Wednesday 30 January 2013

Re: [wanabidii] Upembuzi yakinifu finyu na upendeleo huenda ndio sababu ya uamuzi tata kujenga bomba la gesi ya Mtwara

Leo Mtwara sawa lakini wale ndugu zangu wa Nyamongo
walipokuwa wanadai kupata huduma kwa wawekezaji
pale mgodini wengi wetu tuliwashangaa na kuwaona
hawana uelewa, na si wazalendo. huu ni mwanzo na kama
serikali haitakuwa makini na hili basi ijue ndo mwanzo
wa kila kulipo na raslimali tunazoziita za Taifa kuanza
kuwafaidisha wakazi wa eneo linalozunguka raslimali
hiyo kabla ya kuanza kufikiria eneo kubwa kama nchi.
Huwa sipati picha sahihi mfano unapofika Geita na mazimulizi
ya Geita na hali halisi ya Geita, Viongozi wetu wajaribu
kuweka uhalisia kuliko kudanganyana wakati athari
za uzalishaji huo huwa umewadhuru wananchi wa ukanda
huo zaidi ya sehemu zingine wakati faida huwa imelalia
eneo ambalo halikuathirika.



From: Yona F Maro <oldmoshi@gmail.com>
To: Wanabidii <wanabidii@googlegroups.com>
Sent: Thursday, January 31, 2013 1:25 AM
Subject: [wanabidii] Upembuzi yakinifu finyu na upendeleo huenda ndio sababu ya uamuzi tata kujenga bomba la gesi ya Mtwara

Upembuzi yakinifu finyu na upendeleo huenda ndio sababu ya uamuzi tata
kujenga bomba kusafirisha gesi ya Mtwara kuja Dar es Salaam

Na Dr Antipas Massawe : massaweantipas@hotmail.com


Mgogoro kama huu wa wanamtwara kutoridhika na gesi ya Mtwara kus
afirishwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme huko Dar es Salaam badala
ya Mtwara kabla ya kusambazwa mikoa mingine hapa Tanzania haujawahi
kutokea kwenye vipindi vya utawala chini ya serikali ya awamu ya
kwanza, ya pili na ya tatu hapa nchini. Mgogoro kama huu haujawahi
kutokea kwa sababu maamuzi ya Serikali za awamu hizo kuhusu matumizi
ya raslimali za taifa au mapato yatokanayo na raslimali hizo
yalizingatia kujenga fursa sawa na faida kubwa zaidi kwa watanzania
wote bila upendeleo. Hivyo ndivyo ilivyokuwa na wananchi wote
walielewa hivyo: mambo yanapangwa na kutekelezwa na Serikali bila
upendeleo wowote kwa eneo fulani na Rais alikuwa ni Rais wa nchi nzima
na sio wa mkoa, wilaya au kijiji alikotoka.

Mikoa iliyokuwa imebaki nyuma kuwekewa miundo mbinu ya maendeleo kama
vile gridi za umeme, reli, barabara nzuri, mashule, hospitali na
kadhalika ilielewa wazi kwamba mikoa yote haiwezi kupata kwa wakati
mmoja na fursa zitakapotokea itakuwa ni zamu na wao kupatiwa hiyo
miundo mbinu muhimu kwenye kujitafutia maendeleo yake na ya taifa kwa
ujumla.

Kwa mfano, wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wamevumilia kuishi kwa
muda mrefu bila kunungunika kwa kutokuwa na umeme wa uhakika na sehemu
ya gridi ya umeme ya taifa kwa sababu walielewa vianzio vyenye umeme
wa kutosha na karibu na mikoa ya kusini havikuwepo ili kuwezesha na
wao kupatiwa umeme wa uhakika na kuunganishwa na gridi ya taifa
wakiamini fika kwamba fursa itakapotokea wao ndio wangepewa kipaumbele
cha kwanza kupatiwa umeme wa uhakika na kuunganishwa na gridi ya
taifa.

Pia, wananchi hawa wamevumilia kuishi kwa muda mrefu bila kuwa na
kiungo cha reli au barabara nzuri kati ya bandari yake na masoko ya
nchi nyingine kusini mwa Bara la Afrika ambayo yako karibu zaidi na
Mtwara kuliko yalivyo na Dar es Salaam wakielewa fika kwamba fursa
itakapotokea kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni wao kujengewa reli na
barabara nzuri kuunganisha bandari ya Mtwara na masoko ya nchi
nyingine kusini mwa Bara la Afrika ili na ukanda wa Mtwara uweze
kufaidi bandari ya Mtwara kama ukanda wa Dar es Salaam unavyofaidi
bandari ya Dar es Salaam.

Kwa hiyo ni matarajio ya watanzania wengi wanaojumuisha wanamtwara
kwamba matumizi ya gesi asilia nyingi iliyopatikana huko Mtwara na
Lindi na maeneo yake ya karibu yangelenga kwanza kuipatia mikoa hii ya
kusini mwa Tanzania umeme wa uhakika na kuiunganisha kwenye gridi ya
taifa kwa kuhakikisha mitambo ya uzalishaji umeme utokanao na gesi
asilia ya Mtwara inajengwa huko huko Mtwara na gridi mpya ya
kusafirisha umeme uliozalishwa inajengwa kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam kupitia Mikoa ya Lindi na Pwani.

Pia ni matarajio ya wengi kwamba viwanda vinavyotumia gesi asillia ya
Mtwara na Lindi kama mali ghafi vingejengwa kwanza Mtwara na Lindi ili
kupunguza gharama za uzalishaji na kukuza ajira ndani ya mikoa hii
iliyobaki nyuma katika ujenzi wa sekta ya viwanda.

Pia ni matarajio ya wengi kwamba kipaumbele cha kwanza kwenye matumizi
ya pato la taifa litakalotokana na uchimbaji wa gesi asilia huko
Mtwara na Lindi kitakuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa reli na barabara
nzuri kuunganisha bandari ya Mtwara na masoko ya nchi nyingine kusini
mwa Bara la Afrika yaliyo karibu zaidi na Mtwara kuliko yalivyo na
bandari Dar es Salaam ili na ukanda wa Mtwara uweze kufaidi bandari ya
Mtwara kama ukanda wa Dar es Salaam unavyofaidi bandari ya Dar es
Salaam.

Ni wazi kabisa kwamba vipaumbele vilivyotajwa hapa vimelenga kuleta
faida kubwa zaidi kwa watanzania wote na sio wanamtwara peke yao na wa
kulalamika kutokana na vipaumbele hivyo kupewa chaguo la kwanza
hategemewi kuwepo.

Uamuzi wa kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia ya Mtwara kwenda
kuzalisha umeme Dar es Salaam haukulenga kuipatia mikoa ya Mtwara na
Lindi umeme wa uhakika wala kuiunganisha na gridi ya Taifa mikoa hiyo
iliyosubiria kwa kitambo kirefu na badala yake umelenga kuboresha
uwezo wa miundo mbinu ya umeme ndani ya Mikoa ambayo tayari
imeunganishwa na gridi ya umeme ya Taifa.

Inaelekea Mkoa wa Dar es Salaam umependelewa dhidi ya mikoa ya Lindi
na Mtwara iliyostahili ipewe kipaumbele cha kwanza cha kupatiwa umeme
wa uhakika na kuunganishwa na gridi ya Taifa kwenye uamuzi huu
uliofanywa na Serikali kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia ya
Mtwara kwenda kuzalisha umeme Dar es Salaam na inawezekana upembuzi
yakinifu haukufanyika kikamilifu ili kubaini matumizi yatakayokuwa na
faida kubwa zaidi kwa watanzania wanaojumuisha wanamtwara kati ya
matumizi yote mbadala ya gesi ya Mtwara yanayojumuisha uzalishaji wa
umeme wa gesi asilia Mtwara na ujenzi wa gridi mpya ya kusafirisha
umeme huo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam(1) na ujenzi wa bomba la
usafirishaji wa gesi aslia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji wa umeme
mkoani Dar es Salaam (2)..

Mradi huu wa kuendeleza gesi asilia ya Mtwara ni mradi mkubwa sana
unaogharimu fedha nyingi na kama upembuzi yakinifu haukufanyika
kikamilifu na matokeo yake ikawa ni kosa uamuzi wa kujenga bomba kwa
ajili ya kusafirisha gesi ya Mtwara kuja kuzalisha umeme Dar es Salaam
basi itatugharimu mabilioni ya dola za marekani ambazo tungepata kama
faida kwa kipindi chote cha uhai wa mradi na kama kumekuwepo upendeleo
kwa Mkoa wa Dar es Salaam dhidi ya Mikoa ya Mtwara na Lindi (iliyobaki
nyuma sana kwenye kuwekewa miundo mbinu ya maendeleo) basi hii itakuwa
ni kuhatarisha umoja na kudhoofisha kuaminiana miongoni mwa wa
watanzania wa maeneo tofauti tofauti hapa Nchini.

Inawezekana muda mfupi sana unaohitajika kwa ajili ya ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya uzalishaji wa umeme
Mkoani Dar es Salaam ndiyo kigezo muhimu kilichotumika kuamua gesi
asilia ya Mtwara isafirishwe kwa bomba kuja Dar es Salaam kuzalisha
umeme badala ya kuzalisha umeme huko huko Mtwara na gridi mpya ya
umeme ikajengwa kuuleta Mkoani Dar es Salaam kupitia Mikoa ya Mtwara,
Lindi na Pwani, lengo likiwa ni la kisiasa: kukamilisha mradi kabla ya
uchaguzi mkuu wa 2015. Kuna msemo usemao haraka haraka haina Baraka na
njia fupi mara nyingi haifikishi kwenye lengo.

Ni matumaini Bunge letu tukufu (kwa niaba ya watanzania wote
wanaojumuisha wanamtwara) litahakikisha kuuchunguza huu mradi mgogoro
wa usafirishaji wa gesi asilia ya Mtwara kuja Mkoani Dar es Salaam kwa
ajili ya uzalishaji wa umeme ili kuhakikisha upembuzi yakinifu
ulifanyika kwa kuhusisha matumizi yote mbadala ya gesi ya Mtwara na
vipengele vyote vinavyojumuisha faida kwa kipindi chote cha uhai wa
mradi na kwamba upendeleo kwa Dar es Salaam dhidi ya Mtwara na Lindi
haukuwepo.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com  Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.




0 comments:

Post a Comment