Thursday 30 May 2013

[wanabidii] Ombi la Rais Kikwete la Walimu wa baadhi ya masomo kutoka Jamaica lakubaliwa

Jamaica imeahidi kuisaidia Tanzania kwa kuipatia walimu wa hisabati na
sayansi na pia imesema kuwa itatoa kocha wa kufundisha mchezo wa
riadha kwa nia ya kusaidia maendeleo ya mchezo huo nchini Tanzania.

Aidha, nchi hizo mbili zimeahidi kuongeza ushirikiano katika nyanja
mbali mbali na kuangalia uwezekano wa Tanzania kufungua aina ya
uwakilishi katika Kisiwa hicho cha Caribbean katika miaka miwili
ijayo.

Makubaliano hayo kati ya Tanzania na Jamaica yalifikiwa usiku wa
Jumapili, Mei 26, 2013, katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu
wa Jamaica, Mama Portia Simpson Miller.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Hotel ya Sheraton mjini
Addis Ababa, Ethiopia, viongozi hao wawili walikubaliana kuwa Jamaica
itaangalia uwezekano wa kuisaidia Tanzania kwa kutoa walimu wa
kufundisha hisabati na masomo ya sayansi.

Rais Kikwete alikuwa Addis Ababa kuhudhuria sherehe za miaka 50 tokea
kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Juni 25, mwaka 1963 na Mkutano wa 21
wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU wakati Mama Simpson Miller alikuwa
mmoja wa viongozi mashuhuri wa nchi mbali mbali duniani walioalikwa
kuhudhuria sherehe hizo.

Katika mazungumzo hayo, Mama Portia Simpson Miller ambaye aliapishwa
kuwa Waziri Mkuu wa Jamaica Januari 5, mwaka jana, 2012 baada ya chama
chake cha Peoples National Party (PNP) kushinda uchaguzi mkuu nchini
humo, alimwuliza Rais Kikwete jinsi gani Jamaica inavyoweza kuisaidia
Tanzania.

"Mawili makubwa ambayo mnaweza kutusaidia – moja ni walimu wa hisabati
na masomo ya sayansi kama mnao wa kutosha na pia kocha wa riadha ili
tuweze kufufua upya mchezo huo ambao Tanzania ilikuwa inatamba duniani
katika miaka ya 1970," alisema Rais Kikwete.

Mama huyo alimwahidi Rais Kikwete kuwa Jamaica inao uwezo wa kusaidia
katika maeneo yote mawili. "Hili la walimu tutaliangalia mara moja
nikirejea nyumbani. Tutasaidia kwa kadri inavyowezekana kwa sababu
najua fika juhudi zako kubwa ambazo umekuwa unafanya katika eneo hili
la elimu na mafanikio makubwa ya jitihada zako."

Kuhusu kocha wa riadha, Mama Simpson Miller amesema kuwa na hilo
halina pingamizi kwa sababu yeye alikuwa Waziri wa Michezo kwa miaka
mingi na kuwa kwa sasa Wizara ya Michezo iko kwenye Ofisi yake ya
Waziri Mkuu. "Nilikuwa Waziri wa miaka mingi wa michezo katika nchi
yangu na kwa sababu ya umuhimu wa michezo, nimeamua kuiweka shughuli
ya michezo katika Ofisi yangu ya Waziri Mkuu."

Jamaica ni moja ya nchi zinazoongoza katika mchezo wa riadha duniani
ikiwa imetoa wanariadha wengi mabingwa wa dunia akiwamo bingwa wa sasa
wa Olimpiki na dunia katika mbio fupi za mita 100 na 200 – Usain Bolt.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Mei, 2013


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment