HOJA NA MAONI YETU WAISLAMU JUU YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA
KUPITIA SEMINA SHIRIKISHI ZA MTANDAO WA MISIKITI TANZANIA
SEHEMU YA I: UHUSIANO WA SERIKALI, DINI NA MASHIRIKA YA KIDINI
NA. | HOJA | MAONI |
1 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na uhalali wa mamlaka ya Mwenyezi Mungu | Katiba mpya itambuwe kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na Mamlaka yake juu ya Wanaadamu (kwa mnasaba huu, wananchi wa Tanzania |
2 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui uhalali wa Sheria za Mwenyezi Mungu. Hii inajidhihirisha kwa kauli ya serikali kutokuwa na dini. | Katiba mpya iweke wazi kutambua kwake uhalali wa sheria za Mwenyezi Mungu na kuziheshimu. Maana ya serikali kutokuwa na dini iainishwe na kuwekwa wazi kikatiba. |
3 | Kwamba Katiba iliyopo inamlazimisha mtu kufuata sheria zote hata kama zinakwenda kinyume na imani ya dini ya raia husika. | Katiba mpya isimlazimishe mtu kufuata taratibu au sheria ambazo inakwenda kinyume na imani yake na hivyo kupelekea kuvunja sheria za dini yake. |
4 | Kwamba Katiba iliyopo haitoi tafsiri yakinifu juu ya maana ya ibada na dini. Tafsiri sahihi ya maneno dini na ibada ni muhimu ili kuzuia bughudha kwa wananchi wanapokuwa katika matendo ya dini na ibada. | Katiba itoe tafsiri yakinifu ya ibada na dini kwa mujibu wa tafsiri ya dini husika. |
5 | Kwamba Katiba iliyopo inatenganisha mamlaka ya nchi na mamlaka ya dini. Huu ni mfumo Kristo. | Katiba mpya iruhusu kuchanganya mamlaka ya nchi na ya dini. Mfano uwepo wa Mahakama ya Kadhi itakayoendeshwa kwa hazina ya serikali. |
6 | Kwamba Katiba iliyopo imetoa tafsiri potofu ya neno HALALI. Kwa mfano neno rizki halali linajumuisha mathalani hata rizki ipatikanayo kwa kuuza pombe na kucheza bahati nasibu ni halali. | Katiba mpya itoe tafsiri sahihi ya neno HALALI kwa mujibu wa imani ya dini na tafsiri hiyo iwe ni yenye kukubalika kiutendaji na katika mahusiano baina ya mwananchi wa dini husika na wananchi wengine nje ya dini husika. |
7 | Kwamba Katiba iliyopo haiilazimishi serikali kuitambua siku ya Ijumaa kama siku rasmi ya ibada kwa Waislamu. Hii inasababisha usumbufu mkubwa kwa Waislamu kutekeleza ibada hii hususan wafanyakazi na wanafunzi. | Katiba mpya itambue na kuipa heshima siku ya Ijumaa kuwa ni siku maalum ya ibada kwa Waislamu. Hivyo shughuli zote za serikali zisimamishwe wakati wa kutekelezwa ibada hiyo. |
8 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi. Hii imepelekea Waislamu kutohukumiana kwa sheria za Kiislamu ambayo ni sehemu ya ibada kwao na vile vile kukosekana kwa msimamizi wa haki inapotea mzozo baina ya Waislamu. | Katiba mpya iruhusu na itambue uwepo wa mahakama za kadhi zitazoendeshwa chini ya usimamizi wa Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu wataokao chaguliwa na Waislamu kwa kuzingatia sifa za kielimu katika fani ya sheria ya Kiislamu na kutambuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. |
9 | Kwamba Kutokana na Katiba iliyopo kutokutambua mahakama ya kadhi ajira rasmi za makadhi hazipo. | Katiba mpya itambue uwepo wa tume ya ushauri wa uteuzi wa makadhi na ajira ya makadhi kwa mahakama za kadhi Tanzania ambayo kikatiba itaitwa Tume ya Utumishi ya Mahakama ya Kadhi. Tume hii itachaguliwa na Waislamu. Wajumbe wa Tume hiyo watakuwa wafuatao: 1. Kadhi Mkuu ambaye atakuwa mwenyekiti kutoka bara au visiwani; 2. Naibu Kadhi Mkuu ambaye atakuwa naibu Mwenyekiti kutoka bara au Visiwani; 3. Kadhi mmoja wa Mahakama ya Kadhi ya Rufaa atakayechaguliwa na Waislamu; 4. Wajumbe watatu kutoka mahakama ya kadhi. |
10 | Kwamba suala la kugharimia uendeshaji wa mahakama za kadhi linapaswa liwe jukumu la serikali kupitia mfuko wa hazina ya serikali. Hii kwa sababu Waislamu ni sehemu ya walipa kodi. Kama walivyo raia wengine, wanastahili kufaidika kutokana na kodi wanazolipa. | Katiba mpya iilazimishe serikali kugharimia gharama za kuendesha mahakama za kadhi na gharama za watumishi wote kutoka kwenye mfuko wa hazina ya serikali. |
11 | Kwamba Mahakama ya Kadhi haipaswi kuingiliwa na mahakama ya aina yoyote isiyohukumu kwa sheria ya Kiislamu. Kwamba upo umuhimu wa kuunda kwa Mahakama ya Rufaa ili kusikiliza kesi za rufaa kutoka kwenye mahakama ya kadhi. | Katiba mpya itambuwe uwepo wa Mahakama ya Rufaa ya Kiislamu. |
12 | Kwamba Waislamu kwa sheria zilizopo wanakwazika katika kutekeleza dini yao kikamilifu. Inawawia vigumu kutekeleza sheria kwa mnasaba wa dini yao. Kufuata sheria za Kiislamu ni sehemu ya dini na ibada ya lazima kwa Muislamu, haki ambayo katiba iliyopo imetoa uhuru. | Katiba mpya itambue haki ya Waislamu kutekeleza nakufuata sheria ya Kiislamu katika ukamilifu wake. Katika sehemu zenye Waislamu wengi sheria ya Kiislamu ifuatwe katika ukamilifu wake. Kila Muislamu katika maeneo haya atalazimika kuhukumiwa kwa sheria za Kiislamu. Katika maeneo yenye Waislamu wachache mahakama za kadhi ziwahukumu Waislamu katika sheria zote za Kiislamu isipokuwa za jinai. |
13 | Kwamba Katiba iliyopo haitoi muongozo juu ya ushirikiano baina ya serikali na dini au madhehebu ya dini, hali iliyopelekea kuwepo kwa malalamiko ya kuwepo kwa upendeleo maalum unaoneemesha Ukristo (hususan Ukatoliki) hususan katika sekta ya elimu na afya kwa kutumia hazina ya taifa. Mathalani kwa kupitia mkataba wa ufahamiano [MoU] baina ya serikali na kanisa serikali hutenga mamilioni ya fedha za umma kila mwaka kunufaisha mipango ya afya na elimu ya kanisa. | Katiba mpya iweke uthibiti wa matumizi ya fedha za umma kwa utaratibu wa upendeleo wa madhehebu ya dini yoyote ama kinyemela au kwa njia ya urasimishaji kupitia mikataba au makubaliano. |
SEHEMU YA II: MASUALA YA MUUNGANO NA SERIKALI YA MUUNGANO
NA. | HOJA | MAONI |
14 | Kwamba Katiba iliyopo inatambua uwepo wa serikali mbili katika Jamhuri ya Muungano, jambo ambalo limesababisha utata na kero kubwa ya muungano hususan kwa upande wa serikali ya Zanzibar. Yapo malalamiko kwa upande wa Zanzibar kuwa wameporwa madaraka ya kiinchi (sovereignity) na serikali ya muungano. Hii imepelekea mpaka baadhi yao kudai muungano uvunjwe. | Katiba mpya itambue uhalali wa serikali tatu: Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano. |
15 | Kwamba Katiba iliyopo inaainisha tu maeneo ya muungano ambao chimbuko lake ni makubaliano baina ya viongozi wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar bila ridhaa ya wananchi wa pande mbili hizi. Hali hii imepelekea malalamiko kwamba wananchi hawakuhusishwa. | Katiba mpya iweke utaratibu utaofanya masuala yatakayokubalika kuwa ya muungano yapitishwe kwa kura ya maoni (referandum) kwa kuzingatia uwiano wa sehemu hizi za muungano. Kila upande ukubali masuala hayo kwa asilimia 75 au zaidi ya wananchi wake ndipo yaingizwe katika orodha ya maeneo ya Muungano |
16 | Kwamba Katiba iliyopo iko kimya juu ya mgawo wa madaraka ya rais na naibu rais, mawaziri, manaibu waziri kutoka pande mbili za muungano. Hii imepelekea Wazanzibari kulalamika kwamba huenda muda mrefu rais wa jamhuri ya muungano akatoka bara tu. | Katiba mpya iweke utaratibu utakaowezesha cheo cha rais wa jamhuri ya muungano kiwe cha kupokezana baina ya pande mbili za muungano yaani Tanganyika na Zanzibar. Vyeo vya mawaziri na manaibu mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na makatibu wakuu wasaidizi katika serikali ya muungano vitolewe kwa uwiano uliosawa. Mathalani waziri akiwa mtanganyika naibu wake awe mzanzibari. |
17 | Kwamba Katiba iliyopo haikuweka wazi mgao wa maliasili baina ya pande mbili za muungano. Hii imepelekea kuwe na mvutano kwamba iwapo mafuta yatapatikana yawe ni ya muungano au la. | Katiba mpya iweke wazi kwamba mali ya asili kama vile madini, gesi na mafuta n.k. havitakuwa katika masuala ya muungano. Kila upande mmoja wa muungano uwe unamiliki mali ya asili yake. |
18 | Kwamba Katiba iliyopo iko kimya kuhusu mahusiano ya serikali ya Zanzibar katika medani za kimataifa kwa maeneo yasiyo ya muungano. Hii imepelekea kuwepo kwa malalamiko upande wa Zanzibari kuwa hawanufaiki na wanabanwa kuwa na mahusiano na nchi na taasisi nyingine za kimataifa, mathalani kujiunga na OIC ambayo ingesaidia utekelezaji miradi ya mambo yasiyokuwa ya muungano. | Katiba mpya iweke utaratibu za kuziwezesha pande zote mbili za muungano (Tanganyika na Zanzibar) kuwa na mahusiano na mashirikiano na serikali za nje na taasisi za kimataifa bila pingamizi kutoka kwenye serikali ya muungano. |
19 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui kuwepo kwa Mahakama Kuu ya Katiba. Hii imepelekea kukosekana kwa suluhusho la utata unapojitokeza wa masuala mbali mbali ya muungano na mengineyo. Mathalani, utata wa Zanzibar kama nchi kamili au vinginevyo unashindwa kupewa ufumbuzi wa kisheria. | Katiba mpya itambue uwepo wa Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itakuwa na uwezo na nguvu za Kisheria za kutafsiri vipengere mbalimbali vya Katiba vyenye utata na pia kubatilisha sheria yoyote itakayotungwa ambayo inapingana na Katiba. |
20 | Kwamba Katiba haitambui kuwepo kwa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Katiba ambayo itahusika na kesi za rufaa kutoka Mahakama Kuu ya Katiba. | Katiba mpya itambue uwepo wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Katiba. |
21 | Kwamba Katiba iliyopo iko kimya juu ya nafasi ya Spika na Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Tangu kuasisiwa kwa muungano nafasi hizo zimekuwa zikihodhiwa na watanganyika. Hii imepelekea kuwa ni moja ya kero kubwa za muungano. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kupokezana nafasi ya spika na naibu spika baina ya sehemu mbili za muungano. Yaani spika akiwa mtanganyika naibu wake awe mzanzibari. Nafasi hizo zibadilishwe kila baada ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. |
22 | Kwamba Katiba iliyopo inamtambua Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kama viongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Waziri mkuu kwa utaratibu wa sasa hana shughuli na mamlaka yakinifu upande wa Zanzibar. Cheo hiki si muafaka kwa hivyo kisiwe katika muungano. | Katiba mpya itambue kuwepo kwa mawaziri wakuu kwa kila upande wa muungano kama wakuu wa shughuli za serikali zao. Kisiwepo cheo cha waziri mkuu wa serikali ya muungano. Shughuli zake zifanywe na makamu wa rais wa serikali ya muungano, ambaye ndiye msaidizi mkuu wa rais katika serikali ya muungano |
23 | Kwamba Katiba iliyopo iko kimya juu ya uwezekano wa kuvunjika muungano. | Katiba iweke utaratibu wa kuvunjika kwa muungano iwapo itatokea dharura ya jambo hilo na ianishe sababu zinazoweza kupelekea kuvunjika kwa muungano. |
24 | Kwamba Katiba iliyopo hairuhusu chama cha siasa chenye lengo la kuvunja muungano na chenye lengo la kutumia nguvu au mapambano kufikia malengo ya siasa. | Katika kudumisha uhuru wa maoni chama chochote hata kama kina malengo ya kuvunjwa muungano kiandikishwe endapo kinaona kuna maslahi kwa wananchi juu ya hilo na kwamba kuvunjika kwa muungano ndiyo njia iliyobaki ya kuondoa dhuluma. Chama kiruhusiwe kutumia nguvu kufikia malengo ya kisiasa endapo njia ya amani na mazungumzo imeshindikana kuondoa dhuluma. |
25 | Kwamba Katiba iliyopo hairuhusu kusajili chama cha siasa chenye wafuasi katika upande mmoja tu wa muungano au kuendesha shughuli zake katika upande mmoja tu wa muungano. | Katiba mpya iruhusu kuwepo kwa chama cha namna hiyo. Hii itatoa uhuru kamili kwa raia wa pande mbili hizi kutoa maoni na kutetea maslahi na maendeleo yao hata kama ni wachache [bila kujali idadi yao] |
SEHEMU YA III: HADHI NA MADARAKA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA
NA. | HOJA | MAONI |
26 | Kwamba Katiba iliyopo inampa rais hadhi na mamlaka makubwa kiasi cha kuwa juu ya sheria (asiyeweza kushitakiwa) kwa kosa la aina yoyote akiwepo madarakani au hata akiwa nje ya madaraka | Katiba mpya iruhusu rais kufunguliwa mashtaka kwa kosa lolote akiwa ndani au nje ya madaraka. Hii itasaidia katika uwajibikaji wa rais na kuzuia ufisadi na ubadhirifu wa mali za wananchi kwa kutumia madaraka aliyopewa na wananchi. |
27 | Kwamba Katiba iliyopo imempa mamlaka Rais kutoa misamaha kwa watenda kosa lolote. | Katiba mpya isimpe Rais madaraka ya kutoa msamaha kwa kuwa hili linapelekea kuingilia maamuzi ya mahakama. |
28 | Kwamba Serikali haizingatii uwiano wa kidini katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini na vyombo vyake (viongozi na watendaji waandamizi). Hii inapelekea kuwepo hisia za upendeleo na udini. | Katiba mpya iweke masharti ya kuzingatia uwiano wa kidini kwa wateuzi katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali (viongozi na watendaji waandamizi serikalini) kuondoa hisia za kuwepo upendeleo wa kidini. |
29 | Kwamba Katiba iliyopo inampa madaraka rais kuchagua mawaziri kutokana na wabunge waliochaguliwa na wananchi. Hii imepelekea wabunge kushughulikia maslahi ya majimbo yao zaidi kuliko maslahi ya kitaifa. | Katiba mpya iweke wazi kuwa baraza la mawaziri halitatokana na wabunge waliochaguliwa na wananchi, Rais achague mawaziri kama watendaji wa serikali nje ya bunge. Mawaziri waingie bungeni kama wawakilishi wa serikali na siyo wawakilishi wa majimbo na serikali kama ilivyo sasa. |
30 | Kwamba Katiba iliyopo inampa madaraka makubwa rais kiasi cha kuwaweka watu kizuizini bila kufikishwa mahakamani. Huu ni uvunjifu wa haki za binaadamu. | Katiba mpya isimpe madaraka rais, mkuu wa Mkoa na wa wilaya ya kumuweka mtu kizuizini bila kufikishwa mahakamani. Katiba mpya isimpe rais mamlaka ya kimahakama. |
31 | Sheria imempa madaraka rais kuteua watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kuondoa Rushwa. Hii imepelekea Taasisi hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na kuingiliwa utendaji wake na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kuteuliwa watendaji wa TAKUKURU na Bunge na bila kuingiliwa utendaji wake na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. |
32 | Katiba iliyopo inampa madaraka rais kuteua Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Hii imepelekea kuwepo kwa malalamiko ya kutokuwepo tume huru ya uchaguzi. Kwamba kwa ajili hii matokeo ya uchaguzi wa rais pindi yanapotangazwa na tume ya uchaguzi hayawezi kuhojiwa mahakamani. | Katiba mpya itoe madaraka kwa bunge badala ya rais kuteua Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Katiba mpya vilevile itoe fursa kwa raia kuhoji matokeo ya uchaguzi ya rais mahakamani. Mahakama na sio tume ya uchaguzi kiwe ndicho chombo cha kuthibitisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa rais. |
33 | Kwamba Katiba iliyopo inampa madaraka rais ya kulivunja bunge. Hii ni kuwanyima haki wananchi ya kuendelea kuwa na viongozi waliowachagua kwa ridhaa yao. | Katiba mpya isimpe mamlaka rais kulivunja bunge. |
34 | Kwamba Katiba iliyopo inampa madaraka rais ya kuteua Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Jaji wa Mahakama Kuu na Jaji wa Mahakama ya Rufaa bila ya idhini ya bunge. Hii imepelekea kuwepo kwa malalamiko ya mahakama hizo kutokuwa huru katika kutekeleza majukumu yake. | Katiba mpya iweke utaratibu wa uteuzi wa nyadhifa hizo uwe kwa kushauriana Rais na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuidhinishwa uteuzi huo na bunge. |
SEHEMU YA IV: UWAKILISHI WA RAIA KATIKA MIHIMILI MIKUU YA DOLA
NA. | HOJA | MAONI |
35 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui umuhimu wa kuwepo wawakilishi wa dini katika vyombo vifuatavyo: Bunge, Baraza la Wawakilishi, na Baraza la Madiwani, Mabaraza ya Usalama. Hii inapelekea kufanywa maamuzi ambayo yako nje na maadili na sheria za dini husika. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kuwepo uwakilishi wa dini katika vyombo hivyo vilivyotajwa kwa ajili ya kulinda maadili na maslahi ya dini husika. |
36 | Kwamba Katiba iliyopo inaruhusu mtu kujitangaza kufaa kwake katika kugombea uongozi na hivyo kupelekea mazingira ya rushwa na uongo. Hii imepelekea wanasiasa kujipachika sifa na uwezo wasio nao. | Katiba mpya iweke utaratibu wa wananchi kupendekeza wagombea kupitia vyama vya siasa au vikundi maalum (wagombea binafsi) ili kupigiwa kura. Wananchi wapendekeze na wawanadi wapigiwa kura. |
37 | Kwamba Katiba iliyopo inamzuia raia yeyote kugombea uongozi katika nafasi yoyote mpaka awe ni mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa. Hii inawanyima raia wasio wanachama wa vyama vya siasa kushiriki katika shughuli za uongozi na bila shaka kuzuia wenye sifa za kuongoza taifa kwa kigezo cha kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa. | Katiba mpya itoe nafasi kwa mgombea binafsi kugombea katika nafsi zote za uongozi kwa sharti ya kupendekezwa na kundi la watu raia wa Tanzania wasiopungua kumi na moja. |
38 | Kwamba Katiba iliyopo inapiga marufuku kuwepo wa vyama vya kisiasa vya kidini. | Katiba mpya iruhusu uwepo wa vyama vya kisiasa vya kidini kama ilivyo katika nchi nyingine mathalani Ujerumani. |
39 | Kwamba Katiba iliyopo inapiga marufuku kuandikishwa chama cha siasa chenye malengo ya kutetea maslahi na maendeleo ya dini. Hii inatoa tafsiri potofu ya dini kutorandana na siasa | Katiba mpya iruhusu kuandikishwa chama cha kisiasa chenye lengo la kupigania haki, maendeleo na maslahi ya imani ya dini husika. Katiba itambue uhalali wa raia kupigania maslahi na maendeleo ya dini yake. |
40 | Kwamba Katiba iliyopo inatambua mgawanyo wa nchi katika mikoa na wilaya n.k. kiutawala. Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanateuliwa na rais. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kuigawa nchi katika majimbo yatayoongozwa na serikali za majimbo zitakazochaguliwa na wananchi. Mkuu wa jimbo achaguliwe na wananchi. |
41 | Kwamba Katiba iliyopo inaruhusu kuwepo kwa viti maalum vya wanawake bungeni kwa misingi ya jinsia. Yamekuwepo malalamiko ya kwamba baadhi ya wanaoteuliwa kwa kigezo cha jinsia hawana sifa na uwezo wa kuongoza na kwamba watu wa jinsia ya kiume hawapewi upendeleo na kwamba ipo hatari ya kuzuka mfumo jike (kama Kenya inakoelekea). | Katiba mpya ifute uwakilishi kupitia viti maalum katika bunge kwa misingi ya jinsia. Mtu achaguliwe kwa sifa za kiutendaji na siyo jinsia yake. |
42 | Kwamba Yapo malalamiko dhidi ya wabunge kutowajibika katika majimbo yao na hakuna utaratibu unaowawezesha wapiga kura kuwaondoa wabunge hao. Kwamba wabunge hawana makazi katika sehemu wanazoziwakilisha. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kuwawezesha wapiga kura kuwadhibiti na kuwawajibisha wabunge wao ambao hawatekelezi wajibu wao ipasavyo. Katiba mpya iwawezeshe wapiga kura kuwaondoa wabunge wasiotekeleza ipasavyo wajibu wao bila kusubiri kipindi cha uchaguzi mpya. Katiba iweke masharti ya mbunge kuwa na makazi katika jimbo analoliwakilisha. |
43 | Kwamba Katiba iliyopo inatambua kuwepo kwa uchaguzi mdogo wa mbunge pindi zinapotokea sababu mbalimbali kama vile kufariki kwa mbunge n.k. Hii imepelekea taifa kugharimika sana kwa ajili ya chaguzi hizi. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kujaza nafasi ya mbunge inapokuwa wazi. Nafasi ya mbunge ijazwe mathalani kwa utaratibu wa chama husika au kikundi husika kumteuwa mwanachama au mtu mwingine kurithi nafasi ya mbunge aliyeondoka. |
44 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui uwepo wa serikali ya mseto. Hii inapelekea serikali kuundwa kwa uwakilishi wa watu wachache na hivyo kukosa sifa ya serikali ya umoja wa kitaifa. | Katiba mpya iweke utaratibu wa kuunda serikali ya mseto. |
SEHEMU V: HIFADHI NA MATUMIZI YA ARDHI NA RASILIMALI ZA TAIFA
NA. | HOJA | MAONI |
45 | Kwamba Katiba iliyopo imempa haki mtu ya kumiliki na kutumia mali zake atakavyo bila kuchunga sheria na imani ya dini yake au za watu wengine. (Mathalani mtu kurithithisha mali yake atakavyo yeye kinyume na sheria ya dini yake) | Katiba mpya iweke bayana haki ya mtu kumiliki na kutumia mali yake kwa kuzingatia sheria ya imani ya dini yake. |
46 | Kwamba Katiba iliyopo haizungumzii umuhimu wa sensa katika kujua takwimu za watu. Hii imepelekea kutolewa takwimu zisizokuwa rasmi na zenye malengo ya upotoshaji. | Katiba iitake serikali kufanya sensa baada ya kila miaka mitano kujua idadi ya watu, hali zao na idadi ya wafuasi wa dini mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kuweka uwiano katika kutoa haki sawa na huduma kwa raia wake. |
47 | Kwamba Katiba iliyopo imetoa mwanya kwa ardhi yetu kutumika kwa malengo ya ukoloni mamboleo. Mathalan haitoi pingamizi kwa mataifa ya nje kuweka vituo vya kijeshi na upelelezi katika ardhi ya Tanzania. | Katiba mpya isiruhusu kwa hali yoyote kuwekwa kwa vituo vya kigeni vya kijeshi na upelelezi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. |
48 | Kwamba Katiba iliyopo imeimilikisha ardhi kwa serikali yaani kikatiba ardhi ni mali ya serikali. Hii imepelekea serikali kuwa na mamlaka ya kumilikisha ardhi kwa yeyote bila ridhaa ya wananchi, hata kama ikiwa wanaomilikishwa ni wageni. Imerahisisha pia uporwaji unaofanywa na wageni (mataifa ya kigeni wakishirikiana na baadhi ya viongozi) wa maliasili zilizoko chini ya ardhi (madini) na juu yake (wanyama pori, misitu, mazao ya baharini n.k.) | Katiba mpya iweke wazi kwamba ardhi ni mali ya raia (wananchi) na serikali ni wakala tu wa raia katika kugawa ardhi kwa uadilifu na kwa ridhaa ya raia. Umiliki wa ardhi uweze kuondolewa kwa mmiliki iwapo atashindwa kuiendeleza ardhi kwa miaka mitatu mfululizo. Raia aweze kuuza ardhi aliyomilikishwa kwa raia mwingine au kukodisha kwa asiye raia kwa mkataba unaoweza kuhuishwa kila baada ya miaka mitatu. Rais aweze kusitisha umiliki wa ardhi wa mtu au kikundi kidogo cha watu kwa manufaa ya waliyo wengi maadam mmliki au wamiliki watalipwa fidia inayolingana na thamani ya ardhi wanayopoteza umiliki na vilivyomo kwa wakati huo |
49 | Kwamba Katiba iliyopo haitambui umilikishaji wa ardhi kwa uwiano wa kidini. Hii imepelekea mathalani upimaji wa maeneo mapya kupitishwa bila kuainisha maeneo maalum kwa dini husika na hivyo kupelekea mivutano isiyo ya lazima. Zipo hisia za umilikishaji wa ardhi kwa upendeleo wa kidini. | Katiba mpya itoe maelekezo kwa sheria za mipango miji kulenga ugawaji wa ardhi kwa kuainisha maeneo ya dini kwa mujibu wa uwiano wa kidini katika eneo husika. |
50 | Kwamba Sheria za nchi hazimpi madaraka Mkaguzi Mkuu wa Serikali kumfungulia mashitaka mtumishi wa serikali anayetuhumiwa kufanya ubadhirifu na ufisadi katika mali ya umma. | Katiba impe mamlaka huru Mkaguzi Mkuu wa Serikali kumfungulia mashitaka yeyote anayetuhumiwa kwa ubadhirifu au ufisadi wa mali ya umma. |
51 | Kwamba Katiba iliyopo iko kimya juu ya umiliki, ulinzi, matumizi na udhibiti wa mali za asili za Tanzania, zikiwepo madini, mazao ya baharini, wanyama pori, misitu n.k. Hii imepelekea matumizi ya kiholela, ubadhilifu na uporaji wa mali hizi unaofanywa na mafisadi wa ndani na nje na hivyo kuendelea kusababisha hali ya umasikini kwa Watanzania. | Katiba mpya ibainishe wazi kwamba mali za asili ni mali za raia wa Tanzania tu kwa kila upande wa muungano na iweke utaratibu madhubuti wa kulinda mali hizi dhidi ya ufisadi wa ndani na nje. |
SEHEMU YA VI: VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA WA RAIA
NA. | HOJA | MAONI |
52 | Kwamba Katiba iliyopo imetoa mwanya kwa ardhi yetu kutumika kwa malengo ya ukoloni mamboleo. Mathalan haitoi pingamizi kwa mataifa ya nje kuweka vituo vya kijeshi na upelelezi katika ardhi ya Tanzania. | Katiba mpya isiruhusu kwa hali yoyote kuwekwa kwa vituo vya kigeni vya kijeshi na upelelezi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. |
53 | Kwamba Katiba iliyopo haidhibiti kikamilifu uundwaji kiholela wa tume na majeshi ya ulinzi nje ya yale ya serikali. Mathalani tume ya majeshi ya Kikatoliki katika Jeshi la Ulinzi la Tanzania na kuwepo kwa Jeshi la Wokovu la Wakristo | Katiba mpya iendelee kupiga marufuku kuwepo kwa tume na majeshi haya yasiyo rasmi na kuweka utaratibu thabiti wa kuziba mianya ya kuundwa mengine ya mfano huo. |
SEHEMU YA VI: USAWA, HAKI YA KUISHI NA HAKI ZA BINADAMU
NA. | HOJA | MAONI |
54 | Kwamba Katiba iliyopo inaitambulisha Tanzania kama nchi ya ujamaa tofauti na uhalisia wa mazingira ya kisiasa na kiuchumi na kiitikadi yaliyopo nchini | Katiba mpya isitishe kuitambulisha Tanzania kama nchi ya kijamaa na Watanzania kama wajamaa. Ubaki mfumo wa siasa ya kujitegemea (kutokuwa tegemezi na ombaomba). |
55 | Kwamba Katiba iliyopo haitoi tafsiri yakinifu ya neno USAWA (mfano usawa katika mirathi, usawa katika majukumu ya mwanamke na mwanamume katika jamii n.k). | Katiba mpya ianishe tafsiri sahihi ya USAWA kwa mujibu wa imani za dini ya mtu. Hii itasaidia wananchi kutafsiri USAWA kwa mnasaba wa mafundisho ya imani ya dini zao. |
56 | Kwamba Katiba iliyopo inatoa uhuru na haki ya kuishi usio na mipaka na usiotilia maani uhuru na haki za wengine kuishi. | Katiba mpya iweke mipaka ya uhuru na haki ya kuishi yenye kuzingatia uhuru na haki ya kuishi ya wengine. Mathalani iweke sheria ya kuuawa kwa mtu aliyeuwa mwingine au watu wengine kwa dhulma. |
57 | Kwamba Katiba iliyopo haikatazi mahusiano ya jimai na kimapenzi nje ya ndoa pamoja na mahusiano ya namna hiyo kwa watu wa jinsia moja. Hii imepelekea kuporomoka kwa maadili na mparaganyiko katika jamii, kuenea kwa watoto wa mitaani na maradhi ya ukimwi na maradhi mengine ya zinaa. | Katiba isiruhusu mahusiano yoyote ya kimapenzi nje ya ndoa na mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja na ndoa ya watu wa jinsia moja. Katiba ipige marufuku vitendo au utengenezaji wa mazingira yanayopelekea au kurahisisha mahusiano ya namna hiyo. |
58 | Kwamba Mfumo wa Elimu uliopo hauwapi fursa Waislamu kuchunga maadili na itikadi ya dini yao. Ipo mitaala ya elimu iliyotofauti na ile ya elimu ya Mtanzania ambayo imeruhusiwa (Cambridge, Marekani n.k). Kwamba Waislamu wana haki ya msingi ya kufuata mfumo wa elimu wa Kiislamu kama sehemu ya ibada katika Uislamu. | Katiba mpya iruhusu watu wa dini mbalimbali kuwa na mfumo wa elimu utakaozingatia imani, maadili, mila, itikadi na desturi za dini zao. |
43 | Kwamba Sheria za nchi zinampa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai [DPP] kiasi cha kuwa na hiari kuifikisha kesi mahakamani au kutoifikisha au hata kuifuta kabisa bila idhini ya hakimu. | Katiba mpya impunguzie madaraka Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. Imlazimishe kupeleka kesi mahakamani na isimpe uwezo wa kufuta kesi kwa matakwa yake. Uamuzi wa kuendelea au kufuta kesi uwe ni wa mahakama. |
ANGALIZO: MAONI HAYA YAMEKUSANYWA KWA LENGO LA KUFANIKISHA MCHAKATO WA KUANDIKWA KATIBA MPYA. HIVYO BASI MUISLAMU YEYOTE ANAWEZA KUENDELEA KUCHANGIA KWA KUZIDISHA VIPENGELE AMBAVYO VIMESAHAULIWA AU KUPUNGUZWA NA VIMEKOSEWA KWANI UKAMILIFU NI WA ALLAH [S.W.]
WAKUSANYAJI NA WARATIBU WA HOJA NA MAONI
1. Sheikh Salim A. Barahiyaan [LLB Shariah, LLM Shariah & Law]
2. Dr. Abu-Malik Juma [PhD Economics]
TAKWIMU
IDADI YA MIKOA ZILIPOFANYIKA SEMINA SHIRIKISHI
TANZANIA BARA 17
ZANZIBAR 1
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment