Sunday 25 September 2016

[wanabidii] Tulitaka mabadiliko tukubali maumivu

Maisha yanakanuni zake, kanuni hizi zisipozingatiwa na kufuatwa matokeo yake huwa mabaya lakini zikizingatiwa matokeo huwa mazuri.

Kanuni za kuifanya nchi iondokane na kero mbalimbali ambazo chanzo chake ni Taifa kutawaliwa na uongozi usiofaa ni kufanya mabadiliko ya uongozi. Kwa lugha nyingine twaweza kusema ni kuondoa uongozi wa awali na kuweka mpya ambao utaweza kuleta matokeo mazuri.

Katika hilo watanzania waliamua kumchagua Dk. Magufuli kuwa rais. Tayari matokeo yake yalishaanza kuonekana. Kishindo chake kilishaanza kuleta mabadiliko.

Swali la kujiuliza ni kwamba je, mabadiliko hayo ndiyo watanzania waliyataka? Kama ni hayo, kwanini sauti za lawama nzito dhidi yake zisikike nchini? Hawa wakilaumu kuwa amebana fedha na kuifanya hali ya maisha kuwa ngumu kuliko ilivyokuwa mwanzo. Wengine wakisema ameminya demokrasia?

Wanaodai hali ya maisha imekuwa mbaya, wanamshutumu kuwa amesababisha biashara mbalimbali nchini kuwa mbaya.

Kweli kuna makampuni yanaonesha yameyumba kimapato na mengine hata kufilisika kabisa kwa sababu mbalimbali.

Mfano kuna hoteli zimeripotiwa kufungwa, kuuzwa na hata kubadili matumizi kutokana na sababu mbalimbali ambazo kwa ujumla wake kiini chake ni utendajikazi wa Dk. Magufuli. Kifupi ni ukweli kwamba kwa kiwango kikubwa biashara nyingi zimeathiriwa sana. Sio biashara tu, inasemekana hata kasi ya ujenzi wa majumba imepungua kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, wanasiasa wengi wanapozungumzia suala hilo inaonesha wanajaribu kuzungumzia kwa namna ambayo itawafanya watanzania waone kana kwamba serikali ya Dk. Magufuli imeshindwa kuongoza nchi kwa namna bora.

Kwa hilo binafsi sishangai kwa kuwa natambua aina ya wanasiasa tulionao nchini na vita kubwa aliyonayo rais kwenye nchi hii katika kuhakisha analeta mabadiliko yatakayokuwa na tija kwa kizazi cha leo na cha kesho.

Licha ya baadhi ya watu kulalamika kuwa mdororo wa uchumi nchini umesababishwa na Rais Magufuli sio ishara ya serikali yake kushindwa kuleta mabadiliko ambayo watanzania waliyataka.

Hapana shaka ni dhahiri kuwa mabadiliko ambayo watanzania waliyataka ili yapatikane ilikuwa sharti wapate kiongozi atakayekomesha matumizi mabaya ya mali za umma na rushwa. Pia ilitakiwa wapate kiongozi atakayekomesha tabia za watendaji kutokuwajibika ipasavyo.

Katika hilo walimwamini Dk. Magufuli kuwa ndiye mtu aliyeaminiwa na kupewa jukumu la kuondoa ufisadi, rushwa, pamoja na tabia ya watendaji kutowajibika ipasavyo.

Ili kupambana na ufisadi pamoja na watendaji wabovu hali sasa imekuwa imeathiri mzunguko wa fedha nchini. Imekuwa hivyo kwa kuwa njia nyingi za upatikanaji fedha nchini zilikuwa sio za halali. Kwa maana hiyo uchumi wa nchi yetu kwa kiwango ulijijenga na kujiimarisha kwenye misingi haramu.

Watu walikuwa wanapata fedha nyingi kwa njia ambazo zilikuwa zinaliangamiza kabisa taifa.

Naeleza hivyo kwa kuwa kuna watu ambao walikuwa wanapokea mshahara serikalini, wakati huo huo walikuwa hawafanyi kazi za kiserikali, badala yake walikuwa wanafanya shughuli sehemu zingine ili kujiongezea kipato. Hivyo kuwafanya wawe na vyanzo vya kujipatia kipato zaidi ya kimoja.

Hao ni pamoja na waliokuwa waajiriwa serikalini, ambao muda mwingi waliutumia kufanya biashara zao na wale ambao walikuwa wanautumia kufanya kazi kwenye sekta binafsi.

Lakini pia kuna ambao waligeuza ofisi za umma kuwa vitega uchumi vyao binafsi. Hao ni pamoja na waliokuwa wanajipatia fedha kwa njia mbalimbali haramu kupitia ofisi za umma.

Mfano sote tunajua namna watu walivyokuwa 'wanapiga' fedha kwa kuwa na makampuni bubu ya kugushi nyaraka za serikali kwa mfano vyeti na wengine walivyokuwa wanapata fedha nyingi kwa kutengeneza waajiriwa hewa serikalini.

Niliwahi kuzungumza na wafanyabiashara kadhaa Karikoo jijini Dar es salaam, nilielezwa kuwa mara nyingi bandarini mtu alikuwa anaweza akaagiza mzigo ambao kwa kawaida mtu anapaswa kulipia Sh milioni 10, lakini akalipia Sh milioni nne au tano kama rushwa na akachukua mzigo wake.

Kwa muktadha huo wafanyabiashara wengi waliokuwa wanaitumia bandari yetu kupitishia mizigo yao, walikuwa wanatumia gharama kidogo tofauti na gharama zinazotakiwa kwa mujibu wa taratibu za tozo. Hii yote ni kwa kuwa idara nyeti za serikali ikiwemo bandari yetu viligeuzwa kuwa ni kama mali binafsi ya wajanja wachache.

Wajanja hao walitumia idara za serikali kwa mfano bandari kuingiza matrilioni ya fedha kwa njia haramu, huku serikali ikishindwa hata kupata fedha kwa ajili ya kutengeneza miondombinu ya kusafirisha mizigo inayotoka bandarini hapo kwenda mikoani au kwenye nchi za jirani, kwa mfano reli na barabara.

Hata hivyo ni wazi kuwa mtiririko wa vitendo vya namna hiyo uliotengeneza mzunguko wake wa fedha nchini (mfumo wake wa uchumi) ambao ulikuwa unawafanya watu hasa watendaji wa serikali kuishi maisha ambayo yalikuwa hayasadifu pato na uwezo wa serikali kifedha.

Watu waliporomosha majumba ya kifahari, walinunua magari ya kifahari, walifanya hoteli za kifahari kuwa majumba yao ya kuishi, kuwa ofisi zao, kuwa sehemu za kufanyia mikutano ya kiserikali kwa namna ambayo huwezi ukaamini kuwa ni watendaji kazi wa idara za serikali ambazo zilishindwa kijiendesha kwa mapato, pia ambazo zilishindwa kutoa huduma muhimu za kijamii.

Pombe na kubadilisha makahaba kwao ilikuwa ni kawaida. Wakati huo wao ndio walikuwa mstari wa mbele kulia hali mbaya ya kifedha serikalini. Kitu ambacho kilikuwa kinailazimu serikali kutegemea mikopo na wahisani kwa ajili ya kuendesha mambo ya kiutawala, pia kwa ajili ya kutoa huduma muhimu za kijamii. Hivyo kulifanya deni la taifa kuzidi kuongeza kwa kasi kila kunapoitwa leo, huku ikishindwa kufanya vitu ambavyo vinaendana na kasi ya kuongezeka kwa deni hilo.

Dk. Magufuli katika kutekeleza majukumu yake ya kuleta mabadiliko nchini, tayari alishaanza kuchukua hatua kali dhidi ya njia zote haramu ambazo kwa kiwango kikubwa ndizo ambazo zilitengeneza mzunguko wa fedha. Hii yote ni kwa kuwa pamoja na kuwa zilikuwa zinaufanya mzunguko wa fedha kuonekana mzuri nchini, kila kuitwapo leo zilikuwa zinaliangamiza taifa.

Waliokuwa wanaingiza fedha nyingi kwa kutumia ofisi za umma kama vitega uchumi vyao wamebanwa. Lengo ni kufanya ofisi za umma zitumike kwa masilahi ya umma kama inavyotakiwa. Wafanyabiashara waliozoea kufanya watakayo kwenye nchi yetu ambao ndio walikuwa wamejijaza nchini wamebanwa.

Kama ni hivyo itawawezekana vipi mzunguko wa fedha ulikuwepo kutoathiriwa, ili hali njia ambazo zilikuwa ndio chanzo cha mzunguko wake zimeanza kuharibiwa?

Je, walikuwa wanapata fedha nyingi kwa njia haramu, wataendeleaje kuporomosha majumba ya kifahari, watanunuaje magari ya kifahari, wataendeleaje kubadilisha makahaba kama nguo, wataendeleaje kuzifanye hoteli za kifahari kuwa nyumba zao za kuishi, ili hali njia ambazo walikuwa wanazitegemea kujipatia fedha tayari zilishazibwa kwa kuwa zilikuwa zinaliangamiza taifa?

Huwezi ukaleta mabadiliko ya uchumi juu ya uchumi mbovu. Kufanya hivyo ni sawa na kujenga nyuma mpya imara juu ya nyumba nyingine mbovu.

Lazima tuelewe kuwa huduma kwa maendeleo ya nchi yetu zinatokana na taifa kuwa na misingi mibaya ya mzuko wa fedha. Misingi hiyo ndiyo ambayo Dk. Magufuli alishaanza kuibomoa kwa kuziba njia zake. Akishamaliza kazi hiyo naamini ataanza kujenga misingi mipya ambayo ndiyo itatoa matokeo halisi ya utendaji kazi wake. Ndiyo maana binafsi ninaona sio sahihi kutumia kigezo cha kuathiriwa kwa mzungunguko wa fedha ulikuwepo kabla ya Dk. Magufuli kwa namna itakayoufanya umma uone ameshindwa kuongoza kwa njia bora.

Kweli taifa linapita kwenye hali ya maumivu. Lakini maumivu tunayoyapata kwa sasa yanalenga kuliponya taifa na kuleta mabadiliko makubwa. Ndiyo sababu Dk. Magufuli alijibatiza jina la mkamua majipu. Naamini alijiita hivyo kwa kuwa alijua fika kuwa mabadiliko yanayohitajika ni sharti taifa lipate maumivi ndipo yatokee.

Hatuna budi kuyavumilia kwa kuwa historia inaonesha mabadilko mazuri mara nyingi hayapatikani bila mtu au taifa kupitia kwenye kwenye maumivu. Kwa mfano, taifa la china mpaka kufikia kwenye hali ya uchumi mkubwa tunaouona leo walipitia kwenye vipindi vya maumivu makali sana. Historia inaeleza namna njia zilizotumika zilisababisha mateso makubwa miongoni mwa wananchi na wengine hata kupoteza maisha.

Kwa kigezo hicho watu wasipotaka kupitia maumivu pindi inapohitajika kufanyika hivyo ili kuleta mabadiliko yenye tija ni vigumu taifa kupata maendeleo.

Kweli kabla ya Dk. Magufuli fedha ilikuwa inapatikana kuliko leo, lakini namna ya upatikanaji wake ilikuwa ni sawa na familia ambayo inapata fedha kwa kuuza mali za familia ambazo kimsingi hazipaswi kuleta kwa manufaa ya familia kwa kipindi cha leo na baadaye.

Hapana shaka sote tunatambua kwamba kuuza shamba au nyumba ya familia kunafedha nyingi kuliko kukodisha. Lakini kwa namna nyingine ni hasara hasa ikiwa nyumba au shamba limeuzwa na wahusika wametumia fedha ovyo.

Tutambue kuwa ingawa ni kweli fedha iliyokuwa inapatika kipindi kilichopita ni kubwa kuliko, lakini namna ilivyokuwa inapatana ilikuwa ni sawa wanafamilia iliyokuwa inapata fedha nyingi kwa kuuza mali za familia kila siku kwa ajili ya kufanya starehe kwenye mabaa n,k. Huku wakionesha kutokujali namna gani wataishi ikiwa mali za familia zitaisha kwa kuuzwa.

Kwa maana hiyo kitendo alichofanya Dk. Magufuli hakina utofauti na wanafamilia walizuiwa kuuza ovyo mali za familia ili kupata fedha. Kweli taifa likiwa kama familia watu wake hawatakuwa na fedha kama ilivyokuwa awali kama ambavyo imetokea nchini lakini ni kwa ajili ya kulinda manufaa ya kizazi cha leo na cha kesho.

Najua hata Dk. Magufuli kwa kipindi hiki anakumbana na mambo mengi yenye kumuumiza na kumvunja moyo na pengine alishaanza kukata tamaa. Hata hivyo anapaswa kutambua kuwa shujaa hufia vitani akipambana.

Hapaswi kurudi nyuma wala kulegeza misimamo ingawa kadri siku zinavyozidi kwenda maadui wanaopambana dhidi yake kwa njia mbalimbali wanazidi kuongezeka. Hii ni kutokana na utendaji wake kila kunapokucha kuendelea kuwagusa kwa kiwango kikubwa watu ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wananufaika sana kwa maovu yaliyoshamiri nchini.

0 comments:

Post a Comment