Sunday, 29 March 2015

[wanabidii] UJENZI WA RELI MPYA YA KATI KWA KIWANGO CHA "STANDARD GAUGE "

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

UJENZI WA RELI MPYA YA KATI KWA KIWANGO CHA "STANDARD GAUGE "

(MRADI MKUBWA TANGU UHURU)

Nafurahi kuwajulisha kuwa RAHCO (Kampuni ya Rasimali za Reli)wamekamilisha utaratibu wa kumpata Mshauri wa Mradi ambaye ni Kampuni ya Roths child ambayo itawezesha kupata fedha za ujenzi wa Reli Mpya ya kati kwa Kiwango cha "Standard Gauge "ambayo gharama yake ya ujenzi ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6 ,ambayo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 14.Reli hii itakuwa na urefu wa Kilomita 2561.

Huu utakuwa ndiyo Mradi Mkubwa kutekelezwa na serikali toka tupate Uhuru .Aidha,kwa Mradi huu serikali haitoi hata dola Moja kutoka Hazina bali utagharamiwa na mabenki ambayo ndiyo yatakayotoa fedha.

Mkopo huu utarejeshwa kwa kipindi cha miaka tutakayokubaliana kutokana na gharama za tozo ya mizigo itakayopitishwa kwenye reli hiyo .Tunakadiria Mkopo huo utalipwa ndani ya muda wa miaka 20.

Reli hiyo Mpya kabisa tofauti na iliyopo itakuwa yenye uwezo mkubwa wa Kimataifa "Standard Gauge railway " itaanzia Dar es Salaam Mpaka Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi. 

Pamoja na Masuala mengine, reli hiyo itasaidia kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za DRC, Rwanda, Burundi, na Uganda lakini pia itasaidia Usafirishaji wa wananchi wetu kwenda mikoani kwa wingi na kwa kasi zaidi.

Wengi watajiuliza kwa nini tumeamua kujenga reli Mpya? 
Ni kutokana na sababu kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya Kiwango cha "meter Gauge " uwezo wake wa kubeba mizigo hata baada ya ukarabati kwa mwaka ni tani Milioni 5,ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30 ifikapo mwaka 2025.

Hivyo basi ,tunahitaji kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba Mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda. 

Mradi huu wa kujenga reli ya kati utaajiri watanzania takribani 300,000 watakaohusika na ujenzi wa reli hiyo itakayojengwa kwa muda wa miaka 5 .Reli hiyo itafanya upelekaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam Mpaka nchini DRC kuchukua muda wa takribani saa 12.

Tumejipanga ili Uzinduzi wa ujenzi wa reli hii ya kihistoria ufanywe na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi ifikapo tarehe 30 Juni , 2015 yaani Mwaka huu tulionao kule Mpiji Kituo cha stesheni Mkoa wa Pwani ambako ndiko reli itaanzia. 

Pamoja na hayo , mwaka huu tunatarajia kuweka jiwe mawe ya msingi katika reli nyingine mbili ambazo ni:Reli ya Kusini (Mtwara -Songea -Mbambabay na Mchuchuma -Liganga)na reli ya Kaskazini (Tanga -Arusha-Musoma na Viunganishi vya Engaruka Soda Ash Mines,Minjingu Phospate)ambazo kwa Pamoja zitagharimu kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 6.6. na kutengenezea zaidi ya watanzania 5000,000 ajira Mpya. 

Kwa ujumla reli zote tatu zitagharimu jumla ya kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 14.2 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 26 zitaajiri zaidi ya watanzania Milioni Moja kwa miaka yote zitakapokuwa zinajengwa (2015-2021).

Mungu Ibariki Afrika , Mungu Ibariki Tanzania .

Samuel J.Sitta
WAZIRI WA UCHUKUZI 
29 Machi ,2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment