Thursday 23 May 2013

[wanabidii] Neno La Leo: Mtwara Tunagombania Kivuli..!

Ndugu zangu,

Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre anasema; " Hell is the other people" – Kwamba  jehanam ni wale wengine, anataka pia  tukubaliane, kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.

Na hakika, tofauti ya mwanadamu na mnyama iko kwenye kufiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndio maana ng'ombe anaweza kumpanda mama yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.

Hivyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi hapaswi kabisa kuongozwa na hisia ikiwamo ushabiki. Anapaswa kfikiri.

Vinginevyo, ni ukweli, kuwa kijamii, mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye mahusiano ya kirafiki na kiadui na wenzake. Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha, mashamba, wanawake na hata kivuli cha mti.

Ndio, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa kivulini. Na wanaweza kugombana mpaka akatokea mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Na wanadamu hao watabaki wakitazama  juani.

Hoja yangu hapa, kuwa lililo la msingi ni kuwa wanadamu tunategemeana.  Kwamba panapo kushindania jambo, mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima na busara.

Na kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano.  Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani,  panakosekana mazungumzo ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika kwa amani. Hapa Serikali inapaswa iandae haraka  mazingira ya  mazungumzo katika kuitafuta suluhu.

 Ndugu zangu,

Nilikuwa  shuleni miaka ile ya 80 pale aliyekuwa Waziri Mkuu, Dr. Salim Ahmed Salim alipotembelea Mtwara na kukutana na umasikini uliomstusha sana. Kule Mtwara Dr. Salim alikutana na Watanzania waliovaa magunia na miguuni hawana hata kandambili. Na kwenye jua kali walijipanga kando ya barabara kumpokea. Kwenye jua kali walikusanyika kumsikiliza Waziri Mkuu wao.

Ni kule Mtwara inasemekana Dr. Salim, kwa mara ya kwanza,  alipofikia maamuzi ya kutoa ruhusa ya mitumba kuingizwa nchini. Maana, kulikuwa na Watanzania wengine wengi nje ya Mtwara waliokuwa kwenye hali ya umasikini wa kufikia kuvaa nguo za viraka na kushindwa hata kuvaa viatu vya matairi  ya magari. Tunajifunza nini?

Kwamba ni kweli Mtwara na sehemu nyingine za nchi zimekuwa nyuma sana kimaendeleo. Na leo tunaposikia Mtwara kuna gesi, nakubaliana na Rais Jakaya Kikwete, kuwa gesi hiyo haiwezi kuwa ni ya WanaMtwara tu. Ni gesi ya Watanzania wote.

Ni vema na ni busara, na kwa kuwashirikisha wazee wa Mtwara, kuwa WanaMtwara wakasikilizwa. Kuna ya msingi ambayo WanaMtwara na Serikali wanaweza kukubaliana kwenye meza ya mazungumzo.

Hata kama tunakubaliana, kuwa rasilimali za nchi ziwasaidie pia watu wa eneo inakotoka rasilimali hiyo, lakini kamwe, tusikubaliane na hoja kuwa gesi  iliyo Mtwara ni ya WanaMtwara. Kwamba dhahabu ya Geita ni ya watu wa Geita, twiga wa Ruaha ni wa Wahehe na kadhalika. Haya si mawazo mazuri kuyapandikiza katika nchi.

Ni mawazo ya hatari yanayoweza kupandikiza chuki, sit u miongoni mwa wananchi na Serikali, bali hata miongoni mwa wananchi wenyewe wa maeneo tofauti. Ni mawazo yenye kupandikiza pia fikra za kibaguzi.

Na tufikiri hili, je, kama gesi  ile iliyopatikana kule  Mtwara, Tanzania na  Msumbiji nayo ingesema ni ya kwake, WanaMtwara  wangesemaje kama watu wa mikoa mingine ya nchi hii nao wangesema wapelekwe wanajeshi wa Kimakonde, Kiyao na Kimakua tu wakambapane na majeshi ya  Msumbiji kutetea ' Gesi ya Mtwara!'?

 Naam, ya kule Mtwara isije ikawa yale yale ya kugombania kivuli.

 Maggid Mjengwa,

Iringa,

0754 678 252

http://mjengwablog.co.tz

 

 

 

 

 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment