Saturday 29 March 2014

[wanabidii] Ya Kura Mseto Na Tafsiri Yangu...



Ndugu zangu,

Ningelikuwa Mjumbe kwenye Bunge Maalum la Katiba msimamo wangu ungelikuwa wa dhahiri kwenye hoja ya Muungano na hata namna ya upigaji kura; Kwamba ningepigia kura Muundo wa Serikali Tatu, na hivyo uwepo wa Tanganyika, na ningependelea upigaji kura kwenye masuala muhimu uwe wa SIRI.

Lakini, kwa vile mimi ni Muumini wa Nchi yangu niliyozaliwa, hata kama wenye mitazamo sawa na mimi tungeshindwa kwa wingi wa kura, basi, ningebaki na misimamo yangu na hata kuendelea kuipigia debe kuwashawishi wengine, lakini, ningefanya yote kuunga mkono kilichoamuliwa na wengi. Na hapa ndipo ulipo msingi wa hoja yangu, kuwa Katiba ni Maridhiano.

Maana, nimepata kuandika, kuwa MARIDHIANO ndio msingi wa UHALALI wa mchakato na hata Katiba yenyewe. Na ndio maana ya ukomavu wa kisiasa na kiuongozi.

Nilifarijika sana jana kuwaona na kuwasikia Profesa Ibrahim Lipumba ( CUF), Vuai Ali Vuai ( CCM) na John Mnyika ( Chadema). Waliongea maneno ya hekima na busara sana. Wote hawa ndio waliounda Kamati ya Maridhiano juu ya suala la kura ya Siri au Wazi. Kamati iliyoundwa kwa busara na hekima za Spika Sitta.

Na kauli za wajumbe hao niliowataja zilifunikwa na kawa lililofumwa kwa maneno yenye hekima na busara kutoka kwa Askofu Donald Mtetemela aliyewawakilisha viongozi wengine wa kidini waliokuwemo kwenye kikao cha Kamati ya Mariadhiano.

Askofu Mtetemela alisema; pamoja na tofauti zilizozijitokeza, pande mbili zimekubaliana kuacha kung'ang'ania misimamo yao ili tusonge mbele katika kutimiza lengo la kupata Katiba Mpya.

Hivyo, inanisikitisha ninaposoma habari kuwa wanaharakati wa Jukwaa la Katiba kuwa wanapanga kulivunja Bunge kwa vile limetafuna bilioni 80. Siioni busara na hekima ya wao wanaharakati kufikia hitimisho hili huku wakifahamu kuwa hapa tulipofikia ni moja ya hatua muhimu kwenye mchakato na pengine harakati za Watanzania kupata Katiba iliyo bora kuliko ile ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1984.

Sasa kama wanaharakati wa Jukwaa la Katiba wanatumia muda na fedha kuandaa maandamano ya nchi nzima kwa dhumuni la kuvunja Bunge Maalum la Katiba, swali, ili iweje? Kuna haja ya wanaohusika na mipango hii kujitafakari upya. Ningedhani wangetumia rasilimali walizonazo kwenye kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya Rasimu ya Katiba na yaliyomo. Kuwapa mwanga zaidi wananchi katika kuyaelewa wanayojadili wabunge wao.

Hii ni nchi yetu sote. Na hili la Katiba ni mchakato. Tusiwe wepesi wa kukata tamaa. Ni vema na ni busara tukaupa nafasi na kuendelea kuunga mkono mchakato wa Katiba unaoendelea sasa.

Maggid Mjengwa,
0754 678 252
http://mjengwablog.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment