Njama Mpya Mapato ya Madini (Makala yamechapishwa Uk. 17, Gazeti Raia Mwema, jana Juni 8)
Tanzania ni nchi mwanachama wa mpango wa Extractive Industries transparency Initiative (EITI) tangu mwaka 2009. Mpango huu kwa sasa unatekelezwa na nchi wananchama 51 duniani kote. Mpango huu ulibuniwa tangu mwaka 2002 wakati wa mkutano wa maendeleo endelevu duniani uliofanyika Johanesburg, Afrika ya Kusini. Tanzania iliamua kujiunga na mpango huu kutokana na mapendekezo ya ushauri wa Kamati ya Bomani (2007/2008). Lengo mahsusi la mpango wa EITI ni kuimarisha usimamizi na udhibiti mapato yatokanayo na madini, gesi, mafuta na rasilimali nyinginezo. Katika uhalisia wake, mpango huu ukitekelezwa kama inavyotakiwa, ni mwiba mkali kwa makampuni hususan ya kigeni (makampuni ya kibeberu) na wawekezaji wakwepa kodi na tozo nyingine. Lengo la maendeleo la mpango wa EITI ni kuhakikisha wananchi katika mataifa maskini yenye rasilimali za madini, gesi na mafuta, wananufaika na mapato yatokanayo na rasilimali hizo.
Kwa nchi wanachama, utekelezaji wa mpango huu ni hiari, ila kwa dhamira yake, mwaka jana (2015) Seriali ilipendekeza na kupitisha Bungeni, sheria ya kusimamia utekeleza wa EITI nchini. Kila nchi mwanachama wa EITI hupanga utaratibu wake wa kuendesha na kusimamia mpango husika. Kwa Tanzania kuna wajumbe watano kutoka AZAKI na wengine kama hao kutoka makampuni na serikali.
Muundo wa kitaasisi wa mpango wa EITI unarasimishwa na Kamati ya Utekelezaji inayoitwa Multi-Stakeholders Group (MSG). Vitendo vya serikali au makampuni kuingilia ushiriki wa Asasi za Kiraia (AZAKI) vimeharamishwa. Hata hivyo, AZAKI zenyewe zinawajibika kufuata taratibu, kanuni na itifaki ya EITI katika mchakato wa kuteua wawakilishi au kushiriki shughuli za MSG. Sharti hili ni muhimu ili kulinda hadhi na itifaki ya EITI duniani kote. Kila kundi; AZAKI, makampuni na serikali huteua wajumbe wake. Serikli na makampuni pia hufuata vigezo, kanuni, miongozo na taratibu za EITI kuteua wajumbe wao kuingia MSG. Kanuni na taratibu za EITI hujadiliwa na kupitishwa na wanachama wa mpango huo nyakati za makongamano wa dunia ya wanachama wake yanayofanyila kila baada ya miaka mitatu. Kongamano la hivi karibuni lilifanyika jijini Lima, nchini Peru, Amerika ya Kusini.
Ushiriki huru wa AZAKI na wajibu wa makampuni kuweka wazi ankara za malipo serikalini ndio nguzo kuu mbili za mpango wa EITI. Uangalizi usioingiliwa wa AZAKI hudhibiti njama zinazoweza kujitokea baina ya makampuni (ya madini, gesi na mafuta) na maofisa wa serikali wasiokuwa waaminifu kuliibia taifa. Kwa hiyo, wawakilishi wa AZAKI wanatakiwa kuwa watu waadilifu, imara, walioteuliwa kihalali kuwakilisha makundi mahsusi ya kijamii, wenye uelewa na wasiokuwa vibaraka au kuwa na madoa ya rushwa. AZAKI zikiwakilishwa na vibaraka wa makampuni au maofisa wala rushwa serikalini usimamizi wake hauwezi kuwa na uhakika. Hakuwezi kuwa na usimamizi wa wazi na uwajibikaji unaokusudiwa kuletwa na mpango wa EITI iwapo AZAKi zinawakilishwa na vibaraka wa makampuni au maofisa wa serikali wala rushwa.
Kamati ya kutekeleza mpango wa EITI husimamia kazi ya kuajiri mkaguzi mbobezi wa kimataifa ambaye hukagua vitabu vyote vya makampuni na idara za serikali zilizopokea pesa za kodi na/au tozo nyingine kutoka makampuni ya madini, gesi na mafuta. Ripoti za ukaguzi huchapishwa kila mwaka na kutangazwa ndani na nje ya nchi. Hadi sasa Tanzania imekwishachapisha ripoti sita za mpango wa EITI.
Katika ripoti zote sita zilizochapishwa na mpango wa EITI nchini, takwimu zinaonesha mafanikio kiasi fulani. Kati ya mwaka 2008 hadi Juni 2014 serikali ilipata kiasi cha dola za kimarekani zaidi ya bilioni mbili na nusu ($2,516,283,670) zilizolipwa na makampuni ya madini, gesi na mafuta kama kodi, mirahaba na tozo nyingine. Hata hivyo, kuna makampuni ya madini ya dhahabu yakiongozwa na kampuni kongwe ya ACACIA kutoka Canada ambayo hayajawahi kulipa kodi ya faida ya makampuni, 30% ya faida. Ripoti za EITI za kuanzia 2010 zinaonesha kampuni ya ACACIA imekuwa ikipata faida lakini halipi kodi ya makampuni. Kampuni hiyo inajitetea kuwa hailipi kodi kwa sababu bado inaendelea kufidia hasara iliyoipata miaka ya nyuma wakati wa uwekezaji. Hata hivyo kitendo hiki ni kinyume cha sheria za kodi za kimataifa zinazoelekeza kampuni isiyopata faida baada ya miaka mitano inatakiwa kuanza kulipa tozo ya 3% ya mauzo (turnover) yake kila mwaka kama kodi.
Hadi mwaka 2013 ACACIA ilikuwa ikimiliki na kuendesha migodi minne ya dhahabu nchini – Bulyan'hulu, North Mara, Tulawaka na Buzwagi. Kampuni hii ya Canada ilimiliki na kuendesha mgodi wa dhahabu wa Tulawaka kwa miaka kumi; kumaliza dhahabu zote ardhini bila kupata faida na hivyo kutolipa kodi ya faida ya makampuni! Kampuni hiyo hiyo ni mmiliki na mwendeshaji wa mgodi mkubwa wa dhahabu wa Bulyan'hulu kwa zaidi ya miaka kumi na saba. Miaka 17 imepita bila ACACIA kupata faida, hivyo kutolipa kodi ya faida ya makampuni!
Uwanja wa Vita
Tafiti za kitaalam zinabainisha kuwa katika mgawanyo wa rasilimali ngazi ya kimataifa, makampuni ya kigeni ya madini gesi na mafuta huendesha mahusiano na kimkakati ya siri baina yao na mashirika ya misaada ya kimataifa (INGOs). Hii ni kwa sababu INGOs na makampuni, wote kwa pamoja, hutegemea Afrika na nchi nyingine maskini kuendesha maisha ya anasa huko Ulaya na Amerika. Mashirika ya misaada ya kimataifa hulipwa fedha nyingi kama garama ya kuishi Afrika au 'kupoza' ghadhabu za Waafrika. Pesa hizo hutokana na faida nono (super profit) inayoingizwa na makampuni ya kigeni ya madini, gesi na mafuta yasiyolipa kodi – kwa mfano ACACIA. Katika kutimiza azima zao, mashirika ya misaada ya kimataifa huanzisha kambi (field offices), huajiri na kutumia mawakala na vibaraka ambao hufanya kazi kwa niaba na manufaa ya INGOs.
Mei 31, 2016 wajumbe wa zamani wa Kamati ya kutekeleza EITI walihitimisha jukumu lao, hivyo kutoa nafasi kwa wajumbe wengine kuteuliwa kusimamia mpango wa EITI nchini. Hii ni kazi ya kujitolea kwa manufaa ya nchi; siyo kazi ya kulipwa. AZAKI zilitakiwa kuteua wawakilishi wao kwa mujibu wa kanuni, taratibu na itifaki ya EITI.
Hata hivyo, inaonekana makampuni ya madini na mashirika ya misaada ya kimataifa yalikuwa yanasubiri fursa hiyo kuingiza vibaraka wao kwenye Kamati ya Kusimamia EITI nchini. Kinyume kabisa na taratibu, kanuni na itifaki ya EITI mashirika hayo yalitafuta fedha, 'yaliandaa wadau' yaliitisha mkutano wa wadau na kusimamia uteuzi wa wajumbe wa AZAKI kuwakilisha wananchi katika MSG. Wajumbe watahudumu kwa miaka mitatu hadi 2019.
Wafanyakazi wa mashirika ya Natural Resource Governance Institute (NRGI), Norwegian Church Aid (NCA), Oxfam GB na wakala wa Publish What You Pay (PWYP) kutoka Nairobi walikuwa na kazi kubwa kutimiza maagizo, maelekezo na matakwa ya waajiri na wateja wao. Kinachoshangaza, asasi kama PWYP iliyosajiliwa (cheti cha usajili namba 09533183) London nchini Uingereza Aprili 9 mwaka 2015 kama kampuni isiyokuwa na mtaji nayo ilidai na kupewa uhalali wa kuwakilisha Watanzania katika mpango wa EITI hapa nchini.
Vita ni kubwa. Mashirika ya misaada ya kimataifa kupitia vibaraka wao wanataka kudhibiti mchakato wa mpango wa EITI nchini. Hawataki AZAKI za hapa nchini zenye mtazamo unaojitegemea zishiriki kusimamia mchakato wa kuwezesha wananchi kunufaika na rasilimali zao za madini, gesi na mafuta. Serikali ikifanikiwa kusimamia makampuni ya kigeni ya madini, gesi na mafuta kulipa kodi stahiki, Oxfam GB, NCA, NRGI na mashirika mengineyo hayataweza kupumua. Yatakosa pesa za kuendesha maisha ya anasa huko kwao, kisha kubakiza vijisenti vya kuendeshea ofisi za kambi zao hapa nchini; kuwalipa mawakala, wateja na vibaraka wao. INGO hizo na nyinginezo huko kwao 'zinaheshimika' kwa kuthubutu kufungua ofisi za kambi barani Afrika. INGOs hizi hulipwa pesa nyingi kwa kuweka vibaraka na mawakala wao Afrika. Kwa kufungua ofisi za kambi na kuweka mawakala tu, INGOs hizi hupewa sifa ya kuitwa wataalam wa umaskini wa Afrika.
Mahusiano ya kiuchumi baina ya mashirika ya misaada ya kimataifa na makampuni ya kigeni ya madini, gesi na mafuta ndio wasomi watafiti na wachambuzi wa msigano wa maendeleo kati ya nchi za Ulaya na Afrika huita reverse dependence – yaani utegemezi wa kinyume. Ukisikia makampuni, mashirika ya misaada ya kimataifa, mawakala, vibaraka na wateja wao wanavyoongea, utashangaa kusikia wakisema maisha na maendeleo ya Tanzania (Afrika) yanawatemea wao, wakati ukweli ni kinyume chake.
Lakini njama hii siyo ndogo. Msomaji anaweza kuona, kwa mfano, jinsi shirika la NCA – shirika la kidini (Kanisa?) kutoka nchini Norway – lilivyojipatia jukumu la kuratibu madhahebu ya dini – Waislamu kwa Wakristo – kushiriki katika mpango wa EITI nchini. Tangu 2009 NCA ilijitengenezea ka-Kamati kake inakokaita Kamati ya Madhehebu Yote (Interfaith Committee) ambako NCA inakatumia kudhibiti uwakilishi bayana wa mashirika halisi ya dini katika usimamizi wa EITI nchini. NCA imekuwa ikiteua mwakilishi wake kwenye EITI nchini 'kwa niaba ya' Baraza la Maaskofu (TEC), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Kipentekoste Tanzania (PCT) na mashirika mengine. Hizi ndizo njama za kutengeneza na kuendeleza utegemezi wa kinyume. Bila ujanja huu NCA na INGOs nyingine haziwezi kuishi wala kuendesha ofisi zao za kambi hapa nchini. Hiki ndio kiini NCA kuhakikisha TEC, CCT, PCT, BAKWATA na mashirika mengineyo hayafurukuti wala kupata fursa ya kuteua mwakilishi wa EITI anayewajibika kwao moja kwa moja. Wakati wakatoliki, Waislam, Walutheri, Waangalikana, Wapentekoste na waumini wengine wakisali kwenye nyumba za ibada, NCA na INGOs nyingine wanahesabu kiasi, wanajaza ankara za madai na kuandika invoice kwa makampuni ya madini gesi na mafuta kudai gawiwo/mgao wao.
AZAKI na mashrika ya dini hapa nchini amkeni, kuweni makini na chukueni nafasi zenu za kushiriki katika mpango wa EITI. Vita inaendelea. Vita haina macho lakini mwisho wa mapambano menye haki hushinda vita.
Bubelwa E Kaiza,
Executive Director,
Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA),
P. O. Box 32505,
Ph.: +255784410939,
E-mail: bubelwa.kaiza@fordia.org
Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment