake nyepesi kwamba kitendo cha NHC kudai wadaiwa sugu ni ajenda ya kisiasa.

Takriban miaka 44 iliyopita, yaani mwaka 1972, Freeman Mbowe akiwa na umri wa miaka 11 tu kwani alizaliwa Septemba 14, 1961, Shirika la Nyumba la Taifa lilifanya uamuzi mzito wa kudai wadaiwa wake sugu.

Katika kutangaza uamuzi wake huo, Ofisa Uhusiano wa NHC kwa wakati huo, E. Musabalala, aliutangazia umma namna shirika hilo la umma litakavyolinda maslahi ya umma. Akasema shirika limefanya uamuzi wa kuunda kamati maalumu nchini ili hatimaye kuwafukuza wapangaji ambao ni wadaiwa sugu, waliolimbikiza kodi za shirika hilo.

Kwa kumkumbusha tu Mbowe ni kwamba, kamati ya kwanza kuundwa ilikuwa na watu 14 na ilifanya uchambuzi kwa wapangaji sugu katika nyumba za shirika hilo la umma maeneo ya Ilala, Upanga, Ukonga na Barabara ya Morogoro, mjini Dar es Salaam. Kazi hiyo ilianza Oktoba, mwaka 1972.

Na uamuzi huo wa kuuda kamati ulikuwa wa mwendelezo tu kwa sababu tayari uamuzi wa shirika kuwafukuza wapangaji wadaiwa sugu ulikwishaanza mwezi Mei, mwaka huo wa 1972.

Kwa hiyo, Mbowe asilete siasa kwamba anakandamizwa kwa sababu eti ni mwanasiasa wa upinzani. Ajue tu kwamba rekodi zinaonesha uamuzi wa NHC kushughulika na wadaiwa sugu kama yeye, wenye kufanya hila za hapa na pale, ulianza zamani tena akiwa na umri wa miaka 11. Asimuonee Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Mchechu, ajue shughuli hii ni pevu, uamuzi wa busara kwake ni kulipa fedha za umma, asiishie tu kutamka jukwaani …. Peopleees … power, bali ajue nguvu ya umma sasa inadai chake kupitia NHC.

Si wa kwanza kutupiwa virago
Katika utetezi wake, Mbowe anasema ametupiwa virago na kwamba utekelezaji wa uamuzi wa NHC kupitia dalali wake ni wa uonevu kwake, watu wake wanadai hata taasisi mbalimbali za serikali zinadaiwa lakini kwa nini hazikutupiwa virago kama yeye. Anahoji, iweje yeye pekee na anahitimisha kwamba anapigwa siasa.

Hapa niweke wazi kwamba kuna tatizo la kumbukumbu kuhusu NHC kufanya uamuzi mgumu kwa wateja wake ambao wadaiwa sugu, wadaiwa wanaohujumu umma. Nitajadili mambo mawili muhimu hapa.

Mosi, Mbowe akumbuke kuhusu kile kilichoandikwa katika gazeti linalomilikiwa na familia yake la Tanzania Daima la Oktoba 12, mwaka 2013, habari iliyoandikwa na mwandishi na mpiga picha wa gazeti hilo, Joseph Senga (Mungu amrehemu).
Habari ile ilieleza uamuzi mgumu wa NHC kuwatupia virago madaktari wawili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa sababu mwajiri wao, yaani Muhimbili kulimbikiza deni.

Madaktari hao wawili ni Dk. Wambura Chacha na mwenzake bingwa wa upasuaji katika Kitengo cha Mifupa (MOI), Profesa Joseph Kahamba. Hawa wanaweza kuwa mashahidi kwamba NHC haifanyi siasa, bali inadai fedha za umma.

Madaktari hao, kwa mujibu wa habari hiyo ya Tanzania Daima walikuwa wakiishi katika nyumba namba 355 mali ya NHC, Mtaa wa Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Mwajiri wao alikuwa amelimbikiza deni la miezi 15 lililokuwa limefikia Sh 9,738,000. Sasa itakuwa Mbowe mwenye deni la bilioni takriban 1.2? Halafu unadai eti siasa!

Operesheni hiyo ya wakati ule ya kudai fedha za umma kutoka kwa wadaiwa sugu kama Mbowe iliendeshwa na Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga. Kwa wakati ule wa operesheni hiyo Muhimbili ilikuwa ikidaiwa Sh milioni 135.6, yakiwa ni malimbikizo ya malipo ya pango kwa vipindi tofauti.

Kwa hiyo ya Mbowe na wenzake kwamba anaonewa kwa kutupiwa virago wakati serikali na taasisi zake ni wadaiwa sugu haina ukweli, bali ni porojo za kusaka huruma ya kisiasa. Kama ataweka kumbukumbu zake vizuri, atakumbuka pia kwamba hata Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wakati huo ikiongozwa na

Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilitupiwa virago na NHC. Asilete ndoto za mchana.
Pili, kuna jambo analopaswa kulielewa Mbowe. Kwamba serikali na taasisi zake zinaweza kufanya mawasiliano ambayo Mbowe kama mmoja wa wadaiwa sugu si lazima apewe taarifa za namna wadaiwa wenzake walivyojipanga kulipa madeni yao. Serikali inayo bajeti yake na hili Mbowe anapaswa kulijua vizuri kwa sababu ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, na ajue yeye kama mtu binafsi au kampuni zake bajeti yake ni siri yake.

Kwa hiyo si sahihi kudai kuwa umetupiwa virago na wenzake hawajatupiwa. Usahihi kuwa, na kwa kweli kwa mtu makini anapaswa kutambua kuwa jambo la msingi ni kulipa deni, tena deni linalohusu fedha za umma si kujitetea kuhusu muda wa kulipa kwa wadaiwa wenzako. Kila mdaiwa anaweza kuwa na makubaliano tofauti na anayedai.

Haenei katika ubepari, ujamaa
Chadema, ambacho Mbowe ni mwenyekiti wake kinajinadi kuwa na mrengo wa kibepari. Ni kweli ubepari unahusu kutumikisha watu ili bepari anufaike zaidi lakini katika huo huo ubepari, hasa kwa mabepari wa kweli ni lazima unayemtumikisha aendelee kula, kubaki katika afya njema ili endelee kuishi na uendelee kumtumikia. Hili inaonekana halimo kichwani mwa Mbowe, wale anaojinadi nao kuwa ni nguvu ya umma sasa hao hao ndio wanaomdai kodi aliyolimbikiza kupitia shirika lao la umma – NHC.

Tazama, utu wa mabepari wa kale kwa kurejea kijiji Saltaire, kule Shipley, kijiji ambacho ni sehemu ya Jiji la Bradford, pale Yorkshire ya Magharibi, England, miaka 163 iliyopita, yaani mwaka 1853 au kijiji cha Port Sunlight kule Merseyside, England, mwaka 1888, miaka 128 iliyopita. Hoja ni kwamba mabepari hawa wa kale walisaidia umma wao karne zaidi ya moja lakini Mbowe, Mwenyekiti wa chama cha kibepari, anadaiwa kodi ya umma na bado anakuwa mbishi. Ni kama vile hafafani hata na ubepari wa kale enzi za kikoloni, achilia mbali upebari wa kisasa.

Wakoloni ambao mwaka 1885, baada ya ripoti ya Tume ya Kifalme England walianzisha, kwa mara ya kwanza, mpango wa makazi kwa wafanyakazi kupitia sheria iliyoitwa Housing of the Working Classes Act ya mwaka 1885. Sasa Mbowe hajui kwamba lengo la NHC kudai kodi ya umma ni kusaidia wafanyakazi wa nchi hii katika suala la makazi, wafanyakazi ambao Rais John Magufuli aliahidi kuboresha maslahi yao, maslahi ambayo bila shaka ni pamoja na makazi bora kwa kadiri inavyowezekana.

Mbowe kalipe deni lako, usikwaze umma. Umma unahitaji kufaidika na jengo ulilohodhi kwa kulimbikiza kodi, lile jengo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hima hima Mbowe, jitahidi kuheshimu na kutunza haki ya kiapo ya uadilifu na maadili ya utumishi wa umma, kwa nafasi yako kama mbunge, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na zaidi ya hapo, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini. Lipa deni kuleta utulivu ndani ya umma wa Watanzania, uamuzi wa kulipa unaweza kusaidia kuepusha mpasuko kitaifa na kifamilia.

Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment