Saturday 26 January 2013

[wanabidii] SHULE ZA KATA NI MAKABURI YA KUZIKIA ELIMU YA WATOTO WA WALALAHOI!

Mimi naomba niseme kwa sauti kubwa na bila kumung'unya maneno kwamba KWENYE KATA HAKUNA SHULE pale. Huwezi kuongelea SHULE mahali ambapo hakuna SHULE! Unajua shule ni nini? Shule inajumuisha madarasa (majengo), walimu, wanafunzi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mazingira (surrounding), nk. Sasa niambie hizo mnazoziita shule za kata kama zinavyo vitu vyote nilivyovitaja hapo juu. Ni kama vile unapoweza kununua kitambaa, ukakiita nguo wakati bado hakijashonwa ili kufikia hadhi ya kuitwa nguo! Pale kwenye kata kuna majengo (sema magofu) ambamo vijana wanaomaliza (sio wanaofaulu) darasa la saba wanajazwa na kujipumzikia kwa kipindi cha miaka minne.
 
Ndio maana 'wanafunzi' wengi (zaidi ya 90%) wanaohitimu kwenye 'shule' hizi hufaulu kwa kiwango cha daraja la nne (kwa alama 33 na kuendelea) au daraja la sifuri (zaidi ya alama 35). Serikali haikuwa na malengo ya kueleweka pindi wanaanzisha hizi 'shule' —lilikuwa ni wazo la kisiasa tu ili waendelee kupewa kura na kujikita madarakani. Kama hayo magofu ya kwenye kata ni SHULE ni kwa nini mafisadi hawasomeshi watoto wao huko? Mbona wao wanasomesha watoto wao kwenye 'international academies'? Kwa nini wasiwalete watoto wao nao 'wakosome' kwenye hizo shule? Hili ndiyo swali la kujiuliza. Huwezi kunipa sumu kwa kuniaminisha kwamba ni chakula wakati wewe na wanao hamli hiyo sumu.
 
Katika kuonesha msisitizo kwamba shule za kata ni makaburi ya kuzikia elimu ya watoto wetu, Rais kikwete aliwahi kunena kwamba "watoto wanaosoma kwenye shule za kata watakuwa wakulima, wafugaji na wazazi wazuri pindi wakihitimu". Hii maana yake ni kwamba, hategemei kwamba kuna wanafunzi wa kutosha wanaoweza kupenya kutoka kwenye hizo shule wakaendelea na masomo ya juu zaidi ya hapo. Hata yeye alishasoma alama za nyakati akaona kwamba hizi shule hazina tija yoyote zaidi ya kuzalisha wakulima na wazaaji wazuri! Wanaume wakihitimu wataenda kwenye kilimo na wale wa kike wataenda kwenye kuolewa na kuzaa - na watakuwa walezi wazuri wa watoto kuwa wameishapata elementary knowledge juu ya reproductive health, child care and human nutrition. Hayo tu, basi! Hawasogei zaidi ya hapo.
 
Pia naomba niseme kwamba 'mtu mwenye nusu elimu' ni mbaya kuliko yule asiyekuwa nayo kabisa. Msitegemee kwamba watoto wetu (kama wapo) watakaopata 'nusu elimu' kwamba itawafikisha popote. Na ndiyo maana hata Mh Rais aliliona hilo na kulisemea bila kumung'unya maneno. Ila kwa kuwa watanzania ni wagumu wa kuleewa na wepesi wa kusahau, itachukua muda kufahamu dhana hiyo ya Rais. Ni bora kumyima mtu elimu moja kwa moja kuliko kumpa nusu elimu.
 
Serikali imechakachua ubora wa hizi shule hadi inakuwa vigumu kuchuja watoto wanaojua kusoma na kuandika. Kuma. Alama za ufaulu zilishushwa hadi 65 kwa 250 ili walau kupata watoto wa kujaza 'magofu ya kata' mnayoyaita shule. Hii ni aibu. Mtoto anayepata alama 65 kati ya 250 (wastani wa alama 65/5 = 13 kwa 100) atachaguliwaje kujiunga na elimu ya sekondari?. Mtoto atapataje wastani wa alama 13/100 halafu achaguliwe kwenda sekonfdari 'kujaza nafasi'? Hawa si ndio wale wasojua kusoma na kuandika? Nakumbuka enzi zile za mwalimu Nyerere hakukuwa na ubabaishaji kama huu. Mtu ukienda sekondari unakuwa kichwa kweli.
 
Kumbuka kwamba wananchi wanajitahidi sana kuchangia elimu lakini serikali haichangii chochote (hakuna walimu, vitabu, vifaa vya kufundishia, mazingira bora kwa wanafunzi, nk). Serikali inachojua ni kununua magari ya kifahari na vitu vingine vya anasa. Kila siku serikali wakitakiwa kuborsha elimu, wanadai hawana pesa. Pesa za anasa, kulipana posho na za kuficha uswisi zinatoka wapi? Halafu mtu anakuja kusimama mbele ya umma anatetea udhaifu wa serikali, Tumueleweje?
 
Kazi ya wananchi wa kawaida ni kulipa kodi ambayo tungetegemea itumike kuboresha huduma za jamii. Badala ya kutumiwa kuboresha huduma za jamii (shule, elimu, maji, nk), zinatumiwa na mafisadi kujaza matumbo yao makubwa - ambayo hayajai kamwe!

0 comments:

Post a Comment