Tuesday 1 January 2013

[wanabidii] ZANZIBAR NI KWETU (ZNK) KUENDELEA KUULINDA MUUNGANO KATIKA 2013!

Dear All,
Blogu la Zanzibar Ni Kwetu (ZNK) linawatakia Watanzania wote kila la kheri katika mwaka huu mpya wa 2013.
Sisi kama blogu la jamii tutaendelea kwa vitendo na kwa kalamu kuuhifadhi na kuulinda Muungano wetu – lakini sio Muungano huu wa mkubwa kumuonea mdogo, sio huu unao mruhusu mkubwa kujiunga na chombo chochote kile duniani lakini mdogo anaambiwa afuate Katiba, sio huu unaoendelea kuidhalilisha Zanzibar kama eti sio nchi kamili, sio huu unaowalinda wale wezi wa Kiwira, BAE Radar, BoT Towers (DSM+ZNZ), EPA Account, Richmond, Dowans, Ndege ya Rais, Buzwagi, ATCL plane rental, etc, etc; sio huu unaoshindwa kumrejesha nchini yule aliekimbilia Switzerland na pesa zetu za Radar, sio huu unaotuhadaa kuwa eti unafuatilia kwa makani zaidi juu ya pesa zetu zilizofichwa huko Switzerland wakati huo huo unamlinda kwa nguvu zote yule mzee mwenye tuhuma za kumiliki mabilioni ya shilingi katika akaunti yake ya nje katika kisiwa cha Jersey, sio huu unaotaka kuwaruhusu wezi wa nchi hii kujakugombea urais 2015, sio huu uliotaka kuchukua gesi na mafuta ya Wazanzibari  kuyapeleka DSM, kama vile gesi na mafuta hayo yanatoka Mtwara, sio huu unaowataka wagonjwa waende na mashuka yao ya kulalia kwenye hospital ya hali ya juu ya rufaa ya nchi hii - sio huu, sio huu, sio huu!
Bali ni ule unaotambua kuwa Muungano wa 1964 kwa sasa umepitwa na wakati, kama ulivyopitwa na wakati ule wa USSR, lakini wenzetu Warusi wakatambua mapema na wakauzika kwa haraka, Muungano unaotambua kuwa Zanzibar ni nchi kamili na ipo hai, Muungano unaotambua kuwa ipo haja ya kusikiliza na kuzingatia upande wapili wa Muungano unasema nini, ni ule Muungano utakaotambua haki ya kila upande, ni ule Muungano utakaolipa dividends za BoT kutokana na kiasi gani kila nchi ilichangia mwanzoni na sio kutokana na kila nchi inawatu kiasi gani – huo ndio Muungano tutakaoendelea kwa vitendo na kwa kalamu kuulinda katika mwaka 2013 na huo ndio Muungano tunaotaka ubarikiwe!

ZANZIBAR NI KWETU!

0 comments:

Post a Comment