Wednesday 30 March 2016

[wanabidii] Kusitishwa Msaada wa Marekani Uwe Mwanzo wa Kusitishwa Mingine

Na. M. M. Mwanakijiji
Yapo matatizo mengi sana yanayotokana na nchi kupokea misaada ya kigeni bila kuwa na sera rasmi inayohusiana na sekta hiyo muhimu na yenye kugusa mweleko mzima wa maendeleo ya taifa. Baadhi ya matatizo hayo ni kuwa wenye kutoa misaada hiyo wana uwezo – wakijisikia –wa kuamua kukuambia uiname na kubong'oa bila wewe kuuliza kwanini wanataka uiname! Tena wanasubiri wakusikie unawauliza "hivi nilivyobong'oa inatosha au nibong'oe zaidi"!

Tatizo jingine la kuwa mpokeaji wa misaada hii ya kila namna ya kigeni hasa ile inayoingia kusaidia bajeti ya nchi (direct budgetary support) ni kuwa wewe katika kupanga kwako mipango yako yote ni lazima kwa uwasikilize wachangiaji hawa na uwe tayari kuwabembeleza wachangie kwenye kile kikapu cha fedha za misaada (donor basket) ili mipango yako ifanikiwe.

Wakichelewa kutoa au wakianza kusua sua inabidi wewe mwenyewe uanze kufikiria mara mbili utakamilisha vipi mipango yako bila wao. Unaweza kujikuta unawafuata na kuwauliza "mnataka nibong'oe jamani?" ili waanze kuchangia au kutimiza ahadi zao.

Lakini pia lipo tatizo kubwa la tatu; ukishawategemea na wakisha kukufanikisha kwenye mambo kadha wa kadha basi kifikra wewe mwenyewe unawafikiria hawa mara kwa mara katika mipango yako, n ahata kama huwahitaji kweli kweli unaanza kujisikia kama unawamiss hivi! Wasipokuja kuzungumza nawe unaanza kuwatafuta kwa simu na mawasiliano mengine.

Unaanza siyo tu kuwategemea kwa fedha zao wanazotoa (wakati mwingine wanatoa kwa mkono huu na kuchukua kwa mkono ule wakati umebong'oa) unaanza kuwategemea kifikra. Wakitishia kutokukupa fedha unajisikia kuumwa, unachanganyikiwa, na unaanza kuona au kuamini unaona kuwa watu wako wameanza kuwa maskini ghafla! Unaanza kuona miradi yote ambayo ilikuwa inategemea misaada yao inaelekea kufa.

Na cha kusikitisha ni kuwa wapo watu kati yako ambao wataanza kukufanya uamini kuwa bila ya hao watoa misaada kweli miradi itakufa kwani hakuna "namna nyingine" yoyote ya wewe kuitimiza. Watakuambia "unaona sasa hujabong'oa ndio maana!" na wengine kwa haraka watasema kwa ukali "si unajifanya mbishi wewe hubong'oi! Sasa watu wako watakufa ni bora ukabong'oe haraka na sisi tutakusaidia kukushika ukibong'oa!"

Ndugu zangu, uamuzi wa Wamarekani kusitisha misaada yao ya karibu dola milioni 470 ili kushinikiza Serikali ya Tanzania kufanya vitu visivyowezekana ni uamuzi ambao wenyewe unaweza kuhojika na kuhojiwa. Sababu zilizotolewa na Wamarekani za kwanini wameamua kusitisha fedha hizo kama ukizikubali unaweza kujikuta uko tayari kukubali jambo lolote bila kuhoji. Sababu ambayo taarifa ya Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) inazitaja zinapaswa kumuudhi Mtanzania yeyote mwenyewe kujifahamu na mwenye kuheshimu utu wake. Tamko lao linasema "Tanzania moved forward with a new election in Zanzibar that was neither inclusive nor representative" Yaani, Tanzania "iliendelea na uchaguzi mwingine huko Zanzibar ambao haukuwasisha wahusika wote wala haukuwa wa kiuawakilishi."

Hivi ili uchaguzi uwe wenye kuhusisha na wenye uwakilishi ni lazima wahusika gani wawemo? Marekani leo hii inahangaika na Donald Trump na tunaona jitihada zinavyofanyika kuzuia mwendo wake kuingia Ikulu ya nchi hiyo. Na tena kuna hadi mipango ya njama ya kuvuruga taratibu ili asiwe mgombea. Hivi kweli ikitokea Donald Trump akatupwa nje kwa sababu baadhi ya watu hawamtaki na akaenda kushinda mtu mwingine kweli Watanzania tunaweza kusema uchaguzi wao ulikuwa wenye kuwakilisha wote na wenye sura ya uwakilishi kweli?

Hivi, kuna mtu alikatazwa kupiga kura siku ya Jumapili kwenye marudio? Hivi, ni kweli kabisa kwa vile wanatutakia mema Wamarekani na wengine wamechukua wakati gani kwenda kukaa chini na kuangalia ushahidi au madai ya serikali juu ya kuvurugwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25? Au na wao walitaka tu uchaguzi ufanyike ili ufanyike? Hivi kweli kabisa tunataka tukubali kuwa kwa vile hawa watoa misaada wanasema 'uchaguzi ulikuwa huru na wa haki' ina maana ni lazima uwe hivyo?

Sijataka bado sana kuingia kuzungumzia hili la Zanzibar lakini itoshe tu kusema hapa kuwa kama tumeamua kukubali misaada ni lazima pia tuwe tayari kukubali kubong'oa. Lakini utakuwa tayari kubong'oa mpaka lini? Ni mpaka upigwe mateke mangapi wakati umebong'oa ndio utasema "huu mchezo mimi sitaki"?

Jibu lake linaanzia kwenye jibu la 'je ni kweli bado unahitaji misaada"? Naomba kupendekeza kuwa wakati wa misaada umepita. Hata mtoto kuna wakati unamnyonyesha, unampa chupa, unamlisha, unamsaidia kula mwisho wa siku unampa kijiko ale mwenyewe! Mtoto mkubwa na asiye matatizo yoyote ya kiafya kuendelea kumlisha na kumpa chupa ya kunyonya inasema zaidi kuhusu wewe kama mzazi kuliko yeye mtoto!

Lakini pia ni lazima tuwe wa kweli; kama kweli misaada ingekuwa inainua taifa na kuleta maendeleo ya watu Tanzania ingekuwa mbali sana leo hii. Misaada ambayo Tanzania imepokea ukiangalia na ufisadi uliokuwepo unaweza kujiuliza hii misaada siyo hiyo hiyo inasishia tena kwenye ufisadi na hivyo kuhitaji misaada zaidi?

Hata wanyama wanapolea watoto wao unapofika wakati wa kuwaacha watoke nje na kujitegemea wanyama huwa wanakuwa wakali. Hadi mtoto anapata akili eh, inabidi nikatafute chakula mwenyewe sasa!

Watanzania na labda Waafrika wengine ni lazima tuanze kujiamini kuwa tunaweza bila misaada. Mahusiano yetu na wakubwa hawa hayawezi kuwa na heshima na usawa kwa kadiri ya kwamba bado tunakinga makapu yetu watusaidie. Binafsi ninaamini – katika mwanga wa yaliyotokea siku hizi mbili – kuwa Serikali ya Magufuli ni lazima ikae chini na kufanya maamuzi ya lazima, sahihi na ya makusudi. Maamuzi hayo kwa maoni yangu sehemu yake ni lazima yawe yanaamua mambo yafuatayo:

1. Serikali ikubali kwa moyo mkunjufu na kuheshimu uamuzi wa MCC kusitisha msaada wao huo. Hakuna sababu, ulazima wala haja ya kutoa kauli ya kusikitishwa na uamuzi huo. Wakati Ujerumani Magharibi ilipotishia kuondoa misaada yake ya kijeshi kufuatia uamuzi wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kuendelea na ubalozi mdogo wa Ujerumani Mashariki kule Zanzibar baada ya Muungano Nyerere siyo tu alikasirishwa na hilo lakini alienda mbali zaidi. Aliwaambia Ujerumani wasitoe huo msaada wao na msaada mwingine ambao tayari ulikuwa imepokelewa - karibu dola milioni 1 wakati ule – akawarudishia! Na akasema neno zito sana. Alisema "Sisi si mbwa! Mbwa unaweza kumtishia na chakula, lakini sisi ni binadamu na tuna utu wetu. Ni masikini lakini tuna utu wetu" Kwa maneno mengine kuwa kwa vile tumekubali kusaidiwa haina mamana tuwe tayari kubong'oa!

2. Serikali chini ya Magufuli ifanye uamuzi wa haraka, wa lazima na wa kimkakati wa kutenga zaidi ya shilingi trilioni 1.07 ambazo Wamarekani walikuwa wazitoe kwenye kuchangia sekta ya nishati. Fedha hizi zitolewe (siyo ziahidiwe) na kutengwa kwa ajili ya kuzibba pengo hilo na zianze kwenye bajeti ya mwaka huu na kukamilika si zaidi ya mwakani. Na ni LAZIMA zitoke kwenye fedha za Watanzania wenyewe. Hili ni suala la kisaikolojia; kwamba katika umaskin wetu tunaweza kuficha aibu yetu! Ni kweli ni maskini lakini katika utupu wetu yule anayetaka kutupa hifadhi hatutaki atushikie nguo na kutuambia tuiname kwanza; hata kwenye majani tutajihifadhi kwanza. Kwani maskini hana utu?

3. Serikali ndani ya miezi hii miwili hivi au mitatu ije na sera ya kusimamia suala la misaada ya kigeni na sera hiyo iweke mkazo wa misaada nje ya bajeti. Bajeti ya Watanzania ni lazima itokane na jasho na kazi za Watanzania na si vinginevyo. Misaada yote inataka kutolewa iwe ni katika maeneo ambayo tunaamini yanahitajika – hasa kwenye suala maeneo matatu:
• Kuhamishia ujuzi na maarifa (transfer of knowledge)
• Uwekezaji na Biashara (investment and trade)
• Kurudisha uhamishaji wa wasomi wetu (reverse brain drain)
Misaada ya kigeni itapaswa kuwa kwenye maeneo hayo matatu tu; maeneo mengine yote ya kibajeti Watanzania watapanga na kuyasimamia yenyewe; kwa kupambana na ufisadi, kuleta nidhamu kazi, uwajibikaji, uwazi na usimamizi mzuri wa fedha na mali ya umma. Hatuwezi kuendelea kupokea misaada hata ya kuchimba vyoo ili tu tujisikie tumesaidiwa na kuwafanya watoa misaada huko waliko waseme "tumeisaidia Tanzania"

4. Serikali ya Marekani ikiamu kurudisha msaada wake basi tuingie tena makubaliano nao na iwe nje ya MCC. Na msaada huo uwe kwenye hayo maeneo matato hapo juu; hizo milioni 470 ziende kwenye vyuo vyetu kufundisha wasomi na wataalamu katika masuala ya nishati na wasomi hao wafundishwe ama hapa hapa nchini kwa kuanzisha mahusiano ya vyuo na taasisi za Marekani na taasisi zetu badala ya wanafunzi wetu kwenda kusomeshwa huko Marekani peke yake. Fedha hizo zinaweza kutumiwa vizuri kabis akutengeneza miundo mbinu ya kufundishia wanafunzi yenye kuunganisha vyuo vyetu na vile vya Kimarekani na hivyo kutoa nafasi kubwa ya wengi zaidi kupata mafunzo.

5. Serikali ikae chini na nchi rafiki na kuweka msingi wa mahusiano yetu nao na hili liwe wazi baada ya kuchukua uamuzi wa kutokuwa nchi ya kupokea misaada. Maana ukiwa unapokea misaada ni vigumu kuwaambia watu sikilizeni; wanaweza wakakuambia "tutakusikiliza ukibong'oa kwanza".

Binafsi ninaamini mashinikizo yoyote ya kisiasa kwa serikali yetu yanapaswa kufanywa na Watanzania wenyewe. Sina tatizo kabisa na Watanzania wengine ambao wanailalamikia serikali ya Magufuli au wanapinga mambo mbalimbali yanayofanywa hii ni sehemu ya demokrasia na wana haki hiyo. Kama vile Watanzania wasivyo na sauti wala serikali yao isivyo na sauti mbele yay ale yanayofanywa huko Marekani au nchi nyingine basin a sisi tusitoe hiyo nafasi isipokuwa labda kwenye mazingira ambayo kweli yanapasa. Watanzania wenyewe wanajua vitu vya kushinikiza na vipi washinikize.

Ni wakati wa kusitisha misaada hii ya kigeni mara moja na daima ili kuanza kujenga uchumi kweli unaoendeshwa na shughuli za uzalishaji mali, bidhaa na huduma mbalimbali. Uchumi wetu uko katika hali ya kusahihishwa na tayari tumeanza kuona dalili za kusahihishwa uchumi huo; wakati umefika wa kusahihisha kwenye hili eneo la misaada ya kigeni kwani nalo – na wengine wameshalionesha hili – misaada hii imedumaza sana maendeleo yetu kama taifa na kama bara.
Ni wakati wa kuanza kutumia akili zetu kuendesha maisha yetu nay a watoto wetu. Hatuwezi kuendelea kunyonya na midevu yetu juu! Tunaweza vipi kujiheshimu kama tunafanya mambo ya kutokujiheshimu? Unaweza vipi kulilia kusaidia badala ya kuanza kujiuliza ni vipi nitaacha kusaidiwa ili nianze kujijengea heshima?

MMM
 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment