Monday, 27 June 2016

[wanabidii] Ma-RC na Ma-DC wateule ‘sasa kazi tu’

RAIS wa Awamu ya Tano, John Magufuli juzi aliwateua wakuu wa wilaya 139 na wakuu wa mikoa watatu ili kukamilisha safu yake ya serikali kuu, tayari kwa kuliingiza taifa hili katika uchumi wa kati.

Wapo wakuu wa wilaya wapya 78 huku wa zamani waliobakizwa katika nafasi zao wakiwa 39. Tunapenda kuungana na Watanzania wenzetu, kuwapongeza wakuu wa wilaya wapya na wa zamani pamoja na wakuu hao watatu wa mikoa kwa kuteuliwa na Rais kumwakilisha katika nafasi hizo muhimu za uongozi wa nchi yetu.

Tunaamini kwamba kwa kufanikiwa kupita katika chekeche hadi kufikia hatua hiyo, viongozi wetu hao wana kila sababu ya kujisikia wana bahati kubwa ya kuaminiwa na Rais kiasi cha kuwateua katika nafasi hizo.

Katika taarifa ya kuteuliwa kwao, tumefahamishwa kwamba miongoni mwa wakuu wa wilaya walioteuliwa, wapo 22 ambao awali walikuwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri. Tumefahamishwa kwamba kuteuliwa kwao, kunatokana na kazi nzuri walizokuwa wanafanya katika nafasi zao za awali.

Sisi tunaamini kwamba timu hii ya kazi, itazingatia kwa makini malengo na maelekezo ya serikali yao ya Awamu ya Tano inayonuia kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati kwa kutumia rasilimali lukuki tulizonazo, ikiwa ni pamoja na suala zima la kukuza viwanda.

Tunadiriki kusema kwamba sasa timu nzima ya serikali imekamilika, kilichobaki ni kuhakikisha kwamba viongozi hao na wenzao waliokwisha teuliwa kabla yao, kushirikiana na wananchi katika kulijenga taifa letu kupitia kauli mbiu maarufu katika awamu hii ya 'Hapa Kazi Tu.'

Nchi yetu imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, ikiwa ni pamoja na ardhi nzuri kwa kilimo, mifugo, mbuga za wanyama, madini, mito, bahari, mafuta na gesi ambapo kwa kiwango kikubwa, hatujazitumia ipasavyo kuweza kujikwamua katika lindi la umasikini tulinalo.

Hakuna ubishi kwamba kama kila mmoja wetu, ataazimia kwa vitendo kuchapa kazi kupitia hizo rasilimali zetu, tutaweza kufikia uchumi wa kati kama viongozi wetu wa awamu hii wanavyopania. Hakuna namna ya kuweza kufikia ustawi na maendeleo bila kujipanga na kusimamia malengo kwa vitendo.

Hapa tunapenda kuwakumbusha tu kwamba baada ya kupata Uhuru wetu Desemba 9, 1961, Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya mambo matatu ikiwa ni pamoja maradhi, ujinga na umasikini.

Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania bado tunapambana na vita, hivyo hadi leo pamoja na ukweli pia kwamba viwango vya enzi hizo kwa kiasi fulani, vimepungua ukilinganisha na hali tuliyonayo sasa. Lakini ni ukweli pia kwamba tuna kila sababu ya kuongeza juhudi katika vita hivyo kwa sababu rasilimali tunazo na uwezo wa kukabiliana na vita hivyo ipasavyo tunao.

Tunaweza kusema kwa kujidai kwamba wakati sasa umefika wa kuunganisha nguvu na mshikamano wetu kwa kuchapa kazi ili kujiletea ustawi na maendeleo yetu. Kulifanikisha hilo, hatuna budi kuachana na mambo yanayoashiria kutuletea utengano na mfarakano kwa misingi ya vyama, itikadi, ubaguzi, dini na jinsia. Mungu Ibariki Afrika! Mungu Ibariki Tanzania!

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment