Saturday, 17 September 2016

[wanabidii] Tumekataa EPA, sasa tutaipata


KAMA mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na zile za Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kubaki kama ulivyo sasa, ni wazi kwamba Tanzania itabaki na msimamo wake.

Nimezungumza na baadhi ya mawaziri wa serikali ya Rais John Magufuli na nadhani msimamo huo utabaki ulivyo hata baada ya kupita kwa miezi mitatu kama ambavyo wakuu hao walitangaza wiki iliyopita.

Lakini, hivi kuna nini kibaya kwenye mikataba hiyo ya kiuchumi ambayo inafahamika kwa kifupi cha EPA (Economic Partnership Agreement)?

Kuna mengi lakini nitasema machache tu. Mikataba hiyo inataka Tanzania iondoe ushuru wa bidhaa kutoka nje zisizokuwa za kilimo kwa asilimia 90 na pia ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za kilimo kutoka kwao. Hapa wanataka bidhaa zao zije kushindana na zetu wakati wao wameendelea zaidi kimtaji na kiteknolojia.

Nchi wanachama wa EAC watabaki kuwa masoko ya bidhaa za Ulaya. Wakati huohuo, kwa utaratibu huo wa bidhaa za kilimo, maana yake ni kuwa nchi hizi za Afrika zitabaki kutoa malighafi tu kwa ajili ya viwanda vya Ulaya kuzalisha bidhaa.

Kwa utaratibu huu wa EPA, Tanzania ya viwanda haitawezekana asilani. Hakuna namna ambayo viwanda vya Afrika vinaweza kushindana na vile vya Ulaya. Kuna kipengele pia katika mkataba huo ambacho kinataka nchi za Ulaya zipewe upendeleo uleule ambao watapewa wabia wengine wa kibiashara wa Afrika kama vile India na China.

Yaani, kwa mfano, kama tukisema India tutawapunguzia ushuru wa bidhaa hii kwa kiwango hiki, basi na Ulaya nao wafaidi kwa kiwango hichohicho. Cha ajabu, mkataba huo hausemi kwamba na wao wazungu wakiingia makubaliano ya namna hiyo na rafiki zao, nasi wa EAC tufaidi vilevile. Hakuna !

Ukiniuliza kwanini Kenya, Rwanda na Uganda wanataka kusaini mikataba hiyo, jibu langu litakuwa sijui. Lakini, ninachojua ni kitu kimoja pekee –kwamba wazungu hawataacha hili lipite hivihivi.

Jijini Dar es Salaam, Rais Yoweri Museveni alizungumza wiki iliyopita mbele ya wageni akiomba watu wa EU wasiiadhibu Kenya kwa kuwa imekubali kusubiri hiyo miezi mitatu.

Museveni anawajua wazungu. Anajua visasi vyao. Inawezekana mara moja au mbili kwenye utawala wake amewahi kukumbana na visanga vyao.

Kwenye kitabu chake Trade is War, Profesa Yash Tandon, ameandika kwamba inawezekana Uganda na Rwanda zimebanwa na wazungu kwamba wakikataa kusaini, wanaweza kukosa misaada mbalimbali mingine ambayo haihusiani na EPA kama vile silaha na vita dhidi ya ugaidi.

Tandon, mmoja wa wasomi mashuhuri barani Afrika, ameandika pia kwamba biashara ya maua; inayofanywa na matajiri wengi wa Kenya wakiwamo wanasiasa, itaathirika endapo viongozi wa EPA wasiposaini. Kwa kuishughulikia biashara hiyo, watu wa EU wanafahamu watakuwa wanafanya jambo ambalo linawaumiza wakubwa moja kwa moja.

Nchi za Ulaya, na mabeberu katika ujumla wao, hawapendi nchi masikini kujiamulia mambo yao. Wanafahamu kwamba Tanzania ikiwa na uchumi wa viwanda, itajikwamua kutoka kwenye makucha yao. Wanafahamu kwamba wao waliendeleza viwanda vyao kwa kuvilinda. Sisi wanataka tusivilinde.

Fidel Castro si kiongozi mbaya. Lakini mabeberu hawakupenda siasa zake za kutotaka kulamba miguu ya wakubwa. Matokeo yake ni kuwa nchi yake leo inachechemea. Hali iko hivyo kwa Venezuela ya Hugo Chavez na hata Chile ya Salvador Allende.

Patrice Lumumba alionyesha dalili mapema kwamba atakuwa mwiba kwa mabeberu, akapotezwa. Hapa kwetu, mtu kama hayati Abdulrahman Babu aliishia kuwekwa rumande na kupewa kazi za kutangatanga tu bila utulivu. Mabeberu wasingekubali apewe nafasi ambayo angeonyesha njia ya kweli ya maendeleo.

Hatua hii ya Magufuli na serikali yake si hatua ya mchezo. Endapo mwishowe atakataa kabisa kusaini mikataba hiyo, afahamu kwamba atatangazwa kuwa adui namba moja wa mabeberu.

Habari zake zote zitakuwa mbaya. Ataandikwa kwa aliyoyafanya na asiyoyafanya. Atapewa majina ya kila namna na uchumi wetu utaanza kufanyiwa hujuma. Na kwa sababu mabeberu ndiyo wameshika uchumi wa dunia, safari ya huko tuendako inaweza isiwe rahisi.

Kama ameamua kwa dhati kufuata njia hii, ni muhimu ajiandae na yanayokuja. Ingekuwa vema pia kama angeweza kushirikisha jamii pana ya Watanzania katika kufahamu kiini na sababu za kuchukua hatua anazochukua. Hii ni sawa na kusema anatakiwa pia kuwaandaa watu wake.

Kama serikali ya Magufuli ina nia ya dhati ya kuhakikisha Tanzania inajenga viwanda vyake na haibaki kuwa soko la malighafi kwa ajili ya viwanda vya mabeberu, ni muhimu ikashikilia msimamo wake wa kukataa kusaini EPA kama ilivyo sasa.

Cha msingi, ni kufahamu kwamba mabeberu hawatakaa kimya wala bwete wakati Tanzania ikichukua uamuzi mkubwa na muhimu kama huo.

Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment