Monday 14 January 2013

[wanabidii] DR SLAA JUU YA MOU KATI YA SERIKALI NA KANISA

Wana JF,

Nashukuru mwana JF aliyeweka hadharani MOU husika. Ningependa tu
kuongezea machache na hasa historia ya jinsi na kwanini MOU hiyo
ilizaliwa:-

1) Wote mtakumbuka kuwa huko nyuma Serikali ilitaifisha Shule na
nyingi za madhehebu ya Dini. Utaifishaji huo uliendana pia na Ardhi,
hasa ikizingatiwa kuwa wakati shule zinajengwa zilijengwa kwenye
maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo kukukiwa na kanisa, nyumba za
mapadre na kadhalika. Hii ilikuwa hivyo kwa shule nyingi za Middle
School (Model Schools, Upper Primary kama mnavyojua majina
yalibadilika sana kati ya 1962 hadi 1965 hivi na ndipo pia mtihani au
darasa la nane lilipofutwa rasmi).

2) Kwenye miaka ya 1980 madhehebu yakataka warudishiwe ardhi yao, hasa
ardhi ambayo ina majengo mengine yasiyohusiana na shule hizo. Mchakato
wa mjadala ulishika kasi, mwaka 1986 Baraza la Maaskofu Katoliki TEC,
lilipopitisha azimio rasmi,na kumtaka Katibu Mkuu, awasiliane na
Serikali, kuanzisha mchakato wa kufanya survey na kutenga ardhi ya
shule rasmi kutoka kwenye ardhi inayotumika kwa huduma nyinginezo za
madhehebu ya dini. Wakati huo mimi Dr. Slaa, ndiye nilikuwa Katibu
Mkuu wa TEC baada ya kupokea rasmi kazi hiyo December, 1985. Wakati
huo madhehebu yaliisha kudai yarudishiwe Shule zao kwa kuwa zimegeuka
kuwa aibu kwa kukosa ukarabati, na ziko kwenye hali mbaya sana.
Serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa Shule hizo
zinawahudumia watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo
lilikuwa lengo kuu la utaifishaji, na sababu ya utaifishaji ilikuwa
bado inaendelelea.

3) Wakati mawasiliano yalipoanza na Serikali wakati huo kupitia Ofisi
ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, Serikali iliomba TEC na madhehebu
ya Dini kwa ujumla, kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule hizo kwa
kuwa ziko kwenye hali mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri na
hivyo mapato ya Serikali.

4) Wakati mchakato huo kwa upande wa Elimu umeanza kulikuwa pia na
mgogoro kati ya Serikali na TEC baada ya Serikali kuichukua Hospitali
ya Bugando almost kwa utaratibu huo huo wa kuitaifisha. Hospitali hiyo
ilikuwa kwenye awamu ya Pili ya ujenzi kwa msaada mkubwa wa Shirika la
Misereor( Shirika la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la
Ujerumani) toka Ujerumani.

5) Katibu Mkuu wa TEC alipowasiliana na Wahisani walikataa kata kata
kujihusisha tena na ujenzi au ukarabati wa Shule au Hospitali
( Hospitali, vituo vya Afya na zahanati) kwa kuhofia kuwa Serikali ya
Tanzania imekuwa ikitaifisha huduma hizo bila majadiliano ya aina
yeyte, na hawawezi kuwekeza fedha za walipa kodi wao ( ujerumani
Madhehebu ya dini yanapata fedha rasmi kutoka kodi ya wananchi) kwa
ratio waliyokubaliana kuendana na idadi ya madhehebu ya dini. Lakini
walikuwa tayari kuendelea na huduma mbalimbali za kusaidia madawa na
elimu kwa shule zilizoko bado chini ya madhehebu kwa kuwa hawawezi
kuwaadhibu wananchi na watoto.

6) Kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilikuwa zinaelekea kusimama na
kulikuwa na mgomo kila siku, kwa madaktari na manesi na watumishi,
Serikali ikaomba tujadiliane upya juu ya mambo makubwa mawili :
a) Utoaji huduma katika sekta za huduma za Jamii,
b) Kuwa na chombo cha mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na
madhehebu ya dini, na kwa kuwa madhehebu ni mengi wakaomba chombo
hicho kiundwe na viongozi wakuu wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana
kwa mujibu wa Sheria.

Hivyo Bakwata ( Waislamu- sitaki kuingia kwenye mjadala wa kama
Bakwata ni chombo kinachowasilisha waislamu au la), Tanzania Episcopal
Conference TEC na CCT ( kwa madhehebu zaidi ya 60 yaliyoko chini ya
Christian Council of Tanzania) . Baada ya Mashauriano tuliunda chombo
hicho kikiwakilishwa na Mwenyekiti na Katibu wa vyomb o nilivyovitaja
hapo juu. Uratibu ulikuwa unabadilika kila mwaka katika ya madhehebu
hayo, vivyo hivyo kwa Sekretariat. Kutokana na utaratibu huo tuliweza
kupatia ufumbuzi matatizo yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara na
ikawa rahisi kwa Serikali kuwasiliana na chombo hicho badala ya kila
dhehebu peke yake, na kwa upande wetu pia chombo hicho kikatupa nguvu
ya kujadiliana na serikali (power of negotiation).

7) Kutokana na hali mbaya ya Shule Serikali, ikaomba madhehebu ya dini
kusaidia ukarabati wa shule zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali
mbaya , nasi kwa upande wetu kwa nia njema ya kuisaidia Serikali
lakini pia kuwahudumia watanzania tuliwasiliana na Wahisani ambao
walikazia msimamo wao kuwa hawako tayari kuingia kwenye shughuli za
ujenzi wala ukarabati kwa kukosa msimamo wa wazi na au wa kisheria wa
Serikali ya Tanzania kuhusiana na utaifishaji wa huduma hizo. Serikali
ilipojulishwa, ilichukua hatua ya kuanzisha mchakato mzima wa kupata
suluhu ya jambo hilo. Ndipo akapewa jukumu hilo, Mhe. Anne Makinda
wakati huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, na mkutano wa kwanza
ulifanyika Kurasini Conference Centre (TEC) Mikutano ya baadaye
ilikuwa ina alternate kati ya TEC na CCT. Hii ni kwa sababu huduma
zilizokuwa zinajadiliwa ni za TEC na CCT ( ambao walikuwa wameathirika
na utaifishaji huo). Hatimaye, Serikali ilikubali kuwa haitataifisha
tena, na kwa kuthibitisha hivyo, ikawa tayari kuwekeana MOU na
madhehebu ya Dini.
Ndipo tukaanzisha mchakato wa majadiliano na Wahisani, na wahisani,
nao katika umoja wao kati ya dhehebu la kikatoliki Ujerumani na
Kilutheri pia la Ujerumani tukaanzisha mchakato wa namna bora ya kutoa
huduama za jamii. Daima Serikali ilishirikishwa kama Observer katika
michakato hiyo, na kwa upande wa Ujerumani Serikali yao nayo
ilishirikishwa katika timu za majadiliano. Hatimaye, makubaliano
yalifikiwa, na ndipo ikazaliwa chombo kipya Christian Social Services
Commission (CSSC), chenye Secretariat yake ( Katibu Mtendaji wa kwanza
akawa Dr. F.Kigadye aliyekuwa Mkurugenzi wa Bugando).

Huduma za kilichokuwa Christian Medical Board (ya TEC na CCT ikavunjwa
na kuwekwa chini ya CSSC) na idara za Elimu zilizokuwa chini ya TEC na
CCT huduma zake zikaunganishwa na kuwekwa chini ya CSSC. Ndiyo MOU
iliyosainiwa na Askofu Stanford Shauri wa Diocese ya Ruvuma,
Mwenyekiti/Katibu Mkuu wa CCT wakati huo, na Askofu Josephat Lebulu,
wakati huo Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, na Mwenyekiti wa TEC. Kwa
upande wa Serikali kama sikosei aliweka saini Mhe. Edward Lowassa,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (au Waziri sikumbuki).

8) TEC na CCT nazo zikawekeana na Wahisani Mkataba MOU yao ya ndani
ili kupata misaada ya ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa huduma zote
za jamii . Huduma hizo zinaendelea hata sasa japo sasa kwa kiwango
kidogo baada ya mkataba wa awali kwisha.

Narudia tena, namshukuru sana aliyeweka kwenye JF MOU hiyo. Ninarudia
kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia ya
aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu,
wala kabila wala ukanda. Haya mambo tukiyaendekeza Taifa letu litakuwa
hatarini. Tukumbuke kubomoa ni kazi nyepesi sana, sekunde lakini
kujenga tena inachukua muda mrefu na ni kaz ngumu, na wakati mwingine
hata ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa. Nashauri ili JF ibaki
na heshima yake ya Home of Great Thinkers tupende kufanya Research
zaidi kabla ya kulaumiana au kuhisiana, kama mtu hana taarifa za kina
awaombe wenye taarifa. Kama mnavyoona mimi nilikuwa nafahamu historia
yote, nafahamu MOU, lakini sikuwa nayo. Mtu huwezi kujua kila kitu na
au kuwa na kila kitu, we need to complement each other. Tunaweza
tukidhamiria, na JF itabaki na hadhi na heshima yake daima.

http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/383549-tamko-la-dr-slaa-juu-ya-mou-kati-ya-serikali-na-kanisa.html

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment