Sunday 30 March 2014

[wanabidii] PAC yaanza kuchunguza ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya Kimataifa

Leo tarehe 30 Machi 2014, kamati ya BUNGE ya PAC imeanza rasmi uchunguzi kuhusu ukubwa wa tatizo la ukwepaji kodi na utoroshwaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa ( multinational corporations). Uchunguzi huu unatokana azimio la umoja wa kamati za PAC za nchi za SADCOPAC lilioamuliwa Arusha, Tanzania mwezi Septemba mwaka 2013 ( Azimio lilisomeka – PACs should initiate investigations on the extent of tax avoidance/evasion and illicit money transfer in their jurisdiction).

Leo PAC imekutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Kitengo cha Fedha Haramu ( FIU) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya majadiliano ya awali kuhusu 
uchunguzi huo.

Kamati imeelezwa kuwa tatizo la ukwepaji kodi ni kubwa sana na linagusa sekta zote. TRA imeieleza kamati mifano mbalimbali kwa kila sekta namna gani Taifa linapoteza kodi. Njia zinazotumika ni pamoja na udanganyifu katika mikopo, udanganyifu katika bei za mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje na mikataba ya biashara miongoni mwa makampuni yanayohusiana. Uchunguzi uliofanywa na TRA kwa kampuni mojawapo wa uchimbaji madini unaonyesha kuwa kampuni hiyo iliyotangaza hasara mwaka 2011 iligundulika kuwa kumbe ilipata faida ya dola za kimarekani 327 milioni.

Sekta ya Utalii na mahoteli inaonyesha kugubikwa kiasi kikubwa na ukwepaji kodi kwa kampuni katika sekta hiyo kutumia mikataba na makampuni yanayohusiana yaliyokwenye Tax Havens ambayo inahamisha mapato mengi kwenda offshore (profit shifting and base erosion).
Kamati imeelezwa na BoT kuwa hivi sasa kuna uchunguzi maalumu unaoendelea kuhusu 'illicit financial transfer' kutoka Tanzania.

Pia ameeleza kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kufunga akaunti za makampuni ya madini yaliyopo offshore kwani sababu za makampuni hayo kuwa akaunti nje hazina msingi tena. Hata hivyo changamoto kubwa ni mikataba waliyoingia na Serikali ambayo inawaruhusu kufungua akaunti offshore na kuweka mapato yao yote ya mauzo ya madini huko.

Utoroshaji wa fedha kutoka Tanzania ni changamoto kubwa sana ya maendeleo ya Tanzania katika kupambana na umasikini. Utoroshwaji umekuwa ukikua mwaka hadi mwaka. Taarifa ya benki ya maendeleo Afrika inaonyesha kuwa mwaka 2010 peke yake Tanzania zilitoroshwa jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.3 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 5 ya Pato la Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 20 ya mapato ya ndani ya TRA.

Kamati ya PAC itaendesha uchunguzi na kuandaa taarifa itakayowasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa BUNGE la Tanzania kuendesha uchunguzi wa aina hii. Pia Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la SADC kutekeleza azimio hili. Nchini Uingereza kamati ya PAC ya BUNGE la uingereza iliendesha uchunguzi kama huu na makampuni makubwa kama google, Amazon na Starbucks waligunduliwa kukwepa kodi nchini humo. Kwa nchi za Afrika sekta yenye kutorosha fedha na kukwepa kodi kwa wingi ni sekta ya madini, mafuta na gesi. Mwaka 2013 mwezi Desemba kamati ya PAC Tanzania ilikutana na PAC – UK ili kupata uzoefu wa namna ya kuendesha uchunguzi wa aina hii.

Zitto Kabwe, MB
Mwenyekiti, PAC
Dodoma
30-03-2014

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment