Tuesday, 1 April 2014

[wanabidii] Mfuko wa Afya ya Jamii Wazinduliwa mkoani Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula amezindua rasmi mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii ujulikanao kama Tiba kwa Kadi (TIKA) huku akiwataka wadau kuhakikisha wanapitisha mpango huo kwa maslahi ya wananchi wa mkoa huo.
Magalula ameyasema hayo wakati akizindua mpango huo kwa wadau mbalimbali kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo amesisitiza kuwa bila ya wananchi kujiunga katika utaratibu wa TIKA itakuwa ni vigumu kumudu gharama za matibabu ambazo zinaongezeka kila kukicha.

"Jamani wenzetu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wametuletea mpango huu ni vyema tukaujadili kwa makini na kwa mtazamo chanya ili hatimaye Halmashauri ya Mji ianze utekelezaji wa suala hili…utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua ni mzuri na unakupa uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote," alisema Mkuu wa Mkoa.

Alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiingia kwenye matatizo mbalimbali yakiwemo ya madeni ama kuuza vitu vya nyumbani kwa ajili ya kupata fedha za matibabu hali ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa familia husika hivyo akasisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa TIKA ili kuondokana na matatizo hayo.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa hakusita kuutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha unabadilika au kubadili mbinu zake za uhamasishaji kwa kuwafuata wananchi ambao wako katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mbinu ambayo itarahisisha kuwafikia wananchi wengi zaidi na uchangiaji wake utakuwa ni rahisi tofauti na kumfuata mtu mmoja mmoja. 

"Endeleeni na uboreshaji wa huduma za matibabu na kuangalia ni namna gani mtamaliza au kupunguza tatizo la ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ili wananchi wasiwe na visingizio wakati wa kujiunga na mipango kama hii," alisema.

Aidha aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kuweka utaratibu mzuri wa uwekaji wa kumbukumbu za wanachama kwa kuwa ndizo zinazotoa picha halisi ya mahitaji yaliyopo ndani ya halmashauri ama mkoa kwa ujumla. 

Akizungumzia uboreshaji wa huduma za afya ndani ya Halmashauri hiyo, alimwagiza Mganga Mkuu kutumia fursa zinazotolewa na NHIF za mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa lengo la uboreshaji wa huduma za matibabu.

"Mbali na fursa ya mikopo hii pia ni vyema matumizi ya fedha zitokanazo na CHF/TIKA i zikatumika kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo asilimia 67 itumike kwa kununulia dawa, asilimia 15 itumike kwa uboreshaji wa huduma za afya na inayobaki ndo inaweza kutumika kwa shughuli zingine ambazo zinahusiana na masuala ya afya," alisema.

Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao uliwakilishwa na Meneja wa CHF, Constantine Makalla alisema kuwa lengo la Mfuko ni kuhakikisha kila halmashauri inaanzisha na kutoa huduma kwa kuwa na sheria ndogo ambapo hadi Desema 31, 2013 jumla ya Halmashauri 128 zilikuwa na sheria ndogo.

Alisema kuwa mipango ya NHIF kwa mwaka huu ni kuongeza uwigo wa wanachama, kuanza utaratibu wa kuzizawadia Halmashauri zinazofanya vizuri na uboreshaji wa daftari la CHF/TIKA na taarifa za wanachama wake nchi nzima.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment