Sunday, 25 September 2016

[wanabidii] Hongera Jakaya Kikwete kutunukiwa tuzo

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete wiki hii ametunukiwa tuzo ya uongozi wa kisiasa na utetezi wa makundi ya jamii yanayoishi katika mazingira magumu.

Tuzo hiyo imetolewa kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake na watoto. Kitendo hicho cha Shirika lisilo la kiserikali la Speak up for Africa, kupitia Mkurugenzi wake, Kate Campana kumpa tuzo kiongozi huyo, kimeongeza idadi ya tuzo mbalimbali alizopewa kutokana na kutoa mchango mkubwa katika kutetea makundi mbalimbali.

Tuzo hiyo iliyotolewa juzi jijini New York Marekani, sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa shirika hilo, iliyofanyika, ilitambua mchango wa Rais huyo wakati akiwa madarakani, kati ya Desemba 21, 2005 hadi Novemba 5, 2015 na hata baada ya kustaafu, amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake na watoto.

Rais mstaafu Kikwete amepewa tuzo hiyo kutokana na kusambaza huduma za msingi za afya hususan katika afya ya mama na mtoto, kusimamia kwa dhati kampeni ya kupambana na malaria kupitia mpango wa malaria haikubaliki, na kusimamia bila kuchoka usambazaji wa vyandarua vyenye viuatilifu, amesimamia kampeni ya kuhamasisha lishe bora kwa mama na watoto, lakini pia utoaji wa chanjo kwa watoto wa chini ya miaka mitano.

Rais mstaafu Kikwete pia amekuwa mstari wa mbele katika kulisimamia bara la Afrika katika masuala mbalimbali yakiwamo ya afya ya mama na mtoto. Sisi tunafurahishwa na kitendo cha Shirika lisilo la kiserikali la Speak up for Africa, kumpa tuzo rais wetu mstaafu kwani kinaonesha ni kwa namna gani viongozi wa Tanzania wanajali maisha ya wengine hapa nchini, Afrika na duniani kwa ujumla kiasi cha kutunukiwa tunu mbalimbali.

Aidha inatupasa kukumbuka kwamba kutokana na uongozi wake na usimamizi wa haki hizo, pia alipewa heshima ya kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika Maendeleo Bara la Afrika mwaka 2013. Heshima hiyo ilitolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group.

Kiongozi huyo pia alipokea, Tuzo ya Kiongozi Bora Afrika Mashariki kutoka katika Taasisi ya East Africa Book of Records yenye makao yake makuu jijini Kampala Uganda. Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwake na kiongozi wa Taasisi hiyo, Dk Paul Bamutize wakati wa hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais mstaafu wetu amepewa tuzo nyingi tu, ukiachia mbali tuzo za kimataifa, pia ametunukiwa tuzo mbalimbali ndani ya nchi ikiwamo aliyokabidhiwa na aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh kutokana na kutambua mchango wake katika usimamizi wa taasisi hiyo na kuimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji wakati wa hafla maalumu iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Orodha ya tuzo za heshima na shahada za heshima kwa Rais mstaafu Kikwete ni nyingi, lakini zote zilitolewa kutokana na kutambua mchango wake katika kupigania haki mbalimbali zikiwamo za jamii inayoishi katika mazingira magumu.

Pamoja kumpongeza kiongozi huyo aliyetoa mchango mkubwa katika kutetea jamii inayoishi katika mazingira magumu, tunawahimiza Watanzania kujifunza kutoka kwa kiongozi huyu ambaye alitumikia wananchi kwa namna ambayo imetukuka na hivyo kumpatia heshima.

0 comments:

Post a Comment