Thursday, 10 March 2016

Re: [wanabidii] Ngurumo aliyemkataa Lowassa enzi za JK na kumkubali miezi mitatu ya mwisho ya JK.

Nimekusoma ndugu yangu. Kuna mambo 10 nataka niyaweke sawa, maana umeyakosea.

1. Makala ya Maswali Magumu haikuanza na Rais Jakaya Kikwete. Ilianza na Rais Benjamin Mkapa mwaka 2002 katika gazeti la Mwananchi Wiki Hii.

2. Makala zangu za uchambuzi wa kukosoa serikali hazikuanza na utawala wa Rais Kikwete. Nilizianzia The African na baadaye Rai na Mtanzania katika Habari Corporation ya Jenerali Ulimwengu, Salva Rweyemamu, Gideon Shoo, Shaaban Kanuwa etc. Siku Rais Mkapa alipomvua urais Jenerali Ulimwengu (2000 au 2001) nami nilitumiwa ujumbe na watu wa serikali kuwa nisipopunguza makali katika kukosoa serikali nitakiona cha mtema kuni. Kwa hiyo, wanaonihukumu kwa kutazama makala zangu zinazochambua serikali ya Rais John Magufuli yawezekana ni watoto wadogo tu (kiumri au kiakili) ambao enzi hizo walikuwa hawajajua (au hawataki) kusoma, au ni watu wazima waliobahatika kusoma makala zangu katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Sikosoi serikali kwa chuki bali kama njia ya kuamsha waliolala, kunyosha yanayokosewa ili yasahihishwe, wananchi wapate huduma wanazostahili. Hiyo ni sehemu ya kazi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari. Namwambia rais kupitia gazetini kwa kuwa ndipo pangu, na kwa kuwa wengi waliomzunguka wanaogopa kumwambia ukweli; wanamsifu badala ya kumwonesha kasoro ili asahihishe mambo. Yeyote atakayeingia Ikulu, kama nipo nitafanya kazi hiyo kwa uzalendo mkubwa, bila woga wala upendeleo, nikihoji kuhusu masuala muhimu ya taifa. Kama rais ameamua kujiita mtumbua majipu, lazima wawepo wengine wanaoweza kutumbua majipu yake kila yanapoiva. Mimi nimejipa kazi ya kutumbua majipu ya Ikulu – iwe ya Magufuli, Ngurumo. Lowassa, Abdallah au Juma!

3. Sijawahi kuwa shabiki wa mgombea yeyote wa CCM, kama mwandishi anavyodai. Lakini kama mwandishi wa habari, nimefanya kazi na wanasiasa wote bila kujali itikadi. Kwa hiyo, nisingeweza kuwa shabiki wa Mzee John Malecela, kama inavyodaiwa. Mwaka 2005 nilitafutwa sana, niliombwa sana na watu wa timu ya Kikwete niwaunge mkono, nikakataa. Nilikuwa na sababu mbili. Kwanza, niliamini kwa dhati kwamba Jakaya Kikwete hakuwa mgombea bora katika wenzake 10 katika kundi lao la wagombea 11 ndani ya CCM. Niliona kama kuna wagombea wanamzidi uwezo, upeo, ujasiri, uthabiti, umakini, uadilifu na kadhalika. Msimamow angu huo haujabadilika hata baada ya miaka 10 ya utawala wake. Niliwaeleza walionishawishi kuwa urais una hadhi na viwango vyake. Sikuona kama Kikwete alikuwa anakidhi viwango hivyo, nilipomlinganisha na wenzake 10. Pili, sikuwa tayari kuunga mkono mgombea wa CCM, kwa kuwa sikutamani kuwa na rais kutoka CCM tena. Niliamini katika mabadiliko ambayo yanaambatana na kuondoa mfumo mkongwe na kuweka mpya. Kuunga mkono mgombea yeyote wa CCM kungekuwa kinyume cha ukweli na msukumo huo. Hata hivyo, nilikuwa na mgombea wangu kupitia Chadema - Freeman Mbowe. Nisingeweza kufanya kazi ya kubeba CCM wakati nina mgombea wangu.

Kilichootokea ni kwamba, nikiwa mhariri wa Tanzania Daima Jumapili, nilishirikiana na wenzangu kusaka exclusive interviews na wagombea urais. Mimi nilipangiwa kumpata na kumhoji Mzee John Malecela. Naye hakuwa tayari kuzungumza na waandishi kwa sababu alidhani Kikwete anawatumia kumchimba, kama alivyokuwa amewatumia "kumuumiza" huko nyuma. Baada ya kunikwepa mara kadhaa, baadaye aliridhia kuzungumza na mimi. Maswali niliyomuuliza yaliandaliwa kwa ushirika kati yangu na wahariri wenzangu. Kitaaluma, hata kama hukubaliani na msimamo au  hoja za mtu unayemhoji, unachopaswa kufanya ni kumtendea haki. Unamsikiliza. Unaandika alichosema. Huongezi maoni yako popote.

Hata Mzee Malecela hakuamini kama ningeweza kumtendea haki, hadi aliposoma mahojiano yake gazetini. Nilimnukuu neno kwa neno. Sikujadili kauli zake. Msomaji mmoja alinipigia simu kuuliza, "mbona sioni wewe unasemaje kuhusu Mzee Malecela?" Nikasema, "kitaaluma, sina sababu ya kuweka maoni yangu katika stori ninayoandika. Huo ni msimamo wake, ni maoni yake. Nikitaka kuandika maoni yangu nitaandika mahali pa maoni, si katika stori yake."

Wasiojua msimamo huu, hasa waliokuwa washindani wake, walitaka nimshughulikie katika habari hiyo, au nisimhoji kabisa. Baadhi yao wakadhani mimi ni mtu wa Mzee Malecela. Walikosea. Baadaye nilisikia mahali Fulani, Kikwete, Rostam Azizi na Edward Lowassa wakisema, "Ngurumo ni mtu wa Dk. Salim." Nao hawakuwa sahihi. Sikuwa na mtu katika CCM.
Walipokwenda Dodoma kuchukua fomu za urais katika chama chao, walinikuta. Wote 11 walijieleza na kujibu maswali yetu. Ajabu, niliguswa na maelezo ya Mzee Idd Simba. Kwangu, ndiye alionekana anajua kwanini anataka kuwa rais. Aliniridhisha. Lakini alikuwa anapoteza muda, kwa kuwa hakuwa chaguo la chama chake. Hakuwa na mtandao. Alishapigwa na kuchafuliwa ili asipite. Kama wengine wote waliokuwa wameshachafuliwa na kambi ya Kikwete – Frederick Sumaye, Mark Mwandosya, Dk. Salim Ahmed Salim, Mzee Malecela - naye aliishia hapo.

4. Katika makala zangu kati ya 2006 na 2015, kama umenisoma vema, nimewahi kumshambulia Lowassa mara moja au mbili hivi. Nakumbuka mara ya kwanza nilimsema alipotaka kutumia mabavu kufungia gazeti la Tanzania Daima lilipomkosoa. Nilikuja juu, nikasema anatumia vibaya madaraka yake. Mara ya pili nilimwandama Lowasa na Rostam kwa kosa moja kubwa - kutuletea Kikwete. Nilisema Tanzania haitawasamehe wasipotubu dhambi hiyo, wakaachana na Kikwete; maana kama si wao, Kikwete asingekuwa rais. Baadaye nilipopata fursa ya kuzungumza nao, walikiri kosa hilo, na sasa hivi wanajuta. Tena wanashangaa mimi nilimjuaje kuliko wao; maana wakati namkosoa, nao waliniona mbaya.
4. Lowassa alipojiuzulu uwaziri mkuu, nilimpongeza. Kwanini? Nilibahatika kujua undani wa sakata la Richmond kutoka kwa wahusika waliomsulubisha bungeni. Nilijua kilichongunduliwa na ripoti, ambacho hakikuandikwa; na kwanini Kikwete hakuingizwa kwenye ripoti. Nilijua kuwa Richmond haikuwa mali ya Lowassa. Nilijua ushiriki wake katika mchakato wa kuipa tenda. Nilijua hatua alizotaka kuchukua kuvunja mkataba, rais akakataa. Nilijua jinsi alivyokutana na rais Ikulu Chamwino, mmoja akamdanganya mwenzake, Lowassa akajiuzulu. Nilijua nguvu iliyotumiwa na kamati ya wabunge wa CCM kumshawishi rais aachane na Lowassa. Nilijua jitihada za watu wa usalama wa taifa kuhusu sakata hilo. Nilijua ufa uliojengeka kati ya Lowassa na Kikwete tangu siku hiyo. Nilijua kuwa Lowassa alikua na siri nyingi alizomtunzia rais wake, wakati rais anasmhughulikia kichini chini.

Niliandika baadhi ya mambo hayo, si kwa kumsakama Lowassa, bali kuwa kumtaka atoboe siri. Nilitaka ajue kuwa anamwamini sana Kikwete, lakini Kikwete haaminiki. Katika makala moja, niliandik hivi: "Hongera Lowassa, bado Kikwete." Wakati nafanya hayo yote, Lowassa alikuwa haoni umuhimu wa kauli zangu. Alikuwa miongoni mwa watawala walionichukia. Alikuwa bado nan damu ya CCM. Alikuwa amefumbwa macho, haoni tunachokiona sisi. Lakini nilijua,, na niliandika, wakati mwingine kwa uwazi au kwa mzunguko, kuwa siri ya Richmond iko kwa Kikwete, na kwamba Lowassa aliwajibika kisiasa kutokana na madaraka yake. Alipaswa kuwajibika kwani alihusika.
Hata wakati anawania kuteuliwa na CCM agombee urais, baadhi yetu tulijua kuwa angekatwa tu. Wakati huo, hakusikia ushauri wowote wa kumtenga na CCM. Wakati wake wa kufunuliwa ulikuwa haujafika. Ulipowadia, akaumizwa kwelikweli, ndipo alijua kwamba yumo katika kundi lisilo lake. Akawa na ujasiri usiotarajiwa, akaondoka CCM, akajiunga na Chadema. Si jambo la kawaida kwa mtu aliyewahi kuwa waziri mkuu, katika siasa chafu za Tanzania, tena aliyetangazwa kuwa fisadi na kuhusishwa na uchafu mwingi, kuhama chama tawala – na akawaambia "kama mna ushahidi wa tuhuma zangu, nipeleke mahakamani!" Si rahisi.

5. Ni kweli. "Laana" ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere imekuwa inamwandama Lowassa. Ni ukweli wa kihistoria kwamba kama si Mwalimu Nyerere kumzuia 1995, Lowassa ndiye angekuwa rais. Ni kweli kwamba tangu pale, ndani ya CCM yamejengeka makundi dhidi ya Lowassa kwa sababu ya kile kinachoitwa "kukataliwa na Nyerere." Ni kweli kwamba Kikwete alimteua Lowassa katika mazingira hayo, na hata alipomteua, kuna mbunge mmoja kijana alitaka kulianzisha kwa kuomba wazee wamsaidie kujenga hoja ya kumkataa ili asiidhinishwe na Bunge. Ni kweli kwamba mbunge huyo alikwenda hadi kwa Mzee Malecela, akamwambia "Mzee na wewe umeondolewa kwenye urais kwa sababu Nyerere alikukataa. Kwanini tusimkatae na huyu Lowassa kwa sababu hizo hizo?" Mzee Malecela alimweleza mbunge huyo kuwa asingemuunga mkono katika hilo kwa sababu mbili. Kwanza, asingeweza kuzuia uteuzi wa rais kwa kuwa wanamtandao walikuwa wameshika serikali. Sana sana ilikuwa ni kutafuta ugomvi na serikali mpya, ugomvo ambao mbunge huyo asingeushinda, na ungemsababishia wakati mgumu kwa miaka mitano. Pili, alimwambia kuwa yeye anamjua Lowassa, kwani alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa waziri, alipelekwa ofisi ya waziri mkuu, wakati huo Malecela akiwa waziri mkuu. Alisema kwamba licha ya maneno yanayosemwa dhidi ya Lowassa, ana kasoro zake kama binadamu, lakini kama ni uchapakazi, Lowassa akisema jambo fulani litafanyika, haweki mguu chini hadi lifanyike.

6. Ni kweli kuwa Lowassa aliteuliwa uwaziri mkuu katika mazingira magumu, ambamo Kikwete alikuwa pia amemwahidi Samwel Sitta nafasi hiyo wakati wa kampeni. Kwa sababu hizi za kihistoria, Sitta aliamini kwamba Lowassa asingeteuliwa. Alishangazwa na ushauri aliokuja kupewa na Kikwete baada ya kuapishwa, kwamba "Bunge linahitaji Spika makini kuliko Pius Msekwa, hivyo tunaona ugombee uspika." Baadaye ilipoletwa bahasha yenye jina la waziri mkuu bungeni, akakuta ni Lowassa. Lowassa na Sitta wakawa wanatunishiana misuli ya madaraka – huyu wa serikali, huyu wa bunge. Bifu lililoibuka tangu hapo kati ya Sitta na Lowassa, huku Sitta akisaidiana na akina Harrison Mwakyembe na Lucas Selelii kusumbua Lowassa na Kikwete halijaisha hadi sasa. Hata sakata la Richmond lilichipuka katika mkondo wa Sitta na Mwakyembe kutaka kumwondoa Lowassa kwenye uwaziri mkuu. Sitta ndiye aliingiza Richmond nchini akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TIC. Aliijua vema, lakini alifanikiwa kumshughulikia Lowassa kwa sababu waliona "mkono wake katika Richmond." Ndiyo maana baada ya Lowassa kijiuzulu, Sitta hakutaka bunge lihoji tena sakata hilo, na akafunga mjadala bila hata serikali kutimiza maazimio ya bunge kuhusu Richmond. Maelezo ni marefu. Yapo mengi ambayo jamii haiyajui kuhusu Richmond, na mimi nakumbuka vema kwamba haya ninayoandika hapa nimewahi kuwaandika kwa kirefu katika makala zangu. Katika maandishi yangu nilimkosoa sana Kikwete, na kumsuta Lowassa na wenzake. Nilieleza nilichojua. Kumbukumbu zipo. Siwezi kulishwa maneno.

7. Mimi kufanya kazi na Dk. Willibrod Slaa lilikuwa jukumu nililopewa na chama. Nilikuwa naye kabla ya uchaguzi, wakati wa kampeni na baada ya kampeni. Sikufanya naye kazi kirafiki au kwa kujikomba. Nilifanya nilichopaswa kufanya naye kwa ajili ya jamii pana ya Watanzania. Kimsingi, nilifurahia utumishi wangu huo. Kwa kazi tuliyofanya kwa kushirikiana na Dk. Slaa na wengine wengi, habari zilifika kila kona, na kwa sababu ya kipaji na haiba yake binafsi, alikubalika kwa wananchi. Hadi Julai 2015, alipokuwa akisimama majukwaani, wananchi walikuwa wakimuita "rais wa mioyo wa Watanzania." Leo hana anuani hiyo tena. Sababu zinajulikana. Dk. Slaa hayupo Chadema tena. Alifanya kazi nzuri kama ya Musa tunayemsoma katika Biblia. Musa aliamriwa na Mungu aongoze Wanaisraeli kutoka Misri hadi Kanaani. Walikaa jangwani kwa miaka 40. Hatimaye walifika kwao, lakini Musa hakufika. Tulimwandaa Dk. Slaa agombee, naye alijiandaa agombee tena urais 2015. Lakini hakugombea. Kilichotokea ama mnakijua au mnakikwepa. Yaliyomkuta Dk. Slaa hayawezi kuondoa kazi nzuri aliyofanya akiwa mwanachama na kiongozi wa Chadema.

8. Lakini kama Dk. Slaa si mwanachama tena wa Chadema, na hagombei tena urais, haina maana kwamba tuendelee kumfuata huko alikokimbilia. Kwamba Lowassa alikuwa mwana CCM, tena tuliwahi kumsema akiwa huko, haina maana kwamba hana haki ya kuhama na kujiunga nasi. Na wengi unaowaona leo katika vyama vya upinzani - hata kwa Dk. Slaa ilikuwa hivyo - walitoka CCM. Tena wengi wao waliingia upinzani baada ya kukatwa majina au kufukuzwa na CCM. Lowassa amezungumzwa sana kwa sababu ya ukubwa wa jina lake. Hakuwa mwanachama wa kawaida katika CCM. Hakuwa kiongozi mdogokatika serikali. Lowassa alijijenga akawa taasisi ndani ya CCM. Taasisi hiyo ilipohamia Chadema, isingeweza kutua bila kishindo. Na hawezi kuungwa mkono na kila mtu. Kuna watu hadi sasa hawamwelewi; wengine (wachache) hawamkubali. Ndivyo siasa ilivyo. Katika hali ya kawaida, sitarajii mwanachama au mfuasi wa Chadema, aunge mkono Dk. Slaa aliyeondoka eti kwa kuwa huko nyuma alifanya kazi naye;  amwache Lowassa aliyeingia na kukabidhiwa jukumu jipya la kitaifa.

9. Unazungumzia taswira ya Lowassa kama fisadi? Kwamba hakupaswa kupokelewa Chadema? Tujadili. Mimi ni Mkristo Mkatoliki. Nimebahatika kusoma historia ya Kanisa. Najua mchango wa Mfalme Constantine ambaye alikuwa mpagani katika kukuza Kanisa, kulipa uhuru wa kuabudu hata kabla mwenyewe hajaongoka. Kama Himaya ya Kirumi isingekuwa na mtu kama Constantine, ingechukua miaka mingi sana kwa ukristo kushamiri kwa sababu ulikuwa unapigwa vita na serikali yake. Mchango wake ndio uliwezesha wakristo kusali hadharani, kujenga makanisa, kuhibiri kwa uwazi; na alipoongoka mfalme kila mtu akataka kuingia katika dini mpya ya Mfalme. Wewe endelea kujadili upagani wa Constantine.

Nimesoma pia historia ya maisha binafsi ya Mt. Augustine wa Hippo. Vile vile nimesoma kitabu "Confessions of St Augustine." Anasema wazi kuwa hakuna uchafu ambao hajawahi kufanya akiwa kijana. Alipoongoka akabatizwa, amekuwa mkristo hodari kuliko hata aliowakuta; hadi akawa askofu. Leo historia inatambua kama mmoja wa walimu na mababa wa kanisa.
Nimesoma Biblia nikaona jinsi Sauli alivyokuwa anatesa Wakristo. Aliwafunga. Aliwapiga. Aliwaua. Aliongoka akiwa njiani anakwenda kutesa Wakristo. Akabatizwa jina Paulo. Mwanzoni, Wakristo walimwogopa, hawakuamini kama ana nia njema nao. Alipojitambulisha kwa mitume, kwa kauli ya Mtume Petro, wakampokea, akawa mwenzao.

Kwamba aliwahi kutesa nan kuua wakristo kwa amri za utawala mbovu uliokuwapo, haikumzuia kuhubiri injili kwa kauli na maandishi. Soma  nyaraka zake kwa Wakorinto, Wakolosai, Wagalatia, Wafilipi, Wahebrania, Waefeso; kwa Tito, kwa Timotheo, na kadhalika. Paulo ambaye hakuishi na Yesu, Paulo aliyetesa wafuasi wa Yesu, ndiye alikuwa mhubiri mkuu na mwandishi wa nyaraka nyingi kuliko wanafunzi 12 wa Yesu. Hatujadili tena mateso aliyosababisha kwa Wakristo. Hayo ni maisha ya kale!

10. Kwa miaka ipatayo 20 sasa, nimejipambanua kwa maandishi bila unafiki. Nakosoa, natafakari, nafikirisha. Shabaha yangu ni kusaidia walio madarakani wajirudi. Siandiki kwa chuki. Ni uzalendo unaojitokeza katika kutazama upungufu wa watawala na kupiga kelele. Kelele hizi zinaposikilizwa, zinanyoosha mengi.

Kwa mfano, Jumatatu Machi 7, 2016 niliandika uchambuzi katika safu ya Gumzo la Wiki katika gazeti la MwanaHALISI, nikasema jinsi Rais John Magufuli alivyofedheheka kwa kuchomeka Kiingereza kibovu katika hotuba ya Kiswahili mbele ya viongozi wenzake Jumjuiya ya wa Afrika Mashariki na wageni waalikwa. Nilishauri atumie Kiswahili katika hotuba zake ndani na nje ya nchi, kwa kuwa hana kipawa na kuzungumza Kiingereza fasaha, na kwa kuwa Kiswahili ni lugha yetu ya taifa, yenye hadhi ya kimataifa.

Kuna watu walinishambulia. Wakadiriki hata kupotosha mada yangu, eti nashabikia Kiingereza. Eti nimwache azungumze Kiingereza kibovu. Sikuahangaikia nao, kwani watu wa jinsi hii wanajikomba kwa wakubwa, na ndio wanalea kasoro za wakubwa.
Bahati nzuri, rais mwenyewe amezingatia ushauri wangu. Jumatano, siku mbili baadaye, alimpokea mgeni wake, Rais wa Vietnam, Ikulu, Dar es Salaam. Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Rais Magufuli alitumia Kiswahili. Nilimpongeza kwa usikivu huu. Nilifurahi kwamba alisikia ushauri. Na hii ndiyo kazi ambayo baadhi yetu tumejipa.
Mashabiki wa makosa ya wakubwa ndio wanaonishambulia ninapoyagusa. Sijui wanafaidi nini tusipowakosoa.

Nawasilisha!






Ansbert Ngurumo

Mobile    +255 767 172 665
www.freemedia.co.tz
www.voxmediatz.com
www.ngurumo.wordpress.com
www.ngurumo.blogspot.com



On Thursday, March 10, 2016 12:19 PM, 'lang'itomoni lokomoi' via Wanabidii <wanabidii@googlegroups.com> wrote:


ANSBERT NGURUMO, kwa takribani miaka yote kumi ya utawala wa wa Kikwete, alitumia kalamu yako kumuuliza Rais Kikwete alichokuwa akikita maswali magumu, aliuliza maswali hayo bila kuchoka kwa muda wote huo hakuna kumbukumbu kama aliwahi kujibiwa.

Mwaka 2005, katika mchakato wa uteuzi wa CCM wa kumtafuta mteule wake ambapo Kikwete aliibuka kidedea, Ngurumo alikuwa katika kambi ya Malecela, waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais mstaafu.

Kwa bahati mbaya jina la Malecela lilitupwa mwanzoni kabisa katika mchakato huo kitendo hicho hakikumfurahisha Ngurumo ndipo akaamua kuwa mpinzani wa CCM

Mwaka 2010, Chadema ilipomsimamisha Dk. Wilboard Slaa ambaye kwa kidogo alikuwa mgombea urais kutoka upinzani mwenye muonekano wa uzalendo wa uadilifu wa kweli.

Hapo ndipo Ngurumo akapata pa kupumulia, akaingia front kumuunga mkono Dk. Slaa kabla ya kupata bahati ya kuwa miongoni mwa watu watano muhimu wa kubeba mikoba ya mgombea huyo wa urais katika kipindi chote hicho akifanywa kuwa mratibu na mshauri.

Kila Mtanzania mwenye kuitakia afya njema nchi yake angeweza kuungana na Dk. Slaa kutokana kilele cha ufisadi ambacho nchi ilikuwa imefikia chini ya uongoiizi wa Rais Kikwete, mafisadi wakitamba kifua mbele bila ya kuguswa wakati walikuwa wakifahamika na vitendo vyao vikijulikana

Binafsi nawachukia mafisadi na vitendo vyao kwa nchi hii kama ambavyo niliamini  Kama Ngurumo na Dk. Slaa wanavyowachukia mafisadi  pamoja na vitendo vyao vya kifisadi.

Mwaka 2010 niliamini asalimia zote kwamba ndoa ya Ans Ngurumo na Dk Slaa ilitokana na msimamo wa kuwachukia mafisadi wananchi hii pamoja na vitendo vya kifisadi, hivyo basi iliwahitaji wanyonge hao waunganishe nguvu zao pamoja na wanyonge wengine dhidi ya nguvu ya mafisadi.

Kumbe nilikosea kuamini hivyo kwa Ans Ngurumo ila kwa Dk Slaa nilikuwa sahihi. Kilichowaunganisha mwaka 2010 haukuwa ukombozi wa nchi dhidi ya mafisadi, kumbe Ans Ngurumo  alikuwa anatazama mbali zaidi, maslahi binfsi zaidi ya kiuchumi na kisasa.

Kwa nini nilikosea, Baadhi ya maswali ya Ngurumo kwa Kikwete yalihusu, kwa nini kiongozi huyo alikiuka miiko nya mwalimu Nyerere kwa kumteua Lowassa kuwa waziri mkuu wake?

Na hata mwaka 2008 Rais Kikwete alipolazimika kuvunja baraza la mawaziri na kumfukuza Lowassa kutokana na kashfa ya ufisadi wa richimond, Bado Ngurumo liendelea kusisitiza kwa rais kikwete enzi hizo kwamba mzimu wa Mwl. Nyerere hautamuacha salama kwa kuendelea kumkumbatia fisadi Lowassa ndani ya chama chake cha CCM.

Kwa msimamo huo wa wa  Ngurumo wengi wetu tulidhania baada ya Dk.Slaa kusutwa na nafsi yake hivyo kufanya uamuzi mzito wa kuachana na Chadema, baada ya uongozi kufanya kosa kubwa la kiufundi la kukabidhi chama kwa lowassa na kumfanya kuwa mgombea urais, Ngurumo naye angeonyesha uzalendo wake wa kuunga mkono hatua hiyo ya Dk. Slaa.

Leo hii kwa neema za Mungu, ndani ya CCM amepatikana DK. Magufuli aliyedhamiria kupambana na uchafu wake wote ndani ya serikali na taasisi zake, Kina Ngurumo  hawa wa kumdhikhaki na kumkejeli?

 Eti anadiriki kusema hana dhamira hiyo na wala hakuwa chaguo la watanzania, bali Lowassa ambaye yeye NGurumo alikuwa akimsakama Kikwete usiku na mchana akimtaka kumfunga jela kwa ufisadi ndio huyo huyo leo anasema kuwa ndio chaguo la watanzania?

Huyu Ngurumo hakuwahi kumwamini Kikwete kama kama president material na sasa anandika upuuzi ule ule kama hamuamini Dk. Magufuli kama president material.

Yeye alimuamini Mwalimu NYerere akamuamini Malecela na akamwamini Lowassa wakati Mwalimu aliwakataa wote Malecela na Lowasa, tena miaka takribani kumi akitumia kalamu yake kutuaminisha kuwa fisadi leo anatwambia Lowassa ndiye president material na alikuwa chagua la watanzania na angekuwa rais bora kuliko Dk. Magufuli?
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.


0 comments:

Post a Comment