Friday, 2 September 2016

[wanabidii] Sumaye wakujifananisha na Che Guevara?

MAKALA haya niliyaandika muda mrefu; mara Frederick Sumaye, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipodiriki kujifananisha na Che Guevara.
Hata hivyo nilisita kumpelekea mhariri makala haya. Nilifikiri wapo wanazuoni mahiri, Chadema, ambao wangemshauri Sumaye afute kauli mara moja. Ninamfahamu Profesa Mwesiga Baregu aliyekuwa akifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye alipata kuwa na sauti Chadema. Ninawafahamu John Mnyika, Mbunge wa Kibamba na Mwita Mwikabe, Mbunge wa Ukonga, ambao walikuwa na sauti katika chama hicho na wanamfahamu vyema Guevara.
Nilifikiri hawa wasingelinyamazia jambo hili. Wakati nikijiandaa kumplekea mhariri makala haya mwanzoni mwa mwaka huu nikasikia kwamba Sumaye amelazwa Hospitali ya Taifa ya Rufaa Muhimbili. Nikasita kwa mara nyingine tena kumpelekea mhariri makala haya.
Sasa msimu mwingine wa siasa umewadia. Ni msimu wa minyukano kati ya chama tawala na baadhi ya vyama vya upinzani. Msimu huu unampa Sumaye fursa adimu kujaribu bahati yake na kufanya walau tukio moja la kimapambano ili kudhihirisha kufanana kwake na Che Guevara. Pamoja na kuwa wote ni binadamu kuna tofauti kubwa mno kati ya Guevara na Sumaye.
Tuanze kwa kutazama maisha ya watu hawa wawili. Guevara (tamka Bara) alizaliwa 1928, Argentina, katika familia ya kisomi. Baba yake Guevara alikuwa na vitabu zaidi ya 3,000. Guevara alipata fursa ya kusoma vitabu nyumbani kwao. Aliwasoma, mbali na waandishi wengine, wanamapinduzi kama Karl Marx, Jawaharlal Nehru, Vladimir Lenin, Jean-Paul Sartre, na Friedrich Engels. Sumaye ni mtoto wa mkulima. Sidhani kama kulikuwa na vitabu nyumbani kwao. Nina shaka sana kama Sumaye aliwahi kuwasoma wanamapinduzi wa kijamaa.
Guevara alifanya vizuri zaidi kitaaluma kuliko Sumaye. Alihitimu shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Buenos Aires 1953. Kuna vitabu na machapisho mengi kuhusu maisha ya Guevara. Guevara mwenyewe ni mwandishi wa vitabu. Moja ya vitabu vyake ni Guerrilla Warfare; ambacho kimekuwa msahafu unaosomwa sana na wapiganaji wa vita vya msituni pande zote za dunia. Kutokana na ziara yake, kwa baiskeli aliyoiweka injini ndogo, kuzunguka nchi nyingi katika bara la Amerika Kusini, Guevara aliandika kitabu kinachoitwa The Motorcycle Diaries ambacho kilikuwa kitabu kinachouzwa sana kwa mujibu wa Gazeti la New York Times na ambacho kilitumika kutengeneza filamu maarufu yenye kichwa cha habari kama kitabu hicho. Aliandika pia Congo Diaries. Sina uhakika kama Sumaye aliwahi kuandika kitabu chochote.
Watu wengi mashuhuri walikiri kuwa Guevara alikuwa mtu wa aina yake katika utetezi wa binadamu. Mpiganaji Fidel Castrol, rais Nelson Mandela, mwanafalsafa Frantz Fanon, msomi Graham Greene, Stolely Carmichael na mwanahistoria Hugh Thomas ni baadhi tu ya watu mashuhuri ulimwenguni waliomheshimu sana Guevara. Sidhani kama watu wa aina hii wanamfahamu Sumaye pamoja na kuwa alikuwa waziri mkuu kwa miaka 10.
Tatu, akiwa kijana Guevara alielewa dhana ya umasikini na sababu zake. Lakini pia aliwapenda sana masikini. Sumaye hata akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania, kuanzia 1995 hadi 2005, hakuelewa sababu ya umasikini. Sumaye aliwahi kusema, "Nilikuwa kipofu kwa nini umasikini ulikuwa hauishi Tanzania na Afrika kwa ujumla, lakini sasa naweza kuelewa sababu za mateso yetu. Wakati wa uongozi wangu, nilikuwa nashangaa kwa nini, pamoja na juhudi zote ambazo tulizifanya katika serikali pamoja na misaada kutoka kwa wafadhili, bado nchi yetu iliendelea kuwa masikini na hali ya maisha ya watu wetu iliendelea kuwa mbaya, lakini sasa naweza kuelewa tatizo ni nini hasa." Sumaye anasema shahada ya umahiri katika Shule ya Uongozi ya John Kennedy, Chuo Kikuu cha Havard, ndiyo ilimfanya afahamu sababu za umasikini.
Nne, Guevara alivunja rekodi kama mpiganaji wa msituni. Alimudu kutumia kalamu na bunduki. Katika Death of a Traitor anasimulia umahiri wake katika kupiga risasi wasaliti na waoga. Alishuhudia njaa, maradhi na umasikini na kuamua kuweka pembeni taaluma ya udaktari.
Guevara aligeukia mapambano ya silaha dhidi ya ubepari. Guevara aliongoza mapambano dhidi ya unyonyaji wa kibepari barani Amerika Kusini. Akiwa Mexico Guevara alikutana na Raul Castro, sasa Rais wa Cuba, aliyemtambulisha Guevara kwa Fidel Castrol. Guevara na Fidel Castrol waliongoza mapinduzi ya Cuba na kumfukuza dikteta Fulgencio Batista 1958. Sina hakika kama Sumaye amewahi kuua chochote lakini nina uhakika hajawahi kuongoza vita.
Tano, hakuna kumbukumbu inayoonyesha kuwa Guevara aliwahi kumiliki ardhi mahala popote. Mwaka 2011 nilikwenda Rosario, Argentina na kuzungumza na watu katika mtaa aliyowahi kuishi Guevara mjini humo. Nilizungumza pia na wanazuoni kadhaa niliokutana nao na waliniambia kuwa Guevara alichukia sana tabia ya kujilimbikizia mali pamoja na ardhi.
Mwaka 1953 Guevara alikwenda Guatemala. Alipita katika shamba kubwa sana lililokuwa likimiliwa na kampuni ya kibepari kutoka Marekani; United Fruit Company. Hii ilimfanya Guevara kuona kuwa ubepari wa kampuni mbalimbali ndio ulikuwa ubepari mbaya zaidi kuliko yote. Alifurahi sana Serikali ya Rais Jacobo Arbenz ilipoamua kugawa ekari 225,000 ya ardhi isiyotumiwa na United Fruit Company kwa wananchi wa Guatemala wasio na ardhi.
Sumaye ana mgogoro wa ardhi na wananchi katika eneo la Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni. Vilevile anamiliki ardhi katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro na inasemakana aliipata ardhi hiyo kisheria. Hata hivyo makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero yalilazimika kuhamishiwa yalipo sasa badala ya katika kijiji cha Mvomero kupisha shamba la Sumaye.
Na hili ni jaribio jingine kwa Serikali ya Dk. John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Magufuli atafanyaje ili kuhakikisha kuwa waliojimilikisha ardhi kiujanjaujanja wananyang'anywa ardhi hiyo na kugawiwa kwa watu wasiokuwa na ardhi.
Sumaye alikuwa kiungo muhimu katika harakati zilizosababisha wafugaji, wavuvi na wakulima kupoteza ardhi Ihefu katika Wilaya ya Mbarali. Pamoja na kwamba wafugaji walisemekana kuwa hawahusiki kwa upungufu wa maji katika Mto Ruaha, aliandika Dk. Martin Walsh mwaka 2007 katika taarifa yake kwa TNRF, Sumaye alikwenda London mwaka 2001 na kuwatia ari wale waliokuwa wakiendesha propaganda dhidi ya wafugaji katika Bonde la Usangu.
Katika mkutano huo wa London Sumaye aliahidi kuwa serikali yake ingehakikisha hadi ifikapo mwaka 2010 maji yangetiririka vizuri kwa mwaka mzima Mto Ruaha. Hadi leo mwenendo wa maji katika mto huo hayaridhishi pamoja na kwamba wafugaji walifukuzwa. Baada ya kuwahamisha wafugaji Ihefu mwaka 2006 Hifadhi ya Taifa Ruaha ilipanuliwa kutoka kilomita za mraba 10,300 hadi kilomita za mraba 20,226 na kuviathiri vijiji katika mikoa ya Iringa na Mbeya.
Sita, Guevara akiwa na umri wa miaka 30 alipigwa picha na Alberto Korda akiwa amekasirika. Picha hii, kwa mujibu wa Chuo cha Sanaa cha Maryland ni alama ya karne ya 20 na ni picha maarufu kuliko zote duniani. Janathan Green, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Picha Carlifornia Marekani, anasema picha hiyo huibuka kimiujiza kila kunapotokea mapigano. Anaongeza kuwa hakuna chochote katika historia ya dunia kinachofanya kazi hiyo kama hiyo picha ya Guevara. Nina uhakika kuwa picha ya Sumaye haifahamiki, hasa nje ya mipaka ya Tanzania.
Mwisho, hata kompyuta haipati shida kuandika jina la ubini la mtu mashuhuri kama Guevara na hii ni kutokana na umaarufu wake uliopindukia. Jina Sumaye, kwa upande mwingine, linapigiwa msitari mwekundu kwa sababu mashine inadhani kuwa limekosewa.
Nchini Cuba kila siku wanafunzi huanza siku ya masomo kwa kusema, "Tutakuwa kama Che." Kumlinganisha Guevara na Sumaye ni sawa na kulinganisha Mlima Kilimanjaro na kichuguu.

Chanzo Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment