Sunday 30 March 2014

[wanabidii] WAJIBU WA VIJANA KATIKA KUIMARISHA NA KUENDELEZA MUUNGANO WA TANZANIA

WAJIBU WA VIJANA KATIKA KUIMARISHA NA KUENDELEZA MUUNGANO WA TANZANIA BAADA YA MIAKA 50: UCHAMBUZI WA UTAIFA WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.
Na
Prof. Gaudens P. Mpangala
Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa

1. Utangulizi 
Katika Taifa lolote vijana wana sifa kubwa tatu. Kwanza wana uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya taifa kulingana na vipaji, elimu na uwezo walionao. Pili vijana ni chimbuko kubwa la mabadiliko kwa vile ni rahisi kwao kuendana na mabadiliko ya wakati. Tatu vijana wana uwezo mkubwa wa kufanya utaifiti na uchambuzi kuhusu mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitaifa kwa ujumla. Dhana ya kusema kuwa vijana ni taifa la kesho ni dhana potofu. Vijana ni sehemu muhimu sana ya taifa la leo. Hata watoto ni sehemu ya taifa la leo na sio taifa la kesho. Kutokana na sifa hizi vijana wana nafasi kubwa ya kutoa mchango katika kuimarisha na kuendeleza muungano wetu wa Tanzania.

Tarehe 26 April, 2014 Muungano wa Tanzania utatimiza miaka 50 tangu ulipoanzishwa mwaka 1964. Hiki ni kipindi kirefu cha nusu karne. Katika kipindi hiki Watanzania wamejenga uzoefu mkubwa kuhusu Muungano wa Tanzania kuhusu manufaa na changamoto zake. Licha ya changamoto zilizojitokeza manufaa ya Muungano ni mengi na makubwa . Baadhi ya manufaa hayo ni ulinzi na usalama wa nchi zote mbili na watu wake, umoja wa kitaifa katika ngazi ya Muungano na katika ngazi ya nchi washiriki, ushirikiano wa kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na heshima na hadhi katika macho ya nchi za Afrika na dunia kwa ujumla

Wajibu wa vijana katika kuimarisha na kuendeleza Muungano una husu mambo mengi. Mada hii inajikita katika suala la msingi katika muungano wa aina yoyote nalo ni suala la utiafa katika mnyambuliko wa kihistoria. Muungano maana yake ni mataifa au nchi mbili au zaidi kuungana kuwa taifa moja. Katika kufanya hivyo kutegemeana na muundo wa muungano hutokea utaifa wa aina mbili, utaifa wa ngazi ya muungano na utaifa wan chi washiriki wa muungano na wa kuimarisha na kuendeleza muungano wowote hutegemea sana uwiano baina ya aina hizi mbili za utaifa.

2. Chimbuko la utaifa wa Afrika.
Chimbuko la utaifa wa Afrika (African nationalism) ni harakati za kupambana na ukoloni na kudai uhuru kuanzia miaka ya 1940 hadi miaka 1960. Utaifa wa Afrika ulikuwa ndiyo itikadi kubwa iliyowawezesha viongozi wa harakati hizo kuhamasisha wananchi katika kushiriki katika kupigania uhuru ili kupata mataifa huru ya Afrika. Wakati chimbuko la utaifa Afrika likiwa ni harakati za kupigania uhuru kutokana na ukoloni, sehemu nyingine za dunia kumekuwa na machimbuko tofauti. Mfano mzuri ni Mataifa ya Ulaya . Chimbuko la utaifa wa ulaya (Europian nationalism) lilikuwa ni harakati za kuibuka na kukua kwa ubepari ukipambana na mfumo wa muda mrefu wa kikandamizaji wa kikabaila. Kati ya karne ya 16 na 18 AD. Kutokana na harakati hizo ndipo zitakua fikra na nadharia za uliberali na ujenzi wa demokrasia ya kiliberali. Hivyo nchi za ulaya zikijitambua zaidi kama mataifa yenye mipaka yake na serikali zake za kijamhuri. 

Mpaka sasa tunaweza kuugawa utaifa wa Afrika katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ni ile ya harakati za kudai uhuru hadi uhuru kupatikana. Awamu ya pili ni ile ya kipindi cha kwanza cha takriban miongo mitatu miaka ya 1960 hadi miaka ya 1980. Hiki kilikuwa ni kipindi cha kwanza cha ujenzi wa Taifa. Kila taifa huru la Afrika likijikita katika kupigania maendeleo ya nchi yake na watu wake. Licha ya kuwa kila nchi ilikuwa na mikakati na sera zake za ujenzi wa taifa , mambo matatu yalikuwa ni dira kwa nchi zote. Mambo haya yalijuwa ni umoja wa kitaifa, maendeleo ya uchumi, huduma za jamii na utamaduni na ushirikiano na mataifa mengine ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Lakini katika awamu hii ya pili ya utaifa kulikuwa pia na juhudi za kuunda umoja wan chi zote za Afrika ili kupata taifa moja la Afrika (United States of Afrika). Katika miaka 1960 suala hili lilikuwa na mjadala mkali baina ya viongozi wa nch za Afrika kama vile Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Sekou Toure na kadhalika. Wengine kama vile Nkrumah na Sekou Toune walitaka umoja huo uundwe mara moja na wengine kama vile Julius Nyerere walitaka uundwe kwa kwenda hatua kwa hatua kuanzia na kuundwa kwa mashirikisho ya kikanda kama vile shirikisho la Afrika Mashariki ambalo Julius Nyerere alilipigania sana . Mashirikisho ya kikanda yangeimarika ndipo yangekuja pamoja na kuunda umoja wa Afrika. Jambo lililojitokeza katika mjadala wa wakati huo ni kwamba hata kama umoja huo wa Afrika ungeundwa , utaifa wa kila nchi ushiriki ungeendelea kudumishwa. Kungekuwa na utaifa wa umoja wa Afrika wa kila nchi mshiriki. Hii ilijidhihirisha katika makubaliano mbalimbali kama vile kuheshimu mipaka ya nchi zote za Afrika iliyowekwa na wakoloni. Licha ya kuwa umoja huo haukufanikiwa walao mwaka 1963 uliundwa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) ambao iliratibu shughuli mbalimbali za nchi za Afrika na kuwa jukwaa la kuzikutanisha nchi hizo ili kukubaliana na kutekeleza malengo mbalimbali.

Awamu ya tatu ya utaifa wa Afrika ni ile ya kipindi cha pili cha ujenzi wa taifa. Kipindi hiki ni kuanzia takribani mwaka wa 1990 hadi hivi leo ni zaidi ya miongo miwili. Tunakichukua hiki kuwa ni kipindi cha pili kwa sababu ya mabadiliko mengi na makubwa yaliyozikumba nchi za Afrika. Mabadiliko hayo ni pamoja na vuguvugu la kudai na kujenga demokrasia, kuondokana na mfumo wa chama kimoja na sekikali za kijeshi na kuingia katika mfumo wa vyama vingi, mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yaliyoletwa na sera za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa na nchi kuchukua itikadi za uliberali mamboleo na kuachana na itikadi zao kama vile itikadi za ujamaa na usoshalisti.

3. Utaifa wa Afrika na Chimbuko Muungano wa Tanzania
Fikra na harakati za miaka ya 1960 kuhusu kuundwa umoja wa Afrika kama nchi moja zilikuwa za aina mbili kama tulivyokwisha ona. Aina moja ilikuwa ya kutaka kuundwa kwa umoja huo mara moja na kupata taifa moja la Afrika. Aina ya pili ilikuwa ni kuanzia na umoja wa sehemu mbalimbali za Afrika kama vile shirikisho la Afrika Mashariki. Umoja wa aina hiyo ungeweza kuwa wa kikanda au sehemu ya kanda, kwa nchi mbili au zaidi kuamua kuunda umoja wao.

Mwalimu Julius K. Nyerere alikuwa muumini wa aina hii ya pili ya umoja. Alitaka aonyeshe mfano kwa kuunda shirikisho la Afrika Mashariki. Alikuwa wa kwanza kutoa wazo na ushawishi kwa viongozi wa harakati za kudai uhuru Afrika Mashariki yaani Jomo Kenyatta wa Kenya, Milton Obote wa Unganda na Abeid Karume wa Zanzibar. Kwa ujumla hadi mwaka 1960 wazo la kuunda shirikisho la Afrika Mashariki lilikubaliwa na nchi zote na Mwalimu Julius Nyerer alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika ili kusubiri nchi nyingine, zipate uhuru kwa wakati mmoja ingekuwa rahisi kuunda shirkisho hilo. Hata hivyo azma hiyo ya kuahirisha uhuru wa Tanganyika haikufanikiwa hivyo Tanganyika ilikuwa ya kwanza Afrika Mashariki kupata uhuru Desemba 9 mwaka 1961.

Baada ya nchi zote za Afrika mashariki kupata uhuru hadi 1963 kwasababu mbalimbali shirikisho la Afrika Mashariki halikuweza kuundwa. Lakini katika misingi hiyo ya harakati za umoja wa Afrika kwa kiwango cha sehemu ya Afrika ukaundwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 April, 1964. Walao kiasi fulani cha ndoto za mwalimu kilitimia. Licha ya azma ya umoja wa Afrika na azma ya mwalimu, muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulisababishwa na mambo mengine, mambo hayo ni pamoja na mazingira ya wasiwasi ya kiusalama kutokana na mapinduzi ya Zanzibar ya 12 Januari 1964, uhusiano mzuri wa siku nyingi wa vyama vya ASP na TANU na uhusiano wa karibu wa kihistoria kati ya watu wa Tanganyika na Wazanzibar. Maamuzi ya kuungana yalifanywa baina ya Rais Julius Nyerere kwa niaba ya Watanganyika na Abeid Amani Karume kwa niaba ya Wazanzibar.

4. Muungano wa Tanzania na Utaifa wa Tanganyika na Zanzibar
Muungano wa Tanzania ulitokana na nchi mbili zilizoungana nazo ni Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar. Tanganyika kwanza ilitawaliwa na Wajerumani 1885-1918 na baadae ilitawaliwa na Waingereza 1918-1961. Nchi hizi zote mbili zilipitia kipindi cha awamu ya kwanza ya utaifa yaani kipindi cha harakati za kudai uhuru kutoka kwa ukoloni wa Waingereza.

Nchi hizi zote mbili zilipambana na ukoloni wa Mwingereza kudai uhuru ili kujenga mataifa mapya. Wakati wa kuungana walichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar kama ishara ya mataifa mawili yanayoungana kuunda taifa moja.

Baada ya kuungana jina la muungano lilikuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na jina hili lilidumu kuanzia Aprili hadi Oktoba, 1964. Mwezi Oktoba jina lilibadilishwa na kuita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuhusu muundo wa Muungano kulitokea mjadala mkali kati ya waasisi wa Muungano yaani Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume. Rais Abeid Karume alipendekeza uwe Muungano wa kuunda nchi moja kwa maana kwamba nchi za Tanganyika na Zanzibar zife kabisa na kupata nchi moja. Alipendekeza pia kuwa Mwalimu Julius Nyerere awe Rais wa nchi hiyo mpya na yeye Abeid Karume awe Makamu wa Rais. Lakini Julius Nyerere alipendekeza muundo wa serikali mbili yaani serikali ya muungano na serikali ya Zanzibar. Alisema kwa kuwa Zanzibar ni nchi ndogo kulinganishwa na Tanganyika katika mfumo wa serikali moja Zanzibar ingemezwa na Tanganyika hivyo kupoteza utambulisho wake. Mwishowe wote wakakubaliana na pendekezo la Rais Julius Nyerere la serikali mbili.

Kufuatana na mfumo huo na hasa baada ya kubadili jina la muungano na kuchukua jina la Tanzania, jina la Tanganyika kama nchi washiriki wa muungano likaachwa. Badala yake ukawa ni muungano wa Tanzania baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo kukawa na utaifa wa muungano wa Tanzania, lakini utaifa wan chi washiriki wa Muungano ukaanza kuwa na utata. Utaifa wa Zanzibar ulibaki lakini ule wa Tanganyika ulifunikwa.

Kutokana na hali hiyo kwa kipindi chote cha miaka 50 ya Muungano kumekuwa matukio ya kudai utaifa kama ifuatavyo. Kwa Zanzibar licha utaifa wake kubaki kwa kuwa na serikali yake na Baraza lake la wawakilishi imeendelea kujiona kuwa chini ya mfumo wa serikali mbili bado kuna dalili za kumezwa na Tanzania Bara na kuwa utambulisho wake kama nchi sio kamili. Hivyo mwaka 1984 likatokea vuguvugu la kudai mfumo wa serikali tatu ili kuwe na serikali ya Tanganyika. Katiba ya Zanzibar iwe huru zaidi kama vile, sheria zinazotungwa na Bunge la Muungano zisitumike Zanzibar kabla ya kuhakikiwa na Baraza la wawakilishi.

Katika awamu ya tatu ya utaifa wa Afrika madai ya kuimarika zaidi kwa utaifa wa Zanzibar yamezidi kuongezeka. Chama kikuu cha upinzani Zanzibar, CUF, kwa kipindi chote cha miongo miwili ya mfumo wa vyama vingi kimeendelea kudai muundo wa serikali tatu na hasa wakati wa kampeni za chaguzi. Ni hivi karibuni tu wameanza madai Muungano wa mkataba. Mchakato wa maridhiano, kura za maoni na kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa 2009 – 2010 ulionyesha jinsi gani utaifa wa Zanzibar ulivyozidi kukua. Kilele chake kilikuwa kufanya marekebisho ya katiba ya Zanzibar ili kuifanya Zanzibar ya mwaka 1984 ilifanya Zanzabar iwe nchi ili kuthibitisha hatua zilizokwisha chukuliwa za kuwa na bendera na wimbo wa taifa.

Kuhusu Tanganyika madai ya utambulisho wa utaifa wa Tanganyika yalianza kujitokeza tangu mwanzo wa mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi mwanzoni mwa miaka ya 1990. Tume ya Rais ya mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi Tanzania au Tume ya Nyalali ulikuja na pendekezo la serikali tatu, yaani serikali ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano. Tume ilikuja na pendekezo hilo kutokana na maoni waliyoyakusanya kutoka kwa wananchi. Mara tu baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 baadhi ya vyama vya upinzani vilianza kudai kuwepo kwa serikali ya Tanganyika kwa vile Zanzibar ina serikali yake. Mwaka 1993 kundi la wabunge 55 (G55) wote wakiwa ni wabunge wa CCM waliibua hoja ya kuwepo kwa serikali ya Tanganyika na ni hoja ambayo ilipitishwa na Bunge lakini Baba wa Taifa aliingilia kati kuizima.
Tume ya Jaji Kisanga na kamati mbalimbali nazo zilikuja na mapendekezo ya serikali tatu kutokana na maoni ya wananchi sio tu wa Tanganyika bali pia wa Zanzibar. Pia kutokana na maoni ya wananchi Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti wake Jaji Warioba imekuja na mapendekezo ya serikali tatu katika raimu ya kwanza na rasimu ya pili ya katiba mpya. Katika mapendekezo yake hayo ya serikalr tatu yaani serikali ya Tanganyika ya Zanzibar na ya Muungano Tume imetoa maelezo ya kina kwa nini walifikia uamuzi huo. Sababu nyingi walizozitoa msingi wake ni kukua kwa utaifa wa Tanganyika na wa Zanzibar. Ni wananchi wachache waliotoa maoni ya kutaka Muungano uvunjwe. Wananchi wengi wanapenda Muungano uendelee lakini kuwe na marekebisho ya muundo kwa jinsi kwamba wengi wanapendelea kuwa na serikali tatu ili kuwe na utaifa wa ngazi ya Muungano, yaani utaifa wa Tanzania na utaifa wa ngazi ya nchi washiriki wa Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar.

5. Hitimisho.
Lengo la mada hii limekuwa ni kufanya uchambuzi kuhusu jambo moja muhimu katika kuimarisha na kuendeleza Muungano wa Tanzania. Jambo lenyewe ni nafasi ya utaifa katika kuimarisha na kuendeleza Muungano. Changamoto, matatizo na hata kero za Muungano kwa kipindi cha miaka 50 chimbuko na kiini chake ni suala la utaifa. Uchambuzi uliofanywa na mwandishi wa mada hii ni kidokezo tu. Ni matarijio ya mwandishi kuwa vijana wa Tanzania watafanya utafiti na uchambuzi wa kina zaidi kuhusu utaifa katika majukumu yao ya kuimarisha na kuendeleza Muungano wa Tanzania. Ni wazi kuwa nguzo za utaifa wa Tanzania katika ngazi ya Muungano ni utaifa wa Tanganyika na Zanzibar.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment