Thursday, 23 June 2016

[wanabidii] Hongera Rais Magufuli kuridhia kukatwa kodi

SASA ni rasmi kwamba, viongozi wote wa kisiasa watakatwa kodi katika kiinua mgongo chao kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Katika kundi hilo yumo pia Rais John Magufuli ambaye ameridhia kukatwa kodi, hivyo kutuma ujumbe bungeni kuwa yeye ni mbunge namba moja na anataka mapato yake yakatwe kodi stahiki, hatua inayofuata ni kutoachwa kwa mtu yeyote katika suala la kodi ya mapato.

Hayo yaliwekwa bayana bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyesema ujumbe wa Rais Magufuli wa kuridhia kukatwa kodi alipewa mapema alipopeleka pendekezo la kukata kodi ya mapato katika kiinua mgongo cha wabunge.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, kabla hata ya kuwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alipeleka mapendekezo hayo kwa Rais Magufuli ambaye hakusita, akisema atalipa kodi kwa kuwa yeye ni Mtanzania, huku akisisitiza ni lazima Watanzania wote walipe kodi kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.
Kutokana na kauli hiyo ya Rais, Dk Mpango alisema hata Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu wake, Dk Tulia Ackson, mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, viinua mgongo vyao nao vitakatwa kodi.
Hakika, uamuzi wa Rais Magufuli ni wa kupongezwa mno, kwani ameonesha ni mtu anayeongoza kwa mifano. Na hakika kwa hili ameonesha hakuna aliye juu ya sheria anayepaswa kuachwa katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia kodi. Hatua hiyo ya Serikali imemaliza pia mjadala uliokuwa umeanzishwa na wabunge wa kupinga mafao yao kukatawa kodi.
Walikwenda mbali zaidi na kudai watakuwa katika hatari ya kugeuka ombaomba mara baada ya kukoma ubunge wao. Walijenga hoja za kila aina kuhakikisha hawakatwi kodi na baadaye kuibuka na hoja nyingine kwamba, kama hoja zao hazitasikilizwa, basi viongozi wengine wote wa kisiasa nao wakatwe kodi.

Rais Magufuli, kwa kutaka kuweka usawa kwa watu wote raia wa nchi hii, amekuwa msikivu na kuridhia wote wakatwe kodi, akianza na yeye mwenyewe. Na hii tafsiri yake ni kwamba, hajapenda wachache waumizwe kwa kulipa kodi, ilhali wachache wakigeuka miunguwatu kwa kutoguswa na maumivu ya kodi.

Isingeingia akilini kuona wabunge wanaotajwa kuwa wanalipwa mishahara minono, posho nono na marupurupu ya kila aina, wakiachwa bila ya kulipa kodi, wakati watumishi wengine wakiwemo wa kada za chini kilio chao kikubwa ni mzigo wa kodi ambao hata hivyo Serikali imeanza kuufanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kupunguza makato ya kodi katika mishahara yao kutoka asilimia 11 hadi 9 kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.

Kwa kutambua umuhimu wa kodi katika ustawi wa nchi, na kwa kuwa sasa kila mmoja ataguswa na kodi zetu, ni vyema tukamuunga mkono Rais Magufuli aliyeonesha mfano wa uzalendo kwa nchi yake, lakini pia kwa usikivu wa maoni ya baadhi ya wabunge waliotaka ikiwezekana hata Rais aguswe na kodi katika kiinua mgongo.
Rais Magufuli amekubali na kuonesha njia, nani atakataa? Na tumuunge mkono ili kila mmoja aitendee haki nchi yake, badala ya kusubiri nchi iwatendee wao haki.

0 comments:

Post a Comment