Sunday, 8 July 2012

[wanabidii] UDHALILISHWAJI WA WAISLAM NA VYOMBO VYA DOLA VYA TANZANIA

Utangulizi

Sheikh wa kwanza kudhalilishwa na serikali ya Tanzania alikuwa Mufti
wa Tanzania kwa wakati ule Sheikh Hassan bin Amir ambae kwa amri
iliyotolewa na Julius Nyerere alikamatwa nyumbani kwake usiku wa
manane akiwa kavaa khanga tu na akachukuliwa hivyo hivyo hadi uwanja
wa ndege na kurejeshwa "kwao" Zanzibar. Kisa cha yeye kufukuzwa Bara
ni kirefu na kwa sasa hapa si mahali pake kueleza. Nimekiweka kisa cha
Sheikh Hassan bin Amir mwanzo kwa kuwa kina nafasi ya pekee katika
historia ya Waislam na mapambano yao na serikali toka uhuru upatikane
mwaka 1961. Lakini mwaka wa 1964 masheikh wengi waliwekwa kizuizini
kwa amri ya Nyerere hiki nacho ni kisa kingine kinachohitaji wakati
maalum kuhadithiwa. Baada ya haya ndipo kwa mara ya kwanza moto wa
makumbi ukajitokeza juu na Waislam wakapambana na serikali katika
mitaa ya Dar es Salaam mwaka 1993 na mabomu ya machozi na risasi
zikapigwa. Haya ndiyo yalikuwa maandamano ya kwanza kufanywa na
Waislam baada ya uhuru. Hili lilikuwa sakata la kuvunjwa mabucha ya
nguruwe. Damu ya Waislam ilimwagika. Masheikh kumi na moja wa Wilaya
ya Kinondoni walikamatwa pasi na adabu usiku wa manane majumbani mwao,
wakapigwa pingu na kutupwa katika malendrova ya polisi kama majambazi.
Lakini haya yote si kitu tokeo lililotokea siku ya Jumatano tarehe 4
Julai lilifurtu ada. Sheikh Nurdin Kishki akiwa na ugeni wa masheikh
wenzake kutoka Yemen ndani yao akiwapo Mufti wa Yemen walivamiwa na
askari waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia wakiwa njiani wakitokea
Tanga na wakagaragazwa chini huku wakionyeshwa mitutu ya bunduki. Hii
ilikuwa habari kubwa lakini vyombo vyote vya habari kama ilivyo ada
kwa mambo yanayowahusu Waislam vyombo vyote muhimu vilipuuza stori
hii.

Baada ya utangulizi huu naeleza kisa kilichonifika mikononi mwa vyombo
vya dola miaka sita iliyopita:

Mkasa Wangu wa Kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwl. Nyerere, Dar es
Salaam Mwaka 2006

Mohamed Said

"Mwaka 2006 Radio Tehran walipendekeza jina langu rehekwa Wizara ya
Mambo ya Nje Iran wanialike katika hawli ya Imam Khomeni. Sababu ya ya
mie kualikwa ni kuwa mara kwa mara nilikuwa nikifanya mahojiano na
Radio Tehran Idhaa ya Kiswahili kuhusu siasa za Tanzania hususan
wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na ikatokea kuwa yale mahojiano
yangu yakawa yanapendwa na wasikizaji wa Afrika ya Mashariki na Kati
na sehemu za Emirati. Nilkwenda Iran na waalikwa walikuwa kutoka dunia
nzima na wa kila aina, waandishi, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasomi wa
kawaida, mawaziri wa serikali kutoka nchi tofauti na watu wengine
wengi. Msafara wetu wa wageni kwenda mahali ulikuwa ni msururu wa
mabasi zaidi ya kumi yakisindikizwa na kimulimuli cha polisi. Kutoka
Tanzania nilikuwapo mimi pamoja na waandishi kutoka Daily News na
Kituo Cha TV cha Channel Ten. Nikiwa Tehran niliingia studio za Radio
Tehran Idhaa ya Kiswahili na tukafanya mahojiano na mtangazaji wao
mashuuri Abdulfataa Mussa na wenzake na vilevile kurekodi vipindi
vingi kuhusu hali ya Waislam Tanzania.

Mambo yalianza wakati sasa narudi Dar es Salaam na ndege ya Emirates
iliyokuwa inatua usiku. Inaelekea maofisa wa pasi pale uwanjani
walikuwa na taarifa zangu mapema na walikuwa wakinisubiri kwa hamu
kubwa kwani nilipotoa pasi yangu kwa afisa wa pasi hapo ndipo shughuli
za kunishughulikia zilipoaanza. Mimi sikuwa na hili wala lile. Nikawa
namuona yule dada aliyekuwa kwenye kile kizimba akikukurika na pasi
yangu akiitia katika mashine na kuitoa mara kadhaa. Fikra iliyonijia
kwa haraka ilikuwa mashine ni mbovu na harakati zile zilikuwa ni
kurekebisha mitambo. Kumbe sivyo wahusika nadhani walikuwa
wanahakikisha kuwa mimi ndiyo huyo waliokuwa wakimwinda na kumsubiri
na sasa kapatikana, kaingia mwenyewe kwenye mtego na kanasa. Yule
afisa wa pasi akanambia nikae pembeni natakiwa kwa mahojiano na watu
wa usalama. Hofu haikuwa imeniingia kwa kuwa nilikuwa natambua kuwa
harakati dhidi ya ugaidi zilikuwa zimepamba moto na labda nilitakiwa
kwa mahojiano mafupi kutaka kujua nyendo zangu. Sikujua wala kutarajia
kuwa mshtuko mkubwa ulikuwa unanisubiri.

Nilichukuliwa hadi kwenye chumba kimoja na hapo niliwakuta maofisa wa
usalama watatu wakanikaribisha kwa taadhima kisha wakanambia kuwa niko
chini ya ulinzi kwa kuwa zimewafikia taarifa zangu kuwa mimi
nasafirisha mihadarati. Mpaka hapa sikuwa na hofu bado ilinijia picha
kuwa yawezekana wamefananisha majina. Niliwaambia huenda Mohamed Said
muuza madawa ya kulevya siyo mimi niliye mbele yao. Wakaniambia kwa
kujiamini kabisa kuwa taarifa zao ni madhubuti muuza unga ni mimi na
wamekuwa wakinifuatilia siku nyingi. Hapo ndipo walipotoa pasi yangu
na kuniomba niitambue kama hiyo pasi ni yangu au la. Niliwajibu kuwa
hakika hiyo ndiyo pasi yangu khasa. Wakaniamuru sasa tutoke twende
nikachukue mizigo yangu ili wafanye upekuzi wa mihadarati katika
mizigo niliyotokanayo Tehran. Hapo ndipo nilipojuwa kuwa niko katika
lindi kubwa la matatizo na ubongo wangu ukaanza kufanya kazi kwa
haraka huku nikosoma dua kumuomba Allah ulinzi wake kwani kwa hakika
nilijua kama ni njama zimekamilika na leo imefika siku yangu.
Nikajiuliza itakuwaje watakapotoa madawa kwenye mizigo yangu. Nikaanza
kufikiri vichwa vya habari vya magazeti yatakavyopambwa na habari
zangu. Ikanijia yakini kuwa watu wa usalama wameniwekea madawa ya
kulevya katika mizigo yangu ili waniangamize na maadui zangu wapumzike
na shari yangu.

Nilimgeukia yule ofisa mkuu aliyekuwa ananihoji nikamwambia kuwa
sitokubali kugusa mizigo yangu bila kuwapo mashahidi isijekuwa mizigo
yangu ishawekewa hayo madawa ya kulevya kwani nilikotoka mizigo
ilikuwa imekaguliwa na ilikuwa salama. Hoja yangu kubwa kwao ilikuwa
kupata uhakika kutoka kwao kuwa wananijua vizuri kiasi cha
kuthibitisha kuwa kweli mie ni msafirishaji wa madawa ya kulevya. Jibu
nililopewa ni kuwa wao wanafanya kazi kutokana na taarifa
zilizowafikia. Wakasema, "Sisi tunazo taarifa zako kamili kuwa wewe ni
msafirisha madawa ya kulevya." Nikawauiza, "Baada ya kupata taarifa
hizo zangu nyie mmechunguza kutafuta ukweli?" Wakasema, "Ndiyo maana
leo tumekukamata." Nikawaambia, "Si kweli kama kwa sababu mie
nafahamika Dar es Salaam takriban kwingi maana ndio nilikozaliwa na
kukulia. Hapo Kariakoo ukiwaambia watu kuwa Mohamed ni "Mzungu wa
Unga" kila mtu atacheka maana huo kwao ndugu zangu ni mzaha mbaya."
Walitaka kujua nilkwenda kufanya nini Iran. Niliwaambia nilialikwa na
serikali ya huko kuhudhuria mkutano. Wakataka kujua vipi nilipata
mwaliko. Nikawajibu kuwa hilo swali sina jibu labda waiulize serikali
ya Iran. Nikawaeleza kuwa mbona siku zote napita hapo uwanjani nikenda
sehemu tofauti duniani kwa mialiko na kutoa mada sijakamatwa kimezidi
nini katika hii safari ya Iran? Niliwaeleza kuwa miezi michache
iliyopita nilikuwa Chuo Kikuu Cha Ibadan kwa mwaliko tena mkutano
umefadhiliwa na serikali ya Amerika na wamenipa na tiketi toka Dar es
Salaam hadi Lagos na kuniweka hoteli na kunilipa fedha. "Mbona
hamkunikamata wakati ule?" Ikawa swali na jibu swali. Nikafungua
mlango mwingine nikawaambia, "Nakuapieni nyie msingethubutu kumkamata
Mkristo anaetoka Vatican mkutanoni. Lakini kwa kuwa mie ni Muislam
sina wa kunitetea. Nchi hii nani atakuuliza kwa kumnyanyanyasa
Muislam?" Walishtuka na wakawa wanyonge sana wakasema si kweli kuwa
naponzwa na dini yangu.

Baada ya kukurukakara nyingi na mabishano makubwa kuhusu mie kukubali
kufanyiwa upekuzi wa mizigo yangu alikuja binti mmoja katika wao na
yeye akanihakikishia kuwa wao ni serikali na sio wahuni. Hawathubutu
kuniwekea dawa katika mizigo yangu hivyo akanisihi sana kwa upole
nikubali ili wajitoe wasiwasi na wataniachia endapo hakuna kitu.
Niliomba apatikane shahidi wa kushuhudia mizigo yangu kabla ya
kufanyiwa upekuzi lakini hakuna mtu aliyekubali kuchukua dhima ile
katika maofisa waliokuwa kazini pale uwanja wa ndege usiku ule.
Upekuzi ukafanyika hadi mwilini. Hakuna kitu. Wakanipela katika choo
maalum cha kutolea madawa kwa njia ya haja kubwa. Nikakataa kujisaidia
pale. Ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Choo
chenyewe ni cha aluminium. Tofauti na vyoo vya pale ambavyo siku zote
ni vichafu, hiki kilikuwa kisafi sana kiasi mtu unaweza hata kutengewa
chakula na akala bila ya kuhisi kinyaa.

Nilitegemea wataweka ahadi yao kuwa ikiwa hawatakuta madawa ya kulevya
katika mizigo yangu watanirejeshea uhuru wangu wataniachia niende
nyumbani. Haikuwa hivyo. Wakanirudisha ofisini kwao. Sasa wakaacha
madawa ya kulevya wakahamia katika vitabu na "audio cassette"
nilzokuwa nimepewa kama zawadi kule Tehran wakaniluliza kwa nini
naingiza vitu vile khasa kanda za Khomeni na vitabu vyake nchini.
Nikawauliza, "Kwani kanda na vitabu vya Khomeni haviruhusiwi kuingizwa
Tanzania? Maana mimi hata nyumbani kwangu hii leo mkifika nina vitabu
vya Khomeni na wanafalsafa wengine kama Karl Marx ambao nimesomeshwa
pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam." Sasa hapo ikaja kejeli. "Ala wewe
mtu wa Kariakoo lakini umefika hadi Chuo Kikuu!" Sikujibu kitu. Awali
waliponitia mbarani waliniuliza kwetu na nikawaeleza kuwa nimezaliwa
Kariakoo.

Hawakunipa jibu kuhusu kuingiza vitabu na cassette za Khomeni. Ikawa
sasa kama vile wameishiwa maswali. Nikaona kuwa sasa ni zamu yangu
nami kuwapiga maswali. Yule aliekuwa akinihoji nikamwambia, "Mimi wewe
nakufahamu vizuri sana kwa sababu ukicheza mpira Simba Sports Club na
mie ni mpenzi wa club hiyo toka utoto wangu wakati huo ikiitwa
Sunderland na mmoja wa baba zangu alikuwa mchezaji marufu wa club hiyo
katika miaka ya 1950 akafiikia hadi kucheza Kombe la Gossage."
Nilihisi amepata mfadhaiko kidogo akanambia,"Unanifananisha yule
aliekuwa akicheza Simba ni ndugu yangu." Alikuwa anasema uongo lakini
mie nikamkubalia. Hapo nikajua kuwa nishampata sasa hana nguvu tena ya
kuuliza maswali. Kusema uongo ni dalili ya kujihami. Nikamrushia
kombora lingine, "Sasa tuhuma za madawa ya kulevya zimekwisha tuko
katika kwa nini naingiza vitabu vya Khomeni nchini?" Akanijibu
kinyonge, "Tumeridhika huna madawa." Kufika hapa tukawa tumemaliza
mahojiano.

Wakati huo sasa ni usiku wa manane na nishapeleka SMS kwa sahib yangu
mmoja bingwa wa mambo ya mtandao wa kompyuta kumjulisha kuwa
nimekamatwa uwanja wa ndege kwa tuhuma za uongo za kuvusha mihadarati
na yeye ile kuipata tu ule ujumbe wangu akaifahamisha dunia kuwa
nimekamatwa uwanja wa ndege nikitokea mkutanoni Iran na
nimebambikiziwa tuhuma za kuingiza nchini mihadarati. Waliponitia
mbaroni tu walinionya kuhusu kutumia simu yangu ya mkononi lakini
bahati nzuri hawakuninya'ganya. Aliyenipa onyo hili alikuwa mkuu wa
kituo cha polisi cha uwanja wa ndege. Huyu rafiki yangu akawa
kanisaidia sana maana hadi kumekucha wapenzi wangu wote ndani na nje
ya nchi pamoja na vyombo vya habari vinavyonifahamu walikuwa na
taarifa za kukamatwa kwangu. (Kwa kipindi takriban miaka ishirini
nyuma kwa nyakati fofauti nimekuwa nikifanya mahojiano na radio zote
muhimu kama, BBC, VOA, Sauti ya Ujerumani, Sauti ya Iran nk.).

Nikawaomba wale watu wa Usalama waniachie basi nende zangu kulala
nyumbani nirudi hapo kesho asubuhi kwa kuwa sikuwa nimebeba madawa ya
kulevya. Wakaniambia, "Itabidi tukulaze hapa hadi asubuhi wakubwa wetu
watupe amri ya kukuachia. Maana amri ya kukukakamata wewe imetoka
juu." [IMG]file:///C:/Users/MOHAME~1/AppData/Local/Temp/
msohtmlclip1/01/clip_image001.gif[/IMG]Sasa hapo ikawa nimelipata
jingine. Kumbe wauza unga hawakamatwi hadi amri itoke juu. Sasa kama
amri haikutoka ndiyo muuza unga atapita aingize sumu zake mitaani?
Hili likazidi kunidhihirishia kuwa kukamatwa kwangu hakukuwa na
uhusiano wowote na vita dhidi ya mihadarati bali ni vita vile vile
vikongwe dhidi ya Uislam.

Nikawa pale usiku kucha. Sasa wakati niko pale wakidhani nimelala.
Wakawa wenyewe kwa wenyewe wanazungumza kuhusu hii 'operation' neno
walilotumia ni kuwa 'leo tume-dial wrong number.' Wakawa wanasema,
"Huyu bwana mbona hakuelekea kama muuza unga tena huyu mtu bwana
kasoma kweli kweli" Wanadhani mie nimelala kumbe ni macho
nawasikiliza. (Vipi utalala katikati ya michongoma?). We umeona jinsi
alivyokuwa akijibu na kuchambua mambo." Hilo ndilo likawa gumzo lao
wakinisifia kwa ufasaha na mantiki lakini wakizungumza kwa sauti ya
chini kabisa. Hapa ikanidhihirikia kuwa hawa vijana walikuwa
wanatimiza wajibu wao wa kazi tu lakini kiini khasa cha kukamatwa
kwangu hawakuwa wanakifahamu.


Walionikamata walikuwa vijana kama wanne na wote walijitambulisha kwa
majina ya Kiislam. Nilijua ni waongo kwa kuwa Muislam anonekana katika
uso na katika matumizi ya lugha. Lakini yule mchezaji wa Simba ni
Muislam na yeye ndiye aliekuwa mkubwa pale akiongoza ile shughuli yote
tena kwa kujidai na kujifaharisha sana. Kisa kile kile cha mtumwa
anelimishwa na yule anefanya kazi za ndani nyumbani kwa bwana. Ila
kitu kimoja lazima nikiri. Wale vijana walikaa na mimi kwa wema na
hawakunibughudhi hata kidogo. Hata nilipokuwa nakwenda msalani kijana
alienisindikiza alinitaka radhi akasema, "Nakusindikiza kwa sababu ni
sheria lakini sisi tunakustahi kwa hiyo utuwie radhi kwa kukufuta hadi
msalani."

Asubuhi wakubwa wakaja kazini lakini hakuna alienikabili. Walikuwa
wakinichungulia kutoka mlangoni kama simba ndani ya kizimba kwenye
zoo, nami nikawa najifanya siwaoni. Ndipo akaja mkubwa mmoja tena
akaniita kwa jina langu na kwa heshima na bashasha sana, "Bwana
Mohamed tuwie radhi sana pamekuwa na makosa kidogo tuwie radhi sasa
hivi tutakuruhusu uende nyumbani. " Akatoka nje akawa akipiga simu.
Kisha akarudi ndani akaamrisha nibebewe mizigo yangu na gari la polisi
linirudishe nyumbani. Kistaarabu kabisa nikakataa gari ile huku
nikifanya maskhara kuwa naogopa gari ya polisi asijepiga simu akasema
mrudisheni huyo mtuhumiwa. Ofisi nzima ikacheka. Hapo ndipo wale
wakamataji wangu wa usiku wakabeba mizigo yangu nami nafuata nyuma
tunatoka nje ya uwanja.[IMG]file:///C:/Users/MOHAME~1/AppData/Local/
Temp/msohtmlclip1/01/clip_image001.gif[/IMG]

Kilichobaki sasa ni kueleza sababu ya mimi kukamatwa. Mwaka wa 2006
Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria kilifanya kongamano la kimataifa hapo
chuoni kwao kuzungumza kuhusu Ugaidi katika Afrika ya Mashariki na
Maendeleo ya Afrika (Conference on Islam, Terrorism and African
Development). Mimi ninlitoa mada iliyokuwa na anuani hii: Terrorism in
East Africa the Tanzanian Experience. Katika mada hii nilijikita
mahsusi katika kuisema Marekani kwa udhalimu wao duniani. Nikaeleza
kuwa huo udhalimu wao ndiyo unaopelekea wao kuchukiwa dunia nzima.
Hapa ningependa kufahamisha kuwa mkutano huu wafadhili wakubwa
walikuwa Iran na Marekani. Saudi Arabia ilikataa kuchangia mkutano
ule. Wakati nasema maneno haya ya kuwakanyaga wenyewe Waamerika wapo
hapo mkutanoni.

Baada ya kuwalani Waamerika sasa nikaigeukia serikali ya Tanzania na
kuishutumu vikali kwa kupitisha Sheria ya Ugaidi. Hapa nikaeleza kuwa
Waamerika wasione kuwa Tanzania imepitisha sheria hiyo ya ugaidi kwa
haraka kwa sababu Tanzania ina tatizo na ugaidi. Nikaeleza kuwa sheria
hiyo imepitishwa kwa sababu Bunge la Tanzania limehodhiwa na Kanisa na
kupitishwa kwa sheria hiyo hakuna uhusiano wowote na ugaidi ila
Wakristo wamepata fursa ya bure ya kupambana na Uislam wakitumia
serikali ya Marekani kama upawa wao wa kuopolea chinyango ya moto
kwenye chungu kinachotokota. Nikauchekesha mkutano kwa kuwaambia kuwa
Wamarekani wamefanywa wajinga na Kanisa kwa kuchonganishwa na Waislam
wa Tanzania ambao hawana ugomvi nao asilani. Baada ya kusema hayo
nikahitimisha kwa kueleza nguvu ya Waislam Tanzania, kwanza kwa wingi
wao na kisha kwa historia yao iliyotukuka iliyodumu takriban miaka mia
wakipambana na ukoloni wa Wajerumani kwa silaha (1905 1907), kisha
ukoloni wa Waingereza (1929 1961) na kuhitimisha kwa kuleta uhuru na
kuanzia 1961 hadi sasa wanapambana na nguvu ya kanisa katika kupiga
vita Uislam.

Kufikia hapa ukumbi ukawa umepata joto. Wanigeria wamesimama kutaka
niwaeleze vipi Waislam watakuwa wamepigania uhuru kisha wako wengi
nchini wanaruhusu wao kufanywa raia daraja la pili. Wakashangazwa kuwa
hata historia ya mashujaa Waislam waliopigana Maji Maji na kunyongwa
na wakoloni na mashujaa walipigania uhuru wa Tanganyika hawatajwi
katika historia ya ukombozi. Nilitoa majibu kadri Allah
alivyoniwezesha. Nakumbuka kitu kimoja walichosema wale ndugu zetu
Wahausa. Walisema hali hiyo iliyoko kwenu haiwezekani kutokea Nigeria
kwa kuwa hiyo itakuwa na sawa na kutangaza vita. Kisha
wakanihakikishia kuwa sheria hiyo ya ugaidi haitapitishwa Nigeria hata
siku moja.

Wapashaji habari wangu wakajanieleza baadae ni hili hitimisho langu
ndilo lililosababisha Wamarekani kuleta taarifa Dar es Salaam kutaka
taarifa zangu za "ugaidi" ikawa sasa sababu imeptikana ya mimi
kushughulikiwa na vyombo vya dola. Ndipo ikatengenezwa hadithi ya kuku
jike na ng'ombe dume (cock and bull story) kuwa Mohamed Said ni Mzungu
wa unga kwa hiyo akamatwe.

Mkasa huu ulinifika miaka sita iliyopita lakini hadi leo kovu la mkasa
ule limebaki katika pasi yangu. Sielewi pasi yangu inaonyesha nini
inapotiwa katika compyuta baada ya mkasa huu kwani kama mara tatu
husimamishwa kwa muda na kuombwa nitoe maelezo ya ziada kuhusu
niendako kila nisafiripo nje ya Tanzania. Nimeshuhudia hali hii Uwanja
wa Ndege Amsterdam na Detroit, Marekani. Berlin, Ujerumani niliambiwa
mzigo wangu umepotea lakini hata kabla sijatoka uwanjani nikatafutwa
na kukabidhiwa mzigo wangu na kwa hili sikuwa peke yangu nilikuwa na
mwenzangu, jamaa wa Kiarabu kutoka Misri. Sijui kama mizigo yetu
ilikuwa imebakishwa nyuma kwa upekuzi zaidi. Amsterdam, Uholanzi baada
ya kupita sehemu zote muhimu za upekuzi wakati naelekea kituo cha
mwisho niingie kwenye ndege inayoelekea Detroit, Marekani
nikachopolewa kutoka kwenye mstari na nikawekwa pembeni peke yangu kwa
usaili wa ziada. New York kadi yangu ya benki ilikataa kutoa fedha kwa
siku nzima hadi siku ya pili. Nilikujafahamishwa baadae kuwa "system"
ilikuwa inanichunguza kwanza. Ilikuwa siku ya pili baada ya kuonana na
maofisa wa benki ndipo kadi yangu ikaanza kutoa fedha. Geneva, Uswisi
kadi yangu ilikataa kutoa fedha katika mgahawa. Sikujua kama ni yale
yale au haya yalikuwa mengine. Lakini pasi hii afisa wa uhamiaji wa
Tanzania alipoiingiza kwenye compyuta yake alimwita mwenzake kuja
kutazama kisha wakawa wanacheka. Waliona nini kwenye pasi yangu Allah
ndiye ajuaye."

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment