Tuesday, 12 July 2016

[wanabidii] Niliyoyaona bungeni: Jeuri ni kigingi cha demokrasia ya kweli

RAIS wa Marekani, Abraham Lincoln (1809-1865) anapozungumza kuhusu demokrasia anasema ni serikali ya wananchi inayoendeshwa na wananchi kwa ajili ya wananchi.

Na hii serikali inapatikana kupitia uchaguzi. Lakini pamoja na maelezo hayo, anakiri kwamba mifumo ya demokrasia ni moja ya changamoto kubwa ya uendeshaji wa jamii katika dunia ya sasa kutokana na ukweli kuwa maana hii ya uendeshaji bado ina utata kwa wanasiasa na hata wananchi pia kwa kuzingatia mahitaji ya kundi linalotaka kutawala wakati huo na changamoto zinazokabili ustawi wa jamii. Demokrasia imeasisiwa na Wagiriki ambao mfumo wao wa kutawala ulikuwa ni utawala wa watu wa kawaida.

Ukiangalia uhalisi wake, demokrasia ya sasa imechukua makandokando mengi ya demokrasia ya Wagiriki iliyokuwa inafanya kazi katika miji ya Rome na Athens. Demokrasi ya Wagiriki kama ilivyo ya sasa ilitengenezwa kwa namna ya kukabiliana na matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na watawala au wale waliopata mamlaka.

Pamoja na ukweli huo demokrasia ambayo tunayo sasa ilianza kuwa na mfumo unaoeleweka na wenye kupanuka zaidi katika karne ya 17 na 18 wakati wanafalsafa walipoanza kutoa nadharia zake na tafsiri zake pamoja na misingi yake, katika masuala ya mgawanyiko wa madaraka miongoni mwa vyombo vya dola, haki za msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na kuanza kutofautishwa kwa kanisa na mamlaka ya nchi.

Ikumbukwe kuwa katika siku hizo Kanisa lilikuwa kama ndio watawala katika bara la Ulaya kwani yanayofanyika serikalini yalikuwa na baraka za moja kwa moja na kanisa na taratibu za kanisa ndio zilizokuwa zikitumika kutawala. Ukiachia demokrasia ya sasa ambayo nyingi inaendeshwa kwa mfumo wa jamhuri, zipo bado nchi zenye aina nyingine ya demokrasia ambayo inaendesha utawala. Demokrasia hizo ni pamoja na uongozi wa utawala wa kidini, wa kurithi, wa kifalme na hata wa watu wachache.

Udikteta unaweza kabisa kuwa ni utawala wa wananchi kupitia unyakuaji wa madaraka uliofanywa. Kimsingi demokrasia ina maelezo mwafaka kwa kuangalia utamaduni wa mahali, lakini kwa dunia ya sasa wote tunakubaliana kwamba ilikuwa na demokrasi inayotakiwa ni lazima kuwepo na katiba inayofuatwa si tu na viongozi bali na wananchi pia. Ndani ya katiba hiyo mgawanyo wa madaraka unaelezwa wazi kati ya serikali, Bunge na Mahakama.

Aidha kunakuwapo na ulinzi wa haki za binadamu kwa mtu mmoja, makundi na hata kwa serikali yenyewe. Pia demokrasia ya sasa inadai haki ya kuzungumza na kupokea taarifa na uhuru wa vyombo vya habari. Aidha kunakuwa na haki za kuabudu, kuna uchaguzi unaofanywa kwa mtu mmoja kura moja na utawala wa kisheria ambapo rushwa ni kitu kisichokuwepo.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Winston Churchill (1874-1965) akizungumzia kuhusu demokrasia anasema: "Hakuna mtu ambaye atasema kwa kujiamini kwamba demokrasia imetimilika, au ina kila kitu na ina busara. Hakika, demokrasia ni aina mbaya kabisa ya kuwa na serikali isipokuwa pale tu aina nyingine ya utawala inapokuwa imejaribiwa na kuonwa shubiri yake."

Kimsingi, waziri mkuu huyu wa zamani wa Uingereza anataka kusema kwamba hakuna aina timilifu ya utawala, yaani serikali duniani hapa ila kutafuta nafuu; na demokrasia ya sasa ni nafuu zaidi kwa kuwa hakuna nyingine ambayo imebuniwa na kuonekana kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko hii.

Ukisoma magazeti na mitandao ya kijamii na kuangalia televisheni na kusikiliza radio kuhusu mwenendo wa Bunge la Tanzania kwa mwaka jana na mwaka huu na vijimambo vya vyama vya upinzani kuhusu uchaguzi hadi sasa kuhusu utawala uliopo unaweza kusema kwamba demokrasia Tanzania inaminywa: lakini ukiangalia misingi ya demokrasia utaona kabisa mzizi wa madai hayo umo katika ubinafsi na jeuri inayoambatana na kasi ya kubana waroho, wachoyo wa utajiri na wakwepa kutimiza wajibu.

Wakati anaahirisha mkutano wa bunge mjini Dodoma wiki mbili zilizopita msimamizi mkuu wa shughuli za serikali bungeni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema serikali haijawafunga midomo wabunge wa upinzani au mbunge yeyote labda awe amejifunga mwenyewe. Katika mfumo wa demokrasia uliojengeka nchini, wabunge ndio wanaofanya maamuzi muhimu ya uendeshaji wa nchi na usimamizi wa serikali kwa niaba ya wananchi waliowapeleka kwa kuwapigia kura japo si wote.

Na Bunge la Tanzania linaloendeshwa kwa kuzingatia sheria mama, Katiba Ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uwazi wa uwakilishi unaonekana bungeni na si nje ya hapo kwa kuwa ni katika vikao vya Bunge tu, mbunge kwa lugha safi anaweza kusahihisha, kukosoa au kutokukubaliana na serikali, lakini akifanya mambo ambayo ana kibali nacho bungeni uraiani hilo linaweza kwenda kuwa kosa la uchochezi.

Pamoja na watu kuinyambua siasa na demokrasia kwa namna wanavyotaka (hata wazungu walioileta) wanazuoni na wadau bado wanaona uwakilishi na Bunge si sahihi kutokana na mifumo iliyowekwa na wanaotaka kututawala- soma whatisdemocracy. net) sintofahamu iliyojitokeza katika kipindi cha Bunge ambapo wabunge wa upinzani walikuwa hawaketi bungeni inaweza kuwa na tafsiri mbalimbali.

Moja ya tafsiri ni kwamba upinzani haujakomaa, haujui maana ya uwakilishi na haujui haki zao wakiwa bungeni ila wanataka tu kuleta hisia na kukwamisha mambo kwa kutaka kuwashirikisha wananchi kama ilivyokuwa katika demokrasia changa za Athens na Roma. Tafsiri nyingine ni jeuri ya kutaka madaraka na kutojipanga kuibana serikali kwa kutumia mifumo iliyopo ambayo ukiwa na akili timamu inaweza kabisa kuifanya serikali kusimama makini zaidi.

Mambo yalitokea pale wabunge wa upinzani walipovaa nguo nyeusi na kuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wenye tuhuma nzito kwa serikali, hakuoneshi uwakilishi bali nia ya kundi moja kulipiku jingine ili kuingia katika utawala kwa kuchochea hisia ambazo si za kisheria bali zenye tamaa ya madaraka. Kuna uvunjifu wa sheria katika hili? Elementi zinazobeba siasa ndizo zinazotoa nadharia ya mwisho kwamba vyama vya siasa lengo lake kubwa ni kushika madaraka na kuongoza wengine, kinyume cha hapo ni chama cha burudani.

Na si kila mwananchi atakuwa mwanasiasa lakini wale wanaotaka kutekeleza hisia zao walipaswa kuzingatia muda na kujipanga kuja kueleza wananchi kwamba wao ndio wenye mfumo mzuri zaidi wa kuwatawala kuliko waliopo madarakani lakini si kabla ya kuwabana waliopo humo kutekeleza wajibu wao katika dhana nzima ya utawala wa kisheria. Waziri Mkuu alisema wakati akihutubia Bunge kwamba wabunge wa upinzani kwa makusudi wamekuwa wakijaribu kujenga taswira potofu kwa wananchi na nje ya nchi ili ionekane kwamba kuna kuminywa kwa demokrasia.

Wabunge wa upinzani si tu wamekuwa wakitaka kuyumbisha bali hata maswali wanayouliza hayakulenga kuibana serikali kutekeleza wajibu wake ila kuonesha kwamba inakumbatia upuuzi unaokwamisha maendeleo. Watu wenye akili kama alivyosema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wanaweza kabisa kuona kelele za wapinzani si za kujenga, bali ni kuonesha kutokomaa kwao katika siasa, ambapo maana kubwa ni kutekeleza demokrasia si kwa mtindo wao bali kwa mtindo wa dunia wa kusimamia serikali na kuhakikisha hakuna rushwa na utawala ni wa kisheria.

Kwa mtu aliyekomaa kisiasa hawezi kukurupuka na kusema kwamba kuna udikteta wa kijeshi bali ataangalia kwa nini uvunjifu wa amani hauwezi kuachiwa unaendelea kwa sababu za kisiasa na kukwamisha serikali kufanya shughuli zake. Kiukweli kama alivyosema Waziri Mkuu katika hotuba yake hiyo, si jambo la kawaida kwa mbunge kuzitoa hoja za bungeni na kuzipeleka mitaani eti zijadiliwe na wananchi kisha zitolewe uamuzi.

Uamuzi gani utatolewa na je haki za bunge zinatolewa na wananchi au ndio kutaka kuifunga kamba serikali isitekeleze wajibu wake? Kwangu mimi (mwandishi) ni matokeo ya kuondolewa kwa Bunge 'Live' sasa wanaonekana kwamba hawafanyi kazi kumbe hoja zao za msingi zenye kusimama thabiti zingeweza kujadiliwa ndani na wote wakajua kwamba wanatekeleza wajibu wao wa kutaka wananchi wawe na ustawi.

Siasa za bungeni za kutoshiriki vikao halali zimetia kiwi na wenye akili na maarifa. Ni kweli kama alivyosema Waziri Mkuu kwamba kama hilo la wananchi kuamua linawezekana, basi kusingekuwa na umuhimu wa kuwa na Bunge, bila shaka na uchaguzi pia.

Kama kweli wanasiasa wetu wanajua demokrasia ya kisasa ni nini kazi yake wakitazama msingi mkubwa wa uendeshaji wa serikali na upigaji vita rushwa hawawezi kujifunga na vibweka vya nguo nyeusi au kushona midomo yao bali wataangalia kila hatua ya demokrasia hapa nchini na hasa mapambano dhidi ya rushwa na utawala wa kisheria.

Mbunge anapodai kwamba kashonwa mdomo, anadai kwa kuwa yeye mwenyewe kwa kutumia kanuni za kudumu ameshindwa kutengeneza hoja yenye uhakika na si kufinyanga maneno kiasi cha kujikuta akikiuka kanuni zinazoendesha bunge. Na kutokana na hili unakutana na matatizo ya wabunge kunasa katika mchezo wa uwongo na matusi na wakasimamishwa vikao kwa kuwa wameenda kinyume.

Kwa kushindwa kutumia vyema Ibara ya 100 na 101 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo imetoa haki na kinga kwa wabunge ili waweze kujadili na kuhoji utendaji wa serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza kushtakiwa wanapotimiza wajibu wao huo wakiwa bungeni, kumefanya siasa za upinzani kuonekana kuwa majungu na fitna na kubaki katika majukwaa ya siasa wakitafuta 'kiki' rahisi ili wananchi wawaunge mkono.

Ni dhahiri kinga hiyo ya kikatiba haijatolewa kwa wananchi, kwa maneno mengine mbunge hajafungwa mdomo labda aamue kujifunga mdomo mwenyewe. Ndio kusema kitendo cha baadhi ya wabunge kususa vikao vya bunge pamoja na kwamba hakitoi picha nzuri kwa wananchi waliowachagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge, na wala hakitokana na mkutano wa wanachama wote wa vyama vyao, wanaonesha kiwango cha juu cha jeuri na kiburi (arrogance) ambayo hatima yake ni kuididimiza demokrasia.

Mimi nadhani kama watajitahidi kusoma mifumo mbalimbali ya demokrasia na misingi inayobeba demokrasia hiyo na kuelewa kwamba haijawahi kuwa timilifu, wabunge wa upinzani watarejea bungeni na kushiriki kutoa ushauri kwa serikali bungeni ambao utaliletea taifa maendeleo, na huko wananchi wote watawaona watawasikiliza na watawaelewa.

Waziri Mkuu alisema: "Endapo kuna utata katika jambo lolote ndani ya Bunge letu, zipo taratibu tulizojiwekea na kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo. Kwa kususa kuingia bungeni kunaweza kusiwe tija kwa tunaowawakilisha na taifa letu." Sasa kama Bunge linaongozwa na katiba, sheria na kanuni za kudumu za bunge kwa nini tutengeneze hisia za kuonewa wakati tunachapia wenyewe? Kama tukiendekeza misimamo ya vyama vya uroho wa madaraka na utawala maendeleo na ustawi wa jamii tutausikia katika bomba.


Habari Leo

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment