Friday 14 November 2014

[wanabidii] UTAFITI WA TWAWEZA: KIKAANGO CHA LOWASSA NA CCM


Kuna kila sababu ya kuamini kwamba utafiti ulioendeshwa hivi karibuni na taasisi ya Twaweza na majibu yake kutolewa juzi, ni wa kichumia tumbo na umelenga kumkaanga Lowassa na chama chake, kwa maana ya kumpunguza mbio zake za kuelekea Magogoni na kukizika chama chake rasmi kabla ya 2015. Kwanini?
 
UTAFITI NI WA KICHUMIA TUMBO
Mosi, hakuna sababu maalum ya kuendeshwa kwa utafiti huo na wala hakukuwa na hitaji la kufanya hivyo katika kipindi hiki kigumu ambacho nchi yetu imegumbikwa na sintofahamu za kifisadi (refer Escrow, IPTL, Wizi wa fedha BoT, etc) na mkwamo wa kiuchumi kwa ujumla. Tafiti zote zinazofanywa lazima ziwe na sababu na zilenge kutatua tatizo fulani kwenye jamii (ghairi ya kulikuza). Utafiti huu wa Twaweza haukulenga kutatua tatizo lolote katika nchi hii zaidi ya kuongeza mkanganyiko ama kwa makusudi au kwa kutumiwa na kikundi kidogo cha wachumia tumbo kwa maslahi yao binafsi. Aidha, yawezekana ulilenga kuwaondoa wananchi kwenye reli ya kufuatilia vitendo vya kifisadi vinavyotendwa na kikundi hicho.
 
Pili, utafiti huo umeuliza wahojaji (respondents) maswali ambayo sio ya kitafiti. Kumuuliza respondent kama ni nani anaona angefaa kuwa rais wa nchi hii kwa kutamka jina tu bila kumwekea mipaka ya vigezo ni umbumbumbu mkubwa ambao umeonyeshwa na watafiti katika kuufanya utafiti wao uwe wa kisayansi zaidi. Ukimwachia respondent uhuru wa kutamka jina kwa akili zake binafsi, utaishia kupata majina ya mtu ANAYEJULIKANA ZAIDI na sio mtu ANAYEFAA KUWA RAIS. Zote ni mashahidi kwamba jina la Lowasa hutajwa sana kwenye vyombo mbali mbali vya habari (hasa humu ndani) sio kwa nia njema bali kwa nia ovu ya UFISADI wake. Hii ndio sababu anajulikana kwa wananchi wengi. Sasa unapokuja na utafiti unaotaja tu jina la mwanasiasa anayefaa kuwa rais bila kuweka vigezo unategemea wasimtaje Lowassa wakati ndiye wanayemfahamu zaidi kwa sababu ya UFISADI wake? Sasa swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza ni: je, kujulikana kwa Lowassa kwa sababu ya maovu yake katika jamii kunatosha kumfanya awe rais bora wa nchi hii? Jibu na HAPANA. Sasa huo utafiti kama sio wa kibwege ni nini?
 
Tatu, watafiti wanatuhumiwa kwamba wahojiwa wengi walikuwa wanachama wa chama kimoja cha siasa ambacho inaonekana kimepata kura nyingi kwenye utafiti huu na inasadikiwa kwamba matokeo ya utafiti huu yalikuwa compiled na kada maarufu wa chama hicho ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kutoka Kitivo Cha Sayansi ya Siasa. Kwa vyovyote vile na kwa tabia ya chama hiki, lazima matokeo yatakuwa yalichakachuliwa ili ku-meet interest za chama.
 
 
UTAFITI UTAMKAANGA LOWASSA NA CCM
Mosi, Lowassa amethibitika kuhusika katika matukio mengi ya kifisadi (refer ufisadi wa RICHMOND PLC) matukio ambayo yamelichafua jina lake na la chama chake kwa kiwango cha kutisha. Aidha Lowassa anamiliki mali nyingi sana ambazo upatikanaji wake unatiliwa shaka. Mtu huyu amekuwa akizunguka kwenye makanisa na misikiti na amekuwa akijipendekeza kualikwa kuhudhuria hafla mbali mbali, na kote huko tumemshuhudia akimwaga mabilioni ya fedha kwa lengo la kujitangaza bila kujali kwamba fedha hizo ni chafu. Lowassa hujinadi kwamba yeye sio mtu tajiri sana na kwamba anamiliki jumla ya ngombe wasiopungua 300 pale kijijini kwao Monduli. Na akiona wananchi wanambana sana hudai kwamba fedha hizo hupewa na "marafiki zake". Je hao marafiki zake ni kina nani na wanatarajia kuvuna nini kutoka kwake? Na ikiwa atapata madaraka yoyote katika nchi hii hao marafiki zake watanufaikaje na hizo fedha wanazommwagia kila kukicha? Hili ni swali ambalo watanzania wenye akili zilizotimia wanapaswa kujiuliza kabla ya kumshabikia mtu msiyemjua vizuri.
 
Pili, kuna baadhi ya wanachama wa CCM ambao wanamuona Lowassa kama fisadi aliyekubuhu na ambaye hapaswi kupewa madaraka yoyote katika nchi hii. Lakini pia kuna kundi kubwa la watu liko nyuma ya Lowassa, ambalo tayari limeishaanza "safari ya matumani" pamoja naye. Hapa ndipo pana kitendawili kigumu mno kinachopaswa kuteguliwa kwa uangalifu mkubwa sana. Kwanini? Kuna nadhari mbili katika utata huu.
 
Nadharia ya kwanza ni kwamba baada ya Lowassa "kuchanua" kwenye utafiti huu wa kichumia tumbo, kundi lililo kinyume chake litatumia nguvu nyingi sana kumwekea vihuzi ili kumzuia katika mbio zake za kuelekea Magogoni. Kwa hiyo, utafiti huu utakuwa umemuweka  Lowassa kwenye wakati mgumu zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Ndio maana baada ya majawabu ya utafiti huu kutoka, Lowassa yupo kimya kana kwamba bado majibu hayajamfikia. Bila shaka atakuwa kwanza anatafakari madhara ya utafiti huu na jinsi utakavyomletea athari HASI katika harakati zake za kisiasa.
 
Nadharia ya pili ni kwamba, wapambe wa Baba Yoyoyo, hasa wale wavivu wa kufikiri, wanaweza kumbwetesha akajiona amemaliza mbio na hivyo kumfanya apunguze kasi yake ya kuelekea Magogoni; na hapo ndipo atakapopitwa na wanariadha wengine wanaochanganya miguu yao kuelekea kunako Nyumba Nyeupe. Kwa maana hiyo basi, utafiti huu utakuwa umemuingiza mkenge bila kujua. Ndio sababu ninasema kwamba utafiti huu umebuniwa kiintelijensia na wabaya wa EL kwa ajili ya kumlewesha na kumfanya apunguze kasi ili wampite kirahisi.
 
Na tukijumlisha nadharia ya kwanza na ya pili bado jawabu lake litakuwa gumu sana kwa Bw Lowassa na baya zaidi kwa chama chake cha CCM. Kwanza, ikiwa Lowassa, atatoswa kwa sababu ya tope la ufisadi lililomganda mwilini, wafuasi wake wanaweza kuchukua UAMUZI MGUMU ambao utashuhudia kusambaratika na hatimaye kifo cha CCM. Pili, ikiwa pia atateuliwa kupeperusha bendera ya chama chake bila kujali kama ni fisadi (kama ilivyo kawaida ya chama hiki kuwakumbatia mafisadi), wabaye wake lazima watakinukisha…wataamua kumwaga mboga ili wote wakose! Hili nalo halitaiacha CCM salama. Nadhani mpaka hapo mtakuwa mmeona jinsi ambavyo Lowassa ataimegua na kuia CCM kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
 
 
HITIMISHO
Kwa wale wote ambao mmenisoma katikati ya mistari, mtakuwa mmeng'amua kwamba utafiti huu wa Twaweza (ambao ukiuangalia kwa macho ya makengeza unaweza ukadhani unambeba Lowassa na chama chake), ndio hasa utakaomzika Lowassa na CCM yake rasmi kabla ya 2015.
Siwezi kuonekana adui kwa kusema na kusimamia ukweli.
 
Nawasilisha.

 

0 comments:

Post a Comment