Wednesday, 20 July 2016

[wanabidii] Gome la mti si la mvuka uvundo ( Edward Lowassa hafai kuwa Rais wa 2020 – 2025.)

Imeandikwa na Faustine Sungura

JUMAMOSI ya tarehe 4 Juni, 2016, kupitia moja ya magazeti, nilipata taarifa kwamba, Edward Lowasa anajiandaa tena kugombea Urais mwaka 2020.

Kwamba, pamoja na mambo mengine, ndoto yake ya kuwa rais inaingia giza pale anapoona Freeman Mbowe na Zitto Kabwe hawapikiki chungu kimoja hivyo anafanya mbinu kupitia njia mbalimbali ili watu hao wawe kitu kimoja, na anaamini atafaidika na itakuwa ni njia rahisi ya kumuingiza Ikulu ya Magogoni katika uchaguzi ujao. Mawazo na au nia ya Edward, ndiyo imenifanya nichukue kalamu na karatasi, niandike.

Kazi ya kusoma, kufikiri, kuchambua na kuandika ni kazi ngumu sana, ni kazi inayohitaji muda, utulivu, uvumilivu na ustaarabu. Ni kazi ngumu sana lakini pia ni kazi ya wajibu kwa watu makini. Ninaandika makala haya, siyo kama ninawakilisha taasisi yoyote, bali ninaandika kama mtu binafsi, mwenye haki ya kikatiba (1977) chini ya Ibara ya 18(a), (b), (c) na (d) ya kupokea na kitoa maoni yangu na bila kuingiliwa kwa namna yoyote ile. Ninaandika makala haya, nikiwa muumini mkubwa wa maneno ya wahenga, "mwanzo kokochi, mwisho nazi".

Ninaandika nikiamini mchana kweupe kwamba, Edward Lowassa hafai kuwa Rais wa nchi hii kwa kipindi cha 2020 – 2025. Ninao pia ufahamu wa kutosha kwamba, makala haya yatakabiliwa sana na upinzani wa midomoni mwa baadhi ya wasomaji, nitaheshimu sana mawazo ya wote watakaonipinga, lakini sitaacha kuandika ninayoyaamini. Wahenga walisema, "mwenda kwao haogopi giza".

Ninaandika makala haya, nikiwa siyo miongoni mwa watu maarufu, na ambaye habari zangu hazitaweza kuleta mtikisiko wowote kwa umma wetu, lakini walio wachache na makini na wanaonifahamu kwa namna yoyote, watafuatilia ninachokusudia.

Na hilo ndilo kusudio. Karibuni. Itoshe kujieleza kwa kifupi ya kwamba, mimi ni mwanachama wa kadi na itikadi ya NCCR-Mageuzi, ni mmoja wa waanzilishi wa harakati za kuanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi (1989-1990) na baadaye mmoja wa waanzilishi wa NCCR-Mageuzi, jina langu ni miongoni mwa majina 200 kwenye ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, kutoka mmoja wa mikoa ya nchi hii, kukiwezesha chama kupata usajili wa muda na baadae usajili wa kudumu hadi sasa.

Kusema kuwa Edward Lowasa hafai kuwa Rais kwa kipindi cha 2020-2025 siyo jambo baya, ila ubaya ni kusema kuwa Edward Lowasa hafai kuwa Rais, bila kutoa sababu za msingi au hata zile za paa la nyumba. Ninaandika makala haya huku chaguzi nyingi za nchi zinazoendelea na hususani zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa miongoni mwazo, zikiwa hazina ufahamu wa kutosha kwenye masuala ya uchaguzi.

Wengi wetu tunaongelea tu uchaguzi huru na wa haki, lakini pia tunapenda sana kwenda kuchagua mgombea tunayempenda. Dk Bashiru Ali, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mlimani anasema, "uchaguzi huru na wa haki hauna maana yoyote, kama uchaguzi huo hauwaletei manufaa wananchi".

Ni wakati mzuri sasa, Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, itupatie elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa watanzania, kuacha kwenda kwenye vituo vya kupiga kura na kumpigia kura mgombea tunayempenda, badala yake ituelimishe vya kutosha juu ya umuhimu wa kwenda kumpigia kura mgombea anayefaa.

Mwanzoni mwa mwaka 2014, Mahakama ya wilaya ya Munich nchini Ujerumani ilimhukumu Uli Hoeness, Rais wa klabu ya Buyern Munich, kifungo cha miaka mitatu na nusu kwa kosa la kukwepa kulipa kodi yenye thamani ya Euro 27.2ml (sawa na Sh bilioni 60 za Tanzania). Mahakama hiyo, ilimpa Uli haki ya kukata rufaa ambapo Uli Hoeness alisema: "Baada ya mazungumzo na familia yangu, nimekubali hukumu ya mahakama ya wilaya, ninasumbuliwa sana na nafsi yangu, kwa kosa la kukwepa kulipa kodi, sitaki kukata rufaa. Ninaenda jela."

Nimemrejea mtu huyu, kama moja ya sababu za kusema Edward hafai, hafai kwa sababu, hajaonesha kuguswa na makosa aliyoyafanya katika siku za nyuma. Hapa sizungumzii mambo ya Richmond ya enzi akiwa CCM, bali ninamzungumzia Edward akiwa Chadema na ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ninaandika makala haya, huku jamii ya watu makini, ikiwa na kumbukumbu kwamba, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, viliingia kwenye makubaliano ya kuwa na mgombea mmoja, kwa kila nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani. Aidha, makubaliano hayo, yalifanyika kwa kuapizana na kusainiana baina ya viongozi wakuu wa vyama hivyo, makubaliano hayo yalisambazwa kwa viongozi wote wa ngazi za chini pamoja na wagombea hususani wagombea urais (Edward Lowasa na Maalim Seif).

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, NCCR-Mageuzi kwa kuthamini haki na hadhi ya ushiriki wa vyama vingine, iliomba angalau kuachiwa majimbo 27 kati ya majimbo 264 ya ubunge. Baada ya kuongea na wanachama wetu waliokuwa wameonesha nia ya kugombea urais, Dk Geroge Leonard Kahangwa (Muungano) na Haji Ambar Khamis (Zanzibar), NCCR-Mageuzi ilikubali kuwaunga mkono Edward Lowasa (Muungano) na Maalim Seif (Zanzibar).

Aidha, baada ya kuongea kwa kina na wanachama wake kule Zanzibar, NCCR-Mageuzi kilikubali kutoweka mgombea yeyote Zanzibar na badala yake kiliwaunga mkono wagombea wa vyama vya CUF na Chadema. Mbali na kuonesha ushirikiano huo, vyama washirika wa Ukawa, hasa Chadema na CUF, vilikataa kuiachia NCCR-Mageuzi majimbo hayo 27 na badala yake waliridhia tu majimbo 12.

Wakati viongozi wakuu wa vyama vya Chadema na CUF wakiachiwa majimbo waliyoonesha nia ya kugombea ubunge, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi (Mosena John Nyambabe) aling'ang'aniwa na Chadema kwa kumwekea mgombea wao. Pamoja na NCCR-Mageuzi kuendelea kuwa ndani ya Ukawa kwa hayo majimbo 12 tu, siku ya uteuzi ilishangaza kuona Chadema imeingilia tena majimbo sita ya NCCR-Mageuzi, kwa kuweka wagombea wa Chadema, ili kura zigawanyike na kuinufaisha CCM.

Kwa maelezo haya, NCCR-Mageuzi ikawa imebaki na majimbo sita tu chini ya Ukawa. Edward Lowasa, aliwanyanyasa sana wagombea wanawake wa NCCR-Mageuzi katika majimbo ya Nkenge (Anjelina Mutahiwa), Ngara (Helen A. Gozi ) na Korogwe Mjini (Rosemary Lugendo).

Wagombea hawa walipitishwa kugombea kwenye majimbo hayo kupitia Ukawa, lakini Edward alipofika kwenye majimbo hayo, alikataa kuwanadi na badala yake akawanadi wavamizi wanaume wa Chadema, kitendo hicho kiliwafedhehesha wagombea wanawake na kuwachanganya wapiga kura na kuinufaisha CCM. Hapa ndipo ilipo hoja yangu kumuona yu hafai, hafai kwa sababu, siyo mtu wa kuheshimu ushiriki wa vyama vingine vya siasa na ambavyo vilimuunga mkono kwenye nafasi ya urais, ni mbinafsi, mchoyo, na ni muongo, hana huruma na wala hana haya.

Akiwa na ufahamu wa kutosha, na ukweli ulio wazi kuwa, alikuwa na mvuto na ushawishi mkubwa, Edward Lowasa na Chadema yake, walikuwa radhi kuukosa/kushinda Urais (2015) kwa hata kura moja kuliko kuona majimbo ya Kigoma Kusini, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini na Muhambwe yanarejea tena ndani ya himaya ya NCCR-Mageuzi.

Kwa makusudi na katika hali ya kushangaza, Edward na Chadema yake, wakiamini kuwa wameshashinda uchaguzi, walikataa kwenda kuomba kura za urais katika majimbo ya Kigoma Kusini, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini na Muhambwe mkoani Kigoma, kwa kuhofia ujio wake ungekinifaisha pia Chama cha NCCRMageuzi kwa wagombea wote hao kurejea tena bungeni. Rais wa kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipata kusema wakati wa jioni moja ya maisha yake, "msinipime kwa mafanikio yangu, bali nipimeni kwa makosa niliyoyafanya na kujirekebisha."

Ninaandika makala haya, Edward Lowasa na chama chake, wakiwa hawajui na wala hawajali ni kiasi gani wamewakwaza wenzao na wala kujali maumivu yao, badala yake wanapanga mikakati mingine ya kuwadhuru ACT-Wazalendo. Albert Einstein, ni mwanafalsafa na mtaalamu wa zamani katika fizikia nchini Ujerumani, wakati fulani wa majira ya joto alipata kusema: "Asiyeweza kuaminika kwa kusema ukweli katika mambo madogo, kamwe hawezi kuaminika katika mambo makubwa."

Jamii ya watu makini ndani ya NCCR-Mageuzi inaweza kama ikipenda, ikajiuliza, kama Chadema na Lowasa waliaminiwa na washirika wenzao ndani ya UKAWA, tena kwa kuapizana na kutiliana saini, bado walikiuka makubaliano ya hiari, je wakipewa nchi kutatokea nini?

Wakati NCCR-Mageuzi inaingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ilikuwa na wabunge wanne kutoka majimboni, baada ya uchaguzi huo, NCCR-Mageuzi imeshuka chini ya Ukawa kutoka majimbo manne hadi jimbo moja, na Lowasa ameipaisha Chadema chini ya Ukawa, kutoka majimbo 24 hadi majimbo 36. Mayo Angelou, ni mwandishi mashuhuri wa mashairi nchini Marekani, alipata kusema: "Nimejifunza ya kwamba, watu watasahau yale uliyosema, watasahau uliyoyafanya, lakini kamwe hawatasahau nini umewatendea wakaonekana walivyo leo."

Nimeirejea nukuu hii, kuonesha ninivyomuona Edward na Chadema, hasa ninapokumbuka jinsi NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti wetu, James Mbatia, walivyotoa mchango mkubwa kuijenga Ukawa kwa wananchi, ikilinganishwa na kile kilichovunwa ndani ya Ukawa chini ya Mabadiliko Lowasa, Lowasa Mabadiliko. Sina tena hamu.

Hafai, hafai, hafai. Kwa mtazamo wangu, na hasa kama ningekuwa mtu maarufu ndani na nje ya NCCR- Mageuzi, nisingekwazika kama Chadema na Lowasa wangefukuzwa ndani ya Ukawa, au wakiing'ang'ania Ukawa basi, waachiwe wazunguke nayo wenyewe. Ninaandika makala haya, nikiwa na ufahamu mkubwa ya kuwa, makala haya yanaweza kutumiwa na baadhi ya watu, ndani au nje ya taasisi, kupambana na mimi na au vinginevyo.

Hata hivyo ninaamini kuwa, nitashinda mapambano siyo kwa wingi wa watu, bali kwa nguvu ya yale ninayoyaandika na hata yale nitakayoyaandika. Aliyepata kuwa mpigania haki wa watu wa kabila la Ogoni nchini Nigeria, Ken Saro-Wiwa, alipata kusema wakati wa jioni moja ya maisha yake: "Mnaweza kumkamata, mkamuua na kumzika Ken Saro-Wiwa, lakini kamwe, hamtaweza kuukamata, kuuua na kuuzika ukweli wa Ken Saro-Wiwa."

Mtu huyu, alikuwa anapinga uchafuzi wa mazingira ya watu wa kabila lake (Ogoni), uchufuzi huo ulikuwa unafanywa na Kampuni kubwa ya mafuta ya nchini Uingereza (Shell) iliyokuwa inafanya shughuli zake nchini Nigeria katika miaka ya sabini. Kampuni hiyo ilikuwa inakataa kuweka miundombinu ya usafi kwani ingeigharimu kiasi kikubwa cha fedha, na badala yake ilikuwa inamnyamazisha Ken kwa kuwa karibu sana na viongozi wadhalimu wa wakati huo nchini humo.

Baada ya mapambano makali ya kutetea watu wa kabila lake, serikali ya nchi hiyo, ilimkamata Ken Saro-Wiwa, ilimfungulia mashtaka, Mahakama moja ilimtia hatiani, alihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, alinyongwa, akafa na baadae alizikwa. Hata hivyo, mwaka 2009 (takriban miaka 39 baada ya kifo chake), kampuni ya mafuta ya nchini Uingereza (Shell) ilikiri hadharani na kuiomba radhi Serikali ya Nigeria kwa uchafuzi wa mazingira iliyokuwa inaufanya, kampuni hiyo ilikubali kuwalipa fidia watu wa kabila la Ogoni.

Nimemrejea Ken Saro-Wiwa nikiamini ya kwamba, yeyote anayepambana na makala haya, hapambani na Sungura, mtu huyo atakuwa anapambana na ukweli, ataweza kuwapata watu muda mfupi wa kumuunga mkono, lakini kwa kadiri muda utakapokwenda nuru ya ukweli itawaangaza nao watachukua kalamu na karatasi wataandika.

Kama mwandishi wa makala haya alikuwa pamoja na baadhi ya watu ndani ya NCCR-Mageuzi, wakikuwa wanamuunga mkono Lowasa na wagombea wa Chadema wakati wa uchaguzi mkuu (2015), lakini Lowasa na Chadema wakakataa kuwaunga mkono wagombea wa NCCR-Mageuzi, akiwemo Katibu Mkuu wake (Mosena Nyambabe), je mwandishi na watu hao wakiamua kuiishi methali hii; "kutwanga nisile unga, ninazuia mchi wangu", watakuwa wamemkosea nani? Wahenga walisema, "ukimfukuza sana mjusi, ipo siku ategeuka kuwa nyoka" tena wakasisitiza, "fimbo ya mke mwenza, huumiza kupita kiasi".

Ninapofika jioni ya makala haya, halmashauri ya ubongo wangu inanirejesha tena kwenye methali "Ndezi ipo, usilinganishe na fumba" Wakati Chadema inampata Lowasa kugombea urais, ilibainika haina mwanachama wa kumteua kuwa mgombea mwenza, iliwaomba washirika ndani ya Ukawa iwape mmoja wa wanachama wake ili Lowasa asikwame, CUF wakakubali kumtoa mmoja wa wanachama wake kindandaki, Makamu Mwenyekiti wao (Duni Haji Duni) ajiunge na Chadema.

Baada ya uchaguzi, Chadema ilimpa heshima Edward Lowasa, ateue wanachama watano ili wawe wabunge wa viti maalum. Si Lowasa wala Chadema aliyekumbuka kuwauliza Ukawa kama wana watu ili wateuliwe kuwa wabunge. Unapofika wakati wa mavuno hawataki ushirika na chama wala mtu wa nje, watu makini wanasikitia hapo kumuunga mkono katika uchaguzi ujao, maana hataunda Serikali ya Umoja wa vyama washirika bali ataunda Serikali ya watu wa Kaskazini.

Baada ya watu makini na hasa waliokuwa ndani ya Ukawa kuwashtukia, sasa wanaitafuta ACT-Wazalendo maana hawajui undani wa Lowasa. Ni matarajio yangu, kabla ACT-Wazalendo haijalikubali ombi la Lowasa na Chadema yao, watatembelea pale Bakita (Baraza la Kiswahili Tanzania), pamoja na kurasa nyingine, ukurasa wenye methali ya; "ikiwa kilemba kimelowa, mkuti u hali gani?" utapewa muda wa kutosha na hata ule wa ziada.

"Mwenye tumbo ni tumbole, angalifunga mkaja", hii ni methali kongwe, ikimaanisha ya kwamba, tabia ni tabia, hata kama utajitahidi kuificha lazima kuna wakati itafichuka. Nimeirejea methali hii kama sehemu ya kujengea hoja juu ya Chadema na Lowasa kutokuwa na nia njema kwa NCCR-Mageuzi kabla na baada ya uchaguzi mkuu. Katika Halmashauri za wilaya za Kinondoni na Ilala na hata katika ile ya Jiji la Dar es Salaam, Chadema ina madiwani wengi, CUF inao wachache, kwa kutumia wingi wao, Chadema imechukua nafasi zote za Umeya na CUF imechukua nafasi zote za U-makam meya.

Katika Halmashauri za Manispaa za Bukoba na Halmashauri ya wilaya ya Moshi, NCCRMageuzi ina madiwani kama ilivyo kwa CUF katika Manispaa za Kinondoni, Ilala na Jiji la Dar es Salaam, NCCR-Mageuzi iliwaandikia barua Chadema kuomba kuungwa mkono katika maeneo hayo ili nayo ipate angalau kuongoza Halmashauri mbili katika nchi hii. Kipindi kilichopita NCCR-Mageuzi ilikuwa inaongoza Halmashauri moja tu.

Chadema hawakujibu barua ya wenzao na walichukua nafasi zote (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti) kwa kutumia wingi wao. Katika mazingira kama haya, ni mtu gani mwenye akili timamu anaweza kuwaunga tena mkono? Labda ni yule anayejiandaa kuua NCCR-Mageuzi ili ahamie Chadema.

Katika hali ya kushangaza, baada ya Chadema kuingilia majimbo ya NCCR-Mageuzi ili kura zigawanyike na kuinufaisha CCM, Chadema kukataa kuiunga mkono NCCR-Mageuzi ili iongoze japo Manispaa ya Bukoba (Meya au Makamu Meya), Halmashauri ya wilaya ya Moshi (Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti), Edward Lowasa na Chadema yake, kwa kutumia misuli yao kiuchumi, wanawatumia baadhi ya wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuandaa kanuni za ushirikiano ili sasa zisainiwe na vyama wahusika.

Sina hakika kama na hili linahitaji elimu ya chuo kikuu kubaini ulevi wa madaraka. Kanuni huwa zinaandaliwa kabla ya mashindano, sasa uchaguzi umeshapita na Chadema hawakuwa tayari hata kuwa na wazo la kanuni, leo kanuni hizo zinaandaliwa kwa ajili ya kazi gani? Hivi kuna sheria yoyote katika mchezo ambazo zinamruhusu refa au mwamuzi kutoa adhabu baada ya mchezo?

Ninamalizia makala yangu, nikiwa na imani ya kuwa, kuna baadhi ya watu makini, wanaweza kuwa wameguswa na makala haya na hata kufikiria kuwa na meza za mazungumzo na Chadema na Edward wake, binfsi sina kipingamizi na uwepo wa mazungumzo, lakini pia kuna haja ya kujua undani wa mtu unayefanya naye mazungumzo.

Aliyepata kuwa mwandishi mashuhuri wa vitabu katika ukanda wa Afrika Mashariki, Shaban Robert, alipata kusema wakati wa mchana mmoja wa maisha yake hapa duniani: "Busara kubwa kichwani haina faida, kama moyoni hakuna chembe ya wema". Basi niwaage kwa muda, wakati kurasa zikipekuliwa kuutafuta wema wa watu hawa.


Chanzo Habari Leo

0 comments:

Post a Comment