Friday 22 July 2016

[wanabidii] JK akata mzizi wa fitna

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, utakaofanyika mjini hapa kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete inamaliza minong'ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti katika mkutano huo.

Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua Mwenyekiti.

"Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM," alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.

Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu 'wafitini' walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema "Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe." Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang'atuka kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.

Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; "Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo." Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.

Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.

Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.

Kutoka Arusha, Mwandishi Veronica Mheta anaripoti kwamba CCM mkoani humo imejipanga kumpatia kura zote za ndiyo Rais Magufuli kuhakikisha anapata kura za kishindo ili kumthibitisha kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa kutoka kwa mtangulizi wake Rais mstaafu Kikwete.

Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe aliyasema hayo mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari. Waandishi hao walitaka kujua msimamo wa wajumbe wa mkoa huo kutokana na kuwa mmoja wa mikoa iliyoathiriwa na vuguvugu la baadhi ya viongozi na wanachama kusaliti na kukihama chama hicho siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Mdoe aliondoa hofu kuhusu wajumbe wa Mkoa wa Arusha na kusema kwa ujumla wajumbe wote wamekubaliana kwa kauli moja kumpatia Rais Magufuli kura za ndiyo kwa kuwa hakutakuwa na maana yoyote ya kupiga kura za maruhani na kuelekeza kwa kivuli kwa kuwa mgombea ni yeye pekee.

Alisema wajumbe hao wamefikia hatua hata ya kudiriki kupendekeza kura watakazopiga kuwa za wazi ili kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa kura hizo za maruhani kwani wana imani kubwa na utendaji mzuri wa Rais Magufuli ndani ya chama kutokana na kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi kifupi cha urais wake.

Mdoe alisema kwa sasa hali ya kisiasa ndani ya chama hicho mkoani Arusha ni nzuri kutokana na kila mwanachama na kiongozi kutambua siasa zilishapita wakati wa kupatikana kwa mgombea wa urais ndani ya chama.
Wasifu wa Magufuli

Dk John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato mkoani Kagera (sasa mkoa mpya wa Geita). Alianza elimu ya msingi katika shule ya msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974.

Alijiunga na Shule ya Seminari Katoke wilayani Biharamulo, ambako alisoma Kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 – 1977. Alihamishiwa shule ya sekondari Lake mkoani Mwanza, ambako alisoma Kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978. Masomo ya Kidato cha Tano na Sita aliyapata shule ya sekondari
Mkwawa mkoani Iringa kati ya mwaka 1979 na 1981.

Alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi katika masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu. Alisoma hapo mwaka 1981 – 1982. Baada ya kuhitimu hapo, alianza kazi ya ualimu katika shule ya sekondari Sengerema mkoani Geita, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati kati ya mwaka 1982 na 1983.

Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha kambi ya Makuyuni mkoani Arusha (Januari hadi Machi 1984) na kumalizia kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).

Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988. Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika Kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), akiwa Mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.

Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, ambayo alihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa Shahada ya Udaktari. Dk Magufuli ana mke na watoto.

Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chato mwaka 1995 na aliposhinda Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Miundombinu.

Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu na Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008, alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, ambayo aliiongoza hadi 2015. Mwezi Oktoba mwaka 2015 alichaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Wasifu wa Jakaya Kikwete Kuzaliwa – Msoga, Bagamoyo mkoani Pwani Oktoba 7, 1950.

Elimu ya Msingi – Lugoba wilayani Bagamoyo 1956-1965. Kidato cha Nne na Sita - 1966-1971, Tanga Sekondari na Kibaha. Chuo Kikuu Dar es Salaam - Shahada ya Uchumi 1972-1975. Naibu Waziri Nishati na Madini – 1998 -2000. Waziri wa Maji, Nishati na Madini – 1990 -1994.

Waziri wa Fedha - 1994 -1995. Mbunge wa Kuteuliwa – 1988 – 1990. Mbunge wa Chalinze – 1990 -2005. Uzoefu, Utumishi na Uongozi CCM – miaka 40 Tanu hadi CCM Mjumbe wa Kamati Kuu – miaka 20. Mjumbe wa NEC - miaka 33. Ajira ya mara kwanza CCM – Aprili 3, 1975 Katibu Msaidizi Singida. Mwenyekiti wa CCM – Tangu 2006 hadi sasa.

Habari Leo

0 comments:

Post a Comment