Thursday 29 September 2016

[wanabidii] Profesa Lipumba ni msaliti?

UMECHANGANYIKIWA hujui lipi uamini na lipi usiliamini katika mgogoro unaoendelea ndani ya chama cha upinzani cha CUF? Hauko peke yako. Hata mimi, nazidi kutatanishwa.

Swali moja la msingi sana ambalo nimejiuliza ni je, ni kweli Profesa Lipumba ni msaliti aliyenunuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuleta fujo ndani ya CUF, kama wanavyodai wapinzani wake?
Kumekuwa na ushabiki mkubwa sana katika kulizungumzia suala hili, mara nyingi watu wakiunga mkono upande mmoja au mwingine kutokana na mapenzi na ushabiki, kama ule wa Simba na Yanga.

Hata hivyo, habari ya kambi moja ya vyama vya siasa kutuhumu kambi nyingine kuwa imehongwa imezoeleka sana katika siasa za Tanzania na kwa hiyo hili ni suala la kutazamwa kwa tahadhari, hasa linapotoka kwa watu ambao uongo ni sehemu ya kazi yao.

Ukiangalia historia ya chama cha CUF, wanachama waandamizi wengi wamewahi kutimuliwa au kulazimika kujiondoa baada ya kutuhumiwa kuwa ni wasaliti walionunuliwa na chama tawala, baadhi yao ni Profesa Abdallah Safari na Hamad Rashid na wengine wengi kabla ya hao.

Katika vyama vingine, hali imekuwa hiyo hiyo.  Watu wamekuwa wakituhumiana kwa usaliti, ambao mara nyingi hujitokeza pale watu wanapohoji masuala ya msingi au kutangaza nia ya kugombea nafasi za juu zenye wenyewe.
Si hivyo tu, hata hoja zinazotajwa za kuwatia hatiani wanaoitwa wasaliti ni dhaifu. Kwa mfano, inaweza kutajwa kuwa mtuhumiwa alionekana akizungumza na kiongozi wa CCM au kanunua nyumba mpya, gari na kadhalika.

Katika suala hili la Profesa Lipumba, kuna hoja mpya imeibuka. Kwamba, vyama vya CCM na ACT wanashangilia au hata kumsaidia. Hoja hii ina udhaifu kwa sababu pindi taasisi moja ikikumbwa na  mgogoro, ni jambo la kawaida mpinzani kufurahia na kuunga mkono upande mmoja ambao maslahi yao yameelemea au tu ili mgogoro uzidi kukolea. Hata Maalim Seif naye anaungwa mkono na Chadema.

Ijulikane kuwa mgogoro wa CUF ni nafuu kubwa kwa chama tawala na serikali yake kule Zanzibar kwa sababu unasaidia kupata hoja za kumshambulia Maalim Seif anayejinasibu na  demokrasia na utawala wa bora unaozingatia sheria. 
Pia, CCM wana haki ya kushangilia kwa sababu ushindi wa Profesa Lipumba unamuondoa Maalim Seif katika mambo ya msingi ya kupigania 'ushindi' wao  Zanzibar. Ingawa, adui wa adui anakuwa rafiki, lakini halithibitishi kuwa Profesa Lipumba kalipwa.

Kimsingi CUF ya Lipumba huku bara wana madai ya msingi. Kwa miaka mingi, baadhi ya wanachama wa CUF wamekuwa wakilalamika kukosekana uwekezaji wa kutosha wa kuendeleza chama huku bara. Kama hilo halitoshi, malalamiko ya safari hii ni zaidi ya mambo ya kiutawala na mgawanyo wa fedha wa kuendesha chama.

Safari hii malalamiko yanahusu falsafa na ajenda za chama kutokana na muungano wa Ukawa.  CUF -Lipumba wanaamini muungano huo umevuruga malengo ya chama na kukitoa upande wa bara kafara kwa Chadema.
Tukirudi katika suala la msingi, kahongwa au hakuhongwa. Binafsi naamini kuwa kwanza, si sahihi kutoa madai kama haya bila ushahidi. Pili, kilicho dhahiri ni kuwa hata kama Profesa Lipumba angekuwa amehongwa, wafuasi wake wanaamini wa dhati katika mapambano anayoyaendesha.

Mmoja wa wafuasi wa Profesa Lipumba alinipigia simu kuhusu makala yangu ya wiki iliyopita niliyohoji Profesa Lipumba kuendelea kung'ang'ania uenyekiti hata baada kuharibiwa jina kwa kutuhumiwa kupanga utekaji.

Mfuasi yule alidai walimuomba Profesa Lipumba arudi CUF ili kukirudishia chama hicho hadhi na nafasi yake iliyotwaliwa na Chadema, kama chama cha kikuu cha upinzani, ingawa kipindi CUF ikiwa chama kikuu cha upinzani, mchango mkubwa bado ulitoka visiwani.
Ukiacha uchaguzi wa mwaka jana ilipopata viti 10 bara vya ubunge, CUF haijawahi kuchukua viti zaidi ya viwili.

Jambo moja alilomalizia mfuasi yule wa Profesa Lipumba ni kurudisha tuhuma za kuhongwa kwa Maalim Seif. Akaniambia; "Wewe hushangai alikuwa akifanya mazungumzo yeye peke yake dhidi ya viongozi sita wa CCM na amekuwa akienda Chadema peke yake, pana nini hapo kama si rushwa?"

Tuendelee kufuatilia mchezo utaishaje. Watagawana mbao? Nilichojifunza wiki iliyopita ni kuwa Maalim Seif atakuwa amefanya kosa kudharau nguvu ya Profesa Lipumba ambaye anakubalika kule chini kwa watu ambao hawapo mitandoni hususan sasa baada ya kurudishiwa uenyekiti na msajili wa vyama na ukizingatia kuwa aliapa kutotoka CUF ng'o.

Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment