Monday 28 April 2014

[wanabidii] HOTUBA YA RAIS KATIKA HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA UJENZI WA JENGO LA TATU LA ABIRIA JNIA

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA UJENZI WA JENGO LA TATU LA ABIRIA JNIA, 24 APRILI, 2014

Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi,
Mheshimiwa Waziri wa Fedha,
Waheshimiwa Manaibu Waziri,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam,
Mheshimiwa Balozi wa Uholanzi,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Mheshimiwa M/kiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani,
Waheshimiwa Makatibu Wakuu,
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali,
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege,
Mkurugenzi Mkuu na Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege,
Watendaji Wakuu kutoka Taasisi mbali mbali zilizoalikwa
Wadau wa Sekta ya Usafiri wa Anga,
Muwakilishi wa Benki ya HSBC,
Mtendaji Mkuu Benki ya CRDB,
Waandishi wa habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,


Ndugu wananchi na wageni waalikwa,

Kwanza kabisa nimshukuru Waziri wa Uchukuzi na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunialika katika hafla hii ya kihistoria ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huu muhimu wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Nichukue fursa hii pia kuupongeza Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi, Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya za kundeleza miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini.

Ndugu wananchi na wageni waalikwa,

Kuanza kwa ujenzi wa mradi huu ni muendelezo wa mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Nne kama zilivyoianishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa kuendeleza na kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege.

Tunafanya hivyo tukijua kuwa Usafiri wa Anga ni usafiri wa leo, kesho na keshokutwa, nchi haiwezi kupata maendeleo kama hakuna usafiri wa Anga. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kiwanja hiki kinakua na kutoa fursa kwa watanzania kwenda popote wakitokea hapa kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaongezea uwezo zaidi wa kufanya biashara.

Ndugu wananchi na wageni waalikwa,

Katika sekta ya huduma (service industries), viwanja vya ndege ni kati ya wawezeshaji na watoa fursa namba moja. Kama tunavyofahamu Kiwanja hiki ndio lango kuu la watu kuingia na kutoka nchini. Kwa mfano, mwaka jana 2013, Kiwanja hiki kilihudumia wasafiri i zaidi ya milioni mbili na nusu. Hivyo ni matarajio yangu kwamba kuboreshwa kwa kiwanja hiki kutaongeza uwezo wake wa kuhudumia abiria wengi zaidi na kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine hususan sekta ya utalii ambayo inachangia kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa. 

Kukamilika kwa mradi huu wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja hiki cha Julius Nyerere kitakuwa kichocheo cha uchumi kwa taifa na nchi jirani na hivyo kuvutia wawekezaji wengi wa nchi za nje pamoja na wafanyabiashara kuleta ndege zao kubwa zaidi. Jengo litakuwa kivutio kwa abiria kutokana na miundombinu yake kuwa ya kisasa zaidi. Na zaidi ya hapo mradi utaongeza ajira kwa watanzania. Nimeambiwa kuwa wakati wa ujenzi mradi utakuwa na wafanyakazi zaidi ya elfu moja na utakapokamilika kiwanja cha ndege kitaongeza ajira kutoka 4000 wa sasa hadi 6000. Rai yangu kwenu wananchi ni kuwa mchangamkie fursa za kibiashara na kiuchumi zinazotokana na uwepo wa jengo hili jipya.




Ndugu wananchi na wageni waalikwa,

Mradi huu ni muhimu sana kwa uchumi na taswira ya nchi yetu na ambao watanzania wameusubiri kwa miaka mingi, hivyo Wizara ya Fedha ihakikishe fedha za ujenzi zinapatikana na mradi uendelee na kukamilike kama ilivyopanga. Wizara ya Uchukuzi kupitia Viwanja vya Ndege ihakikishe mradi huu unasimamiwa vizuri kwa muda, kwa na kwa gharama zenye tija.

Napenda kuwakikishia kwamba, jitihada hizi za Serikali hazitaishia katika kiwanja hiki cha Julius Nyerere tu bali ni lengo letu kuona kwamba kila Mkoa unakuwa na kiwanja cha ndege angalau kwa kiwango cha lami na kufungwa taa na vifaa vyote muhimu ili kuweza kutoa huduma saa 24 katika kipindi chote cha majira ya mwaka. Vilevile tutaendelea kujenga majengo ya abiria mazuri na ya kisasa yatakayowafanya abiria kukaa na kupata huduma bila matatizo katika viwanja vyetu.


Ndugu wananchi na wageni waalikwa,

Sote tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kukua kwa sekta ya usafiri wa anga hapa nchini, hivyo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege unapaswa kwenda sambamba na ukuaji huo. Katika kipindi cha awamu ya nne Serikali imefanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kukamilisha kwa kiwango kikubwa miradi ifuatayo:-
(a) 
(b) Ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Songwe chenye uwezo wa kuhudumia ndege ya ukubwa wa abiria ya 150 kwa majira yote ya mwaka ambacho kimeanza kutumika na kurahisisha usafiri kwa mikoa ya Mbeya, Njombe,Iringa, Rukwa na nchi jirani.


(c) Ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mpanda kwa kiwango cha lami ambacho kinaweza kuhudumia ndege ya ukubwa wa kubeba abiria 70 kwa majira yote ya mwaka.

(d) Ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Kigoma kwa kiwango cha lami ambacho kitakapokamilika kitaweza kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 150 kwa majira yote ya mwaka.

(e) Ukarabati na upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha katika kiwanja cha ndege cha Tabora ambacho sasa kinaweza kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 70 kwa majira yote ya mwaka.


(f) Ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba kwa kiwango cha lami ambacho kwa sasa kinauwezo wa kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 50 kwa majira yote ya mwaka.

(g) Kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mafia kwa kiwango cha lami ambacho kinaweza kuhudumia ndege za ukubwa wa kubeba abiria 50 kwa majira yote ya mwaka. Kutokana na jiografia ya Mafia kukamilika kwa kiwanja hicho ni ukombozi kwa wananchi. Katika hali ya mvua nyingi zinazonyesha mwaka, kama hatungefanya uboreshaji huo, Mafia ingetengwa kabisa na dunia kwani ndege zisingetua.

Utekelezaji wa miradi hii yote ni kuhakikisha kuwa wananchi wanasafiri kwa urahisi na haraka zaidi na pia kuwawezesha kufanya biashara kwa ufanisi zaidi ili kuinua vipato vyao.


Ndugu wananchi,
Dhamira hii nzuri ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya viwanja vyetu vya ndege haitaweza kufanikiwa bila kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi hasa wale waishio jirani na maeneo ya viwanja hivi. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote ambao walikuwa wakazi wa eneo hili la Kipawa na Kigilagila ambako leo mradi huu unafanyika, kwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Serikali kwa kukubali kuhama kutoka katika eneo hili kupisha upanuzi wa mradi huu. Natoa rai kwa wananchi wa maeneo mengine ambayo yatahitajika kwa miradi kama hii ya kimaendelea kuiga mfano wa wenzao wa Kipawa na Kigilagila.

Lakini hata baada ya miundombinu hii ya viwanja kukamilika bado tunahitaji ushirikiano wa wananchi katika kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inalindwa na mipaka yake haivamiwi. Nichukue nafasi hii kutoa tahadhari kwa wale ambao wamekuwa na tabia ya kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege kwa lengo la kutegemea kulipwa fidia waache tabia hiyo, vinginevyo Mamlaka husika zisisite kuwachukulia hatua za kisheria na kuwaondoa mara moja watu kama hao.

Natambua kwamba tatizo hili la uvamizi wa maeneo ya viwanja kwa kiasi kikubwa linachangiwa na utaratibu uliokuwepo kwa miaka mingi wa kuyaacha maeneo haya bila hati miliki. Nafurahi kusikia kwamba Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeliona tatizo hilo na kuamua kulitafutia ufumbuzi kwa kufuatilia hati miliki ya maeneo hayo yalitotengwa kwa viwanja vya ndege ambapo kwa sasa viwanja vya Julius Nyerere, Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Musoma, Moshi, Tanga na Kigoma tayari mchakato wa hati miliki umekamilik. Tafadhali mchakato huu uendelee kwa viwanja vyote na naziagiaza Mamalaka husika za Ardhi kutoa ushirikiano katika kufanikisha suala hilo.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Kuhusu changamoto zinazowakabili katika uendeshaji wa viwanja vya ndege, napenda kuwapongezeni Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na taasisi zote zenye jukumu la ulinzi na usalama kwa kusimamia suala la udhibiti wa upitishaji wa madawa ya kulevya ambapo kwa kiasi kikubwa limedhibitiwa.

Pamoja na mafanikio haya ni muhimu viwanja vya ndege vikatoa huduma bora zaidi ili viweze kushindana na viwanja vingine duniani kwa kuweka taratibu za uendeshaji na menejimenti zinazolingana na viwanja vingine vya kimataifa. Hivyo naagiza Wizara zote zenye taasisi katika viwanja vya ndege kushirikiana kuweka kanuni na taratibu zitakazoondoa changamoto nyingi na misuguano ya uendeshaji wa viwanja vya ndege .


--

Yona Fares Maro

Institut d'études de sécurité - SA


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment