Saturday, 28 March 2015

[wanabidii] Rais apokea Ripoti ya CAG na kuagiza hatua kali zichukuliwe kwa wabadhirifu wa fedha za Serikali

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais apokea Ripoti ya CAG na kuagiza hatua kali zichukuliwe kwa wabadhirifu wa fedha za Serikali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameviagiza vyombo vya Serikali kubaini maofisa wote wa Serikali wanaohusishwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, ikiwa ni pamoja na kutoa malipo bila nyaraka zozote, kutumia fedha nje ya Bajeti na kutoa malipo bila idhini ya ofisa masuhuli, ili wachukuliwe hatua kali za kisheria na hatua nyingine.

Aidha, Rais Kikwete ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa maofisa wote wa Serikali ambao wanahusika katika kulipa mishahara hewa kwa watumishi ambao wameacha kazi, wamefariki, wamestaafu lakini ambao wanaendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao za benki.

Rais pia ameiomba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuisaidia Serikali katika kuboresha mfumo wa zabuni ambako Serikali inapoteza fedha nyingi kwa kupitia mchakato mrefu mno wa kupatikana kwa wazabuni wa kutoa vifaa na huduma kwa Serikali.

"Naagiza kuwa tutume ujumbe wenye nguvu za kutosha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Serikali," Rais Kikwete ameviagiza vyombo vya Serikali baada ya kupokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka wa Fedha Unaoishia Juni 30, 2014 katika shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, leo, Ijumaa, Machi 27, 2015.

Rais Kikwete ametoa maagizo hayo baada ya kujulishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad kuhusu nini ukaguzi wake umegundua kuhusu Usimamizi na Matumizi ya Fedha za Serikali.

Miongoni mwa mambo mengine, ukaguzi huo umebaini mapungufu mbali mbali katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile malipo yasiyokuwa na nyaraka, hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha iliyotumika nje ya Bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa (nugatory expenditure) na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maafisa masuuuli.

Profesa Assad amemweleza Rais Kikwete pia kuwa Ofisi yake inapendekeza kuwa taasisi zote za Serikali zisiendelee kununua vifaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EDF), stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.

Rais Kikwete ameagiza: "Kwa wale ambao wanatumia fedha za Serikali vibaya wachukuliwe hatua. Wenye ushahidi wa waziwazi wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kwa wale ambao hakuna ushahidi wa kuweza kuwafikisha mahakamani lakini wamekula fedha za Serikali wachukuliwe hatua nyingine kama vile kuachishwa kazi kwa manufaa ya umma ama kushushwa vyeo ama kuchukuwa hatua nyingine za kiutawala."

Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, Profesa Assad amemwambia Rais Kikwete: "Ukaguzi wangu pia umebaini kuwa mishahara ya watumishi waliocha kazi, waliofariki, waliostaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao. Vile vile, fedha za makato ya mishahara ya wafanyakazi hao zimeendelea kupelekwa kwenye taasisi husika kama vile Bima ya Taifa ya Afya, Mamlaka ya Mapato na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii."

Profesa Assad anasema kuwa tatizo hili linaendelea kuwepo hata kama linapungua kwa sababu ya mfumo wa udhibiti ambao Serikali imeanzisha na kuwa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana, 2014, kiasi cha Sh. Bilioni 141.4 zilitumika kulipa watumishi hao hewa.

CAG amewasilisha Ripoti yake kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na pia kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008.

Profesa Assad amewasilisha Ripoti tano ambazo ni Ripoti ya Serikali Kuu, Ripoti ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Ripoti ya Mashirika ya Umma, Ripoti ya Miradi ya Maendeleo na Ripoti ya Ufanisi (Value for Money Audit).

Rais Kikwete amemshukuru Mkaguzi Mkuu na watumishi wengine wa CAG kwa kuwasilisha ripoti yenye ubora wa kiwango cha juu na ameahidi kuwa ataiwasilisha Ripoti hiyo Bungeni Jumatatu ya Machi 31 ili ipate kujadiliwa.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

27 Machi,2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment