Friday, 17 June 2016

[wanabidii] Re: KISA CHA OMBAOMBA WA KIZUNGU NA MAFISADI WA KITANZANIA

Bwana Muhingo, umenena!

Huwa ninapata shida sana sana kuielewa jamii yetu ya Kitanzania. Ninadhani sasa umewadia wakati muafaka wa kukitafuta kitabu cha Bwana. Shaaban Robert kiitwacho  KUSADIKIKA.


Sote tukisome, labda kitatusaidia kujielewa. Hasa hasa hawa wanasiasa wenzetu. Wanaopigania haki ya kuchinja mbuzi wa kafara kwa kisu cha kuazima. Mwenye kisu kakipiga butu , kabla ya kuwakabidhi , halafu jiwe la kukinolea kalificha!   Anawaeleza kuwa miaka yote hicho kisu hukitumia kwa namna hiyo hiyo.  Kukitumia kukata kebeji au embe haileti shida.

Lakini jaribu kukitumia kukata muwa au kuchununia ngozi ya kiboko, thubutu labda uwe na maguvu ya Goliathi.

Hawa wanasiasa wenzetu walikaa na kisu kwa muda mrefu sana wakijaribu kwa kila namna kumchinja mbuzi, lakini kwa ubutu wa kisu haikuwezekana. Fikara ya kutafuta namna ya kukinoa haikuwahi kuwajilia akilini.

Wakawa wakiimba mapambio ya chinjaaa chinjaaa chinjaaaaaa! Lakini kafara halifanikiwi kwa kuwa mbuzi yupo hachinjiki.

Kaja Bwana mwenye manguvu , kakishika kisu na sasa kaanza kumchinja mbuzi, damu yaanza kutoka maana ile ngozi ya kwanza ya nje imekatwa sasa kisu kinatafuta koromero.

Wenzetu wanakamata upupu na kumwagia Bwana mwenye manguvu machoni, wakidai kwamba uhalali wa kumchinja mbuzi wa kafara ni wao! Yeye Bwana manguvu aende ulingoni akatwangane kule , mtu mmoja atawezaje kumchinja mbuzi aliyewashinda watu hamsini?  Haiwezekani, lazima apuliziwe upupu machoni. 

Ati kuchinja mbuzi wa kafara hakuhitaji namna ile ya Bwana manguvu, ati lazima kisu kiwe na makali ya kutosha. Kwa hiyo mbuzi asubiri hadi pale jiwe la kunolea litakapopatikana.  Ati kinyume cha hapo , huyu mbuzi hatendewi haki ingawa juzi tu , mbuzi huyu huyu kamaliza hekta kadhaa za ngano ya wananchi!

Huwa tunatahadharishwa sana na makadhi , masheikh , pamoja na makasisi ya kuwa kafara ni bora isifanyike kabisa au itekelezwe kwa ukamilifu. Ikitekelezwa nusu nusu, hatima yake kwa wanajamiii huwa ni mbaya mara kadhaa!  Ghazabu ya muagiza kufanyika kafara huwa kuu mnooo, kwa kuwa kuitimiza nusu ni dharau yenye kubeba kufuru! 

Swali laja. Nchi yetu inahitaji kafara litolewe kikamilifu.  Baadhi yetu tunaandamana ati kisu kilichotushinda wao kumchinja mbuzi aloteuliwa kwa kafara kisitumike na Bwana manguvu ambaye ana uwezo wa kukitumia hivyo hivyo kukamilisha kafara yenye nia ya kulikomboa taifa letu. Hawa ni wenzetu kwenye kutoa kafara au wanataka kutuletea balaa kwa kumzuia Bwana manguvu aliyekisha anza kumchinja mbuziiiiiiiiii?



Tutafakari !



On Friday, 17 June 2016 20:39:59 UTC+1, ELISA MUHINGO wrote:

Nimezaliwa na kukulia Tanzania. Nimekutana na jamii za watu mbalimbali. Moja ya jamii niliyowahi kukutana nao ni Ombaomba. Kukutana na wanamama wana baba vijana na watoto wakiombaomba mijini ni jambo lililozoeleka. Nimetembea kwa muda mfupi mfupi nje ya Afrika. Nako nimekutana na ombaomba. Kwanza nilikuwa nakutana na Ombaomba wa kiafrika. Kwangu niliona kawaida. Niliona ni kawaida watu kuomba. Kisanga kikanikuta siku moja mtaani New York. Nikakutana na ombaomba kadhaa wa kizungu. Kwanza haikuingia akilini. Kadri nilivyoendelea kushangaa ikawa inakuwa wazi kuwa hao ni ombaomba. Nikasikia ukakazi! Nikaona Huruma! Nikasikia 'bunyugwizi'. Nikatamani kuwapatia msaada utakaowasaidia kuondoka mitaani kuombaomba. Nikiwa natafakari hilo nikarudi Hotelini kwangu na kuwasimulia wenzangu. Nikakutana na mmoja anayeshangaa kama mimi. Lakini mwenzetu mwingine akatushangaa. ''Kwa nini mnashangaa mzungu kuombaomba?'' Tukagundua kuwa TUNASHANGAA KWA SABABU HATUKUZOEA! Tulijiona wajinga.

Napenda sana kulinganisha hali hiyo na hali inayoendelea hapa Tanzania.
Hata kabla ya wanasiasa kubeba agenda ya ufisadi na Rushwa; wananchi walishaanza kuchoka. Rushwa imetapakaa kila mahala. Kila sehemu zinakotoka huduma muhimu. Polisi, mahakama, Hispitali na kwingineko. Tulikuwa tunaelekea kufikia mahala ambako Rushwa inakuwa MILA ya Tanzania.

Ufisadi nao ulianza kuzoeleka. Watanzania wanafahamu kuwa garama za umeme ziko juu kwa sababu ya ufisadi. Wahuni fulani wameweka 'cha juu' kwenye capacity Charges. Watanzania wanajua kuwa reli yetu imekuwa inang'olewa ili wenye magari ya kubeba mizigo waweze kubeba mizigo. Wanajua kuwa ni kwa sababu hiyo bidhaa nyingine ziko juu. Watanzania wanajua mengi ambayo mtu mmoja anaumiza wengi ili anufaike yeye.

Watanzania wamezoea kuambiwa huduma za jamii haziwezi kuboreshwa kutokana na mapato kidogo. Wanahimizwa na watawala kuwa waongeze uzalishaji. Mapato ya serikali yamekuwa yakiongezeka lakini wimbo kuwa bado nchi ni maskini ndiyo maana hospitali hazina madawa umeimbwa. Watanzania wanaona ongezeko la idadi ya viongozi kama mawaziri, mikoa, wilaya kila mwaka. Pengine watanzania wanasema fulani kateuliwa kama fadhira kwa sababu alimsaidia kiongozi kuingia madarakani.
Watanzania wamezoea. Wamezoea kuona viongozi wa kisiasa wakiongezewa mapato lakini wafanya kazi wakisota na mapato kiduchu. Mbunge kazi yake kukaa bungeni. Analipwa sitting allowance. Za nini!? Hakuna maswali.

Kilichotokea kuwapoza watanzania ni wanasiasa wa vyama vya upinzani kuyabeba na kuyatoa kwenye mikutano ya hadhara. Watanzania wakatulia. Wakawa na matumaini.

Tukafanya uchaguzi. Tukampata rais. Akaanza kuyashughulikia matatizo yaliyowakandamiza watanzania myaka yote hiyo. Watu wakaanza kurudisha matumaini. Angalau waliowaibia wanaanza kushughulikiwa. Watu waliokuwa wanakwepa kodi wanaanza kubanwa. Wamebanwa na wengine wakalipa. Watumishi serikalini wanaanza kufanya kazi kwa woga na ndio mwanzo wa kurudisha nidhamu. Wanyonge wanaanza kuwa na matumaini na kutarajia hata wale mafisadi papa watafikiwa.
Mara wanajitokeza watanzania wenzetu wanaanza kumsonga Rais. Wengine ni wanasiasa walikuwa wakiimba wimbo huu. Tena wanasema Rais anatekeleza sera zao. Halafu wanaanza kumgeuka. Wanasema anavunja haki za binadamu. Kwa nini? Watu wanaohisiwa wamesimamishwa kazi ili kuchunguzwa. Wanataka awaache waendelee kuiba. Watu wanaovurunda kazi wanaondolewa kwenye nafasi za uteuzi. Ukiangalia sana unaona ni kwa sababu watu hawa walizoea kuwaona wanyonge wengi wakipata mateso. Lakini sio wakubwa wachache ambao wanaishi maisha ya ajabu huku wanyonge wakiteseka. Wengine wanasema hakuna haja ya kuwakamata mafisadi au kuwabana wakwepa kodi. Tuweke mifumo itakayozuia ufisadi huo. Wanashindwa kuelewa kuwa mfumo upo na ukitumika utazuia ufisadi. Sababu ya ufisadi ni kutotumika mfumo wala sio kukosekana mfumo. Mfumo ni huu unaotumika kuwabana. Wote wanaoshangaa hatua zinazochukuliwa na Rais na kumlaumu wanahitaji kujua kuwa shida yao ni moja tu: KWA SABABU HAWAKUZOEA! Kuzoea kuona mafisadi papa wakichukuliwa hatua. Kuzoea kuona wafanyabiashara wakubwa wanabanwa wanapokwepa kodi. Kuzoea kuona waziri anavuruga anatimuliwa. Mfumo wowote kama hautasimamiwa hakutakuwa na mabadiliko. Tukubaliane. Sheria itendewe kazi na tufumbe macho kama hatuwezi kuvumilia kuona ikifanya kazi.
Elisa Muhingo
 
 --
 
 Send Emails to wana...@googlegroups.com
 
  
 
 Kujiondoa Tuma Email kwenda
 
 wanabidii+...@googlegroups.com  Utapata Email ya
 kudhibitisha ukishatuma
 
  
 
 Disclaimer:
 
 Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility
 for any legal consequences of his or her postings, and hence
 statements and facts must be presented responsibly. Your
 continued membership signifies that you agree to this
 disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 ---
 
 You received this message because you are subscribed to the
 Google Groups "Wanabidii" group.
 
 To unsubscribe from this group and stop receiving emails
 from it, send an email to wanabidii+...@googlegroups.com.
 
 For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment