Thursday, 27 November 2014

Re: [wanabidii] Taarifa ya VIP Engineering and Marketing Ltd: Umiliki wa fedha za escrow hauna utata, tatizo ni Mawakili

Ndugu Watanzania,
Nimesoma (nadhani taarifa kwa umma) ya VIP Engineering and Marketing Ltd kwenye gazeti la Mwananchi toleo namba 5238 la 25/11/2013, Uk 7. Ikiwa na kichwa, ' NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW'. Najua ni taarifa ndefu lakini isomeni ili pia kupata habari upande wa pili kutimiza ile tunaita natural justice tunavyomhukumu mtu kimaoni.
VIP wamejitetea sana katika taarifa hii. Kwa walio wengi umiliki wa IPTL na uhusiano wake na VIP Engineering and Marketing vinaweza kutuchanganya kidogo. Nitajaribu kuelezea vile ninavyofahamu ili hasa kujua kwa nini VIP Engineering wanajitosa kujibu hoja za wananchi kuhusu sakata la account ya udhamini (escrow account) ya Tageta. VIPEM walifanya ubia na shirika la Mechmar la Malaysia, VIPEM asilimia 30 na Mechmar asilimia 70 na kuunda Kampuni iitwayo Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Kuna maswali kama, Je, wabia hawa walilipia share zao kiasi gani? Je, zilikuwa ngapi na zenye thamani gani kila moja? Faida iliyopatikana kwa mwaka waligawanaje? Gawio hutozwa kodi, walilipa kodi kiasi gani hawa wabia tangu walipoanza kufanya biashara miaka ya 90 hadi leo? Iweje hadi mwaka 2013 VIPEM walikuwa hawajapewa gawio lao hadi wasubiri pesa za akaunti ya udhamini ya Tegeta?
Turudi kwenye taarifa ya VIPEM ya tarehe 25/11/2015 kutoka kwenye gazeti la Mwananchi  kwa umma. Ninayoyaona kwenye taarifa ni haya yafuatayo :
  1. VIPEM wanamtetea Prof Anna Tibaijuka ambaye vyombo vya habari vimeripoti kupewa Shs 1.6bil na mkurugenzi wa VIPEM. Kinachosemwa kuhalalisha mgao huu eti VIPEM walikuwa wanatoa mchango wao kwa shule anayoindesha Prof Tibaijuka na eti kwa sababu ana-promote elimu kwa watoto wa kike. Na taarifa inadai Prof alikuwa ameomba kwa maandishi mchango huu kwa muda mrefu na hivyo VIPEM walipopata gawio lao kupitia akaunti ya udhamini ya Tegeta (escrow account), wakaona ndio wakati mwafaka kuchangia elimu.
  1. Anasema saga Hii ni kwa sababu ya benki ya Standard Chartered kutaka zile hela za escrow ingelipwa yenyewe Kwa madai iliyo nayo kwa kwa kuwahi kuwakopesha IPTL. (hazungumzii kwa nini IPTL ilikuwa hailipi deni lake kwa benki hiyo)
  1. Jambo la escrow account linachochewa na Stanchart bank na eti ndiyo inayotoa information kwa vyombo vya habari.
  1. Anazitetea Mahakama za hapa
  1. Anadai pesa zilizokuwa kwa escrow account si mali ya umma
Hayo ni machache niliyoyaona. VIP wanashindwa kutuambia yafuatayo:
  1. Ukirejea hoja namba moja hapo juu, kutokana na gazeti la Mawio ambalo hakuna aliyekanusha pesa hizi zililipwa kwa account binafsi ya Prof Anna Tibaijuka. Je, hii Shule ya Babro Johanssson haina akaunti yake benki? Je watoto wakisoma ada hulipa kwa Prof au kwa shule? Prof Tibaijuka ni mtu mwenye elimu ya juu sana wenyewe wanaita Uzamivu yaani PhD ya mambo ya uchumi na pia ni mtumishi mwandamizi wa umma, hivi hajui kutofautisha kati ya shughuli binafsi na kampuni au shirika?
  1. Kama hiyo haitoshi inasemekana pesa hizi za escrow zimegawiwa kwa mtu wa RITA (ambaye alikuwa akisimamia ufilisi wa IPTL), Zimelipwa kwa mfanyakazi mwandamizi wa TRA (ambaye juzi Naibu Waziri wa Fedha aliagiza afukuzwe kazi na akaunti zake zishikiliwe), zimelipwa kwa majaji wawili na mmoja wao ni Professor (nadhani yuko EAC siku hizi) na amekiri kupokea zaidi ya million 400, Mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini, na wengine wengi . Amewapa hayo mamilioni aliwapa kwa sababu gani? VIPEM wamekwepa kuzungumzia hayo badala yake wamejikita kumtetea Professor Tibaijuka pekee. Kuna nini hapo?
  1. Kwa nini hizi pesa zitolewe kabla ya kesi ya pingamizi kuamriwa na mahakama? Kesi ya msingi imemriwa February 2014. VIPEM katika habari yake kwa umma haizungumzii kwa nini walisukuma kupewa hizi pesa zilizokuwa chini ya mdhamana badala ya kusubiri maamuzi ya kesi. Hazungumzii ni nini walifanya hadi watendaji wa serikali wakatoa vibali vya kuchota hizo pesa.
  1. Malalamiko ya msingi ya Tanesco ni IPTL kutoza kiwango uwezo cha kuzalisha umeme 'capacity charges' cha juu kuliko fomula ya makubaliano. Gharama hizo zinakokotolewa kutokana na gharama za mwanzo za uwekezaji. VIPEM hazungumzii kwamba gharama iliyopita kiwango ilitokana na IPTL kuumua/kuongeza (inflate) gharama za mwanzo za uwekezaji (ujenzi wa kituo, gharama za mitambo/aina ya tekinolojia n.k) na pia Kwa nini IPTL ikajenga mitambo ya mwendo kati (medium speed) badala ya mwendo pole (slow speed) kinyume na mkataba na Tanesco? Haya yote waraka huu umekwepa kuyazungumzia.
  1. Kudaiwa na benki kama umekopa ni kitu cha kawaida. Kwa nini waraka haulezi hali ya mahusiano kati ya wawekezaji VIPEM, Mechmar na benki ya Standard Chartered? Waraka unasema, 'Baada ya VIPEM kuuza hisa zake kwa PAP (Yule Singa Singa Sethi) na kulipwa stahili yake…' Je, VIPEM alilipwaje stahili yake? Inavyosemekana yule singa singa amenunua IPTL kwa shs milioni 6 na hakulipa kodi. Alipataje Mabilioni ya kumlipa VIPEM kama si zile pesa za escrow zilichotwa kwanza na kugawanwa bila kujali kesi ya Tanesco vs IPTL? Material facts ziko wazi kwamba ile kesi lazima Tanesco wangeshinda kwa hivyo VIPEM na PAP wakatumia ujanja walioujua kulipwa kabla ya maamuzi ya kesi.
  1. VIPEM waelewe kuwa maslahi ya nchi hayaangaliwi na viongozi aliowaita wawili wenye nia mbaya. Tunayaangalia sisi sote wananchi wapenda maendeleo, na hatukubali, iwe Standard Chartered Bank, PAP, VIPEM au yeyote kukwepua mali ya umma. Ninasema hivyo kwa sababu katika waraka huu VIPEM wanajenga hoja indirectly kwamba hizi pesa kuchukua wao ni sawa lakini kuchukuliwa na Standard Chartered Bank si sawa kwa kuwa wao si wazalendo.
  1. VIPEM anadharau kwamba pesa za escrow si mali ya umma ila ziliwekwa pale kutokana invoice (madai) ya IPTL kwa Tanesco. Kutokana habari tunazozipata ambazo hazijakanushwa ripoti ya CAG inaonyesha tayari Tanesco kabla ya kesi walikuwa wamewalipa IPTL zaidi ya billion 320 na pale akaunti ya udhamini (escrow account) kulikuwa na bilioni 306 ambazo tayari zimechotwa, hizi pesa ilikuwa zirudi Tanesco na IPTL wadaiwe bilioni 15 halafu baadaye ndiyo Tanesco waanze kulipa 'capacity charges stahili. Kila mwenye akili timamu hahitaji kwenda shule hata ya kindergarten kujua kwamba pesa za escrow zilikuwa ni mali ya umma.
  1. Madai kwamba IPTL ilikuwa inatoza capacity charge ndogo kuliko makampuni mengine yanayoiuzia umeme Tanesco. Hiyo ni kweli na sisi wananchi haturidhiki na ndiyo maana ishu ya Richmond ilimwondoa Mheshimiwa Lowassa Uwaziri Mkuu. Lakini si hoja halalishi (pretext) ya IPTL kutoza capacity charges zaidi ya kiwango kulichokubaliwa kimkataba. Nasisitiza kama hapo juu mkataba wa Tanesco na IPTL uko wazi kwamba capacity charges zitakokotolewa kufuata gharama za mwanzo za uwekezaji na si kwa kulinganisha na makampuni mengine. Kwanza enzi zile wala hayo makampuni hayakuwepo.
  1. VIPEM analaumu magazeti, anasema yanahukumu. Magazeti ni sauti ya watu na mahala pengi yamesaidia kuongeza uwajibikaji wa viongozi. Kuyabeza magazeti ni kutowatendea haki wananchi wa Tanzania. Cha msingi VIPEM waelewe kuwa vyombo vya habari vinaweza kupata chanzo cha habari kutoka popote na vinafuata misingi ya taaluma kutenda kazi zake. Ikiwemo na 'triangulation of sources of information' yaani kuthibitisha habari kwa kutumia vyanzo kadhaa. Magazeti yetu ya Mwananchi, The Citizen, Nipashe, Mawio, Mitandao ya Jamii kama Jamii Forum, Wanabidii, Mwahalisi Forum, n.k, vyombo hivi vinanaendeshwa kwa ueledi mkubwa na tunavipongeza kwa juhudi za kufichua vichaka vya ubadhirifu vinavyotesa nchi yetu. Vyombo vya habari viko wazi kwa wote hata kwao VIPEM na PAP, badala ya kujificha kwa mgongo wa mahakama walitakiwa wawe huru kujibu hoja za wananchi juu ya uchotaji wa hizo pesa.
  1. Uanzishwaji na hatimaye uzalishaji wa umeme na uendeshwaji wa IPTL umekuwa na utata tangu mwanzo. VIPEM ilitegemewa kama kampuni ya M/Watanzania kuwa mbele kuonyesha kuwa na sisi tunaweza badala ya kufikiria maslahi binafsi mbele zaidi. Kugawa mabilioni hayo kwa wanasiasa na watendaji wa serikali kwa sababu ambazo hata zingekuwa halali inaleta maswali kwenye falsafa ya uendelevu wa biashara (business sustainability) na haitufundishi sisi wajasiriamali kuzingatia maadili tangu mwanzo wa biashara zetu.
Hivyo basi kama haya maelezo katika toleo la 25/11/2014 la mwananchi ndiyo ukweli wa VIPEM na PAP wanaousimamia kutetea uchotaji wa fedha za umma bado unazua maswali mengi kuliko majibu na wananchi bado tunataka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya kila aliyehusika na pia fedha zote zirudishwe.
Saini tamko kukataa vitendo vya ufisadi na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria: bofya hapa

On Tuesday, November 25, 2014 1:13:47 PM UTC-8, Emmanuel Muganda wrote:
Kama fedha ni za iptl kwa nini ziliwekwa escrow account in the first place? Nadhani kitu huwekwa escrow kama kuna pande mbili zenye maslahi na kitu hicho ama?
em

2014-11-25 16:07 GMT-05:00 Abdalah Hamis <hami...@gmail.com>:
Kinachoitwa kwamba ni kashfa ya akaunti ya Escrow ni ngoma ambayo wanaoichezesha wanafanya hivyo kwa matumaini kwamba wakiivutia kwao basi hatimaye watafaidika ipasavyo. Miongoni mwa wanaoishangilia ngoma hii ni baadhi ya mawakili waliokuwa wakiitetea Tanesco na Benki ya Standard Chartered.

Benki ya Standard Chartered inataka kuhakikisha kwamba kunakuwapo na sintofahamu kuhusu akaunti hiyo ya Escrow na kulazimisha imilikiwe ama na Serikali ya Tanzania au Tanesco kwa sababu hiyo inaweza kuisaidia katika lengo lake kuu la kupata fedha isizostahili. Ni wazi kwamba fedha zilizohifadhiwa katika akaunti hiyo ya Escrow si za Serikali wala si za Tanesco kama ambavyo Standard Chartered na wapambe wao wanavyolazimisha iwe. Fedha hizo ni za IPTL.

Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza mwaka 1998 baada ya IPTL kukamilisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mtambo wa 100MW Tegeta Mjini Dar es Salaam. IPTL walitaka Tanesco inunue umeme kwa bei kubwa kuliko ilivyo kuwa halali lakini Tanesco walikataa kwa madai kwamba gharama zilizoainishwa na IPTL zilikuwa kubwa mno kuliko gharama halisi za uwekezaji.

Tanesco katika jitihada za kujinasua iliajiri kampuni ya uwakili ya Mkono & Co. Advocates ili kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani.

Kutokana na tofauti za mitazamo ya gharama za uwekezaji, mawakili hawa waliishauri Tanesco ifungue kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji {ICSID} nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.

Katika uamuzi wa Julai 2001 uliotolewa na ICSID kwenye kesi iliyofunguliwa na Tanesco dhidi ya IPTL mwaka 1998, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba, gharama za uwekezaji zishuke kutoka dola za Marekani milioni 163.53 hadi milioni 121.83.

Uamuzi huo wa mwaka 2001 uliridhia mfumo wa kifedha {financial model} iliyokuwa imekubalika katika kukokotoa viwango {tariff calculation} kati ya Tanesco na IPTL ambayo inaipa IPTL marejesho ya uwekezaji {internal rate of return - IRR} ya asilimia 22.31 badala ya asilimia 23.1 iliyodaiwa na IPTL. Mawakili wa Tanesco Mkono & Co Advocates walishauri kwamba Tanesco itekeleze mfumo huo.

Mwaka 2004, mawakili hao hao wa Tanesco wakiongozwa na Mkono & Co. Advocates waliishauri Tanesco isitekeleze ulipaji wa tozo ya uwezo wa kuzalisha umeme {Capacity Charges} kwa kutumia mfumo wa kifedha uliokubalika mwaka 2001. Kutokana na ushauri huo, Tanesco kwa kuamini ushauri wa mawakili wao mwaka 2006 kwa kupinga thamani ya invoices zilizowasilishwa na IPTL kwa kutumia mfumo wa fedha {financial model} iliyotolewa na ICSID. Kitendo hicho kiliifanya IPTL kuupinga uamuzi huo wa Tanesco wa kutofuata ulipaji wa tariff kwa kutumia mfumo wa fedha wa mwaka 2001.

Baada ya Tanesco kupokea ushauri wa Mkono & Advocates iliutilia mashaka na hivyo kuamua kuomba ushauri kwa kampuni ya Huntons & Williams iliyokuwa ikiishauri Serikali katika mashauri ya nje ya nchi.

Kampuni ya Huntons & Williams ilisisitiza kuwa unaosemekana kuwa ni ugunduzi uliofanywa na kampuni ya Mkono & Co. Advocates ulikosa hoja ya msingi yakuifanya Tanesco ipinge kulipa tozo ya uzalishaji umeme {capacity charge} kama ilivyokubalika mwaka 2001.

Ni wazi kwamba ushauri wa kampuni ya Mkono & Advocates ulikuwa ni wa kuipotosha Serikali na Tanesco kwa manufaa binafsi na kwa mantiki hiyo basi kampuni ya Mkono & Co Advocates ilikusudia kesi kati ya Tanesco na IPTL iendelee ili waendelee kulipwa gharama za kuendelea na kesi.

Ushahidi wa upotoshaji ni mwaka 2012 Mkono & Co. Advocates kuitaka Tanesco kukubali usuluhishi nje ya mahakama katika shauri la Tanesco kukataa kuilipa IPTL capacity charges kwa kigezo kwamba uwezekano wa Tanesco kushinda katika kesi ya kupinga kiwango cha tozo ulikuwa mdogo na unaashiria kuendela kuuiingiza Tanesco kwenye hasara kubwa na kesi zisizokuwa na ukomo.

Aidha, moja ya kesi ambazo zinathibitisha kuwapo kwa mgongano wa kimaslahi wa mawakili ni shauri kati ya Tanesco na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong {SCB-HK} lililoko ICSID.

Shauri hilo linawakilishwa na mawakili wenye asili na historia ya pamoja na kampuni ya Mkono & Co. Advocates. Mkono & Co. Advocates anaiwakilisha Tanesco na kwa upande mwingine Bw. Charles Morison mwenye mahusiano makubwa na kampuni ya Mkono & Advocates kwa kuwa alikwa mwanasheria wake ndiye anaiwakilisha SCB-HK.

Mahusiano haya ya kikazi kati ya mawakili hawa yanaashiria mgongano mkubwa wa kimaslahi na kuifanya Serikali na Tanesco wasinufaike na huduma yao kwa kuwa huduma za mawakili hao zilikuwa zimegubikwa na maslahi binafsi na kuwatwisha Watanzania mzigo mkubwa.

Ukiachilia mbali kizungumkuti hicho cha mgongano wa maslahi tangu kampuni ya Mkono & Co. Advocates kwa pamoja na Huntons & Williams wapewe kazi hiyo ya uwakili na Tanesco mwaka 1998, jumla ya shilingi bilioni 62.9 zimelipwa kwa kampuni ya Mkono & Advocates.

Kadhalika kampuni hizo bado zinaidai Serikali ya Tanzania jumla ya dola za Marekani milioni 4.5.

Ni wazi kwamba gharama zingeweza kuongezeka endapo Serikali na Tanesco wangeendelea kuwatumia mawakili hao kwa kuwa mawakili hao wamekuwa wakishinikiza kujiingiza katika kesi kwa kuipa Serikali na Tanesco matumaini ya kupata ushindi jambo ambalo matokeo yake ni Serikali na Tanesco kuendelea katika kesi zisizoisha kwa hasara kubwa lakini kwa manufaa ya mawakili ambao wamegeuza hizo kesi kuwa miradi yao ya kudumu.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni za Tanzania, ni dhahiri SCB-HK haikusajili hati inayoitwa Deed of Assignment au dhamana nyingine hapa nchini ambazo zingelihalalisha madai ya madeni na dhamana inayodaiwa kuipa benki hiyo uhalali wa kutambulika kisheria kama mdai wa IPTL. 

Baadhi ya mambo yanayoonesha ni jinsi gani mawakili waliipotosha Tanesco ni kwamba SCBHK ilifungua shauri kwenye Mahakama ya Usuluhishi (ICSID ARB/10/20) kimakosa na TANESCO ilipewa ushauri usio sahihi na wanasheria wake kuhusu kesi hiyo.

Jambo linaloshangaza ni kwa vipi mawakili wa TANESCO waliamua kutofuatilia masuala muhimu ambayo yalistahili yafuatiliwe na kujengewa hoja za kisheria. Kwa mfano hoja za kisheria kwamba baadhi ya mashauri mengine hayawezi kusikilizwa nje ya Mahakama za Tanzania lakini mawakili wa TANESCO na Kampuni ya Mkono & Co. Advocates haikutetea hoja hiyo.

Kampuni ya Mkono & Co. Advocates ambayo ilikuwa ni Mawakili wa TANESCO hawakuipasha ICSID kwamba mgororo kati ya TANESCO na IPTL ulimalizika Oktoba 2013. Pia inaelekea kwamba mawakili wa TANESCO walitaka mgogoro uendelee badala ya kufikia mwisho, kwani kila mara walikuwa hawatekelezi kama mteja wao alivyokuwa anataka mambo yawe. 

Mawakili ni waajiriwa waaminifu wa mteja na maafisa wa mahakama. Taaluma yao, licha ya kuwa na umaalumu wake, matakwa ya kutoa ushauri ili mteja awe katika hali ya kujua kila kinachoendelea na pia kama hapana budi kupunguza gharama kama ushauri usingelikuwepo.

Hata hivyo, mawakili wanaofanya kazi wanatakiwa kuwa na uadilifu wa hali ya juu sifa ambazo inaelekea mawakili wa TANESCO wameshindwa kuthibitisha kuwa nazo katika kutimizia wajibu wao kitaaluma. Haya yatajionesha wazi wazi katika kufanya mapitio kwenye maeneo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kibiashara na kiutendaji kati ya TANESCO na IPTL kwa ushauri wa mawakili.

Aidha, katika muendelezo huo huo wa kuivuruga Tanesco Standard Chartered Bank imeiomba ICSID katika shauri ICSID ARB/10/20 kuiamuru TANESCO kuilipa SCB-HK USD 208.3 milioni pamoja na riba ya LIBOR + 4% katika kesi nyingine ya Novemba 14, 2014 deni ambalo uhalali wake unabishaniwa siyo tu na Tanesco bali pia na kampuni ya VIP.

Suala la umiliki wa fedha za escrow halina utata
Kumekuwapo na mchezo mchafu wa kisiasa wa kujaribu kupotosha ukweli kuhusu umiliki wa fedha zilizokuwapo katika akaunti ya escrow iliyojulikana kama Tegeta Escrow.

Ili kuelewa kwamba fedha katika akaunti hiyo zilikuwa zitaendelea kuwa ni za IPTL na kamwe hazijawahi kuwa za Tanesco wala Serikali ni muhimu kutambua ukweli tu kwamba mlipaji wa deni hawezi kuwa mmiliki wa deni analolilipa.

Akaunti ya Escrow ilifunguliwa kutokana na ushauri wa Mkono & Co. Advocates wa mwaka 2004 ambao walitoa hoja kuwa gharama za kununua umeme zilizokokotolewa kwa kutumia asilimia 22.31 ya urejeshwaji wa uwekezaji {IRR} zilikuwa hazikubaliki na hivyo Tanesco walikuwa wakitoa hati ya kupinga malipo kwa kila ankara ya malipo kupinga gharama hiyo kulingana na kifungu Na.6.8 cha mkataba wa ununuzi wa umeme {PPA}. Kifungu hicho kinaeleza kuwa ikiwa upande wowote haukubaliani na usahihi wa malipo katika ankara zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi {Invoice Dispute Notice} kwa upande mwingine.

Vile vile, mawakili wa Tanesco Mkono & Co. Advocates waliishauri kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe akaunti maalum {Escrow Account} kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zilitokana na ankara zilizokuwa zinapingwa.

Ushauri huo ulitekelezwa na Tanesco na mnamo Julai 5, 2006 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini mkataba wa kufungua akaunti maalum kwa ajili ya kuweka fedha zote za ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL.

Kwa mantiki hiyo Akaunti ya Escrow ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya IPTL yaliyokuwa yakisubiri kuthibitishwa na Tanesco kwa pamoja na IPTL kwa pamoja kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 6.8 cha mkataba wa ununuzi wa umeme yaani PPA.

Kwa mantiki hiyo basi ni vema ikafahamika na kueleweka kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na wala siyo fedha za Serikali wala si za Tanesco.

Ni wazi pia kutambua kwamba wahusika walikuwa na uhuru wa kuweka fedha hizo katika akaunti nyingine yoyote kutegemea na makubaliano yao yaani ya IPTL na Tanesco.

Hivyo basi kitendo cha fedha hizo kuhifadhiwa katika akaunti iliyofunguliwa na kuhifadhiwa katika Benki Kuu haina maana kuwa fedha hizo zilikuwa za Serikali.

Kwa mujibu wa kifungu namba 7.7 cha mkataba wa Akaunti hiyo ya Escrow fedha zilizomo kwenye akaunti hiyo zingeendelea kuhifadhiwa na Wakala wa Escrow {Escrow Agent}, hadi muafaka utakapofikiwa kati ya Tanesco na IPTL kuhusiana na mabishano ya ankara.

Kwa mujibu wa mkataba wa escrow, Benki Kuu ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia na kuendesha akaunti ya Escrow hadi hapo Tanesco na IPTL watakapofikia muafaka na akaunti kufungwa.

Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliotolewa na Jaji Utamwa wa kuiondoa IPTL kwenye ufilisi na kuitambua PAP kama mmiliki wa asilimia 100 wa IPTL, Tanesco ilifanya mazungumzo na IPTL na kukubaliana na kiasi ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa na IPTL.

Baada ya makubaliano kati ya Tanesco na IPTL serikali ilisaini makubaliano na IPTL kuruhusu fedha za akaunti ya Escrow zilipwe kwa IPTL na Benki Kuu ikaagizwa kuzilipa fedha hizo na hatimaye kuifunga akaunti hiyo.

Oktoba 21, 2013 Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na IPTL walisaini makubaliano ya kutoa fedha zilizomo katika akaunti ya Escrow ili zilipwe kwa IPTL. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama Agreement for Delivery of Funds to Independent Power Tanzania Limited yaliambatana na muhtasari wa kikao cha pamoja cha uhakiki wa malipo ya tozo kati ya IPTL na Tanesco pamoja na barua ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwasilisha makubaliano hayo na kuiomba Benki Kuu iruhusu malipo hayo kwenda IPTL kama uhakiki ulivyobainisha, na kwa vile matakwa ya kifungu 7.7 cha mkataba wa Akaunti ya Escrow unavyosema yalikuwa yametekelezwa kikamilifu.

Kufuatia maombi ya Benki Kuu kwenda Wizara ya Fedha ya kufunga akaunti ya Escrow kutokana na kumalizika kwa mgogoro kuhusu mali ya uwekezaji na kwa kuzingatia uamuzi wa Mahakama Kuu, mwezi Desemba 2013 akaunti hiyo ya Escrow ilifungwa rasmi.

Wakati wa kufunga akaunti hiyo ya Escrow, Tanesco ilikuwa ikidaiwa na IPTL jumla ya dola za Marekani milioni 79.05 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 125.04 zilizotokana na tozo ya uzalishaji {capacity charges} ambazo hazijalipwa. Kimsingi fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow wakati wa kuilipa IPTL na kufunga akaunti hiyo zilikuwa kidogo kuliko madai ya IPTL.

Ikumbukwe kwamba kuanzia Septemba 2009 Tanesco iliacha kulipa fedha za tozo ya uzalishaji umeme {capacity charges} kwenye akaunti ya Escrow kwa sababu ya ukata wa TANESCO/ Serikali.

VIP ina Tax Credit kubwa na TRA

Kampuni ya VIP ilipouza hisa zake asilimia 30 kwa PAP mwaka 2013 ilideposit tax credit ya jumla ya TZS 38,186,584,322.-ambazo ni asilimia 30 (30%) ya gharama za mauzo kiasi ambacho ni kikubwa kuliko matakwa ya Sheria ya Capital Gains Tax inayotamka kuwa kiwango kinachotakiwa ni asilimia 10 (10%) kwa sababu VIP iliomba suala la kodi lijadiliwe baadaye ikiwa na washauri wa maswala ya kodi.

Tozo ya uwekezaji wa IPTL ni ya chini

Ukweli usiopingika ni kwamba tozo ya uwekezaji ya IPTL ni senti za Marekani 1.06/kWh ikilinganishwa na za Songas ambazo ni senti za Marekani 4.31/kWh, Symbion senti za Marekani 4.99kWh na Aggreko inayotoza senti za Marekani 5.77/kWh.

VIP inasimamia Maslahi ya Taifa

Wakati wote VIP imetetea maslahi ya Taifa katika IPTL na itaendelea kufanya hivyo hata baada ya kuuza hisa zake kwa PAP. Ikumbukwe kwamba VIP iliiomba Mahakama kuweka masharti katika hukumu ya kesi yake ya kutaka kumaliza mgogoro wa IPTL. Masharti ambayo VIP iliyaomba na Mahakama kuyaridhia ni kutaka wamiliki wapya wa IPTL kampuni ya PAP: Kuongeza uwezo wa uzalishaji wa IPTL mpaka MW 500, kupunguza bei ya umeme wa IPTL kuwa kati ya senti za Marekani 6/kWh na senti za Marekani 8/kWh, PAP kulipa madeni yote halali ya IPTL na kubadilisha matumizi ya mafuta mazito kuendesha mitambo na badala yake itumike gesi asilia.

Imetolewa na VIP Engineering and Marketing Limited

--
Send Emails to wana...@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+...@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+...@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment