Monday 4 March 2013

[wanabidii] Neno La Leo: Ningependa Nikumbukwe Pia Kwa Mchango Wangu Huu Mdogo Kwa Nchi Yangu...!

Ndugu zangu,
Kama mwanadamu, wakati mwingine tujiulize; Je, ni yepi ambayo tungependa wanadamu wenzetu waje kutukumbuka nayo? Ni  yale ambayo tutayaacha nyuma yetu- legacy.

Leo niliposoma gazeti la Mwananchi nimekutana na tangazo hilo pichani. Inahusu  wito kwa wanafunzi kujiunga na kozi ya Diploma ya Elimu ya Watu Wazima na Endelevu kwa njia ya masafa.

Hilo ni wazo langu la tangu mwaka 2005. Ni wazo nililoliibua nikiwa na Bw. Edward Lugakingira pale kwenye mhagawa wa Hasty taste, Iringa.

Edward Lugakingira alikuwa Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pale Iringa. Tulifahamiana kupitia makala zangu za kwenye Rai enzi hizo.  Kwa sasa Edward Lugakingira ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kwenye Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Makao Makuu, Dar.

Wazo lilianzaje?

Nilipoajiriwa na Shirika la Forum Syd nikitokea Sweden mwaka 2004 nilipangiwa kufanya kazi Iringa. Huko niliratibu pia mafunzo ya wakufunzi wa Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi.  Zaidi ilikuwa ni kozi fupi fupi za masuala ya mbinu za ufundishaji. Kozi haikuzidi siku 5. Nilizunguka mikoa kadhaa na kukutana na walimu hao.

Ni baada ya mwaka mmoja,  na baada ya kuwa na nafasi ya kuzungumza na wakufunzi wenyewe, ndipo liliponijia wazo la kuwa na kozi ndefu ya Cheti na Diploma kwa njia ya masafa. Kozi ambayo ingetoa fursa pia kwa washiriki kukutana na walimu wao kwenye - face-to-face kila baada ya muda fulani.

Na hakuna jambo ambalo mwanadamu unaweza kulikamilisha peke yako. Tangu mwanzo wa wazo, nilianza kwa kumshirikisha Bw. Lugakingira ambaye baadae, kwa bahati njema, alihamishiwa Makao Makuu ya TEWW. Hapo kasi ya mchakato wa kulifanikisha wazo kuu ikaongezeka.

Wadau zaidi wakajiunga katika harakati za kulikamilisha wazo kuu. Ni pamoja na Chama Cha Walimu Tanzania na Chuo Kikuu cha Linkoping cha nchini Sweden. Ubalozi wa Sweden nao ukaunga mkono jitihada zetu.

Hatimaye, miaka miwili iliyopita, Balozi wa Sweden , Bw, Lennart Hjalmaker alizindua rasmi mafunzo ya kozi hiyo kwa majaribio kwa kundi la wakufunzi 45 kutoka Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi.

Majaribio hayo yamekwenda vema kuliko ilivyotarajiwa. Na kwenye Bunge la Bajeti la mwaka jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Mh. Shukuru Kawambwa, alitangaza rasmi Bungeni , mpango wa Wizara yake kupanua programu hiyo kwa kusajili washiriki wengi zaidi. Tangazo hilo hapo juu ni matokeo ya mpango huo.

Naamini kwa dhati, kuwa aina hii ya programu za mafunzo kwa njia za masafa kwa watumishi walio kazini na wasio watumishi, itasaidia kuwajengea uwezo watumishi hao, na  hivyo, kuinua ubora wa kazi zao. Itainua kipato chao pia.

Kubwa zaidi, walengwa ambao ni  wananchi walio wengi, watafaidika, mathalan, kwa watoto wao na wao wenyewe, kama watu wazima kupata maarifa zaidi na yenye ubora. Hivyo, tija kwa taifa zima.

Hata kama si mkubwa sana, hakika, ningependa nikumbukwe kwa mchango wangu huu kwa nchi yangu.

Na naamini pia, ni wajibu wetu kuifanya kazi hii kwa pamoja. Na kuwa,  kazi ya kuyafanikisha haya yote ni yetu sote.  Ni kwa maendeleo ya nchi yetu, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kiimani. Ni kwa maslahi ya taifa letu.
Maggid Mjengwa,
Msamvu, Morogoro.
0788 111 768
http://mjengwablog.co.tz

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment