Sunday 30 March 2014

[wanabidii] Taarifa ya Tume kuhusu mwenendo wa kampeni Chalinze

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA CHALINZE

1.0 UTANGULIZI

Ndugu zangu wanahabari, awali ya yote nawashukuru sana kwa kuitikia wito wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Natambua mna majukumu mengi ya kuhabarisha umma, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba na uchaguzi huu mdogo wa Chalinze.

Kwanza nianze kwa kuvipongeza vyama vyote vya siasa ambavyo vimeweka wagombea katika uchaguzi huu. Hivi sasa hapa nchini kuna vyama vya siasa ishirini na moja (21) vyenye usajili wa kudumu na ambavyo kisheria 
vinastahili kushiriki chaguzi zote, lakini vyama vya siasa vilivyofanikiwa kuweka wagombea ni vitano (5) tu, AFP, CCM, CHADEMA, CUF na NRA. Pongezi hizi nazitoa kwa kutambua kuwa, kushiriki uchaguzi ni gharama.

2.0 MAJUKUMU YA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UCHAGUZI

Kabla ya kuwaeleza madhumuni ya kuwaita, naomba kwanza nitumie nafasi hii kuwaeleza majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika uchaguzi, kwani kuna wadau ambao bado hawaelewi kwa nini Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo katika jimbo la Chalinze na Ofisi hii inafanya nini katika uchaguzi huu.


Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 7 ya mwaka 2010 katika chaguzi zote ikiwamo chaguzi ndogo za wabunge na madiwani.

Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafuatilia na kutoa adhabu kwa vyama vya siasa vinavyojihusisha na vitendo vifuatavyo:-

a)Chama ambacho wanachama na/au mashabiki wake wanajihusisha na vitendo vya fujo, vurugu na uvunjifu wa amani wa aina yoyote ile;

b)Chama ambacho viongozi na/au wanachama wake wanatumia maneno ya matusi, kashfa na uchochezi; na

c)Chama ambacho kinatumia na/au mgombea wake anatumia mali za Serikali katika kampeni na uchaguzi.

Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kuweka sawa uwanja wa ushindani katika siasa, kwa kufuatilia na kupendekeza/kutoa adhabu kwa chama cha siasa na/au mgombea anayejihusisha na masuala yafuatayo.

a)Kutumia fedha nyingi zaidi ya kiwango kilichowekwa na Sheria katika jimbo husika. Katika jimbo la Chalinze sheria inasema mgombea asitumie zaidi ya shilingi milioni hamsini;

b)Uwazi katika matumizi ya pesa katika kampeni ambapo kila chama, mgombea na taasisi za kiraia zinazoshiriki katika kampeni, zinatakiwa kutoa taarifa ya fedha zitakazotumia katika kampeni na uchaguzi na baada ya uchaguzi kuisha, kutoa taarifa ya fedha zilizotumia katika uchaguzi.

c)Chama cha siasa au mgombea kushawishi kupigiwa kura au kushawishi wananchi kuacha kumpigia kura mgombea mwingine kwa kutoa vitu vya thamani kama pesa, chakula, pombe au ahadi za kupewa cheo au kazi.

d)Matumizi ya mali za Serikali katika kampeni;

e)Vyombo vya habari vya Serikali vinavyopendelea upande mmoja katika kampeni.

Aidha, jukumu lingine la muhimu sana ni kutoa elimu kwa wananchi, vyama vya siasa na wagombea, kuhusu wajibu wao na makatazo yaliyomo katika Sheria tajwa hapo juu.

3.0 MADHUMUNI YA KUONGEA NA WANAHABARI

Ndugu wanahabari, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeona sasa ni wakati muafaka wa kufanya tasmini ya kampeni zinavyofanyika katika jimbo la Chalinze, kwani tumeshavuka nusu ya muda wa kampeni na umebaki muda wa wiki moja tu, ambao kwa maneno ya mitaani naweza kusema ni muda wa lala salama.

Hivyo, tumewaita katika mkutano huu kwa madhumuni yafuatayo:

a)Kuwafahamisha wananchi kupitia kwenu kazi zilizofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi mdogo wa Chalinze zianze mpaka sasa;

b)Kuwafahamisha wananchi tathimini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mwenendo wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Chalinze; na

c)Dhumuni jingine la kuwaita ni kuwaeleza shughuli iliyopo mbele yetu mapaka siku ya uchaguzi.

4.0 KAZI ZILIZOFANYWA MPAKA SASA

Ndugu wanahabari; Kazi kubwa zilizofanywa na maafisa wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi wa Chalinze zianze ni zifuatazo:-

a)Kutoa elimu kwa umma kwa wananchi, vyama vya siasa na wagombea kuhusu wajibu wao na makatazo yaliyomo katika Sheria ya Vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi;

b)Kuonana na wadau wa uchaguzi kupata maoni na malalamiko kuhusu kampeni; na

c)Kufuatilia taarifa na malalamiko ya uvunjifu wa Sheria tajwa hapo juu, ili kujua ukweli na kuwaasa wahusika wajirekebishe, wasipojirekebisha kuchukua hatua za stahiki.

Mpaka sasa tumeonana na wagombea vyama vinne, CUF, CCM, CHADEMA na NRA, bado mgombea mmoja wa AFP ambaye tunaendela kuwasiliana naye.

5.0 TATHMINI YA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA CHALINZE

Ndugu wanahabari, mpaka sasa kampeni zinaendalea vizuri, ila kuna malalamiko na vitendo vichache vya uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambavyo kimsingi malalamiko mengi na vitendo vingine vinahitaji uchunguzi wa kina.

Baadhi ya vyama vya siasa vimealalamikia vitendo vya kuingiliwa na wafuasi au wanachama wa chama kingine katika mikutano yao ya kampeni, mabango yao kuchanwa, bendera kushushwa, viongozi, wanachama na wafuasi wao kupigwa na ununuzi wa shahada za mpiga kura. Aidha, kumekuwa na matumizi ya maneno ya kashfa na dhihaka katika majukwaa ya kampeni.

Kimsingi, ikiondoa matumizi ya maneno za kashfa na dhihaka jukwaani, ambayo yanasikika kwa watu waliopo na muongeaji anaonekana na vitendo vya wanachama na mashabiki wa chama kuingilia mkutano wa kampeni wa chama kingine, vitendo vingine vinahitaji uchunguzi wa kina wa taasisi husika, ili kujua wahusika na mazingira ambayo kitendo husika kimetokea, kwa lengo la kuchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake, Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa inaendelea kufuatilia malalamiko iliyopata kutoka kwa vyama vya siasa na wagombea, ili kupata undani wake na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuchukua hatua stahiki. Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo makini na ufuatiliaji wa masuala ya vyama vya siasa kuvunja Sheria inazozisimamia hasa wakati wa uchaguzi. Ila haiwezi kuchukua hatua stahiki kwa chama husika bila kuwa na ushahidi wa kutosha kuwa, chama hicho kimehusika na kitendo hicho cha uvunjifu wa sheria.

Ndugu waandishi wa habari, natumia nafasi hii pia kusisitiza kuwa, ahadi aliyoitoa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francisi S.K. Mutungi, kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatafuta mwarobaini wa vurugu katika kampeni, haikuwa utani wala ahadi hewa. Kwani uzoefu tunaoupata katika chaguzi hizi ndogo unatusaidia katika kutengeneza mwarobaini huo.

6.0 WITO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KWA VYAMA VYA SIASA NA WAGOMBEA

Ndugu zangu wanahabari, kwa kuzingatia mwenendo wa kampeni na ukweli kuwa, kampeni huwa kubwa na pilika nyingi wiki ya mwisho kuelekea siku ya uchaguzi, naomba nitumie nafasi hii kuviasa vyama vya siasa na wagombea wote katika uchaguzi huu mdogo wa Chalinze ifuatavyo:-

a)Kuepuka kutumia maneno ya matusi, kashfa na mambo yanayofanana na hayo, badala yake wanadi sera zao, kwani licha ya kuwa maneno ya matusi na kashfa ni kinyume na sheria na maadili, lakini wananchi wanahitaji kulikiliza sera si matusi na kashfa;

b)Kuepuka vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, kwani licha ya kuwa vinaleta madhara kwa watu na mali zao, lakini pia vinawaogopesha wananchi kushiriki kampeni na hata kwenda kupiga kura;

c)Kutochukua hatua za kisheria mkononi, badala yake wakiona au kusikia mtu kavunja sheria watoe taarifa katika vyombo husika;

d)Kutojihusisha na vitendo vya uchokozi mfano kuingilia mikutano ya kampeni ya chama kingine;

e)Kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa, mfano kununua au kuuza shahada ya mpiga kura;

f)Kutoa taarifa kwa vyombo husika ili zifanyiwe kazi, badala ya kutoa tu kwa wanahabari na kulalamika;

g)Kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapiga kura.

Aidha, Waandishi wa habari waepuke kutoa taarifa bila kuzifanyia uchunguzi ikiwamo kupata maoni ya upande wa pili, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwapa hofu wananchi wa nchi nzima na wapiga kura ikiwa taarifa iliyotolewa ni ya kuogofya wakati si ya kweli.

7.0 KAZI ZILIZO MBELE YETU

Siku za kampeni zilizobaki, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imejipanga kuendelea kutekeleza majukumu yake niliyoyataja hapo juu, isipokuwa siku ya uchaguzi tarehe 06 Aprili, 2014, Ofisi imejipanga kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufuatilia chama cha siasa na wagombea wanaofanya mambo yalikatazwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ikiwamo kubeba wapiga kura katika vyombo vya usafiri kuwapeleka au kuwatoa katika vituo vya kupiga kura.

8.0 FAIDA YA UWEPO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA CHAGUZI MBALIMBALI

Ndugu waandishi wa habari; naomba nitumie nafasi hii pia kuwaeleza faida za uwepo wa Ofisi ya Msajili ya Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali hasa chaguzi ndogo.

Uwepo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali unasaidia uchaguzi kufanyika vizuri, kwa amani na utulivu na wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa namna zifuatazo:-

a)Kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi vya Msajili wa Vyama vya Siasa inasaidia kuweka uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi kwa kuepusha matumizi makubwa ya fedha katika kampeni, kuweka uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali nyingine katika kampeni na kuepusha matumizi ya mali za Serikali katika kampeni.

b)Kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi vya Msajili wa Vyama vya Siasa inasaidia kuepusha vitendo vya vurugu, matusi na uchochezi kwa kuchukua hatua stahiki kwa chama kinachohusika kwa mujibu wa Sheria.

Aidha, kitendo cha maafisa wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwepo tu katika kampeni, kinawatia hofu wanasiasa na vyama vya siasa vyenye lengo la kuvunja sheria, kwani wanaelewa fika kuwa, Ofisi ya Msajili ipo na inafuatilia. Hivyo, uwepo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kampeni za uchaguzi hupunguza sana vitendo vya uvunjifu wa sheria nilizozitaja hapo juu.

9.0 MWISHO

Namalizia kwa kutoa wito kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu kuelewa kuwa, vinawajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na wagombea wao kuheshimu na kufuata Sheria zote zinazohusika. Hivyo, kila chama kitekeleze wajibu wake, ili uchaguzi huu unafanyike kwa amani na utulivu. Nawaomba pia wanachi wa Chalinze waendelee kuhudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa bila hofu na woga. Aidha, washawishike kwa hoja na sio rushwa. Watoe taarifa kwa vyombo husika pale wanapoona mtu yeyote anajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Sheria na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

Asanteni kwa kunisikiliza na ninawatakia kazi njema katika kazi yenu ya kuwahabarisha wananchi kuhusu kampeni za uchaguzi wa Chalinze.

Sisty L. Nyahoza
Kny: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
30 Machi, 2014

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment