Monday 4 March 2013

[wanabidii] Uchambuzi: Tunajifunza Nini Kutoka Kenya?

Uchambuzi: Tunajifunza Nini Kutoka Kenya?

Ndugu zangu,

AFRIKA vurugu zetu nyingi zinaanzia kwenye chaguzi. Joseph Stalin wa Urusi aliwahi kutamka: "Anayepiga kura hana anachoamua, anayehesabu kura ndiye anayeamua kila kitu".

Na hapa ndipo lilipo tatizo la msingi. Watu kukosa imani na wenye kusimamia uhesabuji wa kura zenyewe. Kuna wanaojisikia kuwa kura zao hazina umuhimu; kwani, mwisho wa yote, kura zitaibwa.

Katika nchi zetu hizi, kukosa imani na wenye kusimamia mchakato wa uchaguzi hadi kuhesabu kura ndio chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani. Tuliyaona hayo kwa jirani zetu kule Kenya mwaka 2007.

Wakenya wale walishiriki mchakato wa kujiandikisha na hata kupiga kura bila matatizo makubwa. Kazi ikaja kwenye kuhesabu kura. Ndipo hapo hesabu zikaanza kuwa ngumu. Kukawa na kufuta hapa na pale. Kukawa na kushinikizana matokeo na kadhalika. Hatimaye damu ikamwagika.

Kila mwenye kufikiri alielewa kuwa kiini cha vurugu za Kenya ni Tume ya Uchaguzi ambayo haikuwa huru. Wakenya wale wakajifunza. Leo wana Katiba mpya. Katiba ya watu wa Kenya.

Hivyo basi, tunachojifunza hapa ni kuwa, dawa ya kuepuka au kupunguza shari kama iliyotokea Kenya ni kwa nchi zetu hizi kuangalia upya Katiba zetu hizi na hususan inapohusu uchaguzi na Tume ya Uchaguzi. Na kikubwa kinachosababisha vurugu na watu kuchinjana ni kukosekana kwa imani kwa wenye kusimamia uchaguzi.

Hapa kwetu tuliyaona hata kwenye Uchaguzi mdogo wa kule Arumeru. Mliokuwa kwenye runinga mkiangalia usiku ule wa uchaguzi na kusubiri matokeo mtakuwa mlikiona pia nilichokiona mimi.
Hakika niliogopa, kwamba televisheni inatumika kuendesha propaganda za kuwaonyesha vijana kuwa ni wenye vurugu wakati hatuonyeshwi vijana hao wakifanya vurugu.
Mtangazaji mmoja alipokuwa hewani moja kwa moja cha kwanza kutuambia ni : " Kuna milio ya risasi inasikika" bila kutuacha watazamaji tuisikie pia hiyo milio ya risasi.

Ndio, kule Arumeru tumeona jinsi baadhi ya vyombo vya habari na wanahabari wakishiriki kusambaza hofu ya vijana kufanya vurugu bila kutuonyesha vijana wanaofanya vurugu. Bila wanahabari hao kutambua au labda walitambua wangeweza kabisa kuwa chanzo cha vurugu na hata mauaji.

Jirani zetu Kenya wameshajifunza kutokana na maafa ya uchaguzi wa 2007 yaliyolifika taifa hilo. Na Wakenya wamegundua, kuwa si tu Polisi wanaoweza kuchochea vurugu na mauaji, bali hata wanahabari kama ilivyokuwa mwaka 2007. Ndio maana, kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa siku hii ya leo, Wakenya walishaamua, tangu mwaka jana, kuendesha mafunzo maalumu kwa wanahabari watakaoripoti habari za uchaguzi mkuu. Lengo kuu hapo ni kuwafanya wanahabari hao wasijikite kuandika habari za uchochezi na zilizoegemea kwenye vyama na makundi. Ni hatua sahihi na ya kuigwa.
Na matokeo ya Uchaguzi wa Kenya yatakuwa kama ' litmus paper'- ni kipimo watakachotumia wakubwa katika mahusiano yao na nchi zetu hizi. Kama Wakenya watafanya uchaguzi wao kwa amani na matokeo yakatangazwa na Tume Huru, Rais akaapishwa na shughuli zikaendelea, basi, huenda matokeo hayo yakaifanya Kenya kuwa ' Kaka Mkubwa' kwa nchi zetu hizi za Afrika Mashariki na Kati. Tutakuwa ni watu wa kuambiwa; " Waangalieni wenzenu Wakenya!"
Kila la Kheri Jirani zetu wa Kenya.
Maggid,
Msamvu, Morogoro.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment