Wednesday, 1 January 2014

Re: [wanabidii] MAONI YA RASIMU YA KATIBA , MLIZINGATIA MAONI YA NANI, WARIOBA?

Kumbe hata wasomi hawana busara. Mwl wa chuo kikuu Sabatho msimamo wako ni upi? Kwasababu hatimaye lazima tuwe na serikali. Mimi sijawahi kuona wala kusikia Muundo wa Muungano ambao nchi mbili ambazo moja ina madaraka kamili, nyingine inaachia madaraka yake. Mwl fanya utafiti zaidi alafu uje na mifano ya MIUNGANO anzia EU, AU, USA, UK alafu atwambie kama nchi zote zinalingana kwa raslimali na namna zinavyoendesha gharama za miungano yao. Atwambie kwanini Muungano wa iliyokuwa Urusi ulikufa? Mimi nadhani Muungano wetu kama unatuuma sana iwe serikali moja kama hilo ni gumu basi dawa ni kwamba kila nchi iwe huru na madaraka kamili. Tunaomba Mwl asituchanganye kabisa katika hili. Tume ilikuwa na watu 34 toka pande zote tafadhali asimtwishe mzigo mzee wetu Warioba tume imefanya kazi yake Mwl SABATHO asilete siasa zake za kiitikadi hapa, kama watu walishinikiza walitaka maoni yao yasikilizwe, kama walivyofanya wale waliotaka serikali mbili na kuzidiwa hoja.


Send from Samsung Mobile



-------- Original message --------
From: Abdalah Hamis <hamisznz@gmail.com>
Date:
To: wanabidii@googlegroups.com
Subject: [wanabidii] MAONI YA RASIMU YA KATIBA , MLIZINGATIA MAONI YA NANI, WARIOBA?


MLIZINGATIA MAONI YA NANI, WARIOBA?

·         Tume imechakachua maoni ya Wazanzibari.

·         Watu elfu 16 kuamua hatma ya taifa la watu milioni 45.

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Ilikuwa majira ya saa 11 jioni, tarehe 30 Desemba 2013, muda mchache baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukabidhi Taarifa yake pamoja na rasimu ya pili ya katiba kwa marais wa Muungano na Zanzibar, simu yangu ya kiganjani iliponiashiria kuwa nimepokea ujumbe. Nikausoma: "Haujambo? Vipi, siku zako za mwisho zikoje?"  Rafiki yangu wa Kijerumani aliyekuja hapa nchini alitaka kujua nimejiandaaje kuondoka nchini siku chache zijazo kwa ajili ya masomo ya juu. Nami kwa uchokozi nikamjibu, "Unaulizia siku za mwisho, unanitakia kifo?" 

"Nilijua tu utasema hivyo", alijibu. Kisha akalipua bomu ambalo lilinifanya nidondoshe machozi: "Nimerudi kutoka Zanzibar leo. Ni kuzuri, na watu wake ni wakarimu kama wa huku Dar. Ama kweli nchi yenu imebarikiwa. Mna kila aina ya utajiri, tangu maliasili hata umoja na ukarimu!"

Eti huyu ndugu anadhani Wabara wanajivunia rasilimali na vivutio vya Zanzibar. Bila shaka huko Visiwani pia aliwasimulia mengi kuhusu mlima Kilimanjaro na uzuri wa Bara na kuwaambia ni vyao. Maneno "nchi yenu" na "umoja" yalijirudiarudia akilini mwangu. Nilisikia mwili ukinisisimka, moyo ukanidunda, kijasho chembamba kikanitoka huku machozi yakidondoka. Mjerumani huyu alikuwa amenisimulia hadithi nyingi za kwao, na namna ukuta wa Berlin ulivyoangushwa mwaka 1989, na Wajerumani wakaiunganisha nchi yao.

Hivyo nikamjibu kijana huyo, "Labda hukukosea kunitabiria kifo. Hivi karibuni naelekea kufa kama Mtanzania, na kuzaliwa upya kama Mtanganyika. Ama kweli, sijui mlitumia uchawi gani kuturoga. Mpaka sasa tunatukuza mabaki ya ukoloni."

Akanipa matumaini, "Usikate tamaa rafiki. Wapenda Muungano endeleeni kupambana. Tanzania yenye marais watatu, na Afrika yenye marais 54 haina mustakabali katika dunia ya leo."
Hebu nieleze, ewe msomaji wangu, ingekuwa wewe ungejisikiaje? Huyu ndugu sio Mwafrika. Ni Mjerumani. Anaihurumia Afrika kwa kuendeleaza siasa za utengano. Yeye anajivunia kwamba nchi yake imeungana, na wanapigana kuunganisha Ulaya. Huku kwetu ndio kwanza tunazalisha vi-nchi, halafu tukitegemea tutakuwa na nafasi katika dunia ya leo?

Pengine kilichoniumiza zaidi sio maneno ya heri toka kwa mzungu huyo. Ni maneno niliyoyasikia katika hotuba ya Jaji Joseph Sinde Warioba, wakati wa makabidhiano ya taarifa ya tume. Kabla sijaichambua nitaomba tukumbushane kitu kimoja: Wakati wa uzinduzi wa rasimu ya kwanza, jaji Warioba alisema kuwa uamuzi wa Tume wa serikali tatu ulizingatia maoni ya watu walio wengi. Baadaye, na hasa baada ya kugundua kuwa mabaraza ya Katiba yamejaa wajumbe wa chama tawala, alibadili msimamo na kusema kuwa katika rasimu ya pili uamuzi wa Tume hautaangalia tena uwingi wa watu bali uzito wa hoja! Alidiriki kuwaambia wajumbe wa mabaraza ya Katiba wajadili mambo mapya, kwani ya zamani yote Tume inayo na hakuna haja ya kuyarudia. Kwa maana nyingine, aliwatisha wajumbe kurudia suala la Muungano, huku akijua wazi kuwa masuala ya msingi kuhusu maisha ya wananchi kama elimu, maji, afya, ardhi, serikali za mitaa n.k hayakuwa masuala ya Muungano, na kuyajadili kwake kungetegemea muundo wa utakaoundwa.

Ilipotoka rasimu ya kwanza, tupo tuliohoji uhalali wa Tume kupendekeza serikali tatu. Je, ilifikiaje uamuzi huo? Ilizingatia maslahi ya nani? Maswali hayo yalikosa majibu kwani Tume haikuwa imetoa ripoti. Ni ripoti ya Tume ndiyo ingetuondoa katika giza.Na sio kweli kwamba tume yoyote hufikia kutoa mapendekezo kwa kuzingatia idadi ya wananchi waliozungumza. Tume ya Nyalali ilipendekeza vyama vingi licha ya kuwa takribani ya asilimia 80 ya watoa maoni walipendekeza tuendelee na mfumo wa Chama kimoja. Hali kadhalika, Tume hiyo ikapendekeza serikali tatu licha ya kuwa watoa maoni wengi walitaka tuendelee na serikali mbili. Uzoefu huu unatuambia kwamba kazi ya Tume ni kusikiliza maoni na kisha kuyafanyia uchambuzi wa kina kwa kuzingatia hali halisi ya nchi na dunia pamoja na misukumo inayowafanya watu watoe maoni ya aina fulani.

Kwa uzoefu ambao nchi iliupitia kutokana na utawala wa kiimla wa chama kimoja pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yakitokea duniani, haikuwa busara kuendelea na Chama kimoja hata kama ndiyo yalikuwa matakwa ya wengi. Lakini watoa maoni wengi ni watu ambao walikuwa wameaminishwa na chama tawala kuwa upinzani ni vita na uvunjifu wa amani. Tume ya Nyalali iliyazingatia haya ikapendekeza vyama vingi. Je, Tume ya Warioba imezingatia hali halisi ya Dunia ya sasa? Imezingatia historia ya nchi za kiafrika zilizojaribu kuungana na kisha muungano kuvunjika? Imezingatia ukweli kwamba watoa maoni wengi kuhusu Muungano ni watu waliolishwa "sumu" na vyama vyao kutaja idadi za serikali (mbili, tatu, mkataba)? Je, iliona wimbi la kuvunjika kwa Muungano?

Na sio kweli kwamba Tume ya Warioba ilizingatia idadi ya wananchi waliotoa maoni. Hebu tuzichambue kidogo takwimu zilizotolewa na Warioba kuhusu Muungano. Kwa Tanzania Bara, waliozungumzia Muungano walikuwa 39,000. Kati yao, ni watu 27,000 tu ndio waliozungumzia Muundo. Na kati ya hao 27,000, watu 3,510 (au 13%) walitaka serikali moja, 6,480 (au 24%) serikali mbili na 16,470 (au 61%) serikali tatu. Kwa Tanzania Visiwani, waliozungumzia Muungano walikuwa 38,000 na ni nusu yao tu (19,000) waliozungumzia muundo. Kati ya hao 19,000, watu 6,460 (au 34%) walitaka serikali mbili, na 11,400 (au 60%) serikali ya mkataba, na watu 25 (0.001%) walitaka serikali moja. Katika mikutano ya Tume huko Visiwani wapo pia waliopendekeza serikali nne : ya Tanganyika, ya Pemba, ya Unguja na ya Muungano, huku wakisisitiza kuwa Muungano uwe kati ya Tanganyika na Unguja. Hao, idadi yao, Jaji Warioba kukwepa kuitaja!

Je, takwimu hizo zinatueleza nini? Ukijumlisha idadi ya watu ambao hawakugusia muundo wa Muungano, Bara na Visiwani, ni 27,000. Hawa ni wengi kuliko watu 16,470 waliotaka serikali tatu. Jumla ya waliotaka serikali moja na mbili ni 16,475, na idadi hii pia ni kubwa kuliko waliotaka serikali tatu. Tume inaweza kujitetea kuwa watakao mkataba wakikosa sana wanaweza kuhamia kwenye serikali tatu. Ukikokotoa jumla ya waliotaka mkataba na serikali tatu ni watu 27,870, na hawa ni 36%  (takribani theluthi moja tu) ya watu waliozungumzia Muungano. Na jumla hii ni kijitone cha maji baharini ikilinganishwa na watu wapatao 333,537 waliotoa maoni katika Tume ya Katiba. Pia hakuna utafiti wowote wa kisayansi unaoonyesha kuwa sampuli ya watu 16,000 inaweza kuwa inawakilisha maoni ya Watanzania milioni 45. Wanaweza kuwa ni watu wa wilaya au mkoa mmoja.

Katika lugha rahisi, ni kuwa waliotaka mkataba au serikali tatu walikuwa asilimia nane tu ya waliotoa maoni. Pia, watoa maoni 287,537 sawa na asilimia 86%  hawakugusia kabisa kuhusu Muungano au muundo wake. Je, uwingi aliousema Jaji Warioba kautoa wapi? Na kwa nini adanganye mchana kweupe?
Ni vema tukajifunza kutokana na mchakato wa Katiba mpya, ambao ulitekwa na Wajasiria-Katiba kutoka vyama vya siasa na asasi zisizo za kiserikali. Na mvutano  baina yao ndio ukateka mijadala na kufifisha maoni ya wananchi wa kawaida. Kuna wakati ambapo baadhi ya asasi zilitaka kwenda mahakamani kuusimamisha mchakato baada ya kuona kuwa umetekwa nyara na chama tawala. Chama kikuu cha upinzani pia kikatishia kujitoa na hata kumwandikia mjumbe wake barua ili ajitoe.

Lakini baada ya kunong'onezwa yaliyomo kwenye rasimu, wakafyata. Rasimu ilipotoka, hata kabla hawajaisoma wakaisifu na kusema imezingatia maoni ya wananchi! Sasa takwimu ndio hizo, je, ni maoni gani ya wananchi yaliyozingatiwa? Huko Zanzibar, hakuna kitu kinachoitwa serikali tatu: wengi hawakugusia muundo. Wowote utakaokuwepo kwao sawa. Kwa waliogusia muundo, wengi wanataka mkataba, kwa maana kwamba Muungano uliopo uvunjike, nchi washirika zipate mamlaka kamili kisha ziamue kushirikiana kama zikipenda. Kwa nini Tume imeyapuuza maoni yao?

Sababu zilizotolewa na Warioba kwamba Muungano kwa sura yake ya sasa hauwezi kudumu pia hazina mashiko. Eti kwamba Zanzibar tayari imeshajitangaza kuwa ni nchi, na Wabara wanaionea wivu. Na hapa, Warioba anasema, kuna majawabu mawili: ama Zanzibar ibadili katiba au Tanganyika nayo ijitangazie uhuru kamili. Kuhusu Zanzibar kubadili katiba, Tume inaona kuwa "ukarabati" huo hauwezekani, hivyo bora Bara nayo iwe na mamlaka kamili. Kwa maneno ya Warioba, "Hii ndiyo sababu kubwa ya kupendekeza muundo wa serikali tatu!" Kwa hiyo, hapa tunaona kabisa kuwa sababu ya kupendekeza serikali tatu sio maoni ya wananchi bali "busara" za Tume.

Lakini kwa busara hizo hizo, Tume ya Jaji Warioba inaiomba Zanzibar ikubali kubadili katiba ili uraia uwe ni suala la Muungano. Kwa maana nyingine, Tume ya Warioba inataka Zanzibar iendelee kuwa nchi (state) lakini isiyo na raia! Na katika busara za Tume ni kuwa hilo ni jambo linalowezekana. Tume inadhani kuwa uraia ukibaki katika nchi washirika kutaibuka utaifa (utanganyika na uzanzibari), na hili ni hatari kwa Muungano. Lakini Tume haioni shida kama kila nchi ikiwa na bendera yake, wimbo wake wa taifa na serikali yake. Wala Tume haikuona hatari kwa nchi washirika kuwa na mamlaka ya kushiriki katika mahusiano ya kimataifa kiasi kwamba siku moja Tanganyika na Zanzibar zitajikuta zimejiunga katika mashirika ya kimataifa, kila moja kivyake, na wakifika huko waanze kupigana vikumbo. Lakini kwa busara za tume, hayo yote ni bora yakawepo, na hayatatishia kuvunjika kwa Muungano.

Tume inatuambia kuwa serikali tatu ndio 'kiboko' cha Tanganyika iliyoendelea kuimeza Zanzibar kwa kisingizio cha Muungano. Serikali tatu zitaleta usawa. Ni kweli zitaleta usawa, lakini usawa wa kisiasa. Je, usawa wa kiuchumi utakuwepo kwa wabia wasio na uwezo sawa wa kiuchumi? Bado Tanganyika, kama mbia tajiri, ndiyo itabeba gharama kubwa ya kuundesha Muungano. Amlipaye mpiga zumari ndiyo huchagua wimbo! Ukaka mkubwa wa Tanganyika ndio utadhihiri. Hata huo usawa wa kisiasa hautakuwapo kwani katika Bunge la Shirikisho, wabunge wengi watatoka Tanganyika (wabunge 50 toka Tanganyika dhidi ya 20 wa Zanzibar). Kwa ufupi, shirikisho litaendelea kutawaliwa na Watanganyika iwe ni katika gharama za uendeshaji, nafasi za kisiasa na hata utumishi wa umma. Watanganyika ni wengi kwa idadi, hivyo wao ndio watakaomua nani awe Rais wa Shirikisho, na uwezekano kwamba Rais wa Shirikisho atatoka Zanzibar ni utandelea kuwa ndoto ya mchana. Uzalendo finyu ndio utatawalaa Shirikisho.

Kwa ufupi, muundo wa serikali tatu una matatizo na kero nyingi kuliko ule wa serikali mbili. Ubabe wa Tanganyika utadhihiri katika mfumo huu kuliko ulivyokuwa katika serikali mbili, ambako Tanganyika alikuwa kaburini. Na kero zenyewe ni zile zinazohusu mamlaka ya wanasiasa kwani ndizo zinazotawala mijadala ya sasa. Wanasiasa wataendelea kupigana vikumbo hata kwa mambo ya kipuuzi; mathalani, katika itifaki  nani awe wa kwanza kutajwa kati ya rais wa Tanganyika na yule wa Zanzibar, au nani mkubwa kati ya Rais wa Tanganyika na makamu wa rais wa Shirikisho. Katika makabidhiano ya ripoti ya Tume ya Warioba tulimsikia Rais Kikwete akilalamika wakati wa kutaja itifaki kwamba vyeo vingi kweli. Huko baadaye katika itifaki wataongezeka rais wa Tanganyika, makamu wake, waziri mkuu, spika wa Tanganyika, jaji mkuu wa tanganyika, n.k. Barabarani wataenda kwa ving'ora, hivyo tutegemee foleni zaidi. Vyeo vyote hivyo vinaendana na mishahara na 'miposho' mikubwa mno ambao ni mzigo kwa wananchi. Na wabara ndio watakaoubeba hasa!

Uchambuzi huu wote unatuambia kuwa tuwe makini wakati wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba. Kabla ya kuijadili lazima kwanza tupate taarifa kamili ya Tume ili kujua vigezo na busara zilizowaongoza kutupatia mzigo huo wa "Danganyika". Nasisitiza mamlaka zinazohusika zitoe taarifa hiyo ya Tume kwa wananchi ili tuijadili na kuikosoa kwani dondoo tu tulizopata toka kwa Warioba zinaonyesha kuwa kuna mengi ya kuhoji! Bado naamini tunaweza kuikoa nchi yetu isitumbukie katika shimo la utengano. Hii ni kama wengi wetu tutapiga kelele kuuokoa Muungano wetu na kuwasihi wenzetu waliokuwa wamedandia "Basi la Warioba" kushuka ili tutafakari kwa kina zaidi!

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment