Friday, 1 November 2013

[wanabidii] DHORUBA ZA MUUNGANO NA UPOTOSHAJI WA TUNDU LISSU

"Serikali mbili ziliwezekana tu kwa sababu za uwepo wa Chama kimoja, Serikali mbili ziliwezekana tu kwa sababu tulikuwa na Utawala wa Kiimla, serikali mbili ziliwezekana kwa sababu tulikuwa na sheria ya kuweka watu kizuizini kwa kuhoji Muungano. Jambo moja baya kuhusu Muungano ni kuwa Wananchi wengi hawajui 'madudu' yake kwa kuwa maandishi na tafiti nyingi juu ya Muungano yako katika Lugha ya Kingereza, Nani anajua alipo Kassim Hanga (aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mara baada ya Mapinduzi)?, nani anajua alipo Abdulaziz K. Twala?, nani anajua alipo Mdungi?, nani anajua alipo Aboud Jumbe?, Muungano huu wa Serikali mbili uliwezekana kwa sababu tulikuwa na utawala wa kimabavu wa Mwalimu Nyerere."

Maneno hayo mazito yalitamkwa na Mheshimiwa Tundu Lissu, Waziri Kivuli wa Sheria na Mnadhimu Mkuu wa "Kambi Rasmi" ya Upinzani Bungeni wakati akitoa hitimisho lake siku ya Jumapili ya Oktoba 27 mwezi huu katika Mdahalo Maalum juu ya Mchakato wa Katiba Mpya uliopewa jina la "Tanzania Tuitakayo".

Mdahalo husika uliomhusisha pia Msomi kutoka Zanzibar Dk. Nassor Aboud Alley na kufanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam uliendeshwa na Mwandishi Rosemary Mwakitwange na kurushwa hewani na Vituo vya ITV na Radio One.

Mdahalo huo uliofana sana, ulijadili mambo mbalimbali yaliyohusu mchakato wa Katiba mpya, Muundo wa Muungano na nafasi ya wananchi na vyama vya siasa katika Bunge la Katiba, japo Mwakilishi wa Serikali katika mdahalo huo, Anjela Kairuki hakutokea kwa sababu ambazo hazikuelezwa.

Nilisikiliza mdahalo husika kwa kina, baada ya kuyatafakari yaliyonenwa kwenye mdahalo nami nimeona niseme machache kutokana na hayo yaliyozungumza. Niseme tu kwamba kwa kirefu machache yangu haya yatajikita, pamoja na mambo mengine, kwenye hilo hitimisho la Mwanasheria mbobezi Tundu Lissu katika mdahalo ule.

DHORUBA ZA MUUNGANO NA UWEPO WA CHAMA KIMOJA

Ziitwazo dharuba za Muungano ni matukio mbalimbali ya mikinzano na mikingamo juu ya masuala kadhaa ya Muungano ambayo kilele chake kilikuwa ni "kulazimishwa kujiuzulu" nafasi zote uongozi, ndani ya Chama na Serikali, kwa Mwalimu Aboud Jumbe Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Ni tukio hilo la mwaka 1984 ambalo lilizalisha kitabu cha Mwalimu Jumbe "The Partnership: Miaka 30 ya Dhoruba" kilichotolewa mwaka 1994 ambacho kwa kirefu kilijikita kwenye kuzieleza hizo dhoruba za Muungano ndani ya hiyo miaka 30 (1964-1994) ya Muungano.

Kitabu husika ni mawazo ya Mwalimu Jumbe juu ya Uzoefu wake serikali, misingi na migongano ya kisheria juu ya Muungano na hata kadhia mbalimbali juu ya kuongezwa mambo ya Muungano kutoka yale 11 yaliyo kwenye Hati ya Muungano.

Miongoni mwa kadhia hizo ni pamoja na Kitendo cha Rais Nyerere na Rais Karume, waliokuwa waasisi wa Muungano huu, kukaa kwa kipindi cha Mwaka mmoja wakiwa hawapikiki chungu kimoja na hawasemezani. Rais Nyerere akitaka kuongea na Rais Karume anamtumia Bhoke Munanka na Rais Karume akitaka kuongea Rais Nyerere anamtumia Mwalimu Aboud Jumbe.

Matukio na kadhia kama hayo na nyengine za aina hiyo ndizo ambazo kwa kirefu zinaonyesha dhoruba ambazo nyenzo hii ya kuendeleza Umoja wetu (Muungano) ilikumbana nazo na ikapita salama.

Tukio la Mwalimu Aboud Jumbe kuondolewa madarakani kupitia vikao vya Chama kwa sababu ya misimamo yake juu ya Muungano lina mengi ndani yake ambayo hayasemwi, kubwa kati ya hayo ni dhamira ya Mwalimu Jumbe juu ya misimamo hiyo "iliyoonekana kuzuka ghafla" juu ya Muungano.

Historia inamuonyesha Mwalimu Jumbe kama mtetezi mkuu wa Muungano na mtu ambaye ameufikisha Muungano huu hapa ulipo. Ni yeye ambaye aliishi Tanganyika (Mara) kwa muda mrefu zaidi akimsaidia Rais wa Muungano majukumu mbalimbali ya kuendesha nchi huku akiiacha Zanzibar ikiongozwa na Waziri Kiongozi, Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki. Ni Mwalimu Jumbe ambaye aliunganisha Chama chake cha ASP na Tanu cha Nyerere na kuasisi CCM.

Wakati wa kuundwa kwa Muungano huu Vyama vya siasa havikuwa katika moja ya mambo ya Muungano, hivyo vyama vya ASP na TANU bado vilibaki kama vyama tawala katika pande mbili za Muungano kwa muda wa miaka 13 ya mwanzo ya Muungano (1964-1977). Hivyo kauli ya Tundu Lissu kuwa Muungano huu wa Serikali mbili umedumu kwa sababu ya uwepo wa Chama kimoja si sahihi sana kwa kuwa hakukuwa na Chama kimoja kwa muda wa miaka 13 ya mwanzo ya Muungano na bado Muungano ulidumu.

Dalili za kutokudumu kwa muundo wa muungano tulionao sasa ambazo zimejitokeza hazitokani na kukosekana kwa uwepo wa chama kimoja bali ni kwa sababu ya kupuuzwa kwa haja ya maboresho ya muungano huu kwa miaka nenda rudi, ushirikishwaji mdogo wa wananchi, muundo husika kutokuwa wa haki na usawa nk.

Kwa hali ya sasa ilivyo hata kama bado kungekuwa na chama kimoja bado tishio la kutokudumu kwa Muungano lingekuwepo tu, maana hata tishio la kuvunjika Muungano lililokuwepo mwaka 1984 halikuweza kutokuwepo hata pamoja na uwepo wa hicho chama kimoja.

Tukio la kushindwa kwa hoja juu ya Muundo wa Muungano wakati ule wa kadhia ya Mwalimu Jumbe si kwa sababu ya uwepo wa Chama kimoja bali ni kwa kuwa hoja husika haikujengwa na dhamira safi katika wakati ule. Madai ya kina Jumbe yalijificha nyuma ya dhamira chafu ya kutaka Zanzibar yenye Mamlaka zaidi kwa lengo la "kutaka kujipa uwezo" wa kuwadhuru vijana wapenda mabadiliko (Frontliners) na si kuwapa Wanzanzibari fursa zaidi.

Katika Mdahalo husika alikuwepo pia Mzee wetu Njelu Kasaka, Kiongozi wa Wabunge 55 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Tanganyika ambao waliibua hoja ya kutaka uwepo wa Serikali ya Tanganyika katika muundo wa Muungano Bungeni. Kundi hilo ni maarufu zaidi kama G55.

Tukio la kuzuiwa kwa Wabunge hawa kutimiza dhamira yao hiyo na Mwalimu Nyerere linatajwa kama msingi mkuu wa kuonyesha nguvu za Chama kimoja katika kudumisha Muundo wa Muungano uliopo sasa kwa mabavu. Lakini wajengao hoja hiyo hawatuonyeshi kwanini sasa ambapo kuna vyama vingi tofauti hakujaibuka kundi la wabunge hata nusu ya idadi hiyo ya G55 kutoka Tanganyika ambao wangejenga hoja juu ya kuihuisha Tanganyika katika muundo wa sasa wa Muungano.

Kwangu kuzuiwa kwa G55 kilikuwa ni kitendo cha busara na hekima zaidi kilichowahi kufanywa na Mwalimu Nyerere. Dhamira ya G55 haikujengwa juu ya haja ya kuboresha na kujenga Muungano wa haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar bali ni juu ya mhemko wa kitendo cha Zanzibar kujiunga na OIC. Hapakuwepo na hali ya kupelekea "muafaka" bali kulikuwa na hali ya kutaka kukomoana, na hoja ile ingeruhusiwa wakati ule tusingekuwa na Muungano huu adhwimu sasa.

Hivyo hapa hoja ya kuwa kilichozuia ni chama kimoja si sahihi, kwa kuwa wakati husika tayari tulikuwa na vyama vingi, na wabunge hao wa G55 walipewa fursa ya kujiunga na vyama vingine ambavyo vitakuwa na sera ya kuihuisha Tanganyika tofauti na CCM.

"KINA LUMUMBA WETU"

Mwaka 1969, raia kadhaa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao waliwahi kuwa Viongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano "walipotezwa" (kuuawa) kidhalimu katika mazingira ya kutatanisha.

Raia hao ni pamoja na Abdullah Kassim Hanga, Abdulaziz K. Twalla, Saleh Sadalla, Othman Sharifu Mussa na Mdungi.

Siku kadhaa zilizopita, wakati wa maadhimisho ya miaka 14 ya Kifo cha Mwalimu Nyerere niliandika makala katika gazeti la "Sura ya Mtanzania" iliyokuwa na kichwa cha habari "Nyerere aliokoa maisha yetu" (Makala husika pia inapatikana hapa kwenye wall yangu kwa kwa kichwa cha habari "Nyerere alituokoa"). Kwa kirefu makala husika ambayo ni sehemu ya masimulizi ya Komredi Ali Sultan Issa kutoka katika kitabu "Race, Revolution and Struggle for Human Rights in Zanzibar: Memoirs of Ali Sulatn Issa & Maalim Seif Sharrif Hamad", imeeleza juu ya matukio yawahusuyo raia hao wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliopotezwa (kuuawa) kwa dhulma na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makala husika ilieleza jambo moja lililo dhahiri, kuwa kuuawa kwa hao wote hakukuwa ni kwa sababu walikuwa wanapinga Muungano, bali ni kwa sababu walikosana na Karume (wengine hata kabla ya Mapinduzi) na baadhi ya wajumbe wa kamati ya watu 14.

Abdallah Kassim Hanga alikuwa adui kwa Sheikh Abeid Amani Karume kama alivyokuwa adui Oscar Salathiel Kambona kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Uadui huo haukuwa ni kwa sababu wawili hao (Hanga na Kambona) walipinga Muundo wa Serikali mbili wa Muungano wetu bali ni kwa kuwa walikuwa tishio kwa utawala wa Karume na Nyerere.

Siamini kama Tundu Lissu haijui historia hii ya mauaji ya kidhalimu ya "Kina Lumumba Wetu" hawa, Abdallah Kassim Hanga, Mdungi, Othman Sharifu Mussa na wenzao, kiasi cha kuyahusisha mauaji haya na suala la kupinga Muundo wa Muungano huu wa Serikali mbili usio wa haki na usawa, naamini lengo lilikuwa ni upotoshaji ili kufikia matlaba.
"KIZUIANI": UBAYA WA SHERIA NA MAZINGATIO YA MAZINGIRA NA NYAKATI

Mara baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe Mwinyi pamoja na Wasaidizi wake kama Aboud Maalim na Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki, aliwekwa kwa muda katika makazi maalum Kigamboni, Jijini Dar es salaam kwa lengo la kujiepusha na "athari za ushawishi wake kwenye utulivu wa siasa za Zanzibar".

Msaidizi wake mwengine, Dk. Bashiru Kwaw Swanzy (Mwanasheria aliyeandaa waraka wa Jumbe uliovujishwa na kusababisha kung'olewa kwake) aliwekwa "kizuizini" kwa muda na kisha kuvuliwa kabisa Uraia (Ikumbukwe kuwa Kiasili Swanzy alikuwa ni Mghana mwenye mafungamano makubwa na Zanzibar tokea harakati za Uhuru) na kisha kupelekwa uhamishoni nchini Uingereza.

Baadaye Mwanasheria Wolfango Dourado naye aliwekwa kizuizini kwa sababu hiyo ya kuuzumza hadharani msimamo wake juu ya kupinga muundo wa Muungano huu wa Serikali mbili.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment