Kuwa na afya bora ni jambo muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Kama una matatizo ya afya hutaweza kutimiza majukumu yako ya kila siku, hivyo maisha yako hayatakuwa katika hali nzuri.
Sote tunajua huwezi kufanya chochote pale unapokuwa mgonjwa na masuala ya afya yanahusisha zaidi mazingira yanayotuzunguka. Ni ukweli kwamba mazingira yetu yakiwa machafu basi afya zetu zitakuwa katika hatari kubwa, kwani uchafu ndiyo mahali mwafaka kwa wadudu wasababishao magonjwa kuzaliana na kustawi.
Ni jambo la kusikitisha kuwa Watanzania wengi hatujali mazingira yanayotuzunguka. Elimu ya kutosha imetolewa kwa njia za mikutano ya kijamii, vyombo vya habari na njia nyinginezo, lakini haieleweki kinachotokea kama ni kutojali au ni kweli kutoelewa. Hebu tuzitafakari tabia hizi.
Unaweza kukuta mtu amevaa vizuri, anapendeza lakini ukienda kuangalia mahali anapotoka yaani nyumbani kwake, utashangaa. Kumejaa uchafu usiofanana na kupendeza kwa mtu huyo. Mtu mtanashati ndiye utakuta anakula ndizi barabarani na maganda akayatupa hapo barabarani bila kujali kwamba atavutia inzi waletao maradhi.
Mtu huyu mtanashati ndiye anayetupa uchafu barabarani akiwa ndani ya daladala bila kujali nani atauokota, kama kweli utaokotwa. Usafi ni tabia, kama ni tabia ina maana mtu atakuwa msafi katika nyendo zake zote, iweje sasa mtu awe msafi katika nguo alizovaa halafu akatupa taka ovyo, kwa nini asijimwagie takataka mwenewe.
Bila shaka mtu huyu ni mnafiki, hata mavazi hayo masafi ni kwa ajili ya kujionyesha tu. Kama kungekuwa hakuna mtu wa kumwangalia, bila shaka hata nguo zake zingekuwa chafu.
Utakuta watu na akili zao wanauza chakula pembeni mwa mifereji ya maji machafu. Wakati mwingine utakuta mtu anafanya usafi sehemu anayofanyia biashara na kuzisukuma takataka pembeni au upande wa pili wa barabara. Watu wa namna hii wanafikiria inzi nao wanaijua mipaka yao.
Bila kujali, utakuta mtu anaukaribisha ugonjwa wa kipindupindu kwa kufanya vitendo vya kinyama kabisa; kwani ni vitendo vya uuaji. Utakuta katika kipindi cha mvua mtu anatumia mwanya wa kunyesha mvua kwa kuzibua choo chake na kuelekeza uchafu wote barabarani.
Watoto wanatembea pekupeku, wadudu wanazaliana na magonjwa nje nje. Cha kushangaza uchafu huo unaelekezwa kwenye barabara ambayo hata yeye na familia yake wanapita. akati mwingine ni watoto wake ndiyo wanaoetembea pekupeku. Wakipata maradhi, ataishia kulalamika kwamba wanawe wamerogwa. Hakumbuki vitendo vichafu alivyofanya. Ukiuliza ni kwa nini watu wanaishi na uchafu watakwambia kwamba Serikali imeshindwa kutoa takataka hizo; sababu ya kawaida kwa Watanzania wasiotaka kutimiza wajibu wao.
Kama nilivyosema hapo mwanzo usafi ni tabia, hivyo hauendeani na usomi, utajiri au sifa nyingine. Wapo watu wenye uwezo ambao nao wana tabia zinazochangia kufanya mazingira yawe machafu. Hawa unakuta wanajenga ukuta kuzuia njia ya maji, hivyo kusababisha kero na madhara ya kiafya kwa watu wananowazunguka.
Kwa kutumia uwezo wa kifedha wanaziba kabisa njia za maji machafu, hivyo kulazimisha maji hayo kuishia kwenye nyumba za watu wanaowazunguka na wenyewe wanaona ni sawa kabisa.
Wengine ni wasomi wazuri lakini usomi wao unashindwa kuwafafanulia kwamba kipindupindu kitakapofumuka, hata wao wapo hatarini kwani hawaruki kwa helikopta kwenda majumbani kwao.
Yaani utakuta maji yenye kemikali hatari yanatiririka kuelekea kwenye makazi ya watu na kusababisha harufu kali na hatari ya magonjwa kama vile saratani na mengineyo. Utaona maji machafu yenye rangi za ajabu na harufu kali yakitiririka kwenye makazi ya watu.
Watu hawa wanatumia fedha nyingi kuhonga wenye mamlaka ili wasiwachukulie hatua, badala ya kutumia fedha hizo kutengeneza miundombinu itakayosaidia kusafirisha majitaka kwa usalama zaidi. Ni tabia za uchafu ndiyo zinazowasumbua na kuwafanya watenda vitendo vya kuchafua mazingira
Tunaweza kufikiri ni gharama kuweka mazingira yetu safi, lakini ukweli ni kwamba ni gharama kubwa zaidi kutibu madhara yanayosababishwa na mazingira machafu. Ukipata magonjwa kwanza shughuli zako zinasimama, pili unatumia muda na fedha nyingi kujitibia, hii yote ni hasara kubwa kwako.
Lakini hasara kubwa kuliko zote ni kwamba, unaweza kupoteza maisha yako na hakuna gharama inayoweza kuifidia maisha. Kwani ungetumia gharama gani kushughulikia maji machafu ukilinganisha na kuharisha wiki nzima?
Mwisho utaona kile kidimbwi kinasababisha mlolongo wa hasara juu ya hasara. Na hapo bado tutaililia Serikali kweli ni sahihi hii?
Ni wakati sasa Watanzania tubadilike na kujali mazingira yanayotuzunguka kwani mazingira bora maana yake afya bora na hakuna maendeleo, bila afya bora. Huu ni wajibu wetu sote kama kweli tunataka kupiga hatua.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment