Thursday, 27 February 2014

[wanabidii] Ya kuzingatia kwenye mapambano dhidi ya kero za Muungano Tanzania

Imeandikwa na: Dk. Antipas Massawe - Mhandisi Migodi - Dar es Salaam.

Muungano Tanzania ulizaliwa tarehe 26 April, 1964. Sababu kubwa iliyopelekea kuzaliwa kwake ni moyo waliokuwa nao waasisi wake (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume) wa kuunda Muungano wa nchi huru za Bara la Afrika wakianzia na shirikisho la Afrika ya Mashariki. Lengo lilikuwa kulinda na kudumisha mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 January, 1964 dhidi ya utawala wa wachache wa kisultani ulioondolewa madarakani na kuanzisha ujenzi wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na Muungano wa Bara la Afrika kwa lengo la kujijengea uwezo wa kulinda uhuru wa waafrika na raslimali zao dhidi ya tamaa mbaya kutoka mataifa makubwa ya kibeberu.

Kuzaliwa Muungano Tanzania kulitokana na matakwa binafsi ya waasisi wake na wananchi wa kawaida pande mbili za Muungano hawakushirikishwa kikamilifu kwenye maamuzi yote husika kwenye kuundwa kwake na haionekani mahali popote chaguo la Muungano chini ya muundo wa serikali mbili lilihusisha
uchambuzi wa kina kubaini ulio bora zaidi miongoni mwa mibadala muhimu kama: moja (ya Muungano), mbili (ya Zanzibar na ya Muungano), tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano) na tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na Muungano wa Mkataba). Kwa kifupi Muungano Tanzania ulizaliwa wakati wa kipindi cha udikteta wa Chama kimoja tawala ndani ya pande zote mbili husika kwenye Muungano, kama chaguo la waasisi wake kutoka pande mbili washirika na matokeo ya mapinduzi ya Zanzibar dhidi ya utawala wa kisultani.

Muungano Tanzania ni wa pekee, haujawahi kuigwa na wengine popote duniani na umedumu chini ya utawala wa udikteta wa Chama kimoja wakati dunia ilipokuwa imegawanyika makundi mawili makubwa ya nchi za kibepari na kikomusti zisizoshirikiana au kuingiliana kwa mengi, na sasa uko chini ya utawala wa demokrasia ya vyama vingi kwenye enzi mpya ya utandawazi inayowezesha nchi zote huru (ndogo na kubwa) ziweze kuwasiliana na kutenda mahali popote ndani ya dunia isiyokuwa na mgawanyiko wa makundi ya nchi zisizo penyeka na wengine.

Kasoro kwenye Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili hazikuweza kujitokeza kwenye awamu yake ya kwanza chini ya utawala wa chama kimoja kwani chama kimoja tawala ndicho kimekuwa kikiamua yote kuhusu maswala ya Muungano na jukumu la wengine wote kutoka Tanganyika na Zanzibar lilikuwa ni kubariki maamuzi hayo ya Chama kimoja tawala. Kwa mfano, Chama kimoja tawala kikishaamua huyu ndiye atakayekuwa rais wa Muungano, basi jukumu la wengine wote kutoka pande mbili za Muungano lilikuwa ni kupiga kura moja ya ndio kuashiria kubariki kwao chaguo la Chama hicho kimoja tawala.

Kwa hiyo kutokuwepo upinzani wa vyama vingine vya siasa dhidi ya udikteta wa Chama kimoja tawala kuhusu maswala ya Muungano na Rais mteule wa chama tawala kutokuwa na ushindani wa wagombea kutoka vyama vya upinzani imekuwa ndiyo sababu kuu ya kutoweza kutambulika kasoro za Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili unaohusisha: Wazanzibari (ambao karibu wote ni waumini wa dini ya kiislamu) na watanganyika (ambao karibu wote ni nusu waumini wa dini ya kiislamu na nusu waumini wa dini ya kikristu); fursa iliyopewa Zanzibar ya kuendelea kudumisha serikali yake ya Zanzibar wakati Tanganyika ikinyimwa fursa kama hiyo ya kuendelea kudumisha yake ya Tanganyika; wazanzibari kuwa na haki ya kumiliki ardhi Tanganyika wakati watanganyika hawana haki kama hiyo ya kumiliki ardhi Zanzibar; wazanzibari 1,303,569 (2012) kupewa theluthi moja ya wawakilishi kwenye Bunge la Muungano wakati watanganyika 43,625,354 (2012) wakipewa theluthi mbili zilizosalia bila kuzingatia umuhimu wa wawakilishi kutoka pande mbili za Muungano kuwakilisha idadi sawa za watu; wawakilishi na mawaziri wa Muungano kutokea Zanzibar kushiriki Bunge na Baraza la Mawaziri Tanzania wakati wa yasiyokuwa ya Muungano yanapojadiliwa huku wenza wao kutoka Tanganyika wakiwa hawashiriki kwenye Baraza la Wawakilishi na Mawaziri Zanzibar wakati kama hayo yakijadiliwa; na kwa sasa wazanzibari kuwa na Katiba yao wakati watanganyika hawana yao.

Kasoro ya kwanza kubwa ya huu Muungano Tanzania inatarajiwa kujitokeza kwa nguvu kwenye awamu yake ya pili chini ya demokrasia ya vyama vingi. Kwa mfano itakapojitokeza kwamba miongoni mwa wagombea kiti cha urais mmoja ni muumini wa dini ya kikristu na mwingine ni muumini wa dini ya kiisilamu basi itarajiwe kwamba mara nyingi wazanzibari wengi (ambao karibu wote ni waumini wa dini kiislamu) watajitokeza na kumpigia mgombea mwenza kidini kura ya ndio bila kuzingatia vigezo vingine vya ubora. Athari ni kwamba Muungano Tanzania mara nyingi utakuwa ukimkosa rais aliye bora zaidi miongoni mwa waliopo na hata kusabisha miibuko ya chuki za kidini kutokana na muundo wake wa serikali mbili kuwapa waumini wa dini moja fursa ya kutumia udini wakati wa kupiga kura zao za kumchagua atakayekuwa rais wa Muungano chini ya mfumo wa vyama vingi. Fikra hii imetokana na kutambua ukweli kwamba viumbe wote wanaojumuisha binadamu wametawaliwa na hulka ya ubinafsi kimaumbile. Kimaumbile binadamu ametawaliwa na hulka ya mimi na familia yangu kwanza, ikifuatiwa na ukoo wangu kwanza, kijiji changu kwanza, kabila langu kwanza, wilaya yangu kwanza, mkoa wangu kwanza, ukanda wangu kwanza, nchi yangu kwanza, dini yangu kwanza-yaani kundi langu la karibu zaidi kwanza. Ubinafsi aliotawaliwa nao binadamu kimaumbile ilibidi uzingatiwe kwenye kuhakikisha muundo wa serikali ya Muungano Tanzania hautoi kwa waumini wa dini yeyote ile, chama chochote kile au mshirika yeyote yule fursa ya kutumia ubinafsi wa kidini ndani ya demokrasia ya vyama vingi kwenye Muungano Tanzania dhidi ya maslahi ya wote ndani ya Muungano au nchi yeyote mshirika. Hili halingekuwa tatizo iwapo uwiano wa idadi za waumini wa dini zote ndani ya Zanzibar ungekuwa ni huo ndani ya Tanganyika. Kuendana na hali halisi ni kwamba maslahi ya watanganyika walio wengi na waumini wa kikristu ndani ya Muungano ndio wanaohujumiwa na ziada ya waumini wa kiislamu waliopandikizwa na Muungano Tanzania kwenye demokrasia yao ya Tanganyika kutokea Zanzibar. Kwa hiyo mojawapo ya mapambano dhidi ya kero za Muungano ni kuchukua hatua thidi ya uwezekano wa kuzuka udini kwenye demokrasia yake kutokana na Zanzibar kuchangia waislamu watupu wakati Tanganyika ikichangia karibu nusu waislamu na nusu wakristu.

Kasoro ya pili kubwa ya huu Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili uliowapa Wanzanzibari fursa ya kuendelea kuwa na serikali yao ya Zanzibar wakati watanganyika wakinyimwa fursa kama hiyo ya kuendelea kuwa na yao ya Tanganyika itarajiwe pia kujitokeza kwenye awamu yake ya pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwani sio haki wazanzibari kufaidi kushiriki ndani ya Bunge na Baraza la Mawaziri Tanzania wakati watanganyika hawana fursa kama hiyo ya kushiriki ndani ya Baraza la Wawakilishi na Mawaziri Zanzibar yanapojajiliwa yasiyokuwa ya Muungano kwani ni kuwapa wazanzibari fursa ya kuyafahamu mazuri na mabaya mengi ya Tanganyika wakati watanganyika hawana fursa kama hiyo ya kuyafahamu hayo kwa upande wa Zanzibar. Ili kuondokana na kero zitokanazo na kasoro hii, ni budi Zanzibar iache kushiki ndani ya Bunge na Baraza la Mawaziri Tanzania wakati wa yale yasiyokuwa ya Muungano yanapojadiliwa.

Kasoro ya tatu kubwa itarajiwe kujitokeza kutokana na Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili kuwapa wazanzibari fursa ya kumiliki ardhi Tanganyika huku ukiwanyima watanganyika haki kama hiyo ya kumiliki ardhi Zanzibar kutakakosababisha ukiukwaji wa uwiano wa asili wa idadi za waisilamu na wakristu ndani ya Tanganyika na uwezeshaji wa makusudi kwa wazanzibari kumiliki raslimali za Tanganyika kutakakowapa wazanzibari na waumini wa dini ya kiislamu fursa za kumiliki hisa nyingi zaidi za demokrasia ya Muungano na raslimali za Tanganyika kuliko watakazomiliki watanganyika na waumini wa dini nyingine, hasa wakristu. Kasoro hii itakuwa kolezo la athari zitakazosababishwa na kasoro ya kwanza. Kuwaondolea wazanzibari fursa maalumu waliopewa na Muungano Tanzania ya kumiliki ardhi Tanganyika ndio njia pekee ya kuondokana na kero zitokanazo na kasoro ya tatu.

Kasoro ya nne kubwa itasabibishwa na wazanzibari (walio wachache sana) kupewa idadi kubwa mno ya wawakilishi ikilinganisha na idadi ya wawakilishi waliyopewa watanganyika (walio wengi sana) ndani ya Bunge la Muungano kutakakosababisha wazanzibari wapate huduma toshelezi zaidi ya Bunge la Muungano Tanzania na uwezeshaji wa makusudi wa wazanzibari na waisilamu kuwa na hisa kubwa zaidi ya demokrasia ya Muungano Tanzania kuliko watanganyika na wakristu. Kasoro hii itakuwa kolezo la athari zitakazosababishwa na kasoro ya kwanza na kugawa nafasi za wawakilishi kwa wazanzibari na watanganyika ndani ya Bunge la Muungano kunakozingatia umuhimu wa wakilishi kuwakilisha idadi sawa za watu ndani ya Bunge hilo ndio njia pekee ya kuondokana na kero zitokanazo na kasoro ya nne.

Kasoro ya tano kubwa itarajiwe kujitokeza pia pale ambapo muundo wa Muungano unaojumuisha serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano Tanzania) utakapokataliwa kama mfano wa kuigwa na hivyo kuwa hata kikwazo kwenye ujenzi wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika unaoshirikisha Zanzibar na Tanganyika. Muundo wa muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ilibidi uwe ni ule unaotarajiwa utakubalika kama mfano wa kuigwa na wengine wote kama msingi kwenye ujenzi wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na hatimaye Muungano wa Bara la Afrika tarajiwa. Vinginevyo huu Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano Tanzania) utaweza hata kuwa kikwazo kwa ushiriki wake kamilifu na wenye manufaa makubwa ndani ya shirikisho la Afrika ya Mashariki na Muungano wa Bara la Afrika tarajiwa. Njia pekee ya kuondokana na kero zitokanazo na kasoro ya tano ni kuhakikisha maswala ya Muungano Tanzania ndio hay ohayo tarajiwa kwenye Muungano wa Shirikisho la nchi za Afrika ya Mashariki na Bara la Afrika au itakuwa rahisi kurekebisha iwapo tofauti zitajitokeza.

Muundo wa serikali moja ya Muungano ni mzuri kwani ndio wenye gharama ndogo lakini kwa Wazanzibari ambao karibu wote ni waisilamu na watanganyika ambao karibu wote ni mchanganyiko nusu waisilamu na na wakristu mfumo huu bado sio mzuri kwani unatoa fursa ya agenda za udini kujijenga ndani ya demokrasia ya Muungano Tanzania chini ya vyama vingi na matokeo yake ni Muungano kujikuta udini ukiuchagulia serikali dhaifu na kuunyimwa ile imara kutakakosabisha utendaji dhaifu serikalini, uwezekano wa migogoro ya kidini kuibuka, pande mbili ndani ya Muungano kushindwa kubuni na kuendeleza fursa nyingi muhimu kwa maendeleo yake binafsi ambazo hazitaonekana muhimu katika ngazi ya Muungano lakini muhimu sana katika ngazi washirika, na athari nyinginezo nyingi. Baya zaidi litokanalo na kuunganisha nchi kadhaa na kuunda Muungano wa serikali moja usiohusisha za washirika ni kuangamiza 'diversity'. Pangekuwepo na mifumo ya utawala tofauti ndani ya nchi washirika kama ilivyo kwenye Jumuia ya Nchi za Ulaya ingependeza sana. Laiti pangekuwepo utawala wa Kisultani ulioboreshwa huko Zanzibar kungeufanya Muungano wa Tanzania kuwa kivutio kikubwa zaidi kwa wageni kutembelea. Utalii ni kutembelea 'diversity' na kinachoifanya dunia ipendeze hivyo ni 'diversity'.

Muundo wa serikali tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano) sio mzuri kwani haitakuwa rahisi kujenga hoja za msingi kudhihirisha manufaa ya kuwa na serikali ya tatu ya Muungano yenye gharama kwa ajili ya kuunganisha Zanzibar ambayo ni kisiwa kidogo sana ndani ya bahari ya Hindi na Tanganyika ambayo ni nchi kubwa sana ndani ya Bara la Afrika. Hata hivyo mfumo huu wa kila mhusika ndani ya muunngano kuendelea kudumisha serikali yake ndani ya serikali ya Muungano unaonekana ndio mfumo mzuri wa kuigwa kwenye ujenzi wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na Muungano wa Bara la Afrika tarajiwa kwani kutokana na wingi wa mataifa shiriki ndani ya Muungano, agenda za ukabila kama zinavyojitokeza huko Rwanda (yenye makabila mawili tuu makuu) na udini zitakosa fursa ya kujijenga na kukua ndani yake na kila taifa shiriki na serikali yake litaendelea kuwa na fursa ya kubuni na kuendeleza zile agenda na sera zake binafsi za maendeleo ambazo hazionekani muhimu katika ngazi ya serikali ya Muungano.

Muundo wa serikali tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na Muungano wa Mkataba) inaonekana ndiyo unaofaa kuzijengea Zanzibar na Tanganyika uhusiano na ushirikiano mzuri, endelevu na uliojengeka kwenye misingi imara ya makubaliano ya hiari miongoni mwa washirika na vipaumbele vyao kuendana na fursa zilizopo kwenye utandawazi. Umuhimu wa nchi jirani Kuungana ili kujijengea uwezo wa kulinda watu wake na raslimali zao dhidi ya tamaa mbaya kutoka mataifa makubwa ya kibeberu haupo tena kwenye enzi yetu ya utandawazi unaowezesha nchi zote kuchangamkia fursa mahali popote duniani kwa njia ya kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na umoja wa mataifa na nchi moja moja ulimwenguni.

Itakuwa vizuri sana iwapo mmojawapo wa wataalumu wachache wanaopigania kwa nguvu zote kuendelea kuwepo Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano) atajitokeza kuelezea kwa kifupi na kwa lugha nyepesinyepesi nia na madhumuni ya kuundwa Muungano Tanzania, faida na madhara ya uliopo wa serikali mbili dhidi ya wa serikali moja, tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika nay a Muungano), tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na Muungano kwa Mkataba), na hata dhidi ya kutokuwepo kabisa Muungano.

Viongozi wetu kwenye ngazi za juu serikalini wanaposimama majukwaani na kuanza kuzungumzia hili swala la Muungano Tanzania huwa nikiwasikiliza kwa makini sana nikitarajia kwamba watataja faida kuu za kuwepo kwake chini ya mfumo wa serikali mbili uliopo dhidi ya hasara zitakazotokana na kuwepo kwake chini ya mifumo mingine ya serikali mbadala, au kutokuwepo kwake kabisa. Majibu kwa maswali hayo ndio yaliyotarajiwa kuwa msingi kwenye mjadala kuhusu umuhimu wa kuwepo Muungano Tanzania na muundo wa serikali yake utakaokuwa bora zaidi.

Huwa nakatishwa sana tamaa ninapoishia kusikia Muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili ni lazima uendelee kuwepo kwa sababu unaunganisha watanganyika na wazanzibari walio na undugu wa karibu ; wazanzibari na watanganyika wanaoleana; wazanzibari wameshawekeza sana Tanganyika; na wa serikali tatu utapelekea Muungano Tanzania na hata Zanzibar kuvunjika. Ukweli ni kwamba majibu kama hayo sio halalishi ya Muungano Tanzania chini ya mfumo wa serikali mbili kuendelea kuwepo.

Kutokana na majibu hayo yasiyokuwa ridhishi ilinibidi nitafakari mwenyewe na kuishia kudhani kwamba huenda agenda nzuri Muungano Tanzania uliokuwa nayo wakati wa kuundwa kwake chini ya demokrasia ya Chama kimoja imeshageuzwa kimya kimya na kuwa agenda ya wachache ndani ya Tanganyika na Zanzibar wenye lengo la kukuza agenda zao binafsi dhidi ya zile za Muungano kitaifa kupitia wingi wa kura zao ndani ya Muungano Tanzania chini ya demokrasia ya vyama vingi.

Kudhani kwangu hivyo kumetokana na wale wa Tanganyika bara kuridhika bila manunguniko wazanzibari 1,303,569 (2012) kupewa theluthi moja ya wawakilishi ndani ya Bunge la Muungano Tanzania wakati watanganyika 43,625,354 (2012) wakipewa theluthi mbili tu za wawakililishi ndani ya Bunge hilo; wazanzibari kushiriki kwenye Bunge na Baraza la Mawaziri Tanzania yasiyokuwa ya Muungano yanapojadiliwa wakati watanganyika hawashiriki kwenye Baraza la wawakilishi na Mawaziri la Zanzibar yasiyokuwa ya Muungano yanapojadiliwa; Wanzanzibari kuwa na Katiba yao wakati watanganyika hawana yao; na Wazanzibari kuwa na haki ya kumiliki ardhi Tanganyika wakati watanganyika hawana fursa ya kumiliki ardhi Zanzibar. Sijui nitakuwa nimekosea wapi ninapohisi kwamba wazanzibari wanapewa fursa za upendeleo ndani ya Muungano Tanzania kama hongo ili kuwavutia wawepo na kufanikisha agenda ya makundi dhidi ya ile agenda ya wote ndani ya demokrasia ya Muungano Tanzania chini ya mfumo wa vyama vingi!!??

Nitaweza tu kuridhika na agenda ndani ya Muungano Tanzania chini muundo wa serikali mbili (ya Zanzibar nay a Muungano) iwapo Zanzibar na Tanganyika zitapewa idadi za wawakilishi ndani ya Bunge la Muungano kuendana na idadi zao za watu (ikizingatiwa kwamba wawakilishi wanatakiwa wawakilishe idadi sawa za watu ndani ya Bunge la Muungano); Wawakilishi na Mawaziri kutokea Zanzibar wasishiriki kwenye Bunge na Baraza la Mawaziri Tanzania yasiyokuwa ya Muungano yanapojajiliwa; watanganyika wawe na Katiba yao kama wazanzibari walivyo na yao; na fursa ya wazanzibari kumiliki ardhi Tanganyika ifutwe kwa vile watanganyika hawaruhusiwi kumiliki ardhi Zanzibar na Zanzibar haina ardhi ya kugawa kwa watanganyika.

Pia, ni vizuri iwapo Muungano Tanzania utatoa kwa Tanganyika na Zanzibar fursa ya kushirikiana na nchi nyingine au kujitoa kwenye Muungano Tanzania au ushirikiano na nchi nyingine yeyote duniani pale inapoamua ni vizuri kufanya hivyo bila pingamizi lolote ikizingatiwa kwamba ili nchi yeyote ile iweze kufaidi utandawazi kwa kiasi kikubwa ni budi ishiriki kwenye mitandao ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kibiashara, n.k. na nchi nyingi iwezekanavyo duniani bila pingamizi kutoka kwa mshirika wake mwingine yeyote na kuachana au kushirikiana na yeyote mwingine pale inapoamua.

Muungano Tanzania usiwe ni sawa ngombe wawili kuwa malishoni huku miguu yao miwili ikiwa imeunganishwa kwa kamba kutakakowasabishia kero kubwa wawapo malishoni. Muungano usiwapunguzie washirika uhuru wao wa kujiamulia mambo yao wenyewe na kushirikiana na wengine kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kibiashara, n.k. kwenye enzi tuliyomo ya utandawazi ulimwenguni.

Tafakari juu njia bora zaidi ya kuwaondolea kero hawa ngombe wawili walioko malishoni huku wakiwa wamunganishwa pamoja kwa kamba migununi kutasaidia sana kutoenyesha njia bora zaidi ya kuondokana na kero za Muungano Tanzania.
Majajiliano yanayohusu umuhimu wa kuendeleza Muungano Tanzania na chaguo la muundo wa serikali yake unaofaa zaidi ni budi yakazingatia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi tulio nao na enzi yetu ya utandawazi inayotoa kwa nchi zote ndogo na kubwa duniani fursa sawa za kuchangamkia fursa mahali popote duniani kuendana na sheria na taratibu zilizowekwa na umoja wa mataifa na nchi moja moja duniani pasipo haja ya kuungana pamoja kujijengea nguvu za kujilinda dhidi ya uvamizi kutoka nchi nyingine.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment