Friday, 28 February 2014

[wanabidii] Neno Fupi La Usiku: Afrika Safari Nyingine Huanza Na Njia Ya Panda..


Ndugu zangu,

Jioni hii kupitia runinga nilimsikia Profesa Costa Mahalu, Mwenyekiti wa Tume ndogo ya Bunge Maalum kwa kazi ya kuandaa rasimu ya kanuni akitamka, kuwa swali la ama kura ya faragha (siri) au ya dhahiri ( wazi) wataachiwa Wabunge wenyewe waamue.

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Mheshimiwa Kificho naye hakuficha kuonyesha kwa sura na hata kauli, juu ya ugumu wa jambo hilo. Akatolea mfano wa mpira, kwamba sasa uko kwa Wabunge.

Kwa kuziangalia baadhi ya sura za Wabunge wale, hakika ni vigumu kuwaonea wivu kwamba wamo ndani ya jengo lile. Wana wakati mgumu, maana, umma nao unawaangalia.

Naam, nimepata kuandika, kuwa Afrika safari zetu nyingi ni za bure tu. Na nyongeza hapa, ni kuwa , safari zetu nyingine Afrika huanza na njia panda. Kwamba unapoianza tu safari unakutana na njia panda.

Na ni kwenye njia panda ndipo mwanadamu unatakiwa utumie hekima na busara. Njia panda inakutaka ufikiri kwa makini. Maana, ukichagua njia kwa makosa, basi, safari yako itakuwa ni ya mwelekeo mwingine. Si kule ulikotaka kwenda. Na kazi ya kuirudia njia sahihi huwa ni ngumu sana.

Jioni hii pia nimesoma tena baadhi ya vifungu vya Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba. Kwa mara ya kwanza nimeipitia rasimu hii kwa masikitiko, maana, mbali ya kwamba ina mambo mengi sana mazuri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake, kwa kizazi hiki na vijavyo, nahofia, kuwa kinachoendelea Dodoma, ambapo, ni dhahiri, kuwa zinaonekana dalili za mijadala kutawaliwa na ushabiki wa vyama kuliko wa nchi na mustakabali wake. Ni dalili za kuwa njia panda na pengine tumeshaanza kuifuata njia isiyo sahihi. Kwamba tunapotea kama Taifa.

Na ninaposoma rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba na kupitia vifungu kama kile cha Sura ya Tisa, kinachohusu Bunge la Muungano, sehemu ya Kwanza, Ibara ya 113 kifungu cha 3 kinachosema;

" Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za Ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamme."

Kabla ya hapo wanawake wengi waliingia Bungeni kwa njia ya Viti Maalum. Kwa rasimu hii ya Katiba, wanawake watapata nafasi ya kushindana wenyewe kwenye majukwaa ya uchaguzi. Ni maendeleo ya kidemokrasia.

Najiuliza, hivi ni kwa nini Tume ya Jaji Warioba hawakuandaa Plan B kwa maana ya mpango 'B' . Na plan B hapa ingelikuwa ni kuandaa mazingira, kuwa endapo rasimu hii ya Katiba itakwama, basi, yale yote mazuri yaliyomo kwenye rasimu na yanayokubaliwa na pande zote, na yenye kuweza kuhamishiwa kwenye Katiba ya sasa bila kusababisha matatizo, basi, yangefanyiwa utaratibu wa kuingizwa, kwa maana ya kuifanyia marekebisho ya ' dharura' Katiba iliyopo. Najaribu kufikiri tu, kwa uhuru.

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252
http://mjengwablog.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment