Monday, 9 July 2012

[wanabidii] “FURSA YENYE TIJA: TAFAKURI YA UTUMISHI WANGU KAMA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA”

Na Dk Asha -Rose Migiro

Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo
moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa
tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu
maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii,
kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.

Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu
mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele
kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku
niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele
mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu
Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo
wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali
mbali zinazoikabili dunia yetu.

Utumishi wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa
uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati
kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na
madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia,
kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili
na udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine
nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za
pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake
katika kipindi cha mazingira magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto
za kipekee kabisa.

Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais
Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia
moyo na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa.
Familia yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na
kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.

Hapana shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha
kufahamiana kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu
mbali mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu
kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa
dunia.

Zaidi ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu
wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka
daima tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya
ziara zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya
kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto
sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde
nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa
kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya
mwanawe.

Maendeleo

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi
wa utendaji wa Sekretariati na kuimarisha uongozi wa Umoja Mataifa
katika medani za uchumi na maendeleo ya jamii. Majukumu ya Naibu
Katibu Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli
zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na
kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa.
Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan tulipoingia katika
utekelezaji wa dhana ya "Huduma ya Pamoja " (Delivering as One - DaO)
ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zetu hususan za maendeleo.

Kwa bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri
yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini.
Takwimu za kuaminika za hivi karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za
kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya
viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia moyo
licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko
wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na
majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha
malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo
yaliyokubaliwa kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha
wadau na washirika wetu wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na
mashirika ya biashara. Kwani wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo
kama kilingo cha msingi katika kutokomeza umaskini.

Katika kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya
milenia nilipewa jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa
kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ).
Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa
umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa
mara ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa
Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za
kisera na kifedha. Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji
wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.

Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika

Kwa mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la
Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika
(MDG Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki
kinajumuisha taasisi zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika
kuchochea kasi ya maendeleo ya Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza
kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo
hilo la viongozi. Baada ya miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo
hilo likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa mapendekezo kamambe ya
utekelezaji. Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa basi yatakuwa
nyenzo muhimu ya kuweka sera na mikakati madhubuti itakayosaidia
maendeleo katika nchi husika na duniani kwa ujumla. Napenda kutoa
mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.

Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba mwaka
2013. Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta
mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi
duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii nyingi
zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa
kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya
kupiga hatua madhubuti za kujiletea maendeleo stahimilivu na
yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.


Mkutano wa Rio + 20

Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta
usawa ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio
+20 uliomalizika hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia
katika kuandaa mfumo wa maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka 2015,
mwaka uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.
Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye
mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja
wa Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio
+20. Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika
masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi
zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba
maazimio ya mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo
stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha
kunakuwa na mustakabali mzuri kwa wanawake na wasichana.

Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia

Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20
tutawajibika kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta
usawa wa kijinsia. Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa
tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii.
Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na
wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za
kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza mamlaka
katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria
zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka
wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii. Ndiyo maana kwa
upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha
uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa kifupi kama "UN Women" mnamo
Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa kwa madhumuni
ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na
ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini
kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na
Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na
wasichana.

Huduma ya Pamoja

Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote
waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia
ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii
tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye
ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao
wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao
wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha
kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na
kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya "Huduma ya Pamoja" (Delivering
as One) Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango
muhimu sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa
nchi wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao
mkubwa katika kufanikisha dhana ya "Huduma ya Pamoja". Ni dhahiri
kwamba uwezo wa nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake
unakuwa imara zaidi pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za
Umoja wa Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau
wengine wa maendeleo. Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana
hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini
kwa dhati kuwa utaratibu wa kutoa "Huduma ya Pamoja" kupitia mpango
mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye tija.

Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa
yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia
mpango mmoja uitwao "Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia
Maendeleo" (United Nations Development Plan – UNDAP). Mpango huu
unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi
Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya
Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa
kujipima na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka
kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa
upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji kazi kwa pamoja
umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali chache
ambapo"ziada" iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za
maendeleo.

Afya ya Jamii

Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo wanaathirika
zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba
kila mwanamke na kila mtoto anakingwa na maradhi, hususan kuzuia
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu Ban Ki-moon, Michel
Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia mfano hai
wa jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na
mwanamke aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha
watatu waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni ya
Umoja wa Mataifa iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika
masuala ya afya ya mama na mtoto (Commission on Information and
Accountability on Women's and Children's Health) ambayo iliendeshwa
kwa umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na Waziri Mkuu Harper wa
Canada, nina imani kwamba jumuiya ya kimataifa hivi sasa imepata
mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji,
usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka
kwamba mfumo huu utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi karibuni.

Hali kadhalika, kazi nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde
Osotimehin, na Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Matokeo ya jitihada
za wenzangu hawa yalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Naibu
Katibu Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya
kazi zao yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika
lenye umuhimu mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia
sana katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani
kama hiyo nikiwa katika ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa
Montevideo, Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu Michelle
Bachelet, Helen Clark na Alicia Barcena, tulisimama kidete kuunga
mkono kampeni ya kitaifa ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa
wanawake.

Nilipozuru Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko
ambalo lilikuwa kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa
kipindi cha takriban karne moja, nilikutana na watu ambao walikuwa
wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia nzima, waliopata ulemavu
wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu hawa walikuwa
na nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na wa
wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru
Laos, ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na
wadau wengine wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa
ni pamoja na kuisaidia Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya
"cluster munitions".

Hii ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa
Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu
zote duniani ni mashuhuda na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa.
Kwa wanyonge na wahitaji walio wengi Shirika hili ni nguzo ya
kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za kujiletea maisha yenye
utu na heshima.

Mageuzi katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko

Ukweli huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu.
La hasha! Ndiyo maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza
kikamilifu kwenye kuboresha masuala ya utawala, uendeshaji na namna
tunavyofanya kazi. Ni wazi kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa
umebadilika kutoka chombo cha huduma za mikutano na kuwa mtendaji
mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa ushirikiano na
msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika
kuhamasisha mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni
pamoja na kujenga desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa
tija zaidi huku tukitumia rasilmali chache.

Ilitubidi pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa
yakijitokeza. Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na
njia ya mkato wala njia mbadala ya kuliimarisha Shirika letu na
kulifanya liwe la kisasa zaidi katika kutekeleza majukumu
yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda sambamba na
changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti,
misimamo tofauti na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama
wa Umoja wa Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi
ili kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba
raslimali chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.

Wafanyakazi ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila
tulipoendelea na jitihada za kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza
vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia fursa za
mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini. Ni jambo lililo
dhahiri kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu
yao katika mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara.
Tunafahamu, tena kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa
- "bendera ya bluu" - hivi sasa si kinga tena. Haituhakikishii
usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga wa
matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko
Abuja, Nigeria, ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na
shambulio la kigaidi la tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu
wanapotangulia mbele ya haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu
ya maisha. Ni faraja kubwa kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo
tuliyasimamia kabla ya kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha mchakato
wa kubaini namna bora ya kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na
familia zao.



Utawala wa sheria

Mojawapo ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga
kulinda haki za binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi
za kitaifa na kimataifa. Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele
suala la kuimarisha utawala wa sheria, hususan kufuatia umuhimu wake
katika ajenda za ujenzi wa amani (peace-building) na maendeleo
stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya
kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji
wa shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa
upande wao nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu
wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba
2012. Nia kubwa ni kuendeleza jitihada katika suala hili ili kukuza
heshima ya watu wote duniani na kujenga amani kati ya mataifa.
Hitimisho

Japokuwa muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia
tamati, naamini hakuna tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi
na maadili ya Umoja wa Mataifa. Ili mradi bado kuna umaskini duniani
na mahitaji ya chakula; bado kuna changamoto ya kutunza utu na heshima
ya binadamu na haja ya kuimarisha amani duniani basi hakika
nitaendelea kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya Umoja wa
Mataifa popote pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya
kukabiliana na changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na
ushirikiano wa karibu baina ya serikali, asasi za kiraia,
wafanyabiashara, mashirika ya hisani, taasisi za kitaaluma na watu
binafsi.

Aidha, ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa
na kiu ya kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani,
watauchukulia Umoja wa Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga
mustakabali wao.


Asha-Rose Migiro

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment