On Monday, 4 January 2016, 15:17, Camillus Kassala <cdnkassala2002@yahoo.co.uk> wrote:
Heri ya Mwaka Mpya 2016!
Tangu tuanze kuimba, kunukuu na kurejea kauli mbinu ya serikali ya awamu ya tano, "Hapa ni Kazi Tu!", sijui ni wangapi wetu wamechukua muda na kutafakari kwa undani maana, athari na yatokanayo na kauli mbiu hii. Mimi nimejaribu, na sasa napenda kuwashirikisha.
Tukianza na jinsi ambavyo imetafsiriwa kitaifa, tumeona kuwa inapewa maana zifuatazo (orodha yangu si kamili!):
1) Kupiga vita uvivu, uzembe, uchelewaji kazini, na kutomaliza kazi uliyopewa; na kutekeleza amri za viongozi mara moja.
2) Kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuongeza mapato kwa kufuatilia ulipaji kodi stahiki, kuziba mianya ya kodi, ushuru na tozo za aina mbalimbali.
3) Kutofanya mzaha na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na nchi.
4) Kumaanisha kwa vitendo kile ambacho kimeamuliwa, kimepangwa na kimwekewa msimamo.
Kama maana hizo ni sahihi, tuangalie athari zake, na athari hizo ni matokeo ya kile ambacho nakiita 'kujikongoja kwa vijana, na baadhi ya watu wazima, kiakili, kitabia na kimahusiano' katika kufanya maamuzi ya kuitikia wito wa kauli mbiu hiyo. Athari hizo ni kama ifuatavyo:
1) Kushtushwa na kupigwa bumbuwazi kutokana na kauli za viongozi wanaotoa amri zinazoendana na mtazamo wa 'Hapa ni Kazi Tu!".
2) Kuona shida au kupata ugumu katika kuondokana na mazoea ya kuwa na maisha tegemezi yaliyo rahisi na yasiyowajibika kigharama na kimalipo.
3)Kuona aibu na kujaribu kuifunika au kuondoa hiyo aibu, kwa njia yoyote ile, inapogundulika mhusika kavunja sheria, kanuni na taratibu za nchi.
4) Kupinda maamuzi, mipango au misimamo ili iwanufaishe watu wachache, kama vile wenye vyeo, pesa na wanamitandao ya wakubwa.
Baada ya kuangalia maana na athari za kaulimbiu ya "Hapa ni Kazi Tu!", napendekeza kuwa yafuatayo ndiyo yatokanayo na maana na athari hizo:
1) Kusubiri kupewa amri, maagizo na maelekezo kwa hofu kuwa mtu asije akafanya kitu, ingawa ni cha kisheria au ni halali kwa kanuni na taratibu zilizopo, ambacho watoa amri za 'Hapa Kazi Tu!' hawakukifikiria.
2) Kiwango cha juu cha maisha kushuka kutokana na kufidia gharama au kodi au tozo ambazo zililimbikizwa na sasa lazima zilipwe katika muda mfupi, hata kama uwezo hauruhusu.
3) Mgongano kati ya viongozi wa siasa na wanataaluma (kama vile wanasheria, wahandisi, mameneja, madaktari, waalimu, wachumi, n.k.) unaotokana na namna tofauti ya kufikiri kati ya wanasiasa (wenye haraka ya matokeo ya mamlaka yao) na wanataaluma (wanoufuata mantiki za taaluma zao ambazo haziangalii matakwa ya mtu).
4) Watendaji kuogopa kutekeleza, au kuchelewesha utekelezaji wa, amri za "Hapa ni Kazi Tu!'" hasa pale amri hizo zinawaathiri wakubwa, vigogo, wenye pesa, wenye 'heshima' ai hadhi fulani!
Katika yote hayo, vijana wetu leo wanajifunza nini kitakachwaandaa kwa miaka mitano, kumi, kumi na tano, .... ijayo?
TAFAKARI!
CDNKassala
0 comments:
Post a Comment