Sunday 26 June 2016

[wanabidii] Chonde waheshimiwa! Mlipofika mtawasusa pia wananchi

WALIANZA kwa kumsusia Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na sasa wametangaza kuwasusa na wabunge wenzao wanaotoka chama tawala. Ama kweli! Itafika siku, wakigundua wananchi ambao hawakuwapigia kura kwenye uchaguzi mkuu, nao watasuswa.

Ngoja nikumegee kilichofanya niseme haya yote. Katika gazeti moja la kila siku, habari ya wabunge hao wa Ukawa kususa, ilipewa ukurasa wa mbele. Wakamnukuu mbunge mmoja (ambaye sina haja ya kumtaja) ambaye hata hivyo hadi sasa najiuliza, tangu lini amekuwa msemaji wa Ukawa?

Yawezekana hayo ndiyo mabadiliko ndani ya umoja huo, wameamua demokrasia ishike nafasi, kila mtu awe msemaji. Kama mbunge angekuwa amejitungia, kwa maana kwamba si msimamo wa wao, kwa vyovyote vile ungetolewa ufafanuzi.

Mbunge huyo alimwambia mwandishi wa gazeti hilo kwamba, maazimio ya Ukawa yaliyofikiwa hivi karibuni, wameamua kuwasusa wabunge wa CCM kuonesha dunia kwamba wanapinga hatua ya Serikali kuwanyima uhuru wa kuzungumza kinyume na katiba ya nchi.

Alinukuliwa na gazeti hilo akisema: Leo tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.

Mbunge huyo aliendelea kusema, "Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu."

Alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge Ukawa hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti. Kilichoendelea kuniacha mdomo wazi, ni nukuu hii "Si katika michezo tu, hata katika masuala ya uhusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana uhusiano wa kimapenzi na wabunge wa CCM usitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo."

Msimamo wa kutoshirikiana na wabunge wa CCM katika michezo ya aina yoyote na hata masuala ya kijamii kama vile uhusiano, umeniacha kinywa wazi, maana sijui itakuwaje kwa wachumba na wenye ndoa. Nimebaki nikijiuliza maswali mengi juu ya uamuzi huu.

Nilianza kwa kutoamini kama huo ndiyo msimamo wa kambi hiyo ya upinzani. Kikubwa kilichonishawishi nisiamini kuwa ni msimamo wao, ni ukweli kwamba bungeni hakuna mtoto; kwa maana hakuna mbunge mwenye umri chini ya miaka 18.

Nilizingatia ukweli kwamba, ndani ya kambi ya upinzani, wamo wasomi, wenye uwezo wa kuchambua mambo, watu wazima, viongozi wa dini, wacha Mungu na hata wabobezi wa masuala mbalimbali. Hata hivyo nashawishika kuamini kuwa huo ndiyo msimamo wao.

Maana kama ingekuwa gazeti limewanukuu isivyo, ingetolewa kauli ya kukanusha na kumruka mbunge huyo aliyenukuliwa. Awali sababu ya kumsusia Naibu Spika ilitokana na uamuzi wake wa kutokubali suala la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), lijadiliwe bungeni.

Mwongozo huo ulianzia kwa mbunge wa chama tawala na kisha kuboreshwa na wa upinzani. Hata hivyo baada ya Dk Tulia kutolea nje mwongozo, Ukawa waliamua kulibeba wenyewe. Bila shaka wametimiza siasa za kuwahiana. Tangu awali, ususaji ulimlenga Naibu Spika.

Sasa kilichonishangaza ni kuona wakiwageukia wabunge wenzao. Haikuelezwa bayana kisa cha kuwaunganisha wabunge wa CCM kwenye 'kesi' ya Naibu Spika. Au ni kwa sababu walishabikia wanaosusa wasilipwe posho?

Sina jibu juu ya hili zaidi ya kuona suala hili ni zaidi ya siasa, usanii, bali linaelekea kwenye 'utoto'. Inawezekana neno 'utoto' likaleta ukakasi ndani ya vichwa vya baadhi ya watu. Lakini ukweli ndiyo huo, kwa sababu wameondoka kwenye msingi wa harakati zao na kuanza kushika huku na kule.

Ikumbukwe hoja yao ilikuwa kwamba Dk Tulia atakapoendesha kikao, watasusa isipokuwa vitakavyoendeshwa na wenyeviti pamoja na Spika Job Ndugai. Sasa kama wamepanua wigo na kuwatenga wenzao wa chama tawala alhali wakifahamu Bunge lina kambi mbili tu, je watakuwa tayari kurudi bungeni ambako watakutana na spika, wenyeviti na wabunge wa CCM?

Kama ni swali la msingi limeulizwa na mbunge wa CCM, je mbunge wa upinzani atakuwa na swali la nyongeza? Si atakuwa ameshirikiana na 'asiyempenda'. Bila kujali kama wana hoja au la, mtindo huu wa kususa kiholela hauwezi kuwaletea matokeo makubwa.

Wakijikita kwenye 'kushinikiza,' wakasahau kwamba, wakati mwingine ushawishi ni mbinu nyingine inayoweza kufanikisha harakati zao, basi wataendelea na ususaji usio na matunda.

Wanapowabagua wenzao wa chama tawala, (ambao ndiyo wengi), je wanatarajia ni lini matakwa yao yataungwa mkono bungeni pale inapohitaji kufanyika uamuzi? Wanapokuja na uamuzi wa kushawishi hata kwenye uhusiano wasusiane, wanatarajia nini kama si utoto? Je haitafika siku, wakasusa hata asilimia 61 ya wananchi waliokiingiza chama tawala madarakani?

Wanasiasa wetu wanapaswa kukumbuka kuwa yapo maisha nje ya siasa na vyama wanavyotumikia. Kitendo cha kutangaza kuvunja uhusiano kwa misingi ya vyama, si cha kushabikia. Inaweza kufika hatua utengano huo ukaingia miongoni mwa wafuasi na hatimaye kwa wananchi wote na kuvunja umoja wa kitaifa.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment