Wednesday 27 March 2013

[wanabidii] Katiba Mpya: Maoni ya CUF

Chama cha CUF kipo tayari kutoa ushirikiano unaostahiki kwa Tume
katika kipindi chote cha mchakato huu pamoja na kushirikiana na
Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti nyinginezo,
kuhakikisha kuwa kwa pamoja nchi yetu inakuwa na katiba bora yenye
kukidhi haja na matakwa ya hali ya kisiasa, kiuchumi na ustawi mwema
wa jamii ya Watanzania.

UTANGULIZI

Kwa niaba ya The Civic United Fronf (CUF-Chama Cha wananchi), na kwa
niaba yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na wajumbe wako kwa kutualika rasmi Chama Cha CUF
mbele ya Tume yako kutusikiliza na kupata maoni ya chama chetu juu ya
mchakato huu muhimu kwa mustakbali mwema wa Taifa letu la Tanzania
pamoja na watu wake.

Aidha, tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya
Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato huu wa mapitio makubwa na
kukusanya maoni ya katiba ya nchi yetu ili ikidhi matakwa ya wakati wa
sasa na kutupeleka mbele zaidi kwa ustawi wa Taifa letu na watu wake.
Madai haya ya kuandaa mchakato wa kuwa na katiba mpya inayokidhi
matakwa ya wakati tulionao ni madai ya msingi ambayo chama chetu cha
CUF kimekuwa kikiyasisitiza tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa
demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992 na mara zote
kuainisha suala hili katika manifesto zake za uchaguzi.

Kutokana na muongozo wa Tume ya Mabadiliko ya katiba maoni yetu
yamejikita katika maeneo yafuatayo; Misingi na Maadili ya Kitaifa,
Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi, Ardhi,
Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala),
Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Muundo na Mamlaka
ya Serikali za Mitaa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Kwa muhtasari maudhui haya Chama Cha Wananchi CUF kinapendekeza
yafuatayo katika mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania:
1. Muundo wa serikali tatu za muungano yaani serikali ya Zanzibar,
serikali ya Tanganyika na serikali ya Mungano.

2. Uanzishwaji wa Tume huru za uchaguzi mapema iwezekanavyo. Kwa kuwa
Tume ya uchaguzi inapaswa kuanza kazi zake mapema ili kufanikisha
uchaguzi wa mwaka 2014/15, Tume haiwezi kusubiri mabadiliko ya katiba
yakamilike ndio ianze kazi zake kwa Muundo mpya utakaopendekezwa.

3. Katiba yenye misingi ya mfumo wa uwajibikaji kwa watendaji wote wa
umma na uainishwaji wa wazi wa Dira ya Taifa.

4. Katiba itakayotoa haki kwa wagombea binafsi kushiriki katika
uchaguzi.

5. Katiba itakayotoa uhuru wa vyama vya siasa kuungana muda wowote
vitakapoona inafaa bila kupoteza usajili wa kawaida wa vyama hivyo.

6. Katiba itakayoweka muundo wa kuwa na Rais mtendaji "Executive
President" mwenye madaraka yanayopimika na kukubalika yasiyobana wala
kuingilia au kuondoa uhuru wa utendaji kazi wa mihimili mingine ya
dola. Rais achaguliwe kwa kupata asilimia 50+1 au zaidi ya kura
zilizopigwa.

7. Katiba yenye kuweka mfumo sahihi wa kulinda rasilimali za Taifa na
kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania wote kwa haki na usawa.

8. Katiba itakayompa kila Mtanzania kwa nafasi yake kushiriki katika
maendeleo ya nchi yake kwa kuwa na muundo wa serikali
itakayoshirikisha kila Mtanzania mwenye uzalendo wa kweli na uwezo wa
kutoa mchango wake kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa.

9. Katiba itakayoweka muundo wa uwakilishi wa uwiano (propotional
representation) ili kila kura itakayopigwa kuwa na thamani tofauti na
utaratibu wa sasa wa mshindi kuchukua vyote (winner takes all) hata
kama ameshinda kwa kura moja.

10. Katiba itakayo hakikisha uwepo wa mgawanyo wa madaraka kati ya
serikali kuu na serikali za mitaa kwa kuondoa mfumo wa kuziburuza
serikali hizo zilizokaribu na wananchi. Wilaya zisianzishwe kiholela.
Vigezo vya halmashauri ya wilaya, miji, manispaa na majiji vitawekwa
na sheria. Utawala wa mikoa uondolewe.

11. Katiba itakayoweka msingi wa kuzuia ufisadi mkubwa wa rasilimali
za nchi hasa kwa njia ya uingiaji wa mikataba, Bunge likiwa ni chombo
cha uwakilishi wa wananchi lazima lishirikishwe.

12. Katiba itakayoweka Muundo wa Tume huru za Taifa za uchaguzi tangu
ngazi ya uteuzi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya chini.
Katiba itakayotoa fursa matokeo ya uchaguzi kwa ngazi zote kuhojiwa
mahakamani ikiwemo matokeo ya uchaguzi wa Rais.

13. Katiba itakayopambanua mgawanyo wa madaraka na mamlaka ya mihimili
yote mikuu katika nchi kwa maana ya Bunge, Serikali na Mahakama.

14. Katiba itakayoeleza wazi kuhusu haki na wajibu wa dola kuhakikisha
elimu ya watoto wetu, matumizi ya rasilimali za taifa, huduma za
msingi za afya, ulinzi wa nchi yetu na sera za ardhi na kilimo
zinasimamiwa na kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi wote. Katiba ndiyo
yenye nafasi ya kulinda haki hizi za mwananchi na si huruma ya mtawala
atakaye kuwepo kwa wakati huo au chama cha siasa. Sera za kitaifa
lazima zifuate na kuheshimu haki zilizoainishwa ndani ya katiba.
15. Kuhakikisha kwamba wananchi wana madaraka ya kujiamulia wenyewe
masuala ya maendeleo yao kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

16. Katiba yenye kulinda haki za binaadamu, na kupinga aina zote za
ubadhilifu, ukandamizaji, ubaguzi wa aina yeyote iwe wa kidini,
kikabila, kijinsia au kikanda.

17. Katiba yenye kuweka misingi endelevu ya kulinda amani ya nchi
yetu.

18. Masuala ya Ardhi yawe na sura kamili katika katiba mpya. Ardhi ni
mali ya Watanzania wote. Mtanzania peke yake ndiye anayeweza kumiliki
ardhi moja kwa moja.

19. Katiba inayohakikisha kuwa haki za msingi za makundi maalum,
wanawake, watoto, wazee wasiojiweza na walemavu zinalindwa kwa
kuainshwa ndani ya katiba.

Chama cha CUF kipo tayari kutoa ushirikiano unaostahiki kwa Tume
katika kipindi chote cha mchakato huu pamoja na kushirikiana na
Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti nyinginezo,
kuhakikisha kuwa kwa pamoja nchi yetu inakuwa na katiba bora yenye
kukidhi haja na matakwa ya hali ya kisiasa, kiuchumi na ustawi mwema
wa jamii ya Watanzania.

Ni matarajio ya Chama Cha Wananchi CUF kuwa maoni haya yatazingatiwa
na kuingizwa katika rasimu ya mabadiliko ya katiba kwa mjadala na
hatimaye kufanyiwa maamuzi yanayofaa kwa mustakbali mwema wa Taifa
letu la Tanzania.

Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.

HAKI SAWA KWA WOTE

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa CUF Taifa

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment