Sunday 27 January 2013

[wanabidii] "Tafuteni Kwanza Maendeleo Katika Elimu" - Jackson Makwetta


Subject: [UDADISI: Rethinking in Action] "Tafuteni Kwanza Maendeleo Katika Elimu"

HALI YA ELIMU KATIKA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA
(1961 – 2011)

Na
JACKSON MAKWETTA

(Watu wenye akili huweka akiba yao katika maarifa - Mithali 10:14)

II. VUGUVUGU LA UJENZI WA SHULE NA VYUO VIKUU NA MATATIZO YAKE

I.                        UTANGULIZI

1.              Nikiangalia matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini, machozi hunilengalenga hasa kutokana na kutambua ukweli kuwa ubora wa Taifa lolote lile hutegemea na ubora wa elimu itolewayo kwa watu wake.  Maana yake ni kwamba, Watanzania tukitaka kuharibu ubora wa Taifa, letu njia nyepesi ni kuua au kuharibu misingi ya kupatia na kutolea elimu bora.  Kwa hiyo Watanzania tukikiuka misingi ya kutolea na kupatia elimu bora misingi hiyo itatukiuka.  Pia soma viambatanisho vilivyoambatanishwa kwenye makala haya.

2.              Kuna wakati Tanzania ikisherehekea uhuru wake, hayati Mwalimu Julius K. Nyerere Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanzanaia aliulizwa swali lifuatalo na waandishi wa habari kutoka nje ya nchi.  Kitu gani hasa kinawafanya Watanzania msherehekee siku hii ya Uhuru wenu?   Hayati J.K. Nyerere aliwajibu kuwa Watanzania walikuwa wakisherehekea siku ile kwa sababu ya kuwa hai hadi siku ile.  Huenda jibu lile lilikuwa sahihi.  Hata sisi tungeulizwa swali kama lile leo bila shaka tungejibu kama alivyojibu hayati J.K. Nyerere.

Mwezi uliopita kulikuwa na makongamano mengi nje na ndani ya Chuo hiki, kuhusiana na suala hili na mengine mengi.  Kwa hiyo mimi sina geni katika suala hili, ila inawezekana kutoa mawazo yale yale kwa njia tofauti kama wasemavyo waswahili kitambaa kimoja lakini mivalio mbalimbali.

3.              Je hali ya elimu nchini ikoje?  Kuna wakati nchi yetu ilisifika sana kwa kufanikisha Elimu ya Msingi kwa kutumia njia za kimapinduzi chini ya ushauri wa mzee Nicholas Kuhanga.  Wakati huo Tanzania ilitoa Elimu ya Msingi na Elimu ya Kisomo bure kwa watoto na watu wazima wote.  Vilevile Serikali ilitoa elimu ya sekondari na ya vyuo vikuu kwa malipo kidogo.  Kumbuka elimu hiyo ilithaminiwa kote duniani.  Dosari kubwa katika utoaji wa elimu ya sekondari na ya vyuo vikuu ni kwamba, kwa muda mrefu hata baada ya Tanzania kupata uhuru iliendelea kutolewa kwa watu wachache sana.  Leo elimu ileile inatolewa kwa watu wengine zaidi na kwa gharama nafuu zaidi.
  
II.             VUGUVUGU LA UJENZI WA SHULE NA VYUO VIKUU NA MATATIZO YAKE

4.              Ni katika miaka ya hivi karibuni tu ndipo vuguvugu la ujenzi wa shule za sekondari za serikali, za binafsi na vyuo vikuu lilianza kujitokeza na kusababisha leo Tanzania kuwa na vyuo vikuu na vyuo vishiriki kufikia 40. Leo shule za sekondari na vyuo vikuu vinaota kama uyoga. Pongezi ziwaendee wananchi na wote waliohusika na ujenzi wa shule hizo. Kwa upande wa sekondari watu binafsi wanajenga shule hizi kwa kutegemea fedha zitokanazo kwa wazazi wa watoto wakati kwa upande wa vyuo vikuu watu binafsi wanajenga kwa kutegemea mikopo toka BODI YA MIKOPO. Kwa hiyo bila mikopo hiyo (Loan Board). Baadhi ya vyuo vikuu haviwezi kudumu.

5.              Hata hivyo mwamko wa wazazi kupenda elimu umesababisha elimu kupatikana kwa njia za ulanguzi. Shule za binafsi ni za watu wenye uwezo, kama zilivyo hospitali binafsi. Leo shule za serikali ndizo shule za watu wa kawaida. Tatizo jingine linatokana na wamiliki wa shule za binafsi ni kuwarubuni walimu wa shule za serikali ili wajiunge na shule zao na ili kuwapata huongeza mishahara na marupurupu mengine mengi. Matokeo ya kufanya hivyo ni shule za binafsi kufaulisha watoto vizuri kuliko shule za serikali. Leo baadhi ya wazazi wako tayari kupelekea watoto wao katika shule za binafsi hata kama wamechaguliwa kwenda katika shule za serikali. Wazazi hawaelewi kwa namna gani shule yenye wanafunzi zaidi ya 300 inaweza kuendelea kielimu wakati ikiwa na walimu watatu au wanne tu. Shule tunazo lakini zinakabiliwa na uhaba wa kila kitu (walimu, vitabu, maabara, vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, maktaba n.k.) Maneno ya kuzingatia hapa ni UHABA na UKOSEFU wa walimu wa masomo, huduma ya maji, umeme, zahanati, mabweni, viwanja vya michezo, vifaa vya michezo na kadhalika. Msamiati huu pia unatawala vyuo vikuu, vya ualimu, shule za Elimu ya Msingi, vyuo vya ufundi na kadhalika. NI UHABA NA UKOSEFU wa mahitaji katika kila ngazi ya elimu. Shule za sekondari za kata au shule za madiwani zote zinakabiliwa na uhaba na ukosefu wa mahitaji ya shule.

6.              Kutokana na UHABA NA UKOSEFU huo elimu inaporomoka KATIKA NGAZI ZOTE. Hii ndiyo hali ya elimu nchini. Watanzania wanaopenda ukweli wanajua ukweli huu. Kazi kubwa ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni kutafuta ukweli wa mambo. Vyuo visipofanya hivyo vitapoteza umuhimu wa kuwepo kwake. Tume ya elimu ya 1982 inasisitiza suala hili. Naomba wale ambao hawajasoma ripoti ya TUME YA ELIMU ya mwaka 1982 na mapendekezo ya tume yake waisome. Sehemu kubwa ya mapendekezo yale ni muhimu zaidi leo kuliko mwaka 1982. Inasikitisha kuona kuwa Watanzania wengi hatuna muda wa kusoma vitabu au maandishi! Tuna muda wa kufanya mambo mengine! Binafsi naamini kuwa TUME ya 1982 ilifanya kazi nzuri. Wajumbe wa tume ile wengi wao wangali hai. Kwa namna gani wanashirikishwa katika kuboresha elimu nchini ni swali zuri la kujiuliza. Kwa tabia ya Watanzaia si rahisi kuwashirikisha watu wengine katika mambo yetu. Kwa mfano, Mwalimu Nicholas Kuhanga aliyefanikisha UPE katika nchi yetu kwa nini tusimshirikishe katika uboreshaji wa elimu nchini?

7.              Leo shule za sekondari na vyuo vikuu vinaongezeka wakati ubora wa elimu unazidi kupungua. Kwa mfano, katika matokeo ya mwaka 2010 nusu ya vijana wa Kidato cha nne waliofanya mtihani wa Taifa hawakufaulu. Hata katika miaka mingine, vijana wengi wanafaulu kwa viwango vya chini yaani, divisheni 3 na 4 na idadi ya wale wanaoshindwa mitihani ya mwisho inazidi kuongezeka. (Tazama kiambatanisho) kuonyesha kuwa ubora wa elimu nchini unaporomoka. Labda wengine hawapendi kusikia maneno, kushuka kwa ubora au kuporomoka kwa elimu. Naomba watushauri tutumie maneno gani?

8.              Sisemi kuwa elimu imekufa bali nasema ubora wa elimu umepungua (vijana wengi kushindwa mtihani wa kidato cha nne). Pia tathimini iliyofanywa hivi karibuni kuhusu hali ya elimu katika nchi za Uganda, Kenya na Tanzania imeonyesha kuwa Tanzania inatoa elimu hafifu kuliko katika nchi za Uganda na Kenya. Ubishi kuhusu vigezo vilivyotumika katika zoezi hili unaweza kuendelea ila naomba tutenganishe utaalamu na siasa. Kwa mfano, kuna baadhi ya wanasiasa wanapendekeza kuwa mitihani ifutwe katika ngazi zote fulani za elimu. Lakini hawapendekezi njia gani zitumike katika kupima elimu itolewayo nchini. Hata hivyo sielewi lengo lao ni nini hasa. Watanzania tukikiuka misingi ya kutolea na kupatia elimu bora, misingi hiyo itatukiuka.

9.              Lazima tujiulize maswali yafuatayo kuhusu Elimu itolewayo katika nchi yetu: Tunataka nini katika elimu yetu .Tunataka elimu yetu itatue matatizo gani? Je elimu hii inatatua au inaongeza matatizo? Je tunataka elimu ya bure na ya lazima kwa watanzania wote na ifikie ngazi gani? (MSINGI AU Y A SEKONDARI AU VYUO VIKUU) Je kuna uhusiano gani kati ya maendeleo katika elimu na maendeleo yetu kiuchumi? Je, kwa namna gani BODI YA MIKOPO itaweza kukidhi mahitaji ya vyuo bila kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sera ya Elimu? Kwa nini watoto wa matajiri ambao tangu elimu ya awali, msingi na sekondari wamekuwa wakisoma katika shule za binafsi kwa gharama kubwa leo wanaomba mikopo na serikali inawapa mikopo hiyo. Tatizo hili halijatatuliwa.

III.           TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA ELIMU LAKINI

10.           Katika makala haya nazungumzia mafanikio na matatizo ya elimu katika miaka 50 ya uhuru wa Tanzania. Takwimu kuhusu idadi ya shule, vyuo, walimu, na wanafunzi zinapatikana kwa urahisi kutoka wizara husika. Takwimu hizo zinaonyesha kuongezeka kwa kila kigezo cha kutolea na kupatia elimu nchini. Nashauri tuzitumie vizuri taarifa hizo. Kwa mfano, idadi ya shule za sekondari za serikali imeongezeka sana. Hali kadhalika, idadi ya walimu wa shule hizo, lakini vipi uwiano kati ya walimu na wanafunzi katika shule hizi? Ukweli ni kwamba walimu ni wachache kwa uwezo wa kufundisha na kwa idadi yao. Kutokana na uchache na uwezo wao mdogo wanafunzi katika ngazi zote za elimu nchini hawapati "dozi" kamili ya elimu wanayotakiwa kupata hali inayosababisha wanafunzi kumaliza elimu wakiwa hawajapata "dozi" kamili ya elimu wanayotarajia kuipata. Kwa hiyo Watanzania tusishangae kwa nini nchi yetu ni ya mwisho katika utoaji wa elimu bora katika Afrika ya Mashariki. Kamwe vijana wetu hawataweza kupata elimu bora ya Msingi au ya Sekondari au Vyuo Vikuu kwa kukaa tu katika majengo yaliyoandikwa "Shule" au Chuo kikuu. Kamwe vijana hawataweza kupata elimu ya ngazi yoyote ile kwa njia ya OSMOSIS. Upatikanaji wa elimu bora una kanuni na misingi yake. Tukikiuka misingi ya utoaji elimu bora misingi itatukiuka. Kama elimu bora ni ufunguo wa maisha bora basi elimu mbaya ni ufunguo wa maisha mabaya.

IV.           TUNAPITA WAKATI MGUMU KATIKA MASUALA YA ELIMU

Watanzania tunapita wakati mgumu kiasi kwamba hata kubaki hapa tulipo ni kazi ngumu, kurudi nyuma ni kazi rahisi, kwenda mbele ni kazi ngumu zaidi. Breki za gari tulilopanda hazishikiki. Kuna hatari ya gari kurudi nyuma. Gari hili ni nchi yetu ya Tanzania. Nchi ikirudi nyuma tutapoteza hata mafanikio kidogo tuliyoyapata katika miaka 50 ya uhuru. Hali inazidi kuwa mbaya. Vyanzo vya maii vinakauka, nchi inakosa umeme, gharama za huduma muhimu zinazidi kupanda, vijana wanakosa aiira na nguvu kazi yao haitumiki. Maana yake ni kwamba mapendekezo yoyote ya kuboresha elimu lazima pia yaonyeshe nchi itapata wapi fedha ya kufanyia kazi hiyo? Kwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa ushuru na kupunguza rushwa, Tanzania ingeweza kupata fedha za kutosha za kuboreshea elimu yake. Fedha ya misururu ya magari makubwa yaendayo Zambia, Malawi na Congo kila siku inatumikaje? Watu wamepata wapi fedha ya kununua utitiri wa malori, magari madogo na mapikipiki yanayosababisha barabara zisipitike katika miji yetu? Pamoja na umaskini wetu lazima Watanzania tujue kuwa maendeleo yetu yataletwa na sisi wenyewe kwa bidii, maarifa, nidhamu, na kwa kuiitegemea. Serikali ina uwezo mkubwa wa kutunga sheria na kuweka taratibu za kusimamia uchumi lakini haina uwezo wa kusimamia taratibu zake. Ni nchi zenye serikali imara kama Marekani ndizo zinaweza kusimamia uchumi wake. Kwa mfano serikali bila kupanga imekabidhi uchumi wa Tanzania kwa watu wachache ambao inashindwa kuwatoza kodi. Kwa nini tusichukue hatua zifuatazo:-

·      Tulipe kodi na ada za shule kwani kujitawala ni kujitegemea
·      Tufufue au kutilia mkazo siasa na Elimu ya Kujitegemea.
·      Tuchangie gharama za maendeleo kwa kufanya kazi ndogondogo za mikono
·      Kwa nini kazi ya kufyeka nyasi katika shule isifanywe na wanafunzi?
·      Tusimamie vizuri shughuli zote za maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha.
·      Serikali isimamie elimu itolewayo nchini ili kuondoa Ulanguzi, Utapeli na Uchakachuaji.
·      TCU iongezewe madaraka zaidi kuhusiana na vyuo vikuu.
·      Tuongoze ufanisi katika kazi zetu na kupenda kufanya kazi.
·      Tubane matumizi na kutumia vizuri kila senti tunayopewa
·      Tuache rushwa, ufujaji mali na uvivu
·      Tupunguze sherehe, tafrija, mikutano, semina na kongamano
·      Tutumie vizuri wakati
·      Tupunguze michango ya starehe (Inner party, Send-off, Bag Party, Kitchen Party na Wedding party)
·      Tupunguze migomo badala yake tujue kwa undani sababu ili kama ni uzembe hatua kali ziwe zinachukuliwa kwa wahusika mapema.
·      Kama idadi ya wanafunzi wa kwenda vyuo vikuu huwa haijulikani hadi mwezi mmoja kabla ya vyuo kufunguliwa tunategemea nini. Tujisahihishe.  Nani alaumiwe? Kama migomo huzaa matunda kwa nini ifutwe.
·      Tuanzishe michango ya maendeleo ya elimu badala ya michango ya Harusi.
·      Tubadili mwelekeo wetu au mtazamo wetu kuhusu umuhimu   wa mambo (mindset). Kwa mfano kuongeza ubora wa elimu bila kuwashirikisha wananchi katika gharama hizo.

11.           Kama kuna wakati mzuri wa kubadili mambo au kufanya mapinduzi katika elimu basi wakati huo ni sasa.  Mwamko wa watu wa kuelewa maana na umuhimu wa kutoa elimu kwa watoto wao umeongezeka.  Matatizo ni mengi, na hakuna nchi isyo na matatizo.

12.           Elimu kwanza.  Inaelekwa treni la elimu liko nje ya reli
Watanzania tunawezaje kulirudisha treni katika njia yake.  Tazama katika baadhi ya shule za Elimu ya Msingi bado baadhi ya wanafunzi wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika na ½ ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanafeli mtihani wa mwisho.  Kama watoto wanamaliza elimu ya msingi bila elimu ya msingi wataendeleaje mbele?  Ni Elimu gani hii ambayo haimwezeshi mwanafunzi kuwaelezea watu kile anachokijua au kubuni na kuibua mambo, kufikiri kisayansi, au kupeleleza na kuchambua mambo, kuumba vitu, kutafuta njia sahihi za kutumia katika kutatua matatizo yake.  Tukubali kuwa elimu yetu ni butu.  Tofauti na wenzao walioachwa nyuma baada ya kumaliza elimu ya Msingi hawa hawawezi kulima, wala kupalilia mimea isipokuwa kupiga simu, kupiga stori, kukaa vijiweni, kuzurura mitaani na kucheza disco. Lakini ajabu ni kwamba vijana hawa wanataka makuu, wanataka wakipanda mahindi asubuhi wavune jioni.  Mara wakianza kazi wanataka kuwa na simu pana, gari la kuendea kazini na nyumba nzuri ya kuishi.  Pale wanapokosa vitu hivi hupauka akili na   huwafanya wafanye yasiyotegemewa.  Vijana hawa ni wengi na wanaongezeka kila mwaka. Serikali isipowatumia vijana hawa watu waovu watawatumia.

V.             HAJA YA KUTUMIA UZOEFU ULIOKO NCHINI

13.           Duniani hakuna kidumucho isipokuwa mabadiliko.
Watanzania wana haki ya kupata kilicho bora katika nchi yao ikiwa ni pamoja na kuwatumia watumishi bora waliostaafu na vijana wenye akili kwa faida ya nchi yao.  Tabia ya kuwatenga au kutowatumia watu hawa ni tabia mbaya inayodidimiza nchi yetu.  Kuwatenga watu kwa sababu za kisiasa au kwa sababu ya kuwaogopa au kwa sababu ya roho mbaya ni ufisadi wa aina yake.  Wenzetu huko Ulaya ambako tunaiga mambo mengi wanafanya hivyo. Si vema kwa baadhi ya Watanzania kuonekana hawatakiwi au wanaishi kwa hisani ya watu fulani. Wale wenye uwezo au madaraka wanaweza kumuua raia yoyote au kumtesa au kumtenga kwa sababu zozote zile ila hawawezi kunyang'anya utaifa na uraia wake, hawawezi kumfukuza katika nchi yake.

14.           Tume ya elimu chini ya uenyekiti wangu ilichambua hali ya elimu iliyokuwa ikitolewa wakati ule hapa nchini.  Pia ilitembelea nchi nyingi zilizoendelea na zisizoendelea ili kujifunza taratibu zao za utoaji elimu. Tume ilijifunza mengi na kutoa mapendekezo kwa serikali.  Ni muda mrefu umepita (1982). Kama serikali inatekeleza au haitekelezi mapendekezo ya Tume mimi sina la kufanya.  Ajabu tangu nitoe ripoti ile sijawahi kuitwa au kuulizwa lolote na wizara husika kuhusu elimu isipokuwa ninyi leo.  Kwa maoni yangu hii ni kasoro kubwa katika nchi yetu.  Nchi haifaidiki na utajiri wa uzoefu wa watu walio nje ya mkondo wa serikali kwa sababu ya sababu zisizoeleweka (wataalamu majaji, wanajeshi, walimu, mawaziri hawatumiki).  Watu hawa ni hazina ya nchi na si tishio kwa yeyote.  Nchi hii ni yetu sote.  Tusiwaenzi watu waliostaafu baada ya kufa kwa kuhudhuria mazishi yao.  Tusisubiri watu wafe ndio tuseme mazuri yao.

VI.           BAADHI YA VIKWAZO VILIVYO MBELE YETU

Huenda mapendekezo ya Tume ya MAKWETTA yamepitwa na wakati.  Hofu yangu ni kwamba tangu Tume ile itoe mapendekezo yake kwa serikali sijawahi kuitwa kutoa ushauri au ufafanuzi wowote kuhusu mapendekezo ya Tume.  Napendekeza iundwe Tume nyingine kwa madhumuni yaleyale ili kukidhi mazingira ya Karne ya 21.  Tusichezee elimu madhara ya uharibifu yatakuja jitokeza miaka michache ijayo.

15.           Hapa chini natoa mapendekezo lakini mapendekezo haya yatafanikiwa tu kama baadhi ya mambo yaliyoko yatabaki kama yalivyo.  Mabadiliko katika baadhi ya mambo yaliyoko leo yataathiri nguzo muhimu za kutolea na kupatia elimu.  Kwa hiyo mapendekezo yoyote kuhusu mabadiliko katika mfumo wa elimu  nchi nzima yazingatie mambo yafuatayo:-

    Kuongezeka kwa idadi ya watu ambako kutasababisha kukua kwa umaskini.
    Kuweko kwa watu wenye uzoefu na kutotumia uzoefu wao.
    Kupungua au kukosekana kwa maji yanayohitajika na binadamu, wanyama na mimea (ukame) kutokana na sababu mbalimbali.
    Kuongezeka kwa milipuko ya magonjwa ya hatari na vifo.
    Kuharibika na kuchafuka kwa mazingira (mito na vijito vyote kukauka).
    Kushuka kwa uchumi kutokana na kupungua kwa mafuta, gesi, maji, madini na kadhalika.
    Uhaba au kukosekana kwa chakula (njaa).
    Kukua kwa umasikini na kukosekana kwa amani.
    Kukosekana kwa ajira na kutotumika kwa nguvukazi.
    Kustawi kwa rushwa na utawala mbovu.
    Ubaguzi wa kipato (maskini na matajiri) na wa rangi. (watu weusi kuzuiwa kwenda Ulaya).
    Kurudi kwa ukoloni na utumwa mamboleo
    Wenyenavyo watashika mali na utawala wan nchi
    Kustawi kwa ukoloni mamboleo.  Nchi itageuka nchi ya ombaomba.  Kesho ni leo na leo ni kesho.  Kwa hivo kila jambo tufanyalo au tusilofanya leo linajenga au kubomoa misingi ya maendeleo yetu ya kesho.  The future is now.

VII.         HATUA ZA KUCHUKUA ILI KUZUIA KASI YA KUPOROMOKA KWA ELIMU NCHINI

16.           Kobe hufanya maendeleo pale tu anapothubutu kutoa shingo yake  nje ya gamba lake.  Kwa hiyo pamoja na yote yanayosemwa kuhusu elimu, ni vigumu sana kutabiri kuhusu mambo yatakavyokuwa kesho.  Labda  tutumie ujuzi na uzoefu wetu katika  kuelezea baadhi ya viini vya matatizo katika shule na vyuo vyetu:-

    Wizara ya Elimu iunde haraka Tume ya Elimu ili kutizama matatizo ya elimu na mwelekeo wake kwa lengo la kuzuia Tanzania kuachwa nyuma kielimu au kuzuia kuporomoka kwa elimu.
    Serikali isimamie na kuratibu elimu katika ngazi zote ili kuzuia biashara na ulanguzi katika elimu chini.
    Kutokana na uwezo mdogo wa walimu hasa walimu wa shule za sekondari, yaanzishwe mafunzo ya kuboresha elimu yao wawapo kazini.
    Serikali itizame upya sera ya kugharamia elimu nchini ili kuhakikisha kuwa fedha ya umma inatumika vizuri na inatolewa mapema kwa wahusika.
    Hatua za kuboresha elimu zianzie katika vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na shule za msingi na mafunzo kazini.
    Sekta ya ukaguzi iimarishwe kwa kuongeza wakaguzi na vyombo vya usafiri.
    Migomo shuleni na vyuoni inaathiri sana maendeleo ya elimu nchini licha ya kuharibu mali ya umma. [Sera ya Mikopo bado hafifu]
    Wanafunzi washirikishwe katika kubana matumizi shuleni na vyuoni kwa kufanya kazi ndogondogo zisizopoteza muda wao mwingi.
    Wanafunzi wajihusishe na ubora na usalama wa mazingira ya shule na vyoo badala ya kubaki na 3Ks tu yaani KUSOMA, KULA NA KULALA.
    Wanafunzi washiriki katika masuala ya usafi, usalama na maendeleo ya shule au vyuo vyao.
    Baadhi ya wazazi watatakiwa kulipa ada yote katika vyuo vikuu ili kupunguza kuelemewa kwa serikali katika suala hili.
    Udhaifu wa serikali usielezwe kwenye vyombo au taasisi zisizohusika (BODI YA MIKOPO) na utoaji wa huduma fulani muhimu.
    Taarifa kuhusu uwezo wa wazazi wa watoto kiuchumi zijulikane mapema.
    Ziundwe BODI ZA ELIMU katika ngazi za wilaya  ili kusaidia Wizara ya Elimu  kusimamia kwa kuwahusisha  wadau wote wa Elimu Wilayani.
    Serikali itizame upya sera kuhusu lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni.  Lugha ya "Kiswakinge" inayotumika leo shuleni inaathiri elimu.  Leo Kiingereza ni Kiswahili cha dunia!
    Serikali iwe na utaratibu wa kuendelea kuwatumia walimu waliostaafu (Sera au Mwongozo)
    Liingizwe somo la Maadili katika ngazi zote za kutolea elimu nchini.
    Itolewe tafsiri sahihi kuhusu maana ya shule na kuhusu maana ya shule na mahitaji ya shule, chuo.  Shule au chuo ni majengo, walimu bora na wa kutosha, vifaa bora vya kutosha n.k.
    Sera ya elimu iwe wazi katika ngazi zote.  Je ni kutoa elimu ya bure kwa watoto wote kuanzia Elimu ya Awali, Msingi (UPE) elimu ya Sekondari (USE) na ya a vyuo vikuu (UUE) na kadhalika.

VIII.       HITIMISHO

17.           Hakuna kidumucho isipokuwa mabadiliko. Kama elimu bora ni ufunguo wa maisha bora basi elimu mbaya ni ufunguo wa maisha mabaya.  Elimu itolewayo katika Tanzania ni ufunguo wa maisha bora au ni ufunguo wa matatizo?  Je, vijana wetu wanasoma kwa malengo?  Je, Elimu itolewayo nchini inakidhi malengo yao?  Kama haikidhi kwa nini umma wa nchi hii uendelee kugharamia elimu isiyo na manufaa?  Kama shule na vyuo vyetu havifundishi kufikiri, kudadisi, haviumbi kazi bali vinaibua tamaa ya kupenda starehe na kazi nyepesi. Tatizo kubwa la nchi hii ni serikali kutofuatilia, wala si tatizo la kukosekana kwa sera.  Hili ni taifa la wasemaji maneno na siyo taifa la watekelezaji.  Mapendekezo ya tume ya MAKWETTA ya mwaka 1982 licha ya kukubalika na serikali yamewekwa kabatini.  Hayatekelezwi kwa sababu wahusika hawataki kupata "taabu".  Baada ya kuichambua tena ripoti ya TUME mimi naona bado yana manufaa hadi leo.

18.           Sasa naelewa kwa nini V.I Lenin alisema matumizi ya nguvu ni lazima kwa mama aliyefikia siku za kujifungua. Kwa maneno yake Lenin alisema 'force is a midwifery of any society pregnant of a new one'. Kwa maoni yangu Tanzania ni kama mama mjamzito ambaye siku zake za kujifungua zimefika lakini hajifungui. 
Bila kumpasua mama, wote wawili mama na mtoto watakufa.  Kwa hiyo:

·               Mama akipasuliwa wote wawili wanaweza kuokolewa (au mmoja wao).  Tanzania inahitaji kupasuliwa ama la sivyo itaendelea kudidimia kiuchumi milele.
·               Nchi ya Tanzania inahitaji kiongozi shupavu mwenye msukumo, mwenye akili na siyo mkusanyaji au mlafi, mwaminifu, mchapakazi mpenda haki na anayeona mbali.
·               Rushwa na utawala usiothubutu. Tanzania ni kama mjamzito: Inahitaji kupasuliwa  ili kuwaendeleza watanzania kiuchumi.

19.           Nimekosa focus kwa sababu kichwa cha habari ni kikubwa na hakiko wazi kwa hiyo kama makala haya hayakukidhi lengo letu naomba tusameheane.  

Tafuteni kwanza maendeleo katika elimu na mengine yote yatafuata.

Twende pamoja
Tushirikiane;
Tuboreshe elimu,
Tujenge nchi yetu, Tanzania




--
Posted By Blogger to UDADISI: Rethinking in Action at 1/27/2013 01:22:00 PM


0 comments:

Post a Comment