Ubia wa TTCL na Bharti Airtel Wafikia Kikomo
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetiliana saini kuzinunua rasmi hiza asilimia 35 za Kampuni ya Bharti Airtel Afrika ndani ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ikiwa ni hitimisho la kuimiliki TTCL kwa asilimia 100 hivi sasa.
Tukio hilo limefanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo Serikali imewakilishwa na Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru huku kampuni ya Bharti Airtel Afrika ikiwakilishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Christian De Faria.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Laurence Mafuru aliishukuru Kampuni ya Bharti Airtel kwa kukubali kuuza hisa zake na kuirejeshea Serikali umiliki wa asilimia mia moja (100) ndani ya TTCL.
"Zipo sababu za kibiashara na maslahi mapana ya nchi ambayo yametuongoza kufikia hatua hii muhimu. Ni imani ya Serikali kuwa, baada ya kusaini nyaraka hizi zinazohitimisha ubia wa Kampuni hizi, tutaiona TTCL mpya iliyo na kasi na Viwango vya hali ya juu vya huduma kwa Wananchi sambamba na kujiendesha kibiashara na kutoa gawio kwa Serikali yenye malengo na matarajio makubwa sana kwa Kampuni hii, Amesema Mafuru."
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Bharti Airtel Afrika, De Faria alisema kampuni yao inayo furaha kubwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuinua mchango wa Sekta ya Mawasiliano katika kukuza uchumi na ustawi wa Wananchi wake.
"Tumeshirikiana kwa muda mrefu na tunaamini kuwa, tutaendelea kuwa pamoja katika kuikuza Sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania. Tunaishukuru Serikali na TTCL kwa kutekeleza makubaliano yetu na kuhitimisha ubia huu, alisema kiongozi huyo wa Bharti Airtel.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete akizungumza alisema kuhitimishwa kwa ubia huo wa kibiashara kati ya TTCL na Bharti Artel kunaleta faraja kubwa kwa uongozi wa TTCL.
"...Tumesubiri kwa muda mrefu ili taratibu za mchakato huu zikamilike, hatimae siku imewadia. Pamoja na shukrani za dhati kwa Serikali na wenzetu wa Bharti Airtel kwa kufanikisha mchakato huu, nirudie wito wangu kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCl, sasa kumekucha. Ni wakati wa kuonesha kwa vitendo uwezo na uzalendo wetu katika kutekeleza mipango yetu ya kibiashara na ndoto yetu kuwa Mhimili na kinara wa Sekta ya Mawasiliano nchini," aliongeza Profesa Mbwete.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura akizungumza katika tukio hilo alisema hatua hiyo itaongeza kasi ya Kampuni ya Simu Tanzania katika kutekeleza mikakati yake ya kibiashara ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu.
"Hivi karibuni, kumekuwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Bodi, Manejimenti na Watumishi wa TTCL katika kuitikia wito wa Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuihuisha Kampuni hii, kuirejesha katika ushindani na kuifanya kuwa moja ya wachangiaji muhimu wa uchumi kupitia huduma za Mawasiliano na gawiwo kwa Serikali," alisema Dk. Kamugisha Kazaura.
Aliongeza kuwa tayari TTCL imeanza kuboresha huduma za mawasiliano ya simu za mezani, mkononi na intaneti ikiwa ni pamoja na kuzindua huduma mpya kama vile 4G LTE, IPTV, FMC (Fixed Mobile Convergency), kuhuisha simu za mezani zifanye kazi.
Aidha katika kujiimarisha TTCL pia imezindua nembo mpya ya Kampuni, inaendelea kuboresha Maduka na Vituo vyao vya kutolea Huduma kwa Wateja na kutumia vyema Vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii kwa kutoa Elimu kwa Umma na kufanya Matangazo na Promosheni. Hizi zote ni juhudi za kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Kampuni ya Zain Group (kwa sasa Bharti Airtel) ilionesha nia ya kujiondoa kwenye umiliki wa hisa asilimia 35 ndani ya TTCL mwaka , 2009. Serikali ya Tanzania kama mmiliki mwenye hisa nyingi (majority shareholder) ilikubaliana na uamuzi wa Mbia Mwenza kuondoka katika umiliki wa TTCL
Hii ilitokana na sababu kubwa kuwa Mbia mwenza alitaka kujikita zaidi na biashara ya simu za mkononi na wakati huohuo Serikali ilitaka kuiimarisha TTCL katika huduma inazotoa zikiwemo simu za mezani na huduma ya data pamoja na simu za mkononi.
Mazungumzo ya kuondoka kwa Mbia Mwenza ndani ya TTCL yalianza rasmi mwezi Julai, 2009 hata hivyo, majadiliano hayakuweza kuhitimishwa kutokana na uamuzi wa Kampuni ya Zain Group ambayo tayari ilionesha nia ya kuondoka TTCL, kuuza hisa zake kwa Kampuni ya Bharti Airtel mwaka 2010. Majadiliano rasmi ya ununuzi wa asilimia 35 ya hisa za Bharti Airtel katika TTCL kati ya Timu ya Majadiliano ya Serikali na Bharti Airtel yalianza tarehe 6 Novemba, 2012 na kuhitimishwa tarehe 20 Novemba, 2014 kwa makubaliano ya Serikali kununua hisa hizo kwa thamani ya shilingi Bilioni 14.9. majadiliano yaliingatia taarifa za wathamini zilizotolewa na pande zote mbili pamoja na haja zingine za msingi.
Baraza la Mawaziri kupitia kikao cha tarehe 19 Februari, 2015 liliridhia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Timu ya Majadiliano ya Serikali na Bharti Airtel ya Serikali kununua hisa za Bharti Airtel ndani ya TTCL kwa thamani ya shilingi bilioni 14.9 na kuagiza yatekelezwe.
Mnamo tarehe 10 Julai, 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania lilikubaliana na uamuzi wa Serikali na kushauri kuwa Serikali iharakishe kutekeleza mpango wake wa kuilipa Bharti Airtel ili iendelee na mipango yake ya kuiboresha TTCL.
Kusainiwa kwa Mkataba wa Bharti Airtel kunahitimisha mbio za muda mrefu za pande zote mbili kutaka hisa zinazomilikwa na Bharti Airtel ndani ya TTCL kurudishwa Serikalini.
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066 / 0756 469470
Web:- www.thehabari.com
http://joemushi.blogspot.com
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment