Monday, 1 June 2015

[wanabidii] NCCR - MAGEUZI YATAKA UWAZI KWENYE UKAWA

MSIMAMO-KITENGO VIJANA NCCR-MAGEUZI KUHUSU UKAWA

Kutokana na mwenendo ndani ya UKAWA usiokuwa wa wazi na ambao umekuwa ukionyesha dhahiri kuna kasoro katika mambo yanayoendelea, niliomba mambo yawekwe wazi na bayana, hii nikutokana na ukweli kwamba pamoja na sababu zingine zote bado pia lazima kuwe na uwiano mzuri wa uwakilishi ndani ya UKAWA katika vyombo vya maamuzi. Hilo nililieleza vyema katika taarifa yangu kwa umma kupitia vyombo vya habari, tarehe 24 Mei 2015.

Kwa kuwa muda wa siku saba tuliotoa kwa viongozi wetu ili waweze kutuweka wazi umepita bila jibu lolote, Mimi kama msemaji wa Kitengo Cha Vijana naweka msimamo wa namna ya kusimama juu ya hali hiyo. Jana nimetoa taarifa hii kufuatia hali ya sintofahamu na kuelezea hali iliyopo kwa undani ili tuweke kuchukua tahadhali kabla chama hakijapotezwa, au ikitokea tahadhali hii haikuchukuliwa basi siku mambo haya yakitokea tusije hukumiwa sote kuwa tulikuwa viongozi ambao hatuwezi kuona tatizo na giza mbele na kuliondosha, aidha ujumbe huu ukizingatiwa tutaweza kujenga ushirikiano wenye nguvu na endelevu kuliko huu na mambo yanayoendelea ndani yake.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Jumatatu 1 June 2015

Ndugu wanahabari na Watanzania wenzangu,
1. Gazeti la Mwananchi la tarehe 24 Machi 2015 limemnukuu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi akilalamikia kuwa hawatakubali UKAWA itumike kwa maslahi ya chama kimoja katika umoja huo. Kauli hii lilikuwa ni tangazo kwamba hali haikuwa shwari ndani ya Umoja wa Katiba (UKAWA). Hata hivyo, viongozi wetu wa juu wamekuwa wazito kusema ukweli wa mambo kuhusu kinachoendelea ndani ya UKAWA. Katika taarifa hii ninaeleza kwa kirefu kidogo kuhusu historia ya ushirikiano wa vyama vya upinzani hapa nchini, na kueleza msimamo wangu kuhusu UKAWA kama Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana wa NCCR Mageuzi.

2. Ushirikiano wa vyama Tanzania haujaanza leo. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, mwaka 2006 uliundwa ushirikiano wa vyama Tanzania uliojulikana kama Umoja wa Demokrasia Tanzania (UDETA), ukishirikisha Chama Cha Wananchi (CUF), wakati huo kikiwa chama kikuu cha Upinzani Tanzania, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR-Mageuzi, na Tanzania Labor Party (TLP). Dhamira ilikuwa ni kujenga upinzani imara kuelekea 2010. Bahati mbaya umoja huu ulikufa kutokana na dhamira ovu ya CHADEMA ambayo malengo yake ilikuwa kujijenga kupitia migongo ya vyama hivyo. Kwa mfano, katika ziara za mikoani zilizofanywa na viongozi wa vyama hivyo, CHADEMA walichukua mawasiliano na viongozi wa vyama vingine na baadae kuwashawishi kujiunga na chama hicho. Hila hizo na ulaghai huo ulipelekea UDETA kufa kifo cha kawaida bila hata kikao cha kuamua kusitisha umoja huo. Ikumbukwe mwaka 2010 chadema baada ya kupata wabunge wengi ilibeza vyama vingine kwa kuviita CCM B, vyama vya mashoga, mamluki wa CCM na kwamba isingeweza kushirikiana nao, ikasahau jinsi chama cha wananchi CUF kilivyowaalika na kuwapa vyeo katika muda ambao kilikuwa na uwezo wa kuunda kambi rasmi ya upinzani pekee bungeni. Baadhi yetu, tulitegemea kwamba wenzetu CHADEMA kwa wakati huu nchi ilipo katika wakati mgumu, watakuwa wamejifunza na kwamba wangebadilika na kufanya siasa za kistaarabu, zinazozingatia maslahi ya nchi na watu wake na washirika wenza wa UKAWA.

3. Hata hivyo, mtiriko wa matendo ya CHADEMA ndani ya UKAWA unaonyesha kwamba chama hiki bado ni walewale na nia yao ni kutumia vyama vingine katika kuficha udhaifu wao na kujipatia maslahi ya kisiasa dhidi ya vyama vingine vinavyounda umoja. Nitatoa mifano michache:

a. Wakati tukielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014, UKAWA ulitengeneza dokezo moja kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Lakini nyuma ya pazia, CHADEMA wakatengeneza dokezo lao na kuwapa viongozi wao maelekezo kuhakikisha kuwa kila sehemu lazima waweke wagombea. Wakati vyama vingine vikifuata muongozo wa UKAWA, CHADEMA wakawa na maelekezo yao tofauti, na zaidi ya hapo walienda mbali na kuwaeleza wagombea wa vyama shirika wanaokubalika kujaza fomu za CHADEMA maana ni UKAWA huohuo. Hali hiyo ya kucheza faulo, na mwamko ule wa wananchi kuchagua umoja huo, kwa kuwa CHADEMA waliweka wagombea wengi mwisho wa siku wakapata viti vingi na viti hivyo wakaja shinikiza viwe vigezo vya uteuzi wa wagombea ubunge 2015.

b. Naibu katibu mkuu wa CHADEMA Zanzibar, kaachiwa jimbo na chama cha wananchi CUF, tena nje ya kikao, kwa utashi wao na kwa nia ya kudumisha mahusiano. Hata hivyo jambo la kushangaza ni kwamba Makamu Mwenyekiti wetu, aliyegombea urais Zanzibar mwaka 2010, na aliyekuwa moja ya nguzo za kuasisiwa kwa UKAWA, hakupewa nafasi ya kuachiwa jimbo hata moja huko Zanzibar. Sasa swali la kujiuliza iweje mtu ambaye kaingia katika harakati za kisiasa juzi anapewa nafasi ya kugombea lakini viongozi wa NCCR-Mageuzi wazoefu hawapewi hiyo fursa? Sisi kama vijana wa NCCR-Mageuzi tunaona kwamba hali hii ina kasoro na inahitaji isemwe, maana kuna walakini katika maamuzi yote haya.

c. Maswali mengine ya kujiuliza ni kama Naibu Katibu Mkuu - CHADEMA, ambaye hana mizizi wala chembe ya siasa huko Zanzibar anaachiwa jimbo, je ni kwa nini imekuwa shida kuliacha jimbo la Serengeti kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi ambaye ana historia ndefu katika siasa za upinzani Tanzania? Na pia kwa nini inakuwa ngumu kuachia jimbo analotaka kugombea Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Tanzania bara? Na kwa nini NCCR tunapewa majimbo tasa, kama Ilala?

d. Aidha, kama ni kweli moja ya kigezo cha chama kuachiwa jimbo ni matokeo ya 2010, ya chama kilichokuwa cha pili, ni kwa nini chadema imeng'ang'ania jimbo la Buyungu ambalo NCCR-Mageusi ilikuuwa ya pili baada ya kuchakachuliwa? Pia kwa jimbo la Mafia, CUF ilipata kura zaidi ya 6000 na CHADEMA ikaambulia kura 200 pekee yake, wanaling'ang'ania kwa vigezo gani? Vigezo hivi vinatumika dhidi ya vyama vingine lakini linapokuja jimbo lenye maslahi ya viongozi wa CHADEMA basi vigezo havizingatiwi na vinachakachuliwa, hii ni double standard na ulaghai wa kisiasa. Na haya majimbo ni mfano mdogo, yapo mengi.

4. Kuhusu Mgombea urais, UKAWA ina mengi ya kujifunza kutoka kwa umoja wa NARC ambao ulifanikiwa kuking'oa chama cha KANU nchini kenya mwaka 2002. Kulikuwa na wanasiasa maarufu wakati huo kama Raila Odinga, Profesa George Saitoti, Kijana Wamalwa na wengine wengi, lakini walimteua mgombea ambaye kwa wakati huo hakuwa na umaarufu sana lakini alikuwa na sifa na mahitaji wa wakati huo, Mwai Kibaki ambaye alitoka katika chama kidogo. Nasi tunapaswa kujifunza na kuangalia mahitaji ya sasa na aina ya mtu na sifa zinazoweza kulivusha Taifa katika kipindi hiki kigumu. Umaarufu sio kigezo cha kuwa Rais mzuri, mahitaji ya kizazi hiki na karne hii yanatakiwa kuwa muongozo katika kuchagua mgombea wa Urais wa UKAWA. Ndiyo maana sisi vijana wa NCCR- Mageuzi tumempendekeza Dkt. George Kahangwa. Kwa tathmini yetu huyu ana sifa za uongozi, elimu nzuri, utumishi wa umma uliotukuka, hana tuhuma za ufisadi, rushwa na ni mtu mwenye familia na anayejiheshimu katika mienendo yake ambaye anafaa kuwa taswira bora katika nchi na kwa vijana, watoto na vizazi vijavyo.

Najua pia kuna wagombea pendekezwa katika vyama vingine, lakini hivi sasa tupate Rais aliyezaliwa baada ya Uhuru na Wazee wetu wawe washauri na watoa muongozo. Tusitumie kigezo cha umaarufu pekee na tukashindwa angalia mahitaji ya nchi.

5. Ukawa kisheria. Chadema haina dhamira ya dhati ya ushirikiano, nina wasiwasi inaendeleza dhamira yake ya siku nyingi ya kuvimeza vyama vingine Tanzania Bara na ibaki yenyewe, na hili kitadhihirika baadae, maana ndiyo mpango mkakati wao. Wanahadaa vyama vingine kuachiana majimbo huku wakifanya maandalizi kwa kila jimbo, kwa kuwa ushirika huu hauna nguvu ya kisheria mwisho wa siku viongozi wa kitaifa wa CHADEMA watasema kuwa walitoa maelekezo lakini viongozi wa jimbo hawakutekeleza, hivyo watagombea kila jimbo.

Ili kuepuka hili, nilipendekeza mgawanyo wa majimbo uweke wazi na yawekwe makubaliano ya kisheria ili kuwe na wajibu na utekelezaji. Tofauti na hapo hatuko tayari kufanya kazi katika mfumo wa DESI ya kisiasa.

6. Rai kwa Mwenyekiti wangu wa Taifa, Ndugu James Mbatia: Sio suala jepesi kumkosoa Mwenyekiti wangu katika umma, anafahamu kuwa namheshimu na anafahamu kuwa suala hili tumemueleza na kumuelekeza katika vikao juu ya kuhakikisha maslahi ya Taifa yanapewa kipaumbele kwanza katika UKAWA. Ni bahati mbaya sana dalili zote zinaonyesha kuwa kuna chama (CHADEMA) kimejimilikisha UKAWA kama mali yake binafsi na wanafanya watakavyo, na Mwenyekiti ambaye ndio taswira ya chama chetu umekaa kimya. Hadi sisi tunahisi ukimya huo unatokana na kulenga zaidi kupata jimbo la Vunjo hata kwa gharama ya kukizika na kufifisha nguvu ya Chama. Sisi tunaamini kwamba mzazi lazima ajitoe kwa ajili ya familia yake, haya mambo unayajua kwa undani na hisia zetu na uhalisia tumekueleza, tunaomba jambo hili ulisimamie vyema kwa dhamira ile ile, maslahi ya nchi kwanza, kisha chama chetu pia. Na pia kuufanya UKAWA kuwa maamuzi ya wenyeviti tu sio sahihi.

7. Rai yangu kwa Vijana na wanachama wa NCCR-Mageuzi: Katika uongozi wangu sipendi kuona vijana wakiendelea kupuuzwa na kuwa watekelezaji wa mambo ambayo wao sio sehemu ya maamuzi hayo, hatutashiriki hatua ya kuua chama chetu na kufaidisha chama kimoja au viwili kwenye ushirika. Kazi ya vijana ni ulinzi na usalama wa Chama, hadi hapo tutakapojiridhisha na dhamira njema na mgawanyo wenye tija ndani ya UKAWA, sisi tutaendelea na mchakato wa kujiandaa na kujenga chama chetu na kushiriki uchaguzi katika kata na majimbo yote ambayo tuna wagombea ambao tunaamini wana dhamira ya kuwatumikia watanzania.

Na nawakaribisha Vijana, Wazee na kina Mama kujiunga na chama chetu na kuchukua hatua ya kushiriki uchaguzi na kuleta mabadiliko ya kweli, ama kwa kuchagua au kuchaguliwa ili kuleta mabadiliko yanayotakiwa katika Nchi yetu.
PAMOJA NA SALAAM ZA CHAMA,

Deo Meck
Mwenyekiti Kitengo Cha Vijana NCCR-Mageuzi – Taifa
Barua pepe: dmecky@hotmail.com Simu: +8615996474235

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment