Saturday, 27 June 2015

[wanabidii] ACT WZALENDO WASAMBAZA UZALENDO MKOANI TNGA

hOTUBA YA ZITTO MUHEZA TANGA NA PICHA

Muheza na Tanga 27.06.2015

Ndugu zangu wanatanga, Nina furaha kubwa mno kuwa hapa nanyi. Furaha yangu kubwa inatokana na mambo mawili makuu:
Mosi: Leo nimezileta Tanga harakati mpya za Siasa za Kizalendo nchini, Siasa za kuirudisha nchi yetu katika misingi yake, Siasa za Chama chetu cha ACT Wazalendo.

Furaha yangu kwenye hili ni kuwa nimezileta Siasa hizi pahala penyewe sahihi, kwa watu watanga, watu wazalendo na wenye fasaha ya matamshi. Jambo hili la harakati za Siasa za Kizalendo kuletwa Tanga si geni kwenu, maana hata historia ya Ujenzi wa Taifa letu inaonyesha hivyo.

Ni harakati za Wazalendo wanaTanga Wazee wetu Stephen na Peter Mhando, Mwalimu wa Mwalimu wa Kihere, Makatta Mwinyimtwana, Bakari Maharage Juma Mwawado, Chifu Erasto Mang'enya, Hamza Kibwana Mwapachu, Rashid Sembe na Hamisi Heri Ayemba kuziingia Siasa za Ukombozi za Taifa hili kuanzia Chama cha TAA na kisha TANU ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zilisaidia kuleta Uhuru wa Tanganyika.


Tanga kilikuwa kitovu cha Uchumi wa Tanganyika, kuanzia Mashamba ya Mikonge mpaka viwanda vidogo, Harakati za wanatanga kuipokea TAA na kisha TANU zilisaidia sana kuharakisha kupatikana kwa Uhuru wetu.

Hivyo sisi katika ACT tumeamua kurudi kwenye misingi, kukileta kwenu Wanatanga Chama chenu hiki cha ACT Wazalendo, ili kama ilivyo ada mzibebe harakati hizi za kurudisha Uzalendo wa Taifa hili.

Sababu ya Pili ya Furaha yangu, ni kwa kuwa nimelileta kwenu Azimio la Tabora, Muongozo wa Kimaadili, Kiuongozi, Kisera na Kiitikadi wa Chama chetu, Muongozo unaohuisha Azimio la Arusha.

Nina furaha kwa kuwa asili ya Azimio hili la Tabora mzizi wake ni Tanga, mzizi wake umejengwa katika kuenzi Mchango wa Mzee wetu wa hapa Tanga, Mwalimu wa Mwalimu wa Kihere, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano uliofanya Uamuzi wa Busara wa Tabora wa 1958 wa Chama cha Tanu.

Hapa Tanga kuna mgahawa unaitwa Patwas, uko mjini pale katika jengo lililo katikati ya Majestic Cinema na Jengo la Bora, mgahawani pale zipo Picha za mwaka 1957, zikimuonyesha Mwalimu Nyerere akifanya hiki ambacho ACT Wazalendo tunakifanya Tanga, kuzikabidhi harakati za Siasa za Kizalendo kwa wenyewe hasaaa, Wanatanga.

Tumekuja Tanga kutambulisha chama chetu cha ACT Wazalendo. Ni chama kipya lakini viongozi wake sio wapya Tanga. Wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya Tanga ili kurejesha nafasi ya mkoa huu katika uchumi wa nchi yetu.

Tanga ni mkoa uliokuwa mstari wa mbele katika kulikomboa Taifa letu. Chama cha TANU kilisheheni viongozi kutoka Tanga katika safu yake ya uongozi. Kina Stephen Muhando na Mwalimu Kihere kwa nyakati tofauti walikuwa watendaji wakuu wa TANU wakati tunasaka uhuru wa nchi yetu. Mwenyekiti wa TANU Tanga ndg.

Hamis Heri Ayemba alikuwa nguzo kubwa sana ya chama hicho na hata mkutano wa Tabora wa kura tatu ulitegemea sana Tanga kuhakikisha ushindi kwa Mwalimu Nyerere. Sisi ACT Wazalendo tunatambua nafasi ya watu wa Tanga katika kupigania uhuru wa nchi yetu na kwa kuenzi historia ya nchi yetu tulitangaza Azimio la Tabora mjini Tabora mnamo tarehe 13 Juni 2015.

Azimio hili linahuisha Azimio la Arusha. Tunataka kuenzi wazee wetu hawa akiwemo Mzee Hamza Mwapachu ambaye alikuwa mhimili wa kuanzishwa kwa TANU na kuchochea harakati za uhuru wa nchi yetu.

Tanga bado ina nafasi kwenye uchumi wa nchi yetu. Tanga inashika nafasi ya 8 katika mchango kwa Pato la Taifa nchini. Hata hivyo mkoa wa Tanga unashika nafasi ya 3 katika makusanyo ya kodi nchini baada ya Dar Es salaam na Arusha.

Wakati mikoa kama Mbeya inachangia zaidi Pato la Taifa, Haifikii Tanga kwa kukusanya kodi. Kodi kutoka Tanga ingekuwa kubwa zaidi iwapo Bandari Ya Tanga ingekuwa inafanya kazi kwa ufanisi. Mchango mdogo wa Tanga katika shughuli za uchumi unatokana na kusinyaa kwa shughuli za uchumi mkoani humu na hasa kilimo cha Mkonge.


Uchumi Mkubwa wa Tanga ni wa Viwanda, kwa kipindi cha Karibuni Viwanda vya Vifaa vya Ujenzi (Cement, Chokaa nk) vimeanza kushamiri Tanga.
Lakini matatizo makuu ni matatu
1. Kwanza Ajira za daraja la juu la kati si za wanatanga
2. Hakuna mpango mkakati wa kuwaandaa Vijana wa Tanga kwenye hizo Ajira za Juu na Kati
3. Ajira zilizoko ni za daraja la chini, na nyingi ya hizi si ajira. Ni Vibarua tu wanaolipwa kwa siku - with no pension wala Social Security. Chama chetu kimeweka suala la Hifadhi ya Jamii kama nguzo muhimu ya kujenga Tanzania ya watu walio sawa.


Athari ya kudorora/kuendeshwa vibaya kwa Uchumi wa Viwanda wa Tanga ni kuzalisha Jamii yenye vijana wengi wasio na ajira, ambao wameelekeza sasa macho yao kwenye Uzungu wa Unga-Kiasi Tanga kila kaya ina mzungu wa Unga au Mwathirika wa Matumizi ya Unga.
Athari ya Madawa ya kulevya imeua kizazi cha Kandanda cha Coastal Union na African Sports, Timu zilizozalisha kina Omari na Salehe Zimbwe, Mweri Simba, Zakaria Kinanda na wengineo. Nawapongeza sana wana Tanga kwa kurejesha timu zenu zote kwenye Ligi kuu. Hata hivyo bado nafasi ya Tanga kwenye Mpira haijawa ile tunayoijua. Lazima kurejesha hali hiyo.


Suluhisho liko ACT, Suluhisho liko kwenye Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha.
Chama cha ACT Wazalendo kina shabaha ya kurejesha zao la Mkonge katika kiwango chake cha miaka sitini. Mwaka 2014 Mkonge umechangia dola za marekani 16 milioni tu katika mauzo ya bidhaa nje. Hiki ni kiwango kidogo mno. Mashamba yapo lakini yameuzwa kwa matajiri wachache na hayazalishi. Chama chetu kinataka mashamba haya wapewe wananchi. Azimio la Tabora limetamka hilo kinaga ubaga.


1 Ardhi na mashamba yote yaliyokuwa ya Mashirika ya Umma na kubinafsishwa yarejeshwe kwa wananchi wasio na ardhi kwa kuwagawia na kushiriki katika uzalishaji kwa kutumia mfumo wa 'outgrowers' scheme'.
2 Mashamba makubwa ya kibiashara yatakapohitajika itakuwa ni jumla ya mashamba madogo madogo ya wananchi na pale uwekezaji utakapohitaji basi wananchi watamiliki theluthi mbili ya shamba husika na mwekezaji wa ndani au wa nje atamiliki theluthi moja tu.


Tunataka Mkonge Ulimwe na wakulima wadogo ili Watanzania wawe na shughuli za kilimo zenye tija.
ACT Wazalendo kurejesha NBC kwa Watanzania
Azimio la Tabora limeagiza dola kumiliki Benki kubwa nchini ili kujitegemea kiuchumi. Nchi yetu haiwezi kuendelea iwapo mabenki makubwa yote yanamilikiwa na watu kutoka nje. Utaifishaji wa Mabenki uliofanyika mwaka 1967 na kuundwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara, Benki ya Nyumba na Benki ya Maendeleo Vijijini ilikuwa ni maamuzi ya msingi sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara na kuuwawa kwa Benki ya Nyumba ilikuwa ni maamuzi ya hovyo kabisa kupata kutokea katika nchi yetu.

Malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye uhuru mkubwa katika soko la mitaji hayawezi kufikiwa bila ya kuwa na Benki zinazomilikiwa na Watanzania wenyewe. Hivyo, Chama cha ACT Wazalendo kitahimiza kuwa Benki ya Taifa ya Biashara irejeshwe kwenye mikono ya Watanzania kwa kumilikiwa na Serikali 50% na Wananchi na taasisi za wananchi kupitia soko la mitaji nusu iliyobakia. ACT Wazalendo itahimiza pia Benki ya Maendeleo na Benki ya Kilimo kuwa na muundo wa umiliki kama wa Benki ya Taifa ya Biashara.


Ubinafsishaji wa NBC ulifanywa holela na benki iliuzwa kwa bei ya bure kimsingi. Msimamo huu wa ACT Wazalendo unaungwa mkono na kazi iliyofanywa na kamati ya Bunge ya PAC iliyoagiza ukaguzi maalumu kwenye mchakato wa ubinafsishaji wa Benki hiyo. Hata Mwalimu Nyerere alikufa na kinyongo cha Benki hii.
Wakati Benki ikiwa inaendelea na shughuli zake kulitokea hasara ya dola za kimarekani milioni 143 zilizotokana na mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya usafirishaji. Mikopo hiyo ilikuwa ya kitapeli. Hata hivyo ili kufidia hasara hiyo Serikali ya Tanzania nayo ilipaswa kulipa nyongeza ya mtaji katika benki. Hii ni sawa na kulipia hasara ambayo waendeshaji wa benki walifanya.


ACT Wazalendo ni chama cha siasa kinachotaka kurejesha nchi yetu kwenye misingi. Tunataka kujenga Tanzania ya kijamaa na yenye demokrasia. Tunataka kurejesha nafasi ya Tanga kwenye Taifa letu. Tunaomba muunge mkono chama chetu. Tunawakabidhi chama hiki watu wa Tanga, ni chama chenu na kiwe jukwaa lenu katika kupaza sauti za wanyonge.

Zitto Kabwe
Kiongozi wa chama ACT Wazalendo

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment