Thursday 10 January 2013

[wanabidii] WAZANZIBARI WASIWASIKILIZE WANA-CHADEMA NA WAPINZANI WENGINE!

"Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu wa kusema Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika, wakumbuke kuwa Muungano ndiyo unaowafanya wanasema 'Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika', nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo: Kuna 'wao Wapemba na wao Waunguja."- Julius Kambarage Nyerere!
JUMAMOSI ijayo Zanzibar inatimiza miaka 49 tangu kufanyika mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yaliung'oa utawala wa kisultani ambayo uliingia madarakani Desemba 10, 1963 baada ya kuondoka wakoloni wa Kiingereza.
Mapinduzi hayo yanatokana na tangazo la Januari 12, 1964 asubuhi, pale sauti ambayo haikuwahi kusikika katika ukanda wa Tanganyika wala Zanzibar ikitangaza kufanyika kwa mapinduzi kisiwani humo.
Tangazo hilo ilikuwa la John Okello, ambaye mpaka mauti yanamfika haikufahamika kama alikuwa ni raia wa Kenya au Uganda. Okello na msaidizi wake Engine walitoa amri ya kukamatwa kwa mawaziri wa Serikali ya Sultan na kukataza watu kutembea.
Itakumbukwa kuwa usiku wa sherehe za Mapinduzi hayo Januari 11, 1964, Hayati Aman Karume alipelekwa mafichoni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumwepusha asikamatwe endapo mapinduzi hayo yasingefanikiwa.
Katika mwendelezo wa juhudi za kukikomboa kisiwa hicho, mamia ya watu wenye asili ya Oman na Comoro walifukuzwa Zanzibar ambapo watoto wadogo walipelekwa maeneo ya bandarini kuonana na baba zao kwa ajili ya safari ya Oman.
Kazi iliyofuata ilikuwa ni kulinda mapinduzi hayo na hatua zilizofikiriwa ilikuwa ni kuwa na Muungano utakaohakikisha kuwapo kwa ulinzi wa kuinusuru Zanzibar isirejeshwe mikononi mwa Sultani baada ya kupinduliwa.
Kupitia waasisi ambao ni Hayati Julius Nyerere na Abeid Aman Karume kutoka kila upande wa Aprili 26,1964 wakaamua kuchanganya udongo kama ishara ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26,1964 na kusaini Hati ya Makubaliano ya kuunda Tanzania.
Sababu nyingine za kulinda kisiwa hicho kupitia Muungano ilikuwa ni kujenga umoja wa Wazanzibar baada ya kuonekana mpasuko uliosababishwa na ubaguzi miongoni mwa Wapemba na Waunguja ambapo hali inaonyesha bila Muungano, visiwa hivyo vingeweza kutengana wakati wowote.
Pamoja na kuwapo Muungano, mpasuko baina ya Uunguja na Upemba umeendelea kuonekana hadi leo na wakati wa kutoa maoni ya Katiba Mpya, wapo waliosema wazi kuwa ziwepo Serikali nne, wakimaanisha Serikali ya Unguja, Pemba, Tanganyika na ile itakayokuwa ya Muungano.
Ieleweke kwamba hata busara ya makubaliano kati ya Rais msaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kupitisha kura ya maoni kwa Wazanzibar na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inatokana na sababu ya kuimarisha uhusiano kati ya Unguja na Pemba.
Pamoja na kubainika kwa upungufu mkubwa ukiwamo kutonufaika na Muungano huo, inasemekana kuna makundi yanayotumiwa sasa kisiasa na Sultani au wafuasi wake, kutaka kuuvunja Muungano wakati huu wa kuandaa Katiba Mpya, ili kuirejesha Zanzibar mikononi mwao.
Hata hivyo, umuhimu wa Muungano huo unazidi kuwapo na kuonekana kama ambavyo hayati Mwalimu alikuwa akisema mara kwa mara, kuwa mgawanyiko huo ukiruhusiwa Zanzibar haitakuwa salama.
Mwalimu anasema: "Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu wa kusema Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika, wakumbuke kuwa Muungano ndiyo unaowafanya wanasema 'Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika', nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo: Kuna 'wao Wapemba na wao Waunguja."
Pamoja na haki ya kutoa maoni waliyo nayo wananchi wa Tanzania, sioni kama ni busara kuuvunja Muungano. Suluhisho pekee ninaloliona ni  kuondoa kero zake lakini si kuuvunja bali kuuimarisha.
Kutokana na umuhimu wake, ndiyo maana hata kwenye mchakato wa Katiba suala la Muungano halitaguswa kwa maana ya kuuvunja.
Katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Muungano ni moja ya vipengele nyeti ambavyo havitagusa  Katiba Mpya, lakini mjadala wake unazidi kuwa moto hasa upande wa Zanzibar.
Kama ni Mtanzania na unayo mapenzi na Kisiwa cha Zanzibar tafakari sana uamuzi ambao utakuwa umeufanya, ili usije kuwa mfano wa visiwa mbalimbali vinavyojuta na kuitafuta amani bila mafanikio.
Chanzo: Mwananchi
Kwa maelezo zaidi kutoka Mwananchi bonyeza hapa: Zanzibar Ni Kwetu

0 comments:

Post a Comment